I: UTANGULIZI
a)
Masuala ya Jumla
Mheshimiwa
Spika,
1.
Leo tunahitimisha shughuli za Mkutano wa Kumi
na Tatu wa Bunge lako Tukufu. Ni jambo
la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku
ya leo.
Mheshimiwa
Spika,
2.
Mkutano huu ulijumuisha kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza: Kujadili
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2014/2015;
Pili: Kujadili
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2013, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments
(No. 3) Bill 2013];
Tatu: Kujadili
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu wa Mwaka 2013
[The GEPF Retirement Benefit Bill, 2013];
na
Nne: Kujadili
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (The Constitutional Review Act) sura ya 83.
3.
Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa
Wabunge wote kwa kushiriki katika Kamati ya Mipango hapa Bungeni kwa kujadili
kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2014/2015. Napenda kuwahakikishia kuwa, maoni na ushauri
kama yalivyotolewa na Waheshimiwa Wabunge yatazingatiwa na Serikali kila moja
kwa uzito wake wakati wa maandalizi ya Bajeti ya 2014/2015. Vilevile
niwashukuru kwa kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Akiba wa
GEPF wa Mafao ya Wastaafu.
b)
Maswali
Mheshimiwa
Spika,
4.
Pamoja
na kukamilisha kazi hizo muhimu, pia katika Mkutano huu, jumla ya maswali 120 ya msingi na 305 ya nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge yalijibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 6 ya msingi na 6 ya nyongeza
yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
c)
Kauli za
Mawaziri/Maazimio
Mheshimiwa
Spika,
5.
Mkutano huu pamoja na kazi za msingi
zilizopangwa, Waheshimiwa Wabunge walipata
fursa ya kujadili Azimio
la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuhusu msimamo wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(d) Hotuba ya Mheshimiwa Rais,
Mheshimiwa Spika,
6.
Katika Mkutano huu pia, Waheshimiwa Wabunge
walipata fursa ya kumsikiliza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na Wananchi kupitia Bunge lako
Tukufu. Mtakubaliana nami kwamba hotuba
ya Mheshimiwa Rais ilikuwa nzito na yenye kuonesha umakini, umahiri na busara
ambazo ni sifa mojawapo za Rais wetu kati ya nyingi nzuri alizonazo.
Tunachotakiwa ni kutumia maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuyafikisha kwa
Wananchi katika maeneo yetu ili nao waweze kuelewa hali halisi ya yanayotokea
katika Jumuiya yetu. Aidha, Hotuba ya Rais imegusa maeneo mengine ambayo sisi
Wabunge tunatakiwa kushirikiana na Wananchi katika kujipanga vizuri namna ya
kukabiliana na matatizo yaliyojitokeza.
II: UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA
2013/2014
(a) Mwenendo wa Mapato na
Matumizi ya Serikali katika Robo ya
Kwanza ya Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa
Spika,
7.
Hotuba yangu kwa leo imejikita zaidi kuelezea
utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2013/2014 na maeneo machache katika
Sekta ya Kilimo na Nishati. Lakini kabla ya kuelezea mwenendo wa Mapato na
Matumizi ya Serikali katika Robo ya Kwanza ya mwaka 2013/2014, naomba kueleza
kwa muhtasari kuhusu mwenendo wa baadhi ya viashiria muhimu vya uchumi hususan
Ukuaji wa Uchumi na Mfumuko wa Bei. Taarifa za awali zilizotolewa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu zinaonesha kwamba Ukuaji wa Pato la Halisi la Taifa katika
kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2013, ulikuwa Asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Sekta zilizoonesha kuwa na Viwango vikubwa
vya ukuaji ni pamoja na Sekta ya Mawasiliano na Usafirishaji ambayo imekua kwa
Asilimia 18.4, Sekta ya Fedha
Asilimia 14.6 na Sekta ya Ujenzi
Asilimia 8.7.
Mheshimiwa
Spika,
8.
