Wednesday, May 21, 2014

Zanzibar kupata madaktari 38 mwaka huu

Zanzibar inatarajia kujenga Historia mpya katika kuzalisha Madaktari  38 kwa mkupuo mmoja ifikapo mwezi Septemba mwaka huu baada ya Vijana wazalendo wa fani ya Udaktari { Medical Doctor - M.D } kukamilisha mafunzo yao ya miaka sita.
Mkuu wa Mafunzo wa Madaktari Mabingwa kutoka Jamuhuri ya Watu wa Cuba wanaoendesha Mafunzo hayo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Irene Nodarse Torres alieleza hayo wakati akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake  mara baada ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kukagua makazi yao.
Balozi Seif alifanya ziara hiyo kuangalia matengenezo makubwa yaliyofanywa ndani ya Nyumba ya Madaktari hao Mabingwa Kutoka Cuba hapo mkabala na Bustani na Victoria iliyopo Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.
Dr. Irene alisema Wanafunzi  Madaktari hao 38 ni miongoni mwa 50 wanaopata Taaluma kutoka mabingwa  wa Taaluma ya Afya kutoka Cuba ambapo wengine 21  wa awamu ya pili wanaendelea na mafunzo kama hayo Kisiwani Pemba.
Alisema ni fahari kwao kuona Wanafunzi hao wanamaliza mafunzo yao kwa mafanikio makubwa katika kiwango kinachokubalika  cha utowaji wa mafunzo ya fani ya Udaktari kimataifa.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Jamuhuri ya Watu wa Cuba kwa juhudi zake ilizozichukuwa katika kusaidia wataalamu wa  kuendesha mafunzo hayo.
Balozi Seif alisema kukamilika kwa mafunzo hayo kutaziwezesha  Hospitali na Vituo vingi vya afya hapa Nchini kupata wataalamu watakaosaidia wananchi kupata huduma za Afya  kitaalamu zaidi.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Saleh Mohamed Jidawi alisema jengo hilo hivi sasa liko katika kiwango cha kuridhisha kufuatia matengenezo makubwa yaliyofanywa katika nyumba hiyo.
Dr. Jiadawi alisema hivi sasa umebaki usumbufu wa upatikanaji wa wakati wa huduma za Maji safi tatizo ambalo Wizara imelazimika kuweka tangi kubwa la kuhifadhia huduma hiyo kwa kutumia mashine maalum ili kuwaondoshea kabisa tatizo hilo.
“ Wizara tulilazimika kuwajengea tangi kubwa la kuhifadhia maji kwa vile baadhi ya wakati hasa kipindi cha mwezi wa Disemba na Januari huduma hii inakuwa adimu kupatikana katika eneo hili kutokana na kukumbwa kwa kiangazi “. Alisema Dr. Jidawi.
Akigusia maradhi ya Dengue yaliyoibuka hapa Zanzibar hivi karibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba juhudi zinaendelea kuchukuliwa na wataalamu wa afya katika kudhibiti maradhi hayo yanayosababishwa na Mbu.
Dr. Jidawi alisema hadi sasa wagonjwa sita wameripotiwa kukumbwa na maradhi hayo ambao wanaendelea kupatiwa huduma na uangalizi chini ya Madaktari katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya aliwaomba wananchi kuendelea kutunza mazingira yao kwa kuondosha vidimbwi vya maji machafu, kutumia vyandarua pamoja na kufika Hospitali wakati wanapopatwa na dalili za maradhi.
Balozi  Seif Ali Iddi mwaka jana alifanya ziara fupi kwenye Makazi ya Madaktari Mabingwa hao wa Cuba kuangalia mazingira halisi ya nyumba hiyo na kuagiza  kufanywa matengenezo makubwa jengo hilo.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Ujumbe wa Watu watatu wa Taasisi ya Kimataifa ya Maonyesho ya Kibiashara kutoka Nchini Uturuki { Meridyen International Fair Organisation Limited }.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Balozi Seif ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Mkurugenzi Mauzo  Kimataifa wa Taasisi hiyo Bwana Nuvit Becan alisema lengo la Taasisi yake ni kufanya maonyesho ya Kibiashara hapa Zanzibar.
Bwana Nuvit alisema juhudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuwasiliana na taasisi husika hapa Zanzibar ili kuona maeonyesho hayo yanafanyika hapa Zanzibar ili kutoa fursa kadhaa kwa wajasiri amali wa Visiwa vya Zanzibar kujitangaza Kimataifa.
Naye Mwakilishi wa Maonyesho ya Atlantic kutoka Nchini Nigeria Bwana Ayodejo Olugbade wanaoshirikiana pamoja na Taasisi hiyo ya Uturuki alisema uwamuzi wa maonyesho hayo ni kuzitangaza kwa pamoja bidhaa zinazozalishwa Bara la Afrika na Uturuki.
Bwana Ayodejo alisema bidhaa za Kilimo, Biashara Viwanda pamoja na vitu vya sanaa vimepewa nafasi zaidi katika kuvitangaza ndani ya maonyesho yanayoandaliwa na kufanya kwa pamoja na Taasisi hizo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitanua shughuli zake za uchumi  kwa kuitumia sekta ya Utalii na Biashara.
Alisema Sekta hizo zinaweza kufanikiwa kwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo endapo zitafikia maamuzi ya kutumia fursa za kujitangaza kupitia maonyesho mbali mbali ya Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia ujumbe huo wa Kimataifa wa Maonyesho ya Biashara kutoka Uturuki kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa msukumo ili kuona maonyesho hayo yanafanikiwa kufanyika hapa Zanzibar.
Taasisi ya Kimataifa ya Maonyesho ya Biashara Kutoka Nchini Uturuki tayari imeshafanya maonyesho ya Kibiashara katika mataifa mbali mbali Barani Afrika ikiwemo Tanzania Bara tokea mwaka 1985.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/5/2014.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif Ali Iddi kulia akibadilishana mawazo na Madaktari Mabingwa kutoka Nchini Cuba hapo kwenye Makazi yao Mnazi Mmoja Mkabala na Bustani ya Victoria ambao wanaendelea kutoa mafunzo ya Udaktari kwa Madaktari wazalendo wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment