Wednesday, February 5, 2014

BARABARA ZAIDI ZA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAGARI KUENDELEA KUJENGWA JIJINI DAR

Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (aliyenyoosha mikono) akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam wakati alipokutana na Kamati ya Bunge ya Miundombinu. Kulia kwa Waziri Magufuli ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Eng. Gerson Lwenge na anayefuata ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga. Kushoto kwa Waziri ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Peter Serukamba na wengine ni Wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na Wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Peter Serukamba (mbele mwenye koti) akiwaongoza Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Segerea Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Eng. Gerson Lwenge akitoa maelezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu ujenzi wa barabara ya Mbezi kupitia Malambamawili kuelekea Kifuru hadi Kinyerezi.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakiwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Eng. Gerson Lwenge na Watendaji wengine kutoka Wizani na Tanroads wakikagua barabara ya Tegeta – Wazo Hill ambayo iko katika ratiba ya kufanyiwa matengenezo kama sehemu ya mradi wa kupunguza msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Halima James Mdee (kulia) Mbunge wa Jimbo la Kawe, akimsikiliza Naibu wa Waziri wa Ujenzi Mhe. Eng. Gerson Lwenge (kushoto) wakati Kamati ya Bunge ya Miundombinu iliposimama eneo la Goba ambapo itapita barabara ya lami kutokea Tangi Bovu kuelekea Mbezi Mwisho katika barabara ya Morogoro.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (aliyenyoosha mikono) akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam wakati alipokutana na Kamati ya Bunge ya Miundombinu. Kulia kwa Waziri Magufuli ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Eng. Gerson Lwenge na anayefuata ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga. Kushoto kwa Waziri Magufuli ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Peter Serukamba na wengine ni Wajumbe wa Kamati hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mhe. Zaina Shamte Madabida (katikati) akichangia jambo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipokutana na Wizara ya Ujenzi kupitia maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Mhe. Mtutura Abdallah Mtutura (kushoto), Mbunge wa Tunduru Kusini (CCM) na Mhe. Ritta Enesper Kabati (kulia), Mbunge wa Viti Maalum (CCM).

Kamati ya Bunge ya Miundombinu imefanya ziara ya kutembelea barabara ambazo zinatarajiwa kuanza kujengwa pembezoni mwa jiji la Dar kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari.

Kamati hiyo ambayo imekutana na Waziri wa Ujenzi pamoja na Watendaji wa Wizara, ilikuwa ikipitia shughuli zinazotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kwa mkoa wa Dar es salaam.

Akiongea na Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge ya Miundombinu, Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Magufuli ameeleza kuwa mbali na utekelezaji wa miradi mbali mbali mikubwa ya maendeleo jijini Dar es Salaam lakini pia upo mradi maalum wa kupunguza msongamano wa magari hapa jijini kwa kuimarisha barabara zilizoko pembezoni mwa jiji ambazo ni viungo muhimu kwa barabara kuu zinazoingia na kutoka mjini.

Mheshimiwa Magufuli amebainisha kuwa katika awamu ya kwanza tayari jumla ya kilometa 22 kati ya kilometa 78.9 za barabara za kuondoa msongamano zimejengwa. Barabara hizo zilizokamilika zimetajwa kuwa ni; kuanzia Kituo cha Mabasi Ubungo kupitia Kigogo hadi barabara ya Kawawa (Km 6.4), kutoka Kigogo Roundabout/Kawawa kupitia bonde la Msimbazi hadi makutano ya Mtaa wa Jangwani na Twiga (Km 2.72) ingawa bado katika barabara hii kuna sehemu zimewekewa pingamizi mahakamani na hivyo kuzuia ujenzi katika maeneo hayo kusimama. Barabara nyingine ni Jet Corner – Vituka – Devis Corner (Km 12) na Ubungo Maziwa - Mabibo External/Mandela (Km 0.64).

Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi ameifahamisha Kamati hiyo ya Bunge kuwa, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 jumla ya kilometa 27.2 zitaanza kujengwa ikiwa ni awamu ya pili ya mpango huo.

Waziri Magufuli alizitaja barabara ambazo katika awamu hii ya pili tayari zimepata Makandarasi na ujenzi wake utaanza mara baada ya mikataba kusainiwa hivi karibuni kuwa ni; Mbezi kupitia Malambamawili kuelekea Kifuru hadi Kinyerezi ambayo ina urefu wa kilometa 14 lakini kwa mwaka huu zitajengwa kilometa 4 zinazoanzia Kifuru hadi Kinyerezi. Barabara nyingine ni Tegeta Kibaoni kupitia Wazo Hill kwenda Goba hadi Mbezi Mwisho yenye urefu wa kilometa 20 ambapo kwa awamu hii zinajengwa kilometa 7. 

Aidha, barabara ya kuanzia Tangi bovu hadi Goba itajengwa kilometa zote 9 na Kimara Baruti hadi Msewe kilometa zote 2.6 pia zimejumuishwa katika awamu hii.

Barabara nyingine ambazo tayari zimepata Makandarasi na zinajengwa katika mwaka huu wa fedha 2013/14 ni Kimara hadi Kilungule External/Mandela ambayo ina urefu wa kilometa 9 lakini katika awamu hii itaanza kujengwa sehemu ya Maji Chumvi hadi External/Mandela ambayo ina urefu wa kilometa 3. Barabara nyingine ni Tabata Dampo hadi Kigogo yenye urefi wa kilometa 1.6.

Barabara zote hizi zinatarajiwa kukamilika katika kipindi cha kati ya mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu.

Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Eng. Gerson Lwenge ambaye aliongozana na Ujumbe wa Kamati hiyo kuzipitia barabara hizo zinazojengwa, alielezea kuwa baadhi ya barabara ambazo ni ndefu imebidi kutoa kazi hizo kwa awamu kulingana na muda uliopo na mgao wa fedha kwa mwaka huu. Hivyo alielezea kuwa yale maeneo ambayo hayakujumuishwa katika awamu hii yameingizwa katika mipango ya bajeti ya mwaka ujao wa 2014/2015.

Mhe. Eng. Lwenge ameeleza kuwa miradi hii itakwenda sambamba na utekelezajiwa mradi wa ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa daraja la Kigamboni, ujenzi wa sehemu ya barabara kati ya Bendera Tatu na Gerezani/KAMATA.

Miradi mingine ambayo iko katika hatua mbali mbali za utekelezaji ni ununuzi wa Boti ya usafiri kati ka Dar es Salaam na Bagamoyo pamoja na ujenzi wa barabara za juu katika maungio yenye mkusanyiko wa magari mengi katika barabara ya Mandela maeneo ya TAZARA na Ubungo.

Wakati akihitimisha ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge ya Miundombinu Mheshimiwa Peter Serukamba ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa namna inavyosimamia utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na matengenezo ya barabara kwa ujumla hapa nchini. Hata hivyo aliitaka wizara hiyo kuangalia uwezekano wa kuijumuisha sehemu ya barabara kati ya Goba hadi Chuo cha Ardhi kuingiza katika mpango huo wa kupunguza msongamano.

Mheshimiwa Serukamba aliongeza kuwa, ingawa barabara hiyo ni ya changarawe imekuwa ikitoa mchango mkubwa kupunguza msongamano hasa katika kipindi hiki ambacho barabara ya Morogoro iko katika ujenzi mkubwa na hivyo magari mengi kuitumia barabara mbadala.

No comments:

Post a Comment