Kwa upande wa Mfumuko wa Bei, takwimu
zinaonesha kuwa kasi ya upandaji bei imepungua kutoka Wastani wa Asilimia 13.5 Mwezi Septemba, 2012 hadi Asilimia
6.1 Mwezi Septemba, 2013. Kushuka
kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa zaidi na upatikanaji wa chakula cha kutosha
ndani ya Nchi. Mwenendo huu mzuri wa viashiria vya uchumi jumla unatupa
matumaini makubwa kwamba jitihada za Serikali za kuimarisha usimamizi wa Uchumi
na kuleta Maendeleo endelevu ya Wananchi wetu zinaanza kuzaa matunda.
Mheshimiwa Spika,
9.
Katika Robo ya Kwanza ya mwaka 2013/2014
kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba 2013, Mapato yote yaliyokusanywa na Hazina
yalifikia Shilingi Trilioni 3.08;
sawa na Asilimia 85.7 ya makadirio
ya Shilingi Trilioni 3.59. Pamoja na
mwenendo huo wa ukusanyaji mapato, changamoto kubwa zinazokabili eneo la Mapato
ya Serikali ni kuchelewa kuanza kwa wakati kwa ukusanyaji wa Mapato katika
baadhi ya vyanzo vya mapato. Changamoto nyingine ni Miundombinu isiyokidhi
mahitaji ya usafirishaji endelevu hasa reli ya kati, bandari, usafiri wa Anga
na barabara. Miundombinu Bora ni muhimu
katika kuchochea ukuaji wa Uchumi na Kukuza Ajira; na hivyo kuiwezesha Serikali
kukusanya mapato zaidi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi.
Serikali inafanyia kazi changamoto hizo ili kuzipatia ufumbuzi mapema.
Mheshimiwa Spika,
10.
Kwa upande wa matumizi, hadi kufikia mwezi Septemba 2013; matumizi yalifikia
Shilingi Bilioni 3,806.5, sawa na
Asilimia 98.5 ya lengo la kutumia
Shilingi Bilioni 3,854.2. Kati ya
matumizi hayo, Shilingi Bilioni 3,058
ni Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni 747.9
ni Matumizi ya Maendeleo. Katika kipindi
hiki, sehemu kubwa ya matumizi ya Serikali ya Kawaida na Maendeleo imeelekezwa
katika maeneo yenye kuleta ufanisi na tija kubwa kama vile kuboresha
miundombinu ya barabara, ambayo mgao
wake ulikuwa Shilingi Bilioni 182.5
za Matumizi ya Kawaida na Maendeleo, Sekta ya Elimu Shilingi Bilioni 229.2;
Sekta ya Nishati, Shilingi Bilioni 159.9; Sekta ya Kilimo Shilingi Bilioni 119.6
na Sekta ya Maji Shilingi Bilioni 51.3. Vilevile, Serikali imelipa Mishahara ya Watumishi wa Umma kwa wakati. Changamoto
kubwa iliyopo kwenye matumizi ya Serikali ni kuwepo kwa mahitaji makubwa ya
matumizi yasiyowiana na mapato; jambo ambalo linailazimu Serikali kukopa kutoka
Mabenki ya Ndani. Serikali itaendelea kuoanisha Matumizi na ukusanyaji wa
Mapato, hasa yale ya ndani pamoja na kuzingatia viwango vya Matumizi
vilivyoidhinishwa na Bunge. Aidha, Serikali itaendelea kuweka msisitizo wa
kuelekeza Matumizi kwenye vipaumbele vilivyoainishwa katika Bajeti ya Serikali
ambavyo ni vyanzo muhimu vya kuongeza Mapato, Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini.
III: UTEKELEZAJI
WA MFUMO MPYA WA TEKELEZA KWA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG RESULTS NOW - BRN)
(a)
Muundo wa
Mfumo
Mheshimiwa
Spika,
11.
Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Serikali ilianzisha Mfumo
mpya wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa
Sasa au Big Results Now (BRN) ili kuongeza ufanisi katika usimamizi,
ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mipango yetu ya Maendeleo, hususan, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2011/2012 - 2015/2016). Hatua hii
ilichukuliwa baada ya kuona namna Mfumo kama huo ulivyoziwezesha Nchi kadhaa,
na hasa Nchi ya Malaysia, kupiga hatua kubwa za
kimaendeleo kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi. Kwa ukumbusho tu, Mfumo huo
unatekelezwa katika Maeneo Sita ya Matokeo muhimu Kitaifa (National Key Results Areas) katika awamu yake ya kwanza, ambayo ni Nishati ya Umeme; Uchukuzi; Kilimo; Elimu;
Maji na Ukusanyaji wa Mapato;
Mheshimiwa Spika,
12.
