Monday, May 19, 2014

WAATHIRIKA WA MAFURIKO MBEYA BADO WANAHITAJI MSAADA - MKUU WA WILAYA

Mkuu wa Wilaya Kyela Margareth Esther Malenga(katika)akiongozana na Mkuu wa Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule na Mwenyekiti wa chama cha Msalaba Mwekundu"Red Cross"Mkoa wa Mbeya Bw.Ulimboka Mwakilili,wakikagua maeneo yaliyoathirika na Mafuriko wakati walipokwenda kukabidhi msaada wenye thamani ya Shilingi Milion 10 kwa wahanga wa mafuriko wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya Kyela Margareth Esther Malenga(kulia)akipokea msaada wa vyandarua kupitia chama cha Msalaba Mwekundu"Redcross"kwa niaba ya wahanga wa mafuriko wa wilaya hiyo toka kwa Mkuu wa Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule(kushoto)pamoja na Mkuu wa Vodacom Tanzania nyanda za juu kusini Bw Macfyden Minja (katikati)Jumla ya shilingi Milioni 10 kwa misaada mbalimbali kwa wahanga wa mafuriko wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya Kyela Margareth Esther Malenga(kulia)akipokea msaada wa vyandarua kupitia chama cha Msalaba Mwekundu"Redcross"kwa niaba ya wahanga wa mafuriko wa wilaya hiyo toka kwa Mkuu wa Vodacom Tanzania nyanda za juu kusini Bw.Macfyden Minja,anaeshuhudia kushoto ni Mkuu wa Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule. Jumla ya shilingi Milioni 10 zimetumika kwa misaada mbalimbali kwa wahanga wa mafuriko wilayani humo.
Mkuu wa Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule,akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa shule ya Msingi Kajunjumele iliyopo wilayani Kyela iliyoathiriwa na mafuriko yaliyotokea hivi karibuni,alipotembelea shule hiyo mara baada ya kukabidhi misaada mbalimbali yenye thamani ya shilingi Milioni 10 kwa Mkuu wa Wilaya hiyo(hayupo pichani)kwa niaba ya wahanga wa mafuriko wilayani humo.
Mkuu wa Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule,akiingia kwenye moja ya darasa lililoathirika na mafuriko hivi karibuni katika shule ya Msingi Kajunjumele iliyopo wilaya ya Kyela,alipotembelea shule hiyo mara baada ya kukabidhi misaada mbalimbali yenye thamani ya shilingi Milioni 10 kwa Mkuu wa Wilaya hiyo(hayupo pichani)kwa niaba ya wahanga wa mafuriko wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Kyela Bi. Margareth Esther Malenga, amesema kuwa Waathirika wa Mafuriko wilayani kyela bado wanahitaji misaada na huduma nyingine za kijamii kutokana na athari kubwa waliyoipata kutokana na mafuriko yaliyotokea wilayani humo siku chache zilizopita.

Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa jamii ya Watanzania kujitolea kuwachangia wahanga hao ambao bado wako katika mazingira magu,u licha ya jitihada zilizofanywa na Serikali na kushirikiana na wadau wengine, kama Msalaba Mwekundu "Red Cross" katika kuwasaidia wahanga hao.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka Vodacom Foundation yenye thamani ya Shilingi Milioni 10, iliyotolewa na kampuni hiyo kwa Shirika la Msalaba Mwekundu na kukabidhiwa kwake kwa niaba ya wahanga hao.

"Tumefarijika kupokea misaada hii, kutoka kwa Vodacom lakini bado, tunahitaji misaada zaidi wahanga hawa walipoteza kila kitu pamoja na mazao yao kuharibika hivyo misaada ya kijamii bado inahitajika, hata wengi mnaweza kuangalia hata mazingira ya shule yetu ya  Kajunjumele ilivyo katika hali mbaya kwa sasa" alisema Bi. Malenga.

Wilaya ya Kyela ni moja ya maeneo yaliyoathirika na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha kwa mwaka huu na kusababisha maafa makubwa kwa kusababisha vifo vya watu saba na kuathiri kaya 3,983 zenye zaidi ya watu 18,976 idadi ambayo imetajwa kuwa ni kubwa.

