Saturday, June 7, 2014

KUPENDA FEDHA ZA ‘CHAPCHAP’KUNAVYOUA UWEKEZAJI

Na, Albert Sanga, Iringa.

Miaka takribani mitatu iliyopita niliandika makala hapa safuni iliyokuwa na kichwa, “Njooni shambani mtajirike”. Ilikuwa ni makala iliyoshirikisha fursa kuhusu uwekezaji katika kilimo cha miti. Kwa rekodi nilizonazo inaonesha kuwa ile ni moja ya makala zangu ambayo iliwavutia maelfu ya wasomaji; kutokana na mamia ya mirejesho ya niliyoipokea.

Si nia yangu kukumbusha habari ya fursa ile, lakini kuna mambo mengi sana nilijifunza [kupitia makala ile] kuhusu hulka za watanzania linapokuja suala la uwekezaji. Kwa mujibu wa rekodi zangu inaonesha kuwa kati ya waliowasiliana nami, asilimia 7% walivutiwa na kuikubali fursa hii lakini kikwazo kikubwa kikawa ni ukosefu wa fedha; wengi wao wakaahidi kwamba wanaendelea kujipanga na ipo siku watawekeza. 

Asilimia 4% tu ndio walioipenda na kuchukua hatua ya kuchangamkia fursa hii katika maeneo mbalimbali nchini; wakiwemo wachache waliosafiri kuja Iringa na wengine walionijulisha kuwa wamefanikiwa kupata mashamba maeneo mbalimbali ikiwemo Tanga, Njombe, Tabora, Bukoba na kule Mbeya. 

Asilimia 89% walinieleza kuwa fursa ya uwekezaji katika miti ni nzuri lakini inachukua muda mrefu mno. Nakumbuka niliwaeleza kuwa wastani wa miti tangu kupandwa hadi kuvunwa inaweza kuchukua kuanzia miaka mine hadi kumi na kuendelea kutegemea na aina ya miti, bidhaa unayotaka kuvuna, kiwango unachotaka kuvuna na hali ya udongo na ya hewa ya mahali ulipopanda. 

Mathalani; miti ya mbao inachukua kuanzia miaka saba hadi kumi na tano tangu kupandwa hadi kuvunwa. Miti ya fito(mirunda) inachukua miaka kuanzia minne hadi mitano mpaka kuvunwa. Hii ina maana kwamba hawa asilimia 89% waliipuuza fursa hii kwa sababu inachukua kuanzia miaka minne, saba, hadi kumi na tano.

Sasa tafakari hili: waliosema kuwa kupanda miti ni kitu kisichofaa kwa sababu inachukua miaka mingi(mf minne); kama leo wangalikuwa walipanda miti ya fito miaka mitatu iliyopita, ingekuwa bado mwaka mmoja tu wavune. Cha kujiuliza ni hiki: Je, katika miaka mitatu iliyopita hadi sasa wamefanya jambo gani la maana lenye faida na tija kubwa kushinda  uwekezaji katika kilimo cha miti? 

Jiulize swali la pili: Shamba pamoja na miti la ekari moja ambalo huenda lingekugharimu (laki mbili hadi sita-sawa sawa na nilivyoainisha maeneo ninayoyafahamu nilipoandika makala ile); ambalo mwaka mmoja ujao(mwakani) wangeweza kuuza miti pekee kwa fedha si chini ya milioni mbili huku ukibaki na ardhi kuwa mali yako; Je, kuna kitega uchumi gani chenye thamani zaidi ya faida hiyo ambacho wamewekeza?

Kupitia tafakari hizo kuna mambo utayagundua kuhusu sisi watanzania tuliowengi. Wengi wa watanzania wanapenda sana hela za chapchap! Ukitaka umpate mtanzania mpe fursa inayoonesha kuwa fedha itapatikana kesho, wiki ijayo, mwezi ujao na ikizidi sana mwaka ujao. Ukitaka mtanzania asiwe rafiki yako, mweleze habari za kufanya mambo yatakayoleta faida ama fedha kuanzia miaka mitano, kumi, ishirini ama hamsini mbele. Kwanza hatakuelewa na pili atakupuuza.

Tatizo la pili linalowakabili watanzania wengi ni uwezo mdogo wa kubaini fursa. Uwezo huu mdogo umesbabishwa na mambo mawili; mosi ni uvivu wa kutafuta taarifa na pili ni utamaduni mbaya wa kupenda kulalamika kila wakati. 

Ninaposema kutafuta taarifa ninamaanisha kutafuta, kusoma, kusikiliza, kutazama, kutafakari, kuchakata na kuzielewa kwa umakini kabisa habari na mambo yenye uwezo wa kuleta tija katika eneo fulani la maisha. Mathalani, kujua fursa kuhusu ardhi ni kutafuta taarifa kuhusu mazingira, kilimo, hali ya chakula na mabadiliko ya hali ya tabia nchi. 

Ukijua kuwa tabia nchi imebadilika pia ukifahamu kuwa yapo mashirika ya Magharibi ambayo yananunua hewa ukaa inayotokana na miti; hutafanya mchezo linapokuja suala la kumiliki ardhi na ukishamiliki ardhi hutaiacha utupu; bali utaipanda miti ili uboreshe mazingira na ujiandae kukinga dola kutokana na kuuza hewa ukaa inayozalishwa na miti iliyopo shambani kwako. 

Sio tu kwenye habari ya miti bali mtazamo huo unatakiwa kuwepo katika ubongo wa kila mtu anapoyatazama maeneo yote katika maisha.Watanzania wangapi wapo makini linapokuja suala la kutafuta taarifa za maana za kuwasaidia?

