Wednesday, November 27, 2013

WAZIRI MKUU AWATAKA MAAFISA MIPANGO MIJI KUJIREKEBISHA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka maafisa mipango miji nchini kurekebisha utendaji wao wa kazi ili waweze kubadili taswira mbaya iliyojengeka miongoni mwa jamii dhidi yao.

Ametoa kauli hiyo huo leo mchana (Alhamisi, Novemba 27, 2013) wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Wataalam wa Mipangomiji waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji ulioanza leo jijini Dar es Salaam.

“Taswira ya utendaji kazi katika taaluma ya mipangomiji na katika  sekta  ya  ardhi  kwa  ujumla miongoni mwa wananchi na Serikali siyo nzuri sana. Watafiti wanatueleza kuwa kati ya asilimia 60 na 80 ya makazi kwenye miji  yetu hapa nchini yamejengwa kiholela. Na kwa kiwango hicho hicho wakazi wa mijini wako kwenye makazi hayo na wanaishi kiholela,” alisema.

“Wako wanaosema ninyi ndiyo chanzo cha hiyo migogoro, wako wanaosema ninyi kwa rushwa ndiyo wenyewe, mimi sishangai madai haya ila ninawasihi muwe na roho ngumu katika kushinda vishawishi hivi,” alisisitiza.

Aliwataka wajadili masuala yanayohusu migogoro ya ardhi bainaya wafugaji na wakulima, baina ya mipaka ya vijiji, baina ya wilaya, baina ya wanavijiji na hifadhi za Taifa au maeneo ya uchumbaji madini na kujadili njia za kutatua migogoro hiyo ili kuwa na mipamgo endelevu.

Aliwataka waangalie suala la ukuaji wa miji iliyokaribu na Jiji la Dar es Salaam kwa kuangalia dhana ya miji mikubwa kubeba vijiji vinavyoizunguka na hasa kuangalia uwezekano wa kupunguza mlundikano wa watu katika jiji hilo. “Miji ya Kibaha, Mkuranga na Bagamoyo inatumikaje kusaidia kupunguza msongamnano katika jiji la Dar es Salaam,” Waziri Mkuu alihoji

Alisema wataalamu wa mipango miji wanapaswa kuwa na maono makubwa ya baadaye kama kweli wanataka kupunguza majanga katika siku za usoni. “Angalieni utafiti wa gesi unaoendelea pale Mtwara na mjipange, angalieni mpango wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na kuunganisha na reli ya kati, angalieni Lindi na upatikanaji wa Liquified Naturala Gas (LNG), pangeni miji kwa siku za baadaye siyo sasa,” alisisitiza.

Aliwataka wanataaluma hao wasimamie vema taaluma yao kwani katika miaka 37 ijayo, (mwaka 2050) inakadiriwa kwamba nusu ya watu wote watakuwa wakiishi mijini. “Kuweni wakweli, tumieni weledi wenu la sivyo katika miaka 37 ijayo kama wanavyosema watafiti, itakuwa balaa tupu,” alisema.

Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wataalamu hao kutoka mikoa yote hapa nchini, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka alisema maafisa mipango miji wanakabiliwa na changamoto ya kufikiri na kubuni aina ya miji ambayo itakidhi mahitaji ya jamii ya baadaye.

Alisema hata hivyo maafisa hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kushindwa kutoa maamuzi ama ushauri wa kitaalamu kwa kuhofia kuadhibiwa na madiwani.

Mkutano huo wa siku mbili unafanyika katika hoteli ya Blue Pearl, Ubungo na unatarajiwa kufungwa kesho na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

No comments:

Post a Comment