Kutokana na athari hizo familia nyingi zimeachwa bila ya mahitaji muhimu ya binadamu kama vile chakula na malazi hali ambayo inahitaji msaada wa haraka kutoka kwa serikali na jamii kwa ujumla ili kunusuru maisha ya waathirika na kuwafanya waishi maisha yao kama awali.

Akizungumza punde baada ya kukabidhi msaada huo kutoka kwa Vodacom Foundation, Mwenyekiti wa chama cha Msalaba Mwekundu"Red Cross"Mkoa wa Mbeya Bw.Ulimboka Mwakilili,, amepongeza hatua hiyo kwani ni mara ya pili kwa kampuni hiyo kufanya hivyo ambapo awali walisaidia shirika hilo kwa waathirika wa mafuriko mkoani Morogoro.

"Kwa mara nyingine tena tunashukuru kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania kwa msaada huu kwani walishafanya hivyo kwa waathirika wa mafuriko mkoani Morogoro. Leo tumepokea msaada wa vifaa kama mablanketi, magodoro pamoja na vyandarua vya kujikinga na mbu, msaada huu unagharimu shilingi milioni kumi, " alisema Ulimboka, na kuongeza kuwa, "Msaada huu utatumika kama ulivyokusudiwa na si vinginevyo, kwa kweli ni matumaini mapya kwa familia zilizoathirika wilayani Kyela."

Ulimboka alisisitiza kuwa tofauti na miaka iliyopita mvua za mwaka huu zimenyesha kwa wingi na kuacha maafa makubwa, hivyo wao kama msalaba mwekundu wanaowajibu wa kutoa msaada wa haraka. Shirika peke yake haliwezi lakini linaamini kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali nchini watafikia lengo.

"Napenda kutoa wito kwa makampuni, mashirika na taasisi nyingine kutoa msaada kwa watanzania wenzetu waliokumbwa na maafa haya. Familia hizi ambazo baadhi zimeondokewa na wapendwa wao, makazi, vyakula na mali nyingi, yatupasa tufikirie wenzetu hawa wanaoshindwa kujihusisha na shughuli za uchumi kwa kutokuwa na makazi pamoja na malazi maalum." Alihitimisha Ulimboka.

Aidha, Mkuu wa Vodacom Foundation, Yesaya Mwakifulefule amesema kuwa msaada wanaoukabidhi ni jitihada za wafanyakazi na kampuni kwa ujumla katika kuhakikisha kidogo walichokuwa nacho wanashirikiana na watanzania wenzao walio katika hali ngumu hivi sasa.

"Msaada huu unajumuisha mablanketi 200 ambapo kila familia itapatiwa mawili ili kuwalinda dhidi ya hali mbaya ya hewa iliyochochewa na makazi yao au kutokuwa na makazi kabisa. Pia tunakabidhi magodoro 200, kila familia itapatiwa moja, magodoro haya yatasaidia malazi kwa familia ambazo zina mazingira magumu. Mbali na hapo pia vyandarua 100 vitagawiwa kwa waathirika hawa kuwakinga na mbu na hatimaye kujikinga na maambukizi ya malaria." Alisema Mwakifulefule

Mwakifulefule alihitimisha kuwa kwa niaba ya Vodacom angependa kutoa pole kwa waathika wa mafuriko hayo na kuwataka wasife moja watanzania wenzao wapo bega kwa bega nao kuhakikisha wanasaidiwa kuikabili hali inayowakumba. Pia ametoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano wa Shirika la Msalaba Mwekundu kwa kuwa mstari wa mbele kujitolea kusaidia kila watanzania wanapopatwa na matatizo. Wao kama kampuni wapo tayari muda wote kushirikiana nao na wasisite kuwafuata pindi wanapohitaji msaada.

Mafuriko hayo katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya yalitokea mwezi wa Aprili mwaka huu na kulingana na takwimu zilizofanyika watu saba walipoteza maisha huku watu 1,087 ambao ni sawa na kaya 235 walipelekwa katika kambi 14 zilizokuwepo shuleni na makanisani.


Familia hizo zinahitaji msaada wa haraka wa chakula, malazi pamoja na msaada wa huduma za kiafya ambazo ni muhimu kulingana na mazingira magumu wanayoishi.

No comments:

Post a Comment