Barua ya Wazi kwa Uongozi wa
CCT juu ya Tamko la Mapatano ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 48 ya Jumuiya ya
Kikristo Tanzania la tarehe 3 Julai, 2014.
• Sio la Kiponyaji, linatonesha
Madonda
• Watu wa Mungu hawategemewi
Kupotosha, Labda Wamepotoshwa
Na John Nkhundi
Si kawaida yangu kulumbana na viongozi wa dini
kwa sababu ya heshima waliyonayo katika jamii na matumaini ya waumini wao
kwao. Hata hivyo, leo nimelazimika
kuandika baada ya kusoma tamko la Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT)
lililotolewa na Mkutano wa Halmashauri Kuu iliyokutana tarehe 3 Julai, 2014
ambalo maudhui yake ni ya kisiasa na limesheni mambo ya dunia.
Tamko hilo lililopewa jina la "Tamko la
Mapatano ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 48 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania wa
Julai 2-3, 2014" limenistua kwa mambo makubwa matatu. Mosi, tamko hili
limetolewa Julai 3, 2014 lakini likatolewa magazetini tarehe 15 Julai,2014 tena
katika gazeti moja tu la Mwananchi. Mtiririko huu wa matukio yaani muda wa
Tamko lilipotolewa na muda lilipochapishwa kunatia mashaka ikiwa ni jambo la
kimkakati au nasibu tu. Zaidi, upana huu wa muda kati ya lilipotolewa na
kuchapishwa kunaleta pia wasiwasi kuhusu uhalisia wa tamko lenyewe. Maana, kwa
kawaida matamko ya aina hii hutolewa mara tu Mkutano unapoisha, tena kwa
kusomwa mbele ya waandishi wa habari.
Safari hii, hali ni tofauti maana tamko
limechapishwa gazetini, wiki mbili baada ya kutolewa, tena bila ya jina la
aliyelitoa zaidi ya jina la jumla yaani "imetolewa na Mkutano wa
Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania". Aina hii mpya ya utoaji wa Tamko inatoa
mwanya wa kuhisi kuwa pengine tamko hili si rasmi na limechakachuliwa kwa lengo
mahsusi la aliyelivujisha. Maana ukilisoma kwa makini, halionekani kuandaliwa
kwa ajili ya umma bali kumbukumbu tu. Wanaoweza
kututoa kwenye kitendawili hiki ni CCT wenyewe.
Pili, lugha yenyewe ya tamko na maudhui yenyewe
ya Tamko yamesheheni siasa na sio utume. Usiposoma kichwa cha habari na
hitimisho, unaweza kudhani limetolewa na chama cha siasa au wanaharakati. Hii inajidhihirisha hata jinsi ambavyo
Mhariri wa gazeti la Mwananchi alivyolitafsiri katika Toleo Na. 5105 lenye kichwa
cha habari tena cha ukurasa wa mbele, yaani "Tamko Zito kwa Kikwete".
Tamko hili haliponyi bali linatonesha madonda, jambo ambalo si kawaida kuliona
katika tamko la watu wa Mungu,
Maudhui ya tamko yamesheheni historia na sio
wakati ujao. Ni tamko lenye kuhukumu na sio kubariki, lenye kubomoa na sio
kujenga. Ni tamko lililojaa lawama na sio toba, lililojaa chuki na sio upendo.
Tamko linazungumzia madonda ambayo taifa imeyapitia, tamko halisherehekei maridhiano
yaliyofikiwa kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar iliyozaa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa, na vurugu za chaguzi na kisiasa zilizozaa mchakato wa Katiba mpya.
Tamko limelaumu pia, kupanuka kwa pengo kati ya maskini na matajiri, maadili ya
viongozi wa umma na kuibuka kwa itikadi kali za kidini.
Haya yote
kwa kiasi kikubwa yanaashiria pia kupwaya kwa baadhi ya viongozi wa katika
majukumu yao ya kulilea taifa kiroho. Maana sote tu mashuhuda namna ambavyo
mafisadi, wala rushwa wanavyopokelewa makanisani na misikitini, na fedha zao
zinavyobarikiwa kwenye harambee. Tumeshuhudia viongozi wa dini wakitenda maovu,
tena makubwa yasiyofikirika. Isitoshe, suala la itikadi kali za kidini,
zinachochewa na tamko kama walilolitoa CCT, ambalo limeacha misingi ya imani na
kujiingiza katika uanaharakati na siasa. Tamko hili linanistua sana kwa kuwa
hata viongozi wa dini nao sasa wanaonekana kuambukizwa ule ugonjwa wa watu wa kumlaumu
kila mtu kwa mapungufu yao isipokuwa wao wenyewe. Kaugonjwa haka ka kulaumu na kulalama
kametamalaki kwenye siasa, nilikuwa na matumaini kuwa viongozi wa dini
watatusaidia kukaponya, la hasha. Kama tumefika hapo, basi taifa linahitaji
uponyaji mkubwa. Kitakachotutoa hapa ni maombi na dua tu.
