Mkurugenzi wa Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke ametoa wito huo wakati akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam kutoa taarifa ya fahirisi za uzalishaji wa bidhaa za viwandani hadi kufikia mwaka 2012 zilizowekwa katika makundi mbalimbali kwa kufuata mwongozo wa Umoja wa Mataifa.
Mtafiti na mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Haji Semboje akizungumza wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es salaam. Pamoja na mambo mengine amesema juhudi zinahitajika katika kuwahamasisha Watanzania kumiliki viwanda vidogo, vya kati na vile vikubwa.
Sehemu ya waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa, Dar es salaam.
Wito umetolewa kwa watanzania kujitokeza kwa wingi katika kuanzisha na kumiliki viwanda vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuongeza ajira, kukuza pato la taifa na kupunguza hali iliyopo ya uagizaji wa bidhaa mbalimbali toka nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke ametoa wito huo wakati akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam kutoa taarifa ya fahirisi za uzalishaji wa bidhaa za viwandani hadi kufikia mwaka 2012 zilizowekwa katika makundi mbalimbali kwa kufuata mwongozo wa Umoja wa Mataifa.
Amesema kuwa ongezeko la viwanda nchini licha ya kuongeza ajira kitakwimu lina mchango mkubwa katika kusaidia kupima fahirisi za uzalishaji wa bidhaa za viwandani na kuongeza kuwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani hupima mabadiliko ya kiasi cha bidhaa zilizozalishwa na wazalishaji mbalimbali ambao kwa wastani wamejiajiri kuanzia wafanyakazi 50 na kuendelea.
Amefafanua kuwa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2012 imekua na kiwango cha juu cha mabadiliko ya fahirisi ya bei ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani kwa jumla ya asilimia 10.8 ikilinganishwa na asilimia 2.1 za mwaka 2011.
Ameongeza kuwa fahirisi za uzalishaji wa bidhaa za viwandani kwa mwaka 2012 zimeongezeka na kufikia 328 ikilinganishwa na 296 za mwaka 2011 na kuongeza kuwa ongezeko hilo limechangiwa na uzalishaji wa vinywaji na tumbaku kwa asilimia 16.8%, Viwanda vya chuma 14.6% na ongezeko na bidhaa za nguo na ngozi kwa asilimia -17.7%.
Bw. Oyuke ameyataja makundi mengine yatokanayo na bidhaa za viwandani kuwa ni pamoja na Mbao na bidhaa za mbao 0.3%, Karatasi na bidhaa za karatasi 5.0%, Kemikali, Petroli na bidhaa za Plastiki -7.9%, Bidhaa za udongo, vioo na bidhaa zisizo za metaliki 7.5% na bidhaa zitokanazo na chuma 11.0% .
Naye mtafiti na mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Haji Semboje akizungumza wakati wa mkutano huo amesema kuwa mfumo wa uzalishaji na biashara nchini unatokana na uwepo wa bidhaa za Kilimo na zile zisizo kuwa za kilimo na kuongeza kuwa juhudi kubwa zinahitajika katika kuwahamasisha Watanzania kumiliki viwanda vidogo, vya kati na vile vikubwa.
“Bado tunakabiliwa na changamoto ya umiliki wa viwanda hapa nchini kwa sababu viwanda vingi vikubwa vinamilikiwa na wageni, watanzania walio wengi wanamiliki viwanda vidogo vidogo” amesema Prof. Semboje.
Ameongeza kuwa hivi sasa kuna ongezeko kubwa la bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo kutoka nje ya nchi jambo ambalo linaathiri uchumi wa ndani na kusisitiza kuwa kuwa juhudi zinahitajika katika udhibiti wa bidhaa zisizokidhi viwango na ambazo hazina chapa ya eneo zilikotengenezwa ambazo zinapatikana katika masoko ya Tanzania.
Prof. Semboje ameeleza kuwa kutokana na kuongezeka kwa uwezo wa watanzania kununua, kuagiza na kufanya biashara nje ya nchi ipo haja ya watanzania hao na serikali kwa ujumla kupitia mamlaka husika za uwezeshaji wananchi kiuchumi kuangalia uwezekano wa kuwajenga uwezo wa kununua mitambo inayozalisha bidhaa hizo na kuileta ndani ya nchini kwa lengo la kuongeza pato la taifa na kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“ Ninapenda kutoa wito kwa Taasisi za Uwekezaji nchini kutoa kipaumbele kwa Watanzania katika suala la uwekezaji wa ndani pia kutoa elimu zaidi kwa watanzania katika uzalishaji wa kisasa kwa sababu tayari serikali imeshaweka mipango mizuri ya kuwaendeleza watanzania, changamoto tuliyonayo ni kuitafsiri mipango na sera zilizopo kwa manufaa ya nchi”
MBAO NA BIDHAA ZA MBAO 0.3% NA KARATASI NA BIDHAA ZA KARATASI 5.0% HII NI......MIMI DARASA MBOVU MWALIMU WANGU ALITOROKA SHULE! KUMBE NILIDANGANYWA KUWA KARATASI NI BIDHAA ZITOKANAZO NA MBAO! SASA KWISHA JUA HANIDANGANYI MTU TENA.
ReplyDelete