Thursday, November 28, 2013

KUORODHESHA MAKAMPUNI KWENYE SOKO LA KUKUZA UJASIRIAMALI NA MASHARTI YA KUDUMU BAADA YA KUORODHESHWA KWENYE MASOKO YA HISA

1. Utangulizi

Soko la Hisa la Dar es Salaam limeweka masharti nafuu na utaratibu uliorahisi zaidi ili kuwezesha makampuni machanga, madogo na ya kati kuorodhesha hisa katika Soko la Kukuza Ujasiriamali.

Soko la kukuza ujasiriamali ni soko jipya kwa ajili ya kuorodhesha hisa za makampuni ambayo ni mapya, madogo na ya kati. Soko hili limeanzishwa kuwezesha makampuni ambayo hayajafikia vigezo vya kuingia kwenye soko kuu kukusanya mitaji kwa ajili ya kuendeleza biashara zao. Soko hili pia ni kwa ajili ya makampuni mapya yasiyo na historia ya utendaji ambayo hutakiwa ili kuingia kwenye soko kuu.

2. Utaratibu wa Kuuza Hisa kwa Umma kwa Mara ya Kwanza (IPO)

Kampuni inayotaka kuorodhesha hisa inatakiwa kufuata utaratibu ufuatao:

(i) Kuwasilisha hoja kwenye board: Utaratibu wa IPO huanza kwa menejiment kuwasilisha hoja kwa bodi ya wakurugenzi – ikijumuisha mpango wa biashara na makadirio ya fedha – ikipendekeza kampuni kuingia katika soko la umma. Bodi ya wakurugenzi hutakiwa kufikiria pendekezo hili kwa makini.

(ii) Kupitishwa kwa pendekezo la kwenda sokoni: Kama bodi ya wakurugenzi ikiafikiana na wazo la kwenda sokoni, basi pendekezo hili lazima lipelekwe kwenye mkutano wa wanahisa wote wa kampuni kwa ajili ya kupitishwa. Baada ya kupitishwa na mkutano mkuu, vitabu vya mahesabu vya kampuni kwa miaka mitano iliyopita lazima vipitiwe upya na kuboreshwa, kama inalazimu, ili kwenda sawa na viwango vya kimataifa vya ripoti za fedha (IFRS) ili kuthibitishwa.

(iii) Kuteua timu ya washauri: Kampuni binafsi inaweza kuwa tayari ina baadhi ya washauri ambao huhitajika wakati wa IPO: wahasibu, wanasheria wakaguzi wa hesabu, na benki au washauri wa uwekezaji. Hata hivyo, kampuni inaweza kupitia mahusiano yake na washauri hawa upya au kuanzisha mahusiano mapya kwa ajili ya mchakato wa IPO. Kurasimisha uhusiano na washauri kupitia barua maalumu na kukubaliana kuhusu malipo hufuatia baada ya makubaliano. Baada ya kuteua timu ya washauri, ratiba ya IPO na matukio yatakayofuatia inabidi kuandaliwa.

(iv) Lazima ateue Mshauri Mteule ambaye atailea kampuni toka wakati ambapo wazo la kutafuta mtaji linaanzwa kutekelezwa;

(v) Lazima kuwasilisha (kupitia Mshauri Mteule) kwa CMSA na DSE maombi ya kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa kwa idhini ya taasisi zote mbili; na

(vi) Lazima aandae waraka wa matarajio kwa ajili ya kuuza hisa na kuorodheshwa sokoni kama inavyotakiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, sheria na marekebisho ya mwaka 2010. Kupitishwa kwa waraka huu wa matarajio ndio kutatoa ruhusa na fursa ya kuuza hisa kwa umma.

