Thursday, January 23, 2014

Tanzania, Afrika ya Kusini zakubaliana kuimarisha mamlaka za uwekezaji

Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru (kulia) akielezea jambo kwa Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Afrika ya Kusini, Bi. Elizabeth Thabethe (katikati) na Balozi wa Afrika ya Kusini nchini Tanzania, Bw. Thanduyise Chiliza (kushoto). Ujumbe wa maafisa mbalimbali uliitembelea EPZA jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru (kulia) na Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha nguo cha Tanzania Tooku Garments Ltd, Bw. Rigobert Massawe (wa pili kulia) wakitoa zawadi kwa Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Afrika ya Kusini, Bi. Elizabeth Thabethe (kushoto) wakati ujumbe huo ulipotembelea kiwanda hicho kilicho ndani ya eneo la EPZA jana. Wa pili kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini, Bi. Radhia Msuya.

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika ya Kusini unazidi kuimarika baada ya nchi hizo kufikia makubaliano ya kuunda vikosi kazi katika nchi hizo ili kuimarisha mamlaka za ukanda maalum za uwekezaji katika nchi hizo.

Hatua hiyo imekuja baada ya ujumbe wa maafisa toka serikali ya Afrika ya Kusini kutembelea Mamlaka ya Ukanda Maalum ya Uwekezaji (EPZA) jana jijini Dar es Salaam.

Ujumbe huo ulioongozwa na Naibu Waziri wan chi hiyo wa Biashara na Viwanda, Bi. Elizabeth Thabethe ulikutana na viongozi waandamini wa EPZA na kupata fursa ya kufahamu kuhusu mamlaka hiyo na jinsi inavyofanya kazi hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt…..Meru alisema Afrika ya Kusini ni nchi yenye uchumi mkubwa barani Afrika na kuwa Tanzania ina mengi ya kujifunza hasa jinsi mamlaka ya uwekezaji katika maeneo maalum ya nchi hiyo inavyofanya kazi.

“Tumekubaliana kuunda vikosi kazi katika nchi zetu ili vifanya kazi ya kuhakikisha kuwa mamlaka zetu zinaimarisha ushirikiano na kuongeza uwekezaji katika maeneo yetu,” alisema Dkt. Meru.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa Afrika ya Kusini imekubali kuisaidia Tanzania kutafuta wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika maeneo ya EPZA hasa katika maeneo ya kuongeza thamani mazao ya kulimo na madini, kuunganisha vipuri kama magari na maeneo mengine.

Kwa upande wake, Bi. Thabethe alisema kuwa uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania ni wa muda mrefu na kwamba ni muhimu ukaimarishwa kwa faida ya watu wa pande zote mbili.

“Ni kupitia biashara na uwekezaji baina ya mataifa ya Afrika ndipo bara hili litaweza kupiga hatua za kweli za maendeleo,” alisema.

Alisema Afrika ya Kusini ina mengi ya kujifunza toka Tanzania na kuwa wako tayari kuimarisha uhusiano huo wa kibiashara na uwekezaji.

Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini, Radhia Msuya alizitaka mamlaka za nchi hizo kufanya kazi kwa karibu ili kufikia maendeleo endelevu.

“Kuna mengi ya kushirikiana na kufanyia kazi kwa faida ya watu wetu,” alisema.

Kwa kushirikiana na Afrika ya Kusini, EPZA itakuwa inaimarisha zaidi mafanikio iliyopata hadi sasa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, pamoja na kujiwekea malengo ya kuvutia mtaji wa Dola za Marekani 300 milioni kwa mwaka jana, mamlaka hiyo iliweza kuvuka lengo na kuingiza nchini mtaji wa jumla ya dola za Marekani 498 milioni nchini, ikiwa ni thamani ya fedha za wawekezaji walioingia nchini kwa mwaka huo.

Pia mamlaka hiyo ilikuwa imejiwekea lengo la kuzalisha ajira 5,200 kwa mwaka jana lakini hadi kufikia mwezi Disemba jumla ya ajira 10,200 zilikuwa zimezalishwa kutokana na uwekezaji mpya uliofanywa kupitia mamlaka hiyo.

Taarifa zinaonyesha kuwa EPZA ilikuwa imejiwekea lengo la kuuza nje bidhaa zenye thamani ya dola milioni 100 2013 lakini lengo lilivukwa na kufikia dola milioni 105 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana.

No comments:

Post a Comment