Tatu, Tamko lina upotoshaji mkubwa kuhusu
mchakato wa Katiba. Upotoshaji wenyewe ni wa dhahiri kuhusu mamlaka ya Rais
kwenye Sheria ya Katiba juu ya uteuzi wa Wajumbe wa Tume na Rasimu. Tamko linasema kuwa Rais aliwateua
wajumbe wa Tume na hivyo aliwafahamu vizuri, kuwaamini na kuwaapisha.
Linakwenda zaidi kusema kwamba Tume ilimshirikisha Rais katika kila hatua na
kuwa kilichotolewa na Tume walikubaliana kwa pamoja na Rais. Hawakuishia hapo,
Tamko likasema, "Tunaamini kuwa kile kilichoandikwa katika Rasimu ya
Pili kilikubaliwa na mwenye kutoa hoja yaani Mheshimiwa Rais na hivyo akaagiza
Rasimu hiyo itolewe kama ilivyo kwani aliamini kuwa huo ndio uamuzi wa wananchi
wengi kuhusu katiba wanayoitarajia. Pia tunaamini kuwa mwenye kutoa hoja
alikuwa na uwezo wa kuzuia Rasimu hiyo isitolewe endapo kuna ibara ambayo ina
mwelekeo ambao ungekuwa hatari kwa mustakhabali wa taifa letu".
Tuhuma hizi ni nzito sana haswa zinapotolewa na
viongozi wa dini, tena Jumuiya ya Kikristo Tanzania. Inaniwia vigumu sana
kuishuku CCT kuwa imepotosha makusudi. Hivyo, napenda kuamini hilo halikuwa
lengo lao ila wamepotoka tu, au wamepotoshwa. Naweka akiba ya kutowatuhumu
maana neno walilotumia zaidi ni "Tunaamini" jambo linalonipa faraja
pengine walisukumwa na imani tu bila utafiti na taarifa sahihi. Ni kwa sababu
hiyo nimeona niandike kwa ajili ya kuwasaidia zaidi kuhusu hili suala la tatu,
kwa imani kwamba, watu wa Mungu walighafirika, na wakiigundua kweli itawaweka
huru.
Mchakato wa Katiba unatawaliwa na Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Sheria
hii ndio rejea ya kila kinachofanyika katika mchakato huu. Moja ya sababu kubwa
ya kuwa na sheria hii ni kuondoa mamlaka ya Rais na Serikali kuhodhi mchakato
wa Katiba kwa kuepusha mgongano na mwingiliano wa maslahi. Katika mchakato wa
Katiba, jukumu la serikali ni la kiuwezeshaji tu, sio hata la kiuratibu.
Ukiisoma Sheria hii, Rais amedhibitiwa katika kuteua wajumbe anaopendekezewa na
Makundi, hana mamlaka ya kuingilia Tume,
kazi ya Tume wala kuibadilisha hata
kuizuia Rasimu ya Tume kuwasilishwa Bungeni.
Pia, Sheria inaweka wazi kuwa Rasimu ya Tume haitokani na maoni ya
wananchi pekee kama CCT wanavyojaribu kuamini na kuaminisha umma.
Ukiisoma Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya
6 (6) inaelezea kuwa "Rais ataalika vyama vya siasa vyenye usajili wa
kudumu, jumuiya za kidini,asasi za kiraia, jumuiya, taasisi zisizo za
kiserikali na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana kuwasilisha orodha ya
majina ya watu ili kuteuliwa kuwa wajumbe". Ibara ndogo ya 1 hadi 3 ya Ibara ya 6
imeainisha kuwa Rais kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar watateua wajumbe kwa
kuzingatia uzoefu, jiografia na mtawanyiko wa watu, umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbalimbali kwa jamii.
Hivyo, si kweli hata kidogo kuwa Rais aliteua watu kama alivyojisikia, na hivyo
si sahihi kusema kuwa wajumbe wa Tume hawawezi kuwa na msimamo tofauti na Rais.
