Mkuu
wa kituo cha polisi Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ASP
Lwitiko Norman Kibanda, akizungumza na madereva wa pikipiki za kubeba
abiria ambao juzi waliandamana hadi kwenye kituo hicho wakipinga kutozwa
fedha sh22,000 na maofisa biashara wa wilaya hiyo, waliodai kuwa tozo
hizo ni amri ya Mamlaka ya Usafirishari wa vyombo vya usafiri wa majini
na nchi kavu (Sumatra).
Madereva
wanaoendesha pikipiki 800 wa kubeba abiria, maarufu kama bodaboda wa
Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiaro Mkoani Manyara, wameandamna
hadi kituo cha polisi Mirerani, wakipinga kitendo cha maofisa biashara
wa wilaya hiyo kuwataka walipe sh22,000 za tozo la Mamlaka ya
usafirishaji wa vyombo vya majini na nchi kavu nchini (Sumatra).
Wakizungumza
mbele ya Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, ASP Lwitiko Kibanda,
waendesha bodaboda hao walidai kuwa wamechoshwa kunyonywa na maofisa
biashara hao kwani tozo hizo hutolewa eneo hilo peke yake hivyo wao
wanagoma kulipa kwani wanaonewa na hawapo yatari kulipa kiasi hicho.
Mmoja
kati ya madereva hao Rashid Omary alisema maofisa biashara hao
waliwaeleza suala hilo siku moja na kesho yake wakaanza zoezi la
kukamata pikipiki zao ili hali hawakupatiwa elimu wala kushirikishwa
kwenye suala hilo, hivyo hawapotayari kulipa kiwango hivyo kwani
wamechoka kunyonywa kila mara.
“Tunashangazwa
kuambiwa tutoe sh22,000 za Sumatra ili hali maeneo mengine ya Arusha,
Kilimanjaro au wilaya ya Simanjiro kule Landania, Orkesumet na Naberera
hawalipishwi, kama sheria ya kunyoa nywele watu wote imepitishwa kwanini
sisi tuwe na vipara wengine wawe na nywele, hatukubali kulipa hizo
fedha,” alisema Omary.
Naye,
Geofrey John alisema wabunge walifuta tozo za pikipiki za kubebea
abiria hivyo wanashangazwa na maofisa biashara wa wilaya hiyo kuwataka
walipe fedha hizo, hivyo watagoma kutoa fedha hizo kwani hivi sasa kila
mmoja anatambua haki zake na hawatakubali kuburuzwa tena.
Kwa
upande wake, Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, ASP Lwitiko Kibanda
aliwaeleza waendesha bodaboda hao kuwa wanatakiwa wakutane tena na
maofisa biashara hao ili kuzungumzia suala hilo kwani kodi ya Serikali
ni lazima ilipwe.'
“Tatizo ni kutotolewa kwa elimu juu ya suala hili kwani wengine waendesha bodaboda siyo mali zao ni waajiriwa
hivyo, tujipange upya kwa maofisa biashara na ninyi bodaboda tukutane
na viongozi wenu ili mueleze ipasavyo na mshirikishwe kutokana na jambo
hili,” alisema Kibanda.
Hata
hivyo, Ofisa biashara wa wilaya ya Simanjiro, Peter Sanga alisema
wanatoza sh22,000 za Sumatra wilayani humo, kwa pikipiki inayosafirisha
abiria yenye magurudumu mawili na pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) na texi kwa mujibu wa sheria ya Bunge.
“Tozo hiyo
ni halali kulipwa na hudumu kwa muda wa mwaka mmoja na endapo mtu
akilipia mwezi Mei au Julai mwaka huu, atatakiwa kulipa tena mwakani
mwezi Mei au Julai na siyo vinginevyo, hivyo waendesha pikipiki za
kubebea abiria ni lazima walipie pikipiki hiyo,”alisema Sanga.
Alisema
Bunge halikufuta tozo hizo, kwani waliziachia na pia ada ya zimamoto
kwenye pikipiki zinazolipiwa sh10,000, bima ambayo hutozwa wastani wa
sh50,000 na sh22,000 ya ada ya Sumatra na ombi la kukatiwa tozo hiyo,
hivyo pikipiki za kubebea abiria zinatakiwa kulipa fedha hizo za
Serikali.
No comments:
Post a Comment