Tuesday, December 10, 2013

TAFITI ZA KISAYANSI ZILENGE KUJIBU NA KUTATUA MATATIZO YA WATU MASKINI- BALOZI MANONGI

Mhe. Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa mkutano wa pembezoni uliokuwa umeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Elimu, Sayansi na Utamaduni ( UNESCO) na Baraza la Kimataifa la Sayani ICSU), Balozi Manongi alikuwa kati ya wanajopo wanne walioongoza majadiliano hayo.Wengine kutoka kushoto ni Bi. Vibeke Jense ambaye ni Mkurugenzi wa UNESCO Ofisi ya New York, katikati ni mwedesha majadiliano na kulia kwa Balozi Manongi ni Bw. Gisbert Glaser Mshauri Mwandamizi kutoka Baraza la Kimataifa la Sayansi ( ICSU).
Bw. Hassan Mshinda, ambaye ni Kamishna kutoka Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia akichangia katika majadiliano hayo.
sehemu ya washiriki wa mkutano huo.
Washiriki wengine wakifuatili kwa makini majadilianyo hayo kuhusu nafasi ya sayansi na teknolojia katika utekelezaji wa Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu, majadiliano hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano wa UNESCO na ICSU.
Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akibadilishana mawazo na Bw. Gisbert Gladser ambaye katika majadiliano hayo, alitaka kufahamu Tanzania inatumiaje uzoefu wake na mafanikio yaliyoainishwa katika majadiliano hayo kuzisaidia nchi nyingine za Afrika akilenga katika uhusiano na ushirikiano baina ya nchi za Kusini ( South- South Cooperation ).

Na Mwandishi Maalum

Balozi Tuvako   Manongi,  Muwakilishi wa Kudumu wa  Tanzania katika Umoja wa  Mataifa, amesema,  kwa kuwa  sayansi na teknolojia ni suala  mtambuka   basi tafiti na uvumbuzi unaofanywa na wanasayansi  na wataalamu mbalimbali  hauna budi  kujielekeza katika kujibu  hoja   na kuzitafutia ufumbuzi  changamoto zinazowakabili watu hususani  katika kuondokana  na umaskini na kujiletea maendeleo  endelevu.

Ametoka kauli  hiyo siku ya jumatatu wiki hii, wakati aliposhiriki katika   majadiliano ya  pembezoni  ( side event)  yaliyokuwa yakijadili   kuhusu ‘Sayansi kama tegemeo la baadaye  la  malengo ya maendeleo endelevu: changamoto  na  fursa zake zake’. 

Balozi Maongi alikuwa  kati ya wanajapo wanne  katika majadiliano hayo yaliyoandaliwa  kwa pamoja  baina ya  Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni ( UNESCO) na  Baraza la  Sayansi la Kimataifa  ICSU). Wanajopo wengine  walikuwa  Mkurugenzi wa UNESCO katika  Umoja wa Mataifa,  Bi Vibek Jensen, Bw. Gisbert Glaser ambaye ni   Mshauri  Mwandamizi kutoka ICSU,   na Bi. Paula Caballero,  Mkurugenzi wa masuala ya  Uchumi, Jamii na Mazingira katika  Wizara ya Mambo ya Nje nchini Colombia.

“ Ninapozungumza na wazee wangu kule kijijini kwangu  nilikozaliwa kuhusu athari za uharibifu wa mazingira kwa kukata ovyo miti, swali wanaloniuliza je unatupa  mbadala gani .  Hii ni sehemu ya changamoto ambazo sayansi kupitia kwa wataalamu wetu wanatakiwa kutoa majibu au kutoa njia mbadala za kuwafanya watu wanaotegemea miti kwa shughuli zao wasiendele kufanya hivyo” akasema Balozi Maongi.

Na kuongeza kwamba Tanzania kama iliyo kwa nchi nyingine zinazoendelea inaamini kwamba  sayansi na teknolojia inayonafasi  na mchango  mkubwa sana katika  kusimamia utekelezaji  wa malengo ya maendeleo endelevu   kutokana  na ukweli kwamba suala hilo linagusa kila nyanja ya maendeleo ya binadamu.

Hata hivyo akabainisha kwamba  licha ya mataifa mengi yakiwamo yaliyoendelea kukiri umuhimu wa sayansi na teknolojia katika maendeleo,  suala hilo halikupewa umuhimu wakati wa utekelezaji wa Malengo ya Maendele ya Millenia ( MDGs) yanayofika ukingoni mwaka 2015. 

Na kwa  sababu hiyo akasema kwamba Tanzania  ambayo ni miongoni mwa nchi 30 ambazo zimeteuliwa kushiriki katika majadiliano ya  kiserikali  ya kuandaa malengo mapya ya maendeleo endelevu  baada ya 2015 (SDGs) inatajitahidi  kuchagiza suala la sayansi na teknolojia liingizwe katika malengo hayo mapya  hasa kipengere  cha utekelezaji. 

Mkutano huo wa pembezoni  umefanyika wakati  ambapo  wajumbe kutoka mataifa mbalimbali  duniani wapo hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ( New York) kuhudhuria   awamu ya sita ya majadiliano  ya kiserikali ,  (Intergovenmental  negotiations ) kuhuhusu Maandalizi ya Malengo Mapya ya Mendeleo Endelevu ( SDGs) baada ya 2015.

Katika  majadiliano hayo Balozi  Manongi alielezea uzoefu wa Tanzania  katika  siyo tu utungaji wa serĂ¡  zinazosimamia masuala ya sayansi ya teknolojia bali hata namna serikali kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje  iliyoweza kupanua wigo wa matumizi ya sayansi na teknolojia, uongezaji wa ufadhili katika masomo ya juu katika eneo  hilo pamoja na  uwezeshaji wa wanawake. 

 Akataja  pia changamoto mbalimbali ambazo Tanzania kama ilivyo kwa nchi  nyingine za Afrika  inakabiliana nazo, baadhi ya  changamoto hizo ni  pengo la  teknolojia katika ya mataifa  yaliyoendelea na yanayoendelea,   tatizo la ubadilishanaji wa  maarifa na  wimbi la wataalam wa Afrika kukimbili nje kutafuta maisha bora.

Na kwa sababu  hiyo akasema, pamoja na jitihada mbalimbali ambazo Tanzania imezifanya na inaendelea kuzifanya katika eneo hilo la sayansi ya teknolojia   bado itaendelea kuhitaji  misaada na ushirikiano wa karibu   hasa katika eneo la uwezeshaji na ubadilishanaji wa maarifa.

Katika  awamu hii ya sita ya majadiliano  washiriki wanajikita  pamoja na masuala mengine  kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu  za utekelezaji katika eneo la  sayansi, teknolojia,  ubadilishaji wa   maarifa na uwezeshaji  na uhusiano wake na  malengo mapya ya maendeleo endelevu.

Ujumbe wa Tanzania  katika  majadiliano  unaongozwa na  Balozi Tuvako Manongi  ukiwahusisha Mkurugenzi wa Idara ya  Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestin Mush na  Bw. Hassan Mshinda ambaye ni Kamishna  kutoka  Kamisheni ya Sayansi na Teknlojia ( COSTECH).

No comments:

Post a Comment