Sheria hii kwa makusudi imeainisha makundi ili kutuepusha na uwezekano wa Rais
kuteua watu wenye mawazo tu ambayo yanayompendeza yeye. Ndio sababu, uteuzi wa
wajumbe wa Tume ulipokelewa vizuri na watu na makundi yote.
Suala la mamlaka ya Tume na uhuru wa Tume limefafanuliwa vizuri katika Sura ya 10
inayotamka kuwa, "Tume itakuwa na mamlaka na uhuru kwa kadri
itakavyokuwa muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu na mamlaka yake chini
ya Sheria hii na haitaingiliwa na mtu au mamlaka yoyote". Ukiangalia
kifungu hiki, hakuna namna yoyote Rais angeweza kuingilia kazi ya Tume. Hata
pale ambapo Tume ilimshirikisha Rais ilifanya hivyo kwa utashi wake tu sio kwa
shurti, na pengine kwa kutaka maoni au ushauri wake ambao pia hawakubanwa
kuukubali au kuuchukua. Hivyo, sio sahihi kuhitimisha kuwa, kwa kuwa Mwenyekiti
wa Tume alikutana kwa mashauriano na Rais katika nyakati mbalimbali, hivyo Rais
ni sehemu ya majumuisho ya kazi ya Tume au Rasimu ya Tume. Kusema kuwa Rais
ameikana Tume ni kupotoka, maana hakuwa na fursa ya kukubaliana na Tume. Rasimu
ya Katiba ni ya Tume, na sio zao la muafaka kati ya Tume na Rais.
Tamko la CCT limeibua hoja nyingine kuwa, Rais
alikuwa na mamlaka ya kuamua kutopeleka Bungeni Rasimu ya Katiba ya Tume kama
asingeridhishwa na kipengele au ibara katika Rasimu ile. Hili nalo halihitaji
maelezo mengi, maana Sheria imefafanua kinagaubaga kuwa dhima, ya Rais si
kuihakiki Rasimu bali kuipokea na kuelekeza iwasilishwe Bungeni. Ibara ya 20
(1) ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba
inatamka wazi kuwa,"Baada ya kukamilisha kazi yake, Tume itawasilisha
ripoti kwa Rais na Rais wa Zanzibar. Ibara
ya 20(2) inaendelea kufafanua kwamba, "Rais, ndani ya siku thelathini
na moja baada ya kupokea ripoti, atachapisha Rasimu ya Katiba katika Gazeti la Serikali na kwenye
magazeti mengine pamoja na maelezo kwamba Rasimu ya Katiba itawasilishwa kwenye
Bunge Maalum kwa ajili ya kupitishwa Katiba inayopendekezwa". Hakuna mahala ambapo Rais, wala Rais wa
Zanzibar wamepewa jukumu la uhariri au uhakiki wa Rasimu.
Hivyo, Sheria inamtaka Rais aelekeze Rasimu
iwasilishwe Bungeni bila kujali Rasimu
hiyo imempendeza au kumchukiza. Jukumu la kuondoa au kurekebisha kipengele
kinachoudhi au kukwaza halikuwekwa mikononi mwa Rais bali Bunge la Katiba. Bila shaka waliotunga Sheria waliongozwa na
busara kuwa Tume ya Katiba haiundwi na malaika na hivyo inaweza kuleta rasimu
yenye makosa au mapungufu. Zaidi, ikaona mbali kwamba jukumu la kuiboresha
likasimishwe Bunge lenye uwakilishi mpana wa jamii na sio Rais katika ile dhana ya kutoa mamlaka ya kutunga
Katiba kutoka kwa watawala kwenda kwa wananchi. Ndio sababu, kilele cha
mchakato huu wa Rasimu ya Tume, sio Bunge la Katiba bali kura ya wananchi.
Tunachokiona katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambacho ni kizuri ni kule
kupanuka kwa ushiriki mpana wa wananchi katika kila hatua ya mchakato wa
Katiba. Yaani, maoni ya wananchi waliojitokeza, kwenda kwenye mabaraza ya Kata,
Bunge la Katiba na hatimaye Kura ya maoni.
Binafsi napata sana tabu na maelezo ya CCT tena
yenye kuhitimisha kuwa Rasimu ya Tume ya Katiba ndio maoni ya wananchi.
Upotoshaji huu ndio unaozaa hoja kuwa Rasimu ijadiliwe kama ilivyo, na
isibadilishwe katika ngazi ya Bunge ambayo ina uwakilishi mpana kuliko ule
uliozaa Rasimu ya Tume. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Ibara ya 9(1) a-d
inaeleza wazi majukumu ya Tume yatakuwa ni "kuratibu na kukusanya maoni
ya wananchi;kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba
yanayohusu mamlaka ya wananchi, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa
sheria na utawala bora ; kutoa mapendekezo kwa kila hadidu ya rejea; na kuandaa
na kuwasilisha ripoti.
Aidha,
Ibara ya 19(1) inatamka ifuatavyo: " Kwa msingi wa mahojiano na
uchambuzi uliofanywa kwa kuzingatia vifungu vya 17 na 18 (yaani maoni ya wananchi, tafiti na mabaraza ya
kutoa maoni), Tume itatayarisha ripoti itakayokuwa na : (a) muhtasari wa maoni
ya wananchi kwa kila hadidu ya rejea; (b) mapendekezo ya Tume kwa kila hadidu
ya rejea;(c)ripoti za wataalam waeleekezi ambao Tume iliwatumia; (d) Rasimu ya
Katiba. na (e) taarifa nyingine yoyote muhimu. Hoja hapa ni kwamba, msingi wa Rasimu ya Tume
ya Katiba iliyotolewa na Tume si maoni ya wananchi peke yake. Hata pale Tume ilipobanwa kuhusu usahihi wa
takwimu zilizopelekea hitimisho kuwa wananchi wengi wanataka serikali tatu,
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Warioba alitoa utetezi kuwa, Sheria haikuwabana kuzingatia
takwimu au maoni ya wananchi peke yake. Hivyo, hoja kwamba Rasimu ya Tume ndio
maoni ya wananchi ni hoja dhaifu na muflisi. Rasimu ya Tume ni mseto wa maoni
ya sampuli ya wananchi waliofikiwa, tafiti na maoni ya Tume yenyewe.
Hata tukiamua kwa imani kuwa watu wa Mungu wako
sahihi kusema Rasimu ya Tume ni maoni ya wananchi, bado msingi wa imani yenyewe
ni dhaifu mno. Tume tukufu ya Katiba kwa makusudi iliamua kupuuza maoni ya
Mabaraza ya Katiba yaliyokuwa na uwakilishi mpana zaidi watu, kwa hoja kuwa ni
maoni ya CCM, au ya kupikwa. Ni Tume hiyo hiyo iliyokuwa na ujasiri wa kupokea
maoni yaliyotolewa na wanachama wa CUF kule Zanzibar yaliyotolewa katika awamu
ya kwanza ambayo walikuwa wakisoma maoni kama yalivyoandikwa. Maoni hayo mengi
ambayo yalitaka "Muungano wa Mkataba" Tume iliyachukua, tena ikaamua
kuyatakasa ili yamaanishe Muungano wa Shirikisho wa Serikali Tatu. Wingi wa
maoni hayo kiidadi na kitakwimu ndio yaliyofanya rasimu ya kwanza na baadaye ya
pili ionekane kuwa wananchi wengi wanataka Serikali tatu. CUF walikuwa wa
kwanza kukataa na kudai wao walipendekeza Muungano wa Mkataba.
Iweje, katika awamu ya pili ambapo uwakilishi
umepanuka kwa nchi nzima kuchagua mabaraza ya Katiba ambayo maoni yao
yamepuuzwa kabisa na Tume. Je, maoni ya
Mabaraza ambayo Tume imeamua kwa makusudi kuyapuuza siyo sehemu ya maoni ya
wannachi? Iweje, viongozi wa CCT
wabariki zao la matokeo ya kile kilichofanywa na CUF Zanzibar kisha waungane na
Tume kuharamisha kile wanachodai kilifanyika kwenye mabaraza ya Katiba katika
mchakato wa kutengeneza rasimu ya pili.
Kama maoni ya muundo wa serikali mbili si ya wengi, na mabaraza yalipika
maoni, si jukumu hilo lingeachiwa Bunge la Katiba katika ule utaratibu wa kila
hatua ya mchakato kuchuja maoni ya hatua iliyoitangulia? Je, hili ndio jambo
ambalo watu wa Mungu wanalisimamia?
