Wednesday, December 18, 2013

Makosa makuu 3 wanayokutana nayo kwa wingi watumiaji wa website na maana zake

Kama wewe ni mtumiaji wa website, basi moja ya vitu vinavyokera ni pale unapofungua website halafu haifunguki. Kutofunguka kwa website kunaweza kusababishwa na matatizo mengi. Kuna matatizo ambayo yanaweza kuwa ni upande wako wewe 

mtumiaji kama (intaneti yako kuwa chini sana, au programu ya ulinzi (anti virus) inakuzuia kufungua hiyo website nk, pia inaweza kuwa ni tatizo la website husika. Ili kuweza kusaidia kutambua chanzo cha tatizo na kurahisisha matumizi, kila kosa linalotokea kwenye website limepewa namba husika ambayo italitambulisha, ama kwa watumiaji ama kwa wamiliko na hii tunaiita namba ya utambulishi wa error (error status code) .
Kuna rundo la makosa unayoweza kukunana nayo, ila leo hii tutaangalia yale yanayotokea mara kwa mara;

Kitu unachotafuta hakipo - Not found (404)

Kosa hili ni moja ya makosa yanayoongoza kuonekana kwa watumiaji wa website. 404 hutokea pindi website inaposhindwa kukupatia unachotaka, iwe makala ya website, iwe picha nk.

Tukirudi kwenye uhalisia, chukulia mfano, umesikia au kufahamu kuwa Ngoswe anakaa Sinza kwa Remi, ukaelekezwa hadi nyumba yake, ukafunga safari kwenda kumtembelea Ngoswe, unapofika kwenye nyumba ya kwanza wanakuambia mtaa wa sinza kwa Remi ulioenda si ule wa zamani kwani ulibadilishwa, sasa unaitwa Sinza kwa Wajanja, wakakuelekeza mtaa mpya ulipo, ulipofika pale ile nyumba wanakuambia, baada ya kubadili jina lamtaa, majina ya nyumba yamebadilika, hivyo nyumba hiyo ipo kuleee. Haukukata tamaa ukaendelea, kufika kwenye hiyo nyumba, wanakuambia, samahani Ngoswe kashahama zamani. Ukapigwa na butwaa.

Stori hii ya kumtafuta na kutompata Ngoswe ni sawa na 404 kwenye website. Unapoona kosa hili inamaanisha, ama unachotafuta kimefutwa, kimebadilishwa jina au kumetokea mabadiliko ya anuani. Hii inaweza kutokea hasa kwa wale wanaobadilisha website, mfano zamani website ilikuwa inaitwa hosting.dudumizi.com na sasa tumebadili jina na kutumia www.dudumizi.net , hivyo kwa picha ambazo bado zinaelekeza kwenye anuani ya kwanza ni dhahiri hazitopatikanika na hapo ndipo utapata 404.

Hii pia huweza sana huchangiwa sana na mitambo ya utafutaji (search engines)  kama Google ambayo huifadhi taarifa za website kwa muda mrefu.
Ingawa siku hizi kuna njia nyingi za kukabiliana na mabadiliko ya majina nk, ila ni wamiliki wachache wa website wenye kulifahamu au kulifanya hilo kwani wengi wanasema kama hakijaharibika, basi usikirekebishe.

Ushauri: Kwa wamiliki wa website, hakikisha unatumia linki zisizotegemea website ya mwanzo kwa mfano hivyo basi hata kama kutatokea mabadiliko ya mpangilio kwenye website, haitoathiri upatikanaji, hii pia ni sawa kwa picha nk. Pia hakikisha unatimia kurasa maalumu kuwaongoza watembeleaji pindi kukitokea makosa, mfano ukitembelea http://dudumizi.com/haupo utakutana na kurasa nzuri inayokuongoza, hivyo mtumiaji wa website haachwi hewani.


Kuna matatizo ya kimtambo - System error (500)

Hii ni moja kati ya makosa yanayoiudhi pindi yanapotokea. Tofauti na 404 ambapo inaweza kusababishwa na mtumiaji au website, pia hukuwezesha kutumia website bila matatizo, 500 mara nyingi husababishwa na website yenyewe kushindwa 
kutoa ushirikiano na wakati mwingi (si zote) mtumiaji hatoweza kutumia website. Hii inawezekana kuna matatizo ya kiprograma, matatizo ya mtambo (server) na mengine mengi.

Kuna wakati tatizo hili husababishwa na muingiliano wa machaguo (configurations) na kuifanya website isijue nini cha kufanya, na kama ikiwa imesababishwa na muingiliano wa machaguo , basi kuna uwezekano utaweza kutumia website kama utaachana na ulichokifanya. Ukionana na tatizo hili, kitu cha kufanya ni kuwasiliana na mmiliki wa website ili aweze kubadilisha machaguo na mambo yataenda kama kawaida. Na kama ikiwa ni tatizo la kiufundi zaidi, basi mmiliki wa website atatakiwa kulirekebisha.
Ushauri: Kwa wamiliki wa website, hakikisha unaonesha email yako kwenye kila kurasa ya makosa ya 500 ili kuweza kupata mrejesho toka kwa kwa watumiaji.


Umezuiwa kufungua kurasa hii - Forbidden (403)

Haa,hii ni moja ya makosa ambayo si mara nyingi kwa watu kukutana nayo, na unapokutana nayo inamaanisha website imekuzuia kutembelea sehemu hiyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya muda website huzuia watu kuifungua pindi wakiwa kwenye VPN, mfano niVodacom.co.tz. Hii inawezekana ni kwa sababu za kiusalama nk. Unapoonana na matatizo kama haya, kitu unachoweza kufanya ni kuwasiliana na wamiliki wa website au kuangalia kwenye sheria na kanuni za sehemu unayotembelea.

Ukiacha makosa hayo makuu matatu, kuna makosa mengine ambayo hujitokeza mara chache, kwa mfano sasa kuna watu wanashauri utambulishi wa kosa endapo utatembelea website zilizozuiwa (Censored) ambayo itajulikana kwa namba 451), hii ni moja ya makosa ambayo kwa siku jinsi zinavyozidi kwenda ni dhahiri itakuwa maarufu sana.


Chukulia mfano,kwa sasa ukiwa China hauwezi kufungua Facebook wala Youtube, hii ni moja ya error itakayotumika, pia kwa baadhi ya watoa huduma za intanet (ISP) huzia watu kwenda kwenye website fulani kama Piratebay nk, hii error itakuwa na matumizi sana na kuwapa watumiaji wa mtandao kujua utofauti kati ya haipatikani, umeuziliwa au hautakiwi kwenda.
Hivyo basi, wewe kama mtumiaji wa website, pindi unapokutana na makosa kama haya, usichanganyikiwe, tulia na jua nini cha kufanya.
Sources:   Web: Dudumizi.com  Linked In: Dudumizi

No comments:

Post a Comment