Sunday, July 20, 2014

Wakazi wa Vijijini Mkoani Ruvuma kupatiwa umeme

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amezindua mradi wa kusambaza umeme vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) utakaowanufaisha wakazi wa Mkoa wa Ruvuma utakaochangia kuongeza kasi ya maendeleo vijijini. 
 Rais Jakaya Kikwete yuko katika  ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika mkoa huo lengo likiwa ni kutimiza azma ya serikali ya kuwa kila mwananchi anapata huduma ya nishati ya umeme. 
 Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amewahakikishia wakazi hao kwamba hadi ifikapo mwezi Novemba mwaka huu vijiji vyote vilivyoko katika mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya II watakuwa tayari wanatumia nishati hiyo kwa wale watakao wamemudu gharama ya Shilingi Elfu Ishirini na Saba ya kuunganishiwa nishati hiyo. 
 Imeelezwa kwamba mradi wa usambazaji wa umeme vijijini katika mkoa wa Ruvuma utagharimu kiasi cha Tsh. 26.53 bilioni zitakazohusisha ujenzi wa njia za umeme zenye msongo wa kilovolti 33 zenye jumla ya urefu wa km 538, ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolti 11 yenye urefu wa km 23, ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa km 272, ufungaji wa transfoma 129 za ukubwa mbalimbali pamoja na kuunganisha wateja 7,488. 
 Mradi huu utatekelezwa na kampuni ya Lanka Transfomers Limited, (LTL) ya nchini SRILANKA kwa mkoa wa Ruvuma. Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2015 na kunufaisha wakazi wa wilaya za Songea, Tunduru, Mbinga na Nyasa. 
 Pamoja na uwepo wa mradi huo pia kuna mradi wa kuongeza nguvu ya umeme kwenye wilaya za Mbinga na Tunduru unaotekelezwa na kampuni ya Taikai Co.Ltd ambapo tayari amekamilisha survey ya vituo vyote na ameshawasilisha transifoma ya kituo cha Tunduru. Prof. MUHONGO amesema mradi wa kuongeza nguvu ya umeme utagharimu kiasi cha pesa za kitanzania Shilingi bilioni 2.27 zitakazohusisha ujenzi wa vituo viwili vya kuongeza nguvu ya umeme kutoka kilovoti 11 hadi kufikia kilovoti 33 kwa ajili ya kufikisha umeme katika vijiji vilivyoko mbali. 
Vituo hivyo vitakuwa na transifoma zenye uwezo wa kilowati 3,000 (3.0MW) kila kimoja. Kwa upande wake Mbunge wa MBAMBABAY Captain JOHN KOMBA ameishukuru serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama hicho ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara hasa madaraja, kuwawekea umeme, na kupandishwa hadhi kituo cha afya na kuwa hospitali ya wilaya. 
 Miradi ya REA awamu ya II imeanza kutekelezwa rasmi Novemba 2013 na inatakiwa kukamilika ifikapo Juni2015 kwa nchi nzima hivyo kuchangia katika kuongeza kiasi cha wananchi waliofikiwa na huduma ya umeme kufikia asilimia 30.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akielekea eneo la jukwaa mara baada ya kuwasili katika eneo palipofanyika uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) wilaya ya Nyasa mwishoni mwa wiki, kushoto kwake ni Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo.

Meneja wa Shirika la umeme nchini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi,   Bi Salome Nkondola akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa miradi ya umeme kwa mkoa wa Ruvuma mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete.

Rais Jakaya M. Kikwete akichukua mkasi kwa ajili ya kukata utepe tayari kuelekea katika eneo la uzinduzi wa mradi wa usambazaji wa umeme wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kulia kwake ni Waziri mwenye dhamana na nishati Prof. Sospeter Muhongo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mama Salma Kikwete pamoja na viongozi wa serikali wakiwepo Waziri wa Ardhi na maendeleo ya Makazi, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ujenzi wakiwa wameshika utepe tayari kwa Rais kuukata na kuelekea kubonyeza kitufe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa mradi huo wa umeme.

Rais akifunua kitambaa mahali palipowekwa kitufe kwa ajili ya uzinduzi rasmi
Rais akifunua kitambaa mahali palipowekwa kitufe kwa ajili ya uzinduzi rasmi
Rais akibonyeza kitufe
Rais akifurahia uzinduzi mara baada ya zoezi hilo kukamilika
Burudani wakati wa sherehe hizo

No comments:

Post a Comment