Tuesday, December 24, 2013

Waziri Mkuu Apokea Msaada wa Pikipiki 44 Kutoka China

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amepokea pikipiki 44 zikiwa ni msaada kutoka Ubalozi wa China na Kampuni ya Fu-Tang ya kutoka China.

Amekabidhiwa msaada huo leo mchana (Jumanne, Desemba 24, 2013) mbele ya viongozi wa wilaya ya Mlele katika hafla fupi iliyofanyika kijiji cha Kibaoni, wilayani Mlele, mkoani Katavi na kushuhudiwa na wakazi wa kijiji hicho.

Akizungumza na viongozi wa wilaya hiyo pamoja na wakazi wa kijiji hicho kabla ya kukabidhi msaada huo, Balozi wa China hapa nchini, Dk. Lu Youqing alisema anaamini kupatikana kwa pikipiki hizo kutasaidia kuleta maendeleo ya haraka ya wilaya hiyo.

“Tunataraji matumizi ya pikipiki hizi yatasaidia kuleta maendeleo ya haraka na hatimaye kuongeza kipato cha wakazi wa wilaya hii,” alisema Balozi Lu ambaye ofisi yake imekabidhi pikipiki 20.

 Alisema wakazi wa nchi yake wanafikia bilioni 1.3 na yeye anatamani kuona walau kila raia wa China akinunua walau kilo moja ya chakula kutoka hapa nchini ili waweze kuongeza soko kwa mazao yanayozalishwa na wakulima wa Tanzania.

 Naye Meneja Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza pikipiki cha FEKON ambayo ni kampuni tanzu ya Fu-Tang, Bw. Zheng Bing alisema mara taratibu zitakapokamilika, wana lengo la kujenga kiwanda cha kutengeneza pikipiki na kompyuta ili kuongeza ajira kwa Watanzania. Kampuni hiyo ilikabidhi pikipiki 24.

  Akipokea msaada huo, Waziri Mkuu alimshukuru Balozi Lu pamoja na kampuni ya Futang kwa msaada huo na kuahidi kuzigawa ili ziwasaidie watendaji kusimamia kazi na hivyo kuharakisha kuleta maendeleo kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Tuna kata 24, kwenye wilaya yetu kwa hiyo kila kata itapewa pikipiki moja. Hiyo pikipiki siyo ya Katibu Kata binafsi bali ni ya kata, kwa hiyo Katibu Kata atakuwa ndiyo msimamizi...,” alisema.   Waziri Mkuu ambaye yuko kijijini kwake Kibaoni kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka, alisema pikipiki saba zitapelekwa kwenye vituo vitano vya afya vya Mamba, Usevya, Inyonga, Katumba na Kanoge na zahanati za Nsimbo na Kasansa.

“Pia tutapeleka pikipiki nyingine nane katika shule za sekondari za Sitalike, Machimboni, Magamba, Nsimbo na Mtapenda. Nyingine ni Utende, Inyonga na Kasokola,”  aliongeza.

  Mbali na hao, wengine watakaofadika na mgao huo ni watendaji wa Chama cha Mapinduzi wa wilaya ya Mlele ambao watapatiwa pikipiki moja, jumuiya za chama katika wilaya hiyo zitapatiwa pikipiki tatu na moja iliyobakia itagawiwa kwa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi.

Waziri Mkuu aliwashukuru Balozi Lu na Bw. Tang Hulin kwa msaada huo ambao alisema anaamini utasaidia kusukuma maendeleo ya wakazi wa wilaya hiyo.

Kuhusu uzalishaji wa chakula cha kutosha wakazi bilioni 1.3 wa China, Waziri Mku alisema itabidi Tanzania izalishe magunia milioni 13 ya nafaka ili iweze kufikisha lengo alilolisema Balozi Lu.

Waziri Mkuu Pinda alishapokea msaada wa pikipiki 23 kutoka kwa wafadhili wengine na kugawa pikipiki sita kwa Jeshi la Polisi, pikipiki 13 kwa vikundi vya vijana na zilizobakia nne alizigawa kwa shule za sekondari.

No comments:

Post a Comment