Friday, June 27, 2014

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YAWASILISHA MPANGO MKAKATI WA TAKWIMU ZA KILIMO KWA WADAU.

 Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke  akizungumza na wadau mbalimbali  wakati wa kujadili Mpango Mkakati wa Takwimu za Kilimo leo jijini Dar es salaam. Mpango huo utaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kukusanya takwimu sahihi zinazokidhi viwango vya ndani na vile vya kimataifa.
 Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) nchini Tanzania Bi. Diana Tampelman  akizungumza na waandishi wa habari kupongeza  hatua iliyofikiwa katika kukamilisha Mpango mkakati wa Takwimu za Kilimo nchini Tanzania  na kueleza  kuwa hatua hiyo inaendana na  Mpango wa Dunia  ulioanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kuboresha takwimu za kilimo maeneo ya vijijini.
 Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Kijadili Mpango Mkakati wa Takwimu za Kilimo wakifuatilia masuala mbalimbali wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es salaam.Picha na Aron Msigwa - MAELEZO.
======= ==== =====
 

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)  inakamilisha  Mpango mkakati  wa Takwimu za Kilimo wa mwaka 2014/15  mpaka 2018/19  utakaoiwezesha Ofisi  hiyo kuendesha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za kilimo nchini kila baada ya miaka 5.

Akizungumza wakati wa mkutano uliohusisha wadau mbalimbali wa kupitia  na kujadili rasimu ya mwisho ya mpango huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa mpango huo utaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kukusanya takwimu sahihi zinazokidhi viwango vya ndani na vile vya kimataifa.

Amesema  mpango mkakati huo unalenga kuboresha shughuli za ukusanyaji wa takwimu za kilimo  hapa nchini  kwa kujenga mfumo mmoja wa utoaji wa takwimu za Kilimo kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuliko ilivyo sasa na kubainisha kuwa taarifa zote za shughuli za kilimo nchini zitaingizwa kwenye mfumo wa serikali.

“Hapa tumekutana wadau mbalimbali kutoka  serikalini kwa maana ya wizara husika  na  wawakilishi kutoka mashirika ya maendeleo, lengo letu ni kupitia na kujadili rasimu hii ya mwisho itakayotuwezesha kujenga uwezo wa ndani wa  ukusanyaji wa takwimu za kilimo kuanzia ngazi ya kijiji mpaka taifa’’ Amesema

Amefafanua  kuwa mpango huo utaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bara na ile ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar kupata takwimu za shughuli zote za kilimo kuanzia wazalishaji wenyewe, hali ya kilimo, mazao, masoko pia kutoa mwelekeo wa nini kifanyike kuboresha sekta hizo kupitia takwimu zitakazokusanywa.

Aidha, amesema kuwa vipaumbele vya mpango huo vimeshaainishwa na kuwekwa mbele ya wadau ili kuwezesha upatikanaji wa nyenzo na uwezo wa kutekeleza mpango huo.

Kuhusu kufanikisha  mpango huo Bw. Oyuke  amesema kuwa jopo la taifa la wataalam  limeundwa likihusisha wataalam kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu na ile ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar, Wizara husika za Kilimo, Chakula na Ushirika,Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Maliasili na Utalii pamoja na wataam kutoka mashirika ya maendeleo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani(FAO) nchini Tanzania Bi. Diana Tampelman  amepongeza  hatua iliyofikiwa katika kukamilisha Mpango mkakati huo nchini Tanzania  na kueleza  kuwa hatua hiyo inaendana na  Mpango wa Dunia  ulioanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kuboresha takwimu za kilimo maeneo ya vijijini.

“Tunapongeza hatua hizi na tutaongeza nguvu zetu katika mpango huu ili kupata uhalisia wa shughuli za kilimo Tanzania kuhusu nani kazalisha nini na kwa kiwango gani ingawa watu wanaweza kushindwa kuona umuhimu wake lakini tunajua kuwa taarifa hizi ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi” Amesema Diana.

Naye mtaalam kutoka Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar Bw. Mzee Mohammed Mzee akiwasilisha mada kuhusu Hali ya Takwimu za kilimo nchini amesema kuwa kwa kipindi kirefu takwimu za kilimo zimekuwa zikipatikana kupitia Wizara na Taasisi zenye dhamana ya usimamizi wa sekta ya kilimo na kusababisha upatikanaji wa takwimu zinazotofautiana kutokana na njia zilizotumika wakati wa ukusanyaji wa takwimu hizo.

“Kisheria Ofisi ya Taifa ya Takwimu hapa nchini ndio yenye dhamana ya kukusanya  na kusambaza takwimu, suala la ukusanyaji wa takwimu lina njia zake, kumekuwa na shida ya ya njia za ukusanyaji wa takwimu hizi na wakati mwingine takwimu kutofautiana ,kukamilika kwa mpango mkakati huu kutaliondoa tatizo hili” Amesema.

No comments:

Post a Comment