Saturday, June 28, 2014

EVANS AVEVA AMALIZA KAMPENI ZA URAIS SIMBA KWA KISHINDO

 Mgombea wa nafasi ya urais Evans Aveva, akiwa na Mlinzi wake 'Board Guard' (nyuma) akijinadi kwa wanachama, wakati wa mkutano wake wa kampeni za mwisho na waandishi wa habari kuelekea uchaguzi mkuu wa Klabu hiyo kesho, kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuiongoza Klabu ya Simba kwa kipindi kijacho cha miaka minne. Hitimisho hilo la kampeni zake limefanyika leo kwenye Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam. 
 Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, akimnadi mgombea Urais Evans Aveva.
 Sehemu ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo.
 Baadhi ya wanachama wa Simba waliohudhuria mkutano huo.
 Baadhi ya wazee wa Simba waliohudhuria mkutano huo....
 Meza kuu....
***********************
*Amwaga sera kabambe, kula sahani moja na mafisadi, makomandoo

Na Majuto Omary
WAKATI Kampeni za uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba zikifungwa rasmi leo kuelekea zoezi kamili la uchaguzi huo linalotarajia kufanyika kesho (Jumapili) kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, mgombea anayepigiwa ‘chapuo’ kubwa na wanachama wa klabu hiyo katika nafasi ya Urais, Evans Aveva amemaliza kampeni zake kwa kishindo na kutoa ahadi ya kula sambamba na Makomandoo na mafisadi wanaoihujumu klabu hiyo.

Mbali ya ahadi hiyo, Aveva pia amesema, iwapo atapewa ridhaa ya kuiongoza Simba, atarudisha heshima ya klabu hiyo kwa kutwaa ubingwa na kushiriki mashindano ya kimataifa kwa kusajili wachezaji bora wazawa wenye uwezo na kuongeza wageni iwapo watahitajika baada ya kukosa mzawa wa kumudu nafasi husika. 
Akizungumza katika mkutano wake wa mwisho uliofanyika kwenye hotel ya Hyatt Regency Kulimanjaro, Aveva alisema kuwa atatumia vyombo vya sheria kupambana na wauzaji bidhaa za klabu hiyo wanaotumia nembo ya Simba ili kukusanya mapato ya klabu kwa ajili ya kutumika katika maendeleo ya klabu.

Aidha, Aveva alisema kuwa katika kuhakikisha anaondoa mianya hiyo, atatumia matawi ili kukamata bidhaa hizo na lengo kubwa la kufanya hivyo ni kuweka utaratibu ambao utaiwezesha klabu hiyo kujikusanyia mapato na kuweza kujitegemea.
“Bidhaa zenye nembo ya klabu zinauzwa kiholela na kufaidisha wachache huku klabu ikiendelea kuwa tegemezi, mimi sitavumilia hali hiyo na nitahakikisha nakula nao sahani moja ili kuokoa klabu,” alisema Aveva.
Alisema kuwa uongozi wake utakuwa wa kushirikisha zaidi Matawi na ataunda kamati mbali mbali ili kuweza kufanikisha mpango mkakati wake wa kuendeleza klabu.
“Sitaweza kufanya kila kitu mimi, nitaunda kamati ambazo zitawajibika katika kamati ya utendaji na kufanya majukumu hayo, lengo kubwa ni kufikia lengo na kuhodhi madaraka, nitafanya hivyo kwa maendeleo ya klabu na wala si vinginevyo,” alisema.

Pia alisema kuwa atasajili wachezaji ambao wataiwezesha timu hiyo kufanya vyema katika ligi na kurejesha hadhi na heshima yake ya kushiriki mashindano ya kimataifa.
Uchaguzi huo utashirikisha jumla ya wagombea 27 ambapo mbali na Aveva, nafasi hiyo pia inagombewa na Andrew Tupa. Wagombea  wengine ni Swedi Mkwabi, Bundala Kabulwa , Geofrey Nyange na  Jamhuri Kihwelo ambao wanagombea nafasi ya makamu Rais.

Wanaowania ujumbe ni Said Tulliy,  Yasini Mwete, Ally Suru,  Rodney Chiduo,  Said Pamba,  Ally Chaurembo , Abdulhamid Mshangama , Chano Almasi,  Damian Manembe,  Ibrahim Masoud, Kajuna Noor,  Hamisi Mkoma,  Alfred Elia na Saidi Kubenea.
Wagombea wengine ni Idd Mkamballah, Juma Mussa, Maulid Abdallah na Collin Frisch. Wagombea kwa upande wa wanawake ni Asha Muhaji, Amina Poyo na Jasmine Badour.

No comments:

Post a Comment