Jibu la swali hili ni rahisi kwani linapatikana unapoyaangalia maisha ya watanzania wengi kiuchumi: Ni maisha ya kubahatisha ambayo hayana uhakika kamili kiuchumi kwa miaka ishirini ama hamsini ijayo. Tafuta watanzania mia moja, kisha waulize swali hili, “Unategemea maisha yako kiuchumi yatakuwaje miaka 10 ijayo?” Ninakuthibitishia kwamba watakaokuwa na uhakika wa maisha yao baada ya muda huo hawatazidi wawili; waliobaki watakujazia porojo na kujitetea kwingi kulikojaa kukata tama! Unajua tatizo linapoanzia?Nitakueleza.

Tatizo linaanzia katika hulka ya watanzania wengi kuhangaikia na kuchekelea habari na taarifa nyepesi nyepesi zinazojadili matukio, zinazojadili maisha ya watu; ambapo kimsingi hazina chochote cha maana zaidi ya kuwafanya watu wazidi kuchanganyikiwa na ugumu wa maisha. Bahati mbaya ni kwamba vyombo vyetu vingi vya habari vinahangaika kujaza bongo za watanzania kwa matukio na taarifa nyepesi nyepesi kiasi kwamba watanzania wengi wanaendelea kuwa wepesi mno wanapopimwa kwenye mizani ya kiuchumi.

Jambo la pili linalopelekea watanzania wengi kuwa “mambumbumbu” wa kubaini fursa ni hulka ya kulalamika. Kulalamika huwa ninakufananisha na utumiaji wa madawa ya kulevya; yanampa mtumiaji faraja kwa muda yawapo katika damu lakini yakiisha mtumiaji anabaini kuwa hakuna kilichobadilika. Bila kujali ni nani aliyekusababishia ugumu wa maisha, kulalamika hakuwezi kukuondolea ugumu wa maisha wala tatizo linalokukabili.

Katika historia haijatokea mahali popote mtu aliyewahi kupewa taji ama tuzo ya umahili wa kulalamika. Ni kweli matatizo yapo, ni kweli kuna wakati serikali inakwama kufanya hili na lile katika maeneo kadhaa; lakini kulalamika unapokabiliwa na matatizo na kuilalamikia ama kuilaani serikali hakuwezi kukupa nafuu ya matatizo yako kwa namna yeyote ile. Kulalamika huwa kuna zalisha upofu wa kutoona mambo yanayoweza kukukwamua likiwemo suala la kubaini na kuzitumia fursa. 

Lazima utembee na mtazamo wa utele, lazima utembee na mtazamo unaoamini kuwa wewe ndie unaewajibika kuboresha maisha yako; sio UKAWA, CCM wala CHADEMA! Kinyume na hapo utaendelea kusema kuwa fedha ni ngumu ilhali wengine wanapata fedha kila siku; tena katika mazingira hayo hayo uliyomo. Kulalamika hakuna mafuta yeyote yanayoweza kulainisha ugumu wa maisha ama kusafisha matatizo!

Suala jingine ambalo limekuwa sababu ya kupooza kwa hali za kiuchumi za mamilioni ya watanzania ni kushindwa kusoma alama za nyakati. Waingereza wanasema “timing”. Kuna jambo ambalo unaweza kuwa na uwezo wa kulifanya leo; ukilipuuza utajikuta huwezi kufanya tena wakati ujao. Nitakupa mifano miwili.
Mosi; kuna mzee wangu mmoja ambae alinionesha kiwanja kilichopo katikati ya mji hapa Iringa ambacho alipuuza kukinunua kwa shilingi laki moja mwaka 1998, lakini mwaka 2013 kikauzwa kwa shilingi milioni mia mbili na themanini! Alichokoseani “timing”. 

Mfano wa pili: Kabla ya mwaka 2010 kuna maeneo katika wilaya za Kilolo na Mufindi ambapo ekari moja ya shamba uliweza kununua kwa shilingi elfu ishirini (20,000/=) tu; lakini mara baada ya kuingia makampuni ya uwekezaji katika kilimo cha miti; maeneo hayo sio tu kwamba yamepanda mara dufu lakini pia hata kuyapata ni kwa mbinde.

 Swali la kujiuliza ni hili: kwa nini watanzania wengi tunakwama “timing” linapokuja suala la uwekezaji? Jibu lipo:  ni kwa sababu hatupendi kutafuta taarifa za maana, ni kwa sababu hatuna maono, ni kwa sababu hatuna mipango na malengo ya muda mrefu, ni kwa sababu tunapenda hela za chapchap na ni kwa sababu tupo bize mno kulalamika kiasi kwamba tunapokuja kushtuka tunabaki tukilia baada ya kila fursa kuchukuliwa na “wengine” walio ‘bize’

Kabla sijahitimisha makala hii leo ninapenda kulisema jambo lifuatalo. Huwezi kuwa mwekezaji ikiwa huna tabia ya kujiwekea akiba pamoja na kutenga sehemu ya kipato chako maalumu kwa ajili ya uwekezaji. Huwezi kuwa na mafanikio imara na  ya muda mrefu kiuchumi ikiwa hutakuwa na maono na mipango ya muda mrefu na ikiwa hutaachana na hulka ya kupenda fedha za chapchap, fedha za madili na za mikato-mikato ambazo nyingi huwa hazina usafi wala haki. 

stepwiseexpert@gmail.com 0719 127 901

No comments:

Post a Comment