Tamko
la CCT pia limeshusha lawama kubwa kwa Rais Kikwete eti ameuvuruga mchakato wa
Katiba. Wamemlaumu kwa hotuba yake kwa Bunge kuwa imeingilia madaraka ya Bunge
la Kikatiba. Rais analaumiwa kwa kuipinga Rasimu inayotokana na Tume
aliyoiunda. Ukaingizwa ushabiki kuwa Rasimu ile ya Tume haina doa na ni
timilifu. Napata tabu sana pale mtu anapotia shaka juu ya dhamira ya Rais
Kikwete kutaka Katiba mpya ipatikane, tena Katiba itokanayo na wananchi. Uamuzi
huu wa kuanzisha mchakato karibu umgharimu katika chama chake, ambapo amefanya
ushawishi mkubwa kuwafanya walipokee jambo hili jema. Isitoshe, kila
panapojitokeza mkwamo, amekuwa akijitokeza kutoa uongozi ikiwemo kukutana na
wapinzani katika hatua za mwanzo za utungwaji wa Sheria. Lugha yake daima na
hata sasa imekuwa ni kuwataka pande zote kuzungumza na kuridhiana. Hiyo ndio
lugha iliyosheheni katika hotuba yake aliyoitoa Bungeni tarehe 21 Machi, 2014
akilizindua Bunge. Katika hotuba ile, hakuna mahali Rais alitoa maelekezo zaidi
ya kuonyesha mapungufu machache katika Rasimu, kukumbusha wajibu wa Wajumbe wa
Bunge la Katiba wa kujiridhisha na vifungu, sentensi na dhana. Kwa mfano,
kuhusu Muundo wa Serikali Tatu, Rais anasema:
“...mzitazame hoja zote kwa marefu
na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa sasa wa
Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na kama zipo mabadiliko hayo yaweje? Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi wa hoja
zenye mashiko”. Hii inaonyesha wazi
kwamba Mhe. Rais hakuelekeza Bunge Maalumu la Katiba kupitisha Muundo wa
Serikali Mbili.
Wakati tamko hili linatolewa, kumekuwepo na rai
kutoka kila upande ya kujaribu kukwamua mchakato kwa kusihi pande zote kurejea
Bungeni na kuwepo kwa maridhiano. Wadau wa siasa tayari wanakutana kutafuta
namna nzuri ya kwenda mbele. Matarajio ya wengi wetu ni kuwa huu ndio wakati wa
viongozi wa dini kuwaombea wadau hawa na kuhubiri upendo, kusameheana na
unyenyekevu. Badala yake, tamko la CCT linaturudisha kwenye uhasama, badala ya
kujadili kipi ni sahihi, tamko linajadili nani yuko sahihi. Tamko la CCT
halituunganishi, linatugawa. Maana tamko linazungumzia Serikali moja na
kusisitiza kuwa msimamo wake ndio sahihi, bila kukumbuka kuwa CCT ni mmoja tu
ya wadau walio wengi, tena hata miongoni mwa wakristo wenyewe. Kwa vyovyote vile maoni yao hayawezi kuwa ya
mwisho. Wakati tamko la CCT linalaumu juu ya kuibuka misimamo mikali ya kidini,
tamko lenyewe linabeba msimamo mkali. Tamko limejaa kiburi, hukumu na lawama.
Hii sio lugha tuliyoizoea kutoka kwa watu wa Mungu. Au ndio tufuate wanachosema
sio wanavyoenenda?
Tamko la CCT kinyume na matarajio ya wengi
halijahubiri upendo na maridhiano bali kuchonganisha Tume, Rais na Bunge.
Nimeshangazwa na tamko la Viongozi wa dini kusengenya kwa kushindwa kukitaja
Chama inachodai kimevuruga mchakato wa Katiba. Ni nadra sana kusikia viongozi
wa dini wakizungumzia Chama kimoja kisha wasikitaje. Hii si hulka ya uzazi wala
ulezi. Haitegemewi kuwa ndio hulka ya viongozi wa dini na kwa kweli wanapoamua
kulaumu upande mmoja tu ilihali kila mtu aliona kwenye televisheni ambavyo kila
chama kilishiriki kwenye kukwamisha mjadala Bungeni, unapata hisia kuwa CCT
katika hili imeegemea upande. Napata wasiwasi ikiwa kweli hili ni tamko la CCT,
naendelea kuhofu kuwa limechakachuliwa. Ikiwa ni tamko rasmi la CCT, basi
napenda kuamini kwa kuchelea kuchuma dhambi ya kuhukumu kuwa, CCT haikuwa na
lengo la kupotosha umma, bali aidha wameghafirika au wamepotoshwa. Sio lazima
wajitokeze hadharani kuomba radhi watanzania, bali waseme na mioyo yao na
kumpigia goti mwenyezi mungu awasamehe. Kweli itawaweka huru.
umesema unatia shaka kwa kuwa hata tamko lenyewe halisemi limetolewa na nani. mbona hata wewe hizi hadithi zako ndeefu hujasema wewe ni nani?.
ReplyDeletetuna mashaka hata hii hadithi yako itakuwa imechakachuliwa pia. huna lolote !!