3. Masharti ya kuorodheshwa kwenye Soko la Kukuza Ujasiriamali (EGM)

Yafuatayo ni masharti ambayo makampuni tarajiwa yanatakiwa kuyatimiza kabla ya kujiunga na EGM: 
S/NO
VIGEZO
SOKO LA KUKUZA UJASIRIAMALI (EGM)
1.
Historia ya biashara
Hakuna.Iwapo kampuni haina historia ya kufanya biashara, inatakiwa kuonesha kuwa ina mtaji wa kutosha kuanzisha mradi uliofanyiwa utafiti na gharama zake kujulikana
2.
Historia ya kupata faida
Hakuna
3.
Mtaji wa kampuni uliokwisha kulipiwa
Angalau TZS 200 million * (None as per CMSA Requirements)
4.
Kusajiliwa
Kampuni imesajiliwa Tanzania kama kampuni ya umma, au kama ni kampuni inayojisajili kutoka nje ya Tanzania, sheria ya makampuni iwe inafanana na ya Tanzania.
5.
Mali za kudumu
Kampuni iwe na angalau 50% ya mali za kudumu ndani ya Tanzania
6.
Aina ya kampuni itakayoorodheshwa
Makampuni yanayokua - kutoka sekta zote za uchumi
7.
Njia ya kutoa hisa kwa umma
Toleo kwa umma, toleo kwa wawekezaji wachache, kudhamini, au njia zote tatu
8.
Shughuli za biashara
Maelezo ya kina yanayohusu biashara husika ikiwa ni pamoja na mpango wa biashara wa miaka mitano na uchambuzi yakinifu kwa biashara zenye uzoefu wa chini ya mwaka mmoja.
9.
Umiliki wa umma
Angalau 20% ya hisa kumilikwa na umma.
10.
Idadi ya wanahisa baada ya kuorodheshwa na kutoa hisa kwa umma
Angalau wanahisa 100
11.
Kipindi cha kizuizi
Ikiwa kampuni haina historia ya miaka mitatu, waanzilishi hawaruhusiwi kuuza hisa zao kabla ya miaka mitatu
12.
Matumizi ya mtaji uliotolewa
Kutoa maelezo ya kiasi kitakachopokelewa (baada ya kutoa gharama) ikibainisha kwa kina matumizi ya mtaji huo. Endapo makusanyo hayatatosha kuanzisha mradi uliotarajiwa, kampuni inatakiwa kuonesha ni wapi itapata mtaji wa ziada. Endapo matumizi halisi hayafahamiki kwa kiwango chochote kilichokusanywa, kampuni itatakiwa kutoa maelezo ya ujumla ya matumizi ya mtaji utakaopatikana. Kampuni pia itatakiwa kutoa maelezo ni kiasi gani cha chini kitakachokubaliwa kama mtaji wa kuendeshea kampuni.
13.
Washauri Maalum
Kampuni lazima iwe na mshauri maalum kwa kipindi chote cha kuorodheshwa
14.
Wakarugenzi na viongozi waandamizi
Kuwepo na viongozi wenye uzoefu maalum wa angalau mwaka mmoja kabla ya kuorodheshwa
15.
Taarifa za Fedha
Lazima zitayarishwe kwa kufuata misingi ya kimataifa (IFRS) na kukaguliwa na mkaguzi wa mahesabu ya fedha
16.
Wakaguzi wa hesabu
Wawe wamesajiliwa na bodi ya usajili wa wahasibu (NBAA)
17.
Uongozi usiobadilika
Hakuna haja. Mkazo umewekwa kwenye uzoefu wa viongozi hawa.
18.
Kamati za ukaguzi
Lazima kuwe na kamati za ukaguzi kulingana na ushauri wa CMSA na misingi ya utawala bora
19.
Utoshelezi wa Mtaji wa kufanyia biashara
Wakurugenzi watoe maoni yao kuhusu utoshelezi wa mtaji kwa angalau kipindi cha miezi 12
20.
Barua ya kuridhika toka kwa wasimamizi wa kisheria
Kampuni itabidi kuleta barua hii toka kwa wasimamizi wake wa kisheria
21.
Katiba ya kampuni
Katiba kuwa na kipengele chenye kuonesha kuwa kampuni inaruhusiwa kutoa hisa kwa umma, inalinda maslahi ya wanahisa wadogo, kuhamisha umiliki wa hisa, majukumu ya wakurugenzi ya kukopa, misingi ya utawala bora wa kampuni
22.
Wajumbe wa bodi ya wakurugenzi
Kampuni iwe na angalau 1/3 ya wakurugenzi ambao sio watendaji
23.
Waraka wa matarajio kupitishwa na Mamlaka
Waraka wa matarajio lazima upitishwe na mamlaka
24.
Kutimiza masharti ya utawala bora wa kampuni
Kampuni iahidi kutekeleza masharti ya utawala bora wa makampuni kulingana na matakwa ya Mamlaka (CMSA)
25.
Sera ya gawiwo
Kampuni iwe na sera bayana ya gawiwo
26.
Kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari
Kampuni inatakiwa kutoa muhtasari wa waraka wa matarajio kwenye vyombo vya habari.

