Thursday, January 30, 2014

MKUTANO WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA AU WAFUNGULIWA LEO ADDIS ABABA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye Mkutano wa  Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) ambao  umefunguliwa  rasmi  leo tarehe 30 Januari, 2014 mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mwenyekiti wa Kamisheni  ya Umoja wa Afrika (AU), Mhe. Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma akisoma hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja huo mjini Addis Ababa, tarehe 30 Januari, 2014. Katika hotuba yake Dkt. Dlamini-Zuma alisisitiza umuhimu wa matumizi ya Lugha ya Kiswahili kwani ni moja ya lugha kubwa Barani Afrika.
Jopo la Marais Wastaafu wakiwa kwenye mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mhe. Olusegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Thabo Mbeki, Rais  Mstaafu wa Afrika Kusini na Mhe. Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana.
Rais Mpya wa Madagascar, Mhe. Henry Rajaonarimampianina akitoa hotuba yake ya shukrani kwa nchi za Afrika kwa michango yao iliyopelekea uchaguzi wa amani na demokrasia nchini Madagascar na pia kwa  Madagascar kurejea AU.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. hailemariam Dessalegn akitoa hotuba kama Mwenyekiti wa AU  anayemaliza muda wake kabla ya kukabidhi nafasi hiyo kwa Rais wa Mauritania, Mhe. Mohamed Ould Abdel Aziz.
Rais wa Mauritania, Mhe. Mohamed Ould Abdel Aziz  akitoa hotuba kama Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Afrika kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Januari 2015.
Picha ya Pamoja ya Viongozi wa AU.
Mhe. Membe akiongozana na Rais wa Zimbabwe, Mhe. Robert Mugabe mara baada ya hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa AU
Mhe. Membe akiteta jambo na Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Jacob Zuma nje ya Ukumbi wa Mikutano wa AU.

Kiswahili chazidi kupaa Umoja wa Afrika

Na Mwandishi wetu, Addis Ababa

Umoja wa Afrika umeitaja Lugha ya Kiswahili kuwa ndiyo lugha kubwa na rasmi Afrika na ndio Lugha inayofundishwa zaidi katika Vyuo Vikuu mbalimbali duniani kutoka Afrika.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma wakati akifungua Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia leo tarehe 30 Januari, 2013.

Dkt. Zuma katika hotuba yake ya kusisimua ambayo ilielezea maendeleo yaliyofikiwa Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, changamoto mbalimbali zinazolikabili Bara hili na matarajio alisema kwamba katika kipindi hiki ni muhimu kuitumia Lugha ya Kiswahili kuiunganisha Afrika.

“Wajukuu zetu waliona ni kichekesho tulivyokuwa tukihangaika na  tafsiri za Lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kireno wakati wa mikutano ya AU, na vile tulivyokuwa tukizozana kwamba chapisho la Kiingereza halifanani na lile la Kifaransa au Kiarabu, sasa tunayo Lugha yetu pamoja na hizo lugha nyingine huo ndio ustaarabu wa sasa” alisema Dkt. Dlamini-Zuma.

Akizungumzia maendeleo yaliyofikiwa Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Mhe. Dkt. Dlamini-Zuma alisema  kuwa Afrika sasa imepiga hatua kubwa katika maendeleo ambapo kwa sasa Afrika ndio msafirishaji mkubwa wa chakula nje na pia imekuwa kituo cha viwanda na kituo cha maarifa na hivyo kuleta manufaa kwa maliasili zilizopo ikiwemo mazao ya kilimo kama kichocheo cha mapinduzi ya viwanda.

“Rafiki zangu, kwa hakika Afrika imepiga hatua kubwa katika maendeleo, kutoka usafirishaji wa malighafi katika kipindi kilichopita na kuwa msafirishaji mkuu wa chakula nje, hii itasaidia maliasili iliyopo Afrika kubaki na kuwa kichocheo cha mapinduzi ya viwanda” alisema Dkt. Dlamini-Zuma. Aidha aliongeza kuwa, Kampuni nyingi za Afrika kuanzia zile za madini, fedha, chakula, vinywaji, utalii, madawa, uvuvi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni miongoni mwa zinazoongoza duniani katika sekta hizo.

Dkt. Dlamini-Zuma alieleza kuwa Afrika sasa ni ya tatu duniani kiuchumi. Hata hivyo alisisitiza bado kuna umuhimu kwa nchi za Afrika kuchangia katika maendeleo. Vile vile, alisema kwamba njia pekee ya kuleta amani ni kuwekeza kwa watu hususan kuwawezesha vijana na wanawake. ‘Afrika inahitaji mapinduzi katika ujuzi kwa kubadilisha mfumo wa elimu ili kuwaandaa vijana ambao ni wabunifu na wenye mawazo ya ujasiriamali ili kuleta maendeleo katika Bara lao’ alisema Dkt. Zuma.

Kuhusu hali ya amani na usalama huko, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Dkt. Dlamini-Zuma alielezea kusikitishwa kwake na hali katika nchi hizo na kusisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta amani ya kudumu katika nchi hizi. 

"Tunavyouanza mwaka 2014 mioyo yetu ipo na watu wa Sudan Kusini na  wale wa Jamhuri ya Afrika Kati hususan wanawake na watoto hivyo ni muhimu tufanye kazi kwa pamoja ili nchi hizi zipate amani ya kudumu na kutimiza lengo letu la kuzima kabisa mitutu ya bunduki katika Bara letu" alisisitiza Dkt. Dlamini-Zuma.

Aidha, alimtangaza Bibi Binta Diop kuwa Mjumbe Maalum wa Amani na Usalama Afrika ambaye atakuwa na jukumu la kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika katika masuala ya kujenga amani na utatuzi wa migogoro.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika pia ulishuhudia ubadilishanaji wa Uenyekiti wa Umoja wa Afrika kutoka kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn kwenda  kwa   Rais wa Mauritania, Mhe. Mohamed Ould Abdel Aziz. Aidha, Mkutano huo ulimkaribisha  Rais mpya wa Madagascar, Mhe. Hery Rajaonarimampianina baada ya miaka minne ya kufutwa uanachama wa AU.

Akitoa hotuba yake kabla ya kukabidhi uenyekiti, Mhe. Dessalegn alizishukuru nchi zote za Afrika kwa ushirikiano na kusisitiza umuhimu wa kuweka vipaumbele vya maendeleo Barani Afrika katika Agenda ya Maendeleo ya Kimataifa baada ya mwaka 2015 na ile ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU uliongozwa na Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye alimwakilisha Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment