Tuesday, July 15, 2014

MAALIM SEIF AKUTANA NA PAC

  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa fedha za Serikali ya Baraza la Wawakilishi (PAC), Ofisini kwake Migombani.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa fedha za Serikali ya Baraza la Wawakilishi (PAC), Mhe. Omar Ali Shehe, akizungumza wakati kamati yake ilipokutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, Ofisini kwake Migombani.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa fedha za Serikali ya Baraza la Wawakilishi (PAC), pamoja na baadhi ya watendaji wakuu wa ofisi yake, Ofisini kwake Migombani.


ZANZIBAR           15/07/2014.
Na: Hassan Hamad (OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, Serikali inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuongeza vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato hayo.

Akizungumza na Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya ukaguzi wa fedha za Serikali (PAC) Ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema ikiwa mianya ya upotevu wa mapato ya serikali itadhibitiwa ipasavyo, serikali itaweza kuongeza mapato yake na kuweza kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati.Aidha amesema serikali inapaswa kutafakari zaidi kuona kuwa sehemu kubwa ya matumizi kwa ajili ya kazi za maendeleo inatokana na mapato ya ndani, badala ya kutegemea wafadhili na mikopo kutoka nje.

“Sasa hivi mapato ya ndani yanatumika kwa kazi za kawaida wakati kazi za maendeleo zinasubiri wafadhili na mikopo kutoka nje, ukweli serikali tunapaswa tujifunze juu ya hali hii ili tumewe kuiepuka kwa mustakbali mwema wa maendeleo ya nchi yetu”, Maalim Seif aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo. Amesema Serikali inathamini juhudi zinazofanywa na kamati hiyo katika udhibiti wa fedha za umma, na kuishauri iendelee kuwa wazi katika kueleza matumizi ya fedha za Serikali.

Maalim Seif amesema Ofisi yake imekuwa ikiyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na kamati hiyo, na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo na Serikali kwa ujumla.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa fedha za Serikali ya Baraza la Wawakilishi Mhe. Omar Ali Shehe amewapongeza watendaji wakuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kuweza kusimamia vyema matumizi ya fedha za Ofisi hiyo.

Amebainisha kuwa kamati yake ambayo ndiyo yenye jukumu la kufuatilia ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, haikubaini kasoro yoyote ya matumizi ya fedha, licha ya kuwepo mapato madogo tofauti na yale yaliyoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi. Ameishauri Serikali kuyafanyia kazi mapendekezo ya Ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali  ya mwaka 2011/2012 ili kuweza kukabiliana na changamoto zolizojitokeza.

Wakati huo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amekutana na balozi mpya wa Tanzania nchini Urusi balozi Wynjones Kisamba na kusema kuwa Tanzania ikiwa nchi isiyofungamana na upande wowote kisiasa, itaendelea kushirikiana na pande zote katika kukuza na kuendeleza mahusiano ya kimataifa.

Amesma Tanzania ni nchi iliyojijengea sifa kubwa katika medali ya Kimataifa, na itaendelea kuienzi sifa hiyo. Amemtaka balozi Kisamba kuendelea kuitangaza Tanzania kwa kueleza fursa za uwekezaji zilizopo nchini, huku Zanzibar ikitilia mkazo katika maendeleo ya sekta ya utalii.

Maalim Seif amesisiza kuwa mabalozi wa Tanzania nchi za nje wana jukumu kubwa la kuendeleza diplomasia ya kiuchumi katika nchi wanazokwenda, ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi.Amempongeza balozi huyo kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchi Urusi, na kumtakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake.

Nae balozi Kisamba amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Urusi unaimarika kwa maslahi ya pande zote mbili. Amesema nchi hizo zina uhusiano wa muda mrefu tokea wakati wa kupigania uhuru, na kwamba uhusiano huo kamwe hauwezi kupuuzwa, na badala yake utazidi kuimarishwa.

Akizungumzia uzoefu wake kuhusu Urusi, balozi Kisamba amesema nchini hiyo ni miongoni mwa nchi zinazotoa watalii wengi duniani hasa wakati wa msimu wa baridi, na kuahidi kulishughulikia suala la kuendeleza utalii, ili watalii wengi wa Urusi waweze kuja Tanzania.

No comments:

Post a Comment