4. Taratibu za kuorodhesha kampuni DSE

Taratibu za kufuatwa na kampuni inayotaka kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) zimewekwa wazi kwenye Sheria za DSE. Taratibu hizo ni pamoja na; kupata idhini ya CMSA, kuteua Mshauri Mteule, udhamini wa Dalali wa DSE, maombi kufanya katika fomu maalumu, vigezo vya vielelezo (uthibitisho wa kusajiliwa kampuni toka kwa mwanasheria, uthibitisho wa utii wa sheria toka kwa mdhamini, kopi kumi za waraka wa matarajio, kopi 10 za taarifa ya ukaguzi wa hesabu za fedha, kopi 10 za fomu za maombi, maelezo ya ugawanywaji wa hisa za kampuni, na kadhalika.

5. Masharti ya kudumu ya kuorodheshwa kwenye masoko ya hisa
Masharti ya kudumu ya kuorodheshwa kwenye soko la hisa ni muhimu ili kuendeleza soko lenye kufuata taratibu na mfumo unaowezesha watumiaji wa soko kupata habari za soko kwa pamoja. Masharti hay hujumuisha:
1.      Masharti ya jumla na wajibu kutoa taarifa;
2.      Kutoa taarifa za fedha kwa vipind maalumu; na
3.      Vigezo vinginevyo.

Kila kampuni itatakiwa kufuata masharti haya kama yalivyobainishwa kwenye sheria za DSE and CMSA. Kampuni itatakiwa kwa haraka sana iwezekanavyo na si zaidi ya masaa 24, taarifa zinazohusiana na:
·        Mazingira au matukio yanayoweza kuwa na athari kwa kiwango kikubwa kwenye taarifa za fedha, msimamo wa fedha, au mtiririko wa fedha na/au taarifa zote muhimu zitakazowezesha wamiliki na wawekezaji kufanya maamuzi sahihi ya kuwekeza au kutokuwekeza kwenye kampuni husika.
·        Maendeleo yoyote mapya yenye athari kwenye utendaji wa biashara na mafanikio au matatizo ya utendaji na kifedha ya kampuni na habari yoyote ile ambayo yaweza kuathiri bei ya dhamana za kampuni iliyoorodheshwa
·        Mshauri Mteule wa Kampuni lazima aendelee kuwa na mahusiano na kampuni hiyo kwa muda wote ambao itakuwa imeorodheshwa kwenye EGM;

6. Hitimisho
Moduli hii ilikusudia kuwawezesha wajasiriamali kuzielewa taratibu za kuuza hisa na hatimaye kuorodheshwa kwenye kitengo cha kukuza ujarisiriamali (EGM) cha soko la hisa la Dar es Salaam (DSE). Imeelezea mchakato na vigezo muhimu vya kutimizwa na kampuni inayotaka kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa kwenye EGM ya DSE. Moja ya masharti ya kudumu ya kuorodheshwa ni ulazima wa kuwa na Mteule Maalumu kwa muda wote ambao kampuni itakuwa imeorodheshwa. Makampuni yaliyoorodheshwa yatahitajika pia kutangaza taarifa zote ambazo ni nyeti na zinazoweza kuathiri bei ya hisa zao sokoni. EGM ya DSE sio tu inatoa nafasi kwa makampuni ya kati kupata mitaji kwa njia rahisi na nafuu, inatoa pia urahisi wa kutimiza masharti ya kudumu ya kuorodheshwa sokoni.

Wasalaam

Sanctus Mtsimbe
CEO & Managing Director

ConsNet Group Limited
Eastern Africa Professionals & Business Network (EAPBN)
Tancot House, Sokoine Drive, 2nd Floor
Sokoine Drive /Pamba Rd.
P.O. Box 21605, Dar Es Salaam

No comments:

Post a Comment