Wednesday, April 16, 2014

KIKUNDI CHA KINAMAMA OFISI YA MKUU WA MKOA RUKWA WATOA MSAADA KWA WANAFUNZI WA SHULE YA WASIOONA YA MALANGALI MJINI SUMBAWANGA

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Wasioona Malangali Mwl. Orthor M. Mkangara akitoa maelezo mafupi ya shule hiyo iliyoanzishwa rasmi mwaka 1998 ambapo mpaka hivi sasa ina jumla ya wanafunzi 71 wengi wao wakiwa wasioona na baadhi wakiwa ni walemavu wa ngozi "Albinism". Alisema kwa sasa shule hiyo inahitajio kubwa na vifaa vya kufundishia pamoja na usafiri kwa ajili ya kurahisisha shughuli mbalimbali shuleni hapo. Alisema kuwa zipo changamoto nyingi shuleni hapo ambapo wadau mbalimbali wanakaribishwa katika kusaidia kuzitatua. Aliwashukuru kikundi cha kinamama kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa (pichani kushoto) kwa msaada waliotoa na kuomba wadau wengine kuwa na moyo kama huo katika kusaidia watoto wenye ulemavu hapa nchini. 
Katibu wa Kikundi cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Bi. Joyce Mwanandenje akizungumza kwa niaba ya umoja huo ambapo alisema lengo la ujio wao Shuleni hapo ni kutimiza desturi yao ya kila mwaka ambapo hutembelea makundi ya wahitaji mbalimbali katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani. Katika salam zao shuleni hapo walitoa msaada wa magodoro 20, Sukari, sabubi na zawadi mbalimbali kwa aijili ya wanafunzi. Kikundi hicho cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa kinaundwa na watumishi wanawake kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Hazina Ndogo, Ukaguzi wa Ndani, Chuo Kikuu Huria na Baraza la Nyumba na Ardhi Mkoa.
Baadhi ya wanafunzi shuleni hapo wakiimba wimbo mwanana wa kuwakaribisha kikundi cha kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa walipofika shuleni hapo.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Bi. S. Mwasilu akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Msingi Wasioona ya Malangali Mwl. Orthor M. Mkangara msaada wa magodoro na zawadi mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo.Mwenyekiti wa Kikundi cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Bi. S. Mwasilu na Katibu wake Bi. Joyce Mwanandenje wakigawa zawadi za biskuti kwa wanafunzi wasioona wa Shule ya Msingi Malangali katika hafla fupi ya kutoa msaada shuleni hapo.
Sehemu ya Msaada uliotolewa shuleni hapo.
Baadhi ya wanafunzi walemavu shuleni hapo wakiimba wimbo wa kushukuru kwa hisia kubwa.
Msafara wa kikundi cha kinamama wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa wakiingia kuangalia mabweni shuleni hapo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Wasioona Malangali Mwl. Orthor M. Mkangara akitoa maelezo mafupi kwa kikundi hicho cha kinamama walipoingia kukagua mabweni shuleni hapo, Mwalimu huyo alishukuru kwa msaada walioutoa wa magodoro na kusema utasaidia sana kuondoa tatizo la upungufu wa magodoro uliokuwepo.
Hakika msafa huu wa kikundi cha kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ulikua na mengi ya kujifunza shuleni hapo. Uandishi na namna ya kusoma kwa watu wasioona ni tofauti kabisa na uandishi wa kawaida. Hutumia kifaa maalum kuandikia, kalamu maalum na karatasi maalum, hali kadhalika usomaji wa maandishi hayo huwa ni wa kupapasa.
Wanafunzi wasioona hutumia kifaa maalum kwa ajili kuandikia maandishi yenye nundu ambayo husomeka kwa njia ya kupapasa. Kalamu ya kuandikia huwa na ncha kali kama sindano ya fundi viatu. Karatasi za kuandikia huwa ngumu kuweza kutoa vinundu ambavyo husomeka kwa kupapaswa.
Mwanafunzi S. Ngajiro ambae alikuwa haoni kabisa alipojiunga shuleni hapo na kubahatika kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam na kufanikiwa kuona akitumia mashine maalum ya kuandikia ("Tyre Writter") kwa ajili wanafunzi wasioona shuleni hapo. Mashine hiyo maalum kwa ajili ya watu wasioona ina vitufe sita tu vya kuandikia ambavyo hutumika kutengeneza Alfabeti zote katika uandishi  wa lugha kwa kutumia ujuzi wa hali ya juu.
Moja ya darasa dogo kabisa shuleni hapo ambalo huchukua wanafunzi wasiozidi tisa.
Kikundi cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa wakiangalia bustani ya mbogamboga  ambayo ina hudumiwa na wanafunzi  shuleni hapo.
Picha ya Pamoja kati ya uongozi wa shule ya wasioona Malangali, kikundi cha kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo.
(Na Hamza Temba - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa @Rukwareview.blogspot.com)

No comments:

Post a Comment