Katika Hotuba yangu ya
kuahirisha Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge, tarehe 6 Septemba 2013, nilitoa
taarifa ya awali kuhusu utekelezaji wa Mfumo huu Mpya kwa kipindi cha kuanzia
mwezi Julai hadi Septemba, 2013. Katika taarifa hiyo, nilieleza kuwa tumepiga hatua za kuridhisha katika
uundaji wa Mfumo wa kuleta matokeo ya
haraka, ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuteua Uongozi wa juu wa Taasisi Maalum
yaani "President’s Delivery Bureau
(PDB)” inayomsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia ipasavyo utekelezaji wa
Miradi na Programu zilizoainishwa. Hivi
sasa zoezi la kuajiri Watumishi wa Taasisi ya "President’s Delivery Bureau” na Vitengo vya Wizara vya
Ufuatiliaji yaani Ministerial Delivery
Units (MDUs) watakaochukua nafasi za Watumishi walioazimwa kutoka kwenye
Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali, Sekta Binafsi, na Asasi Zisizo za
Kiserikali ambao walikuwepo katika hatua zake za maandalizi limeanza. Ninapenda
kutumia fursa hii kuwashukuru wote waliotumika katika chombo hiki tangu
kilipoundwa kwa uzalendo na weledi waliouonesha katika kipindi hiki cha mwanzo
na cha mpito;
Mheshimiwa
Spika,
13.
Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba hadi sasa
vitengo vya ufuatiliaji katika Wizara zote sita (6) zinazosimamia utekelezaji
chini ya Mfumo huu mpya vimeanzishwa na vinaandaa Taarifa za utekelezaji za
kila wiki na kila mwezi, na kuziwasilisha kwenye Chombo cha President’s Delivery Bureau. Aidha,
Kamati Maalum za kusimamia utekelezaji zinazoongozwa na Mawaziri husika
zinakutana kila mwezi kujadili mwenendo wa utekelezaji na kushughulikia
changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji. Baraza la Kusimamia
Mageuzi na Utekelezaji (Transformation
and Delivery Council – (TDC)) limeundwa na lilikutana tarehe 11 Oktoba,
2013. Katika Kikao hicho, Baraza lilipokea na kujadili muhtasari wa Taarifa ya
utekelezaji wa Mfumo mpya wa Kusimamia, Kufuatilia na Kutathmini Miradi ya
Kipaumbele katika Maeneo Sita ya Matokeo ya Kitaifa. Baraza liliridhika na hatua za awali za utekelezaji na lilitoa mwongozo
stahiki wa hatua za kuchukuliwa pale ilipohitajika. Baraza litaendelea kukutana mara kwa
mara ili kutathmini na kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa Mikakati iliyowekwa ya
Mfumo huu mpya;
(b)
Utekelezaji wa Mikakati katika Maeneo Makuu
Sita ya Matokeo Kitaifa;
Mheshimiwa Spika,
14.
Utekelezaji wa mikakati katika maeneo makuu sita ya
matokeo kitaifa ulianza mara baada ya uchambuzi wa maabara kukamilika.
Mafanikio ya kuridhisha yamepatikana katika kila moja ya maeneo yale sita, hasa
ikizingatiwa kwamba Mfumo huu ni mageuzi makubwa sana katika utendaji
Serikalini. Katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu wa fedha,
kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2013; baadhi ya matokeo yaliyopatikana ni
pamoja na yafuatayo:
(a)
Katika Sekta ya
Kilimo, Serikali inatekeleza miradi 26
ya umwagiliaji kwa Wakulima wadogo na pia imekarabati maghala 26 ya mpunga kati ya 39 yanayotumiwa na wakulima katika
maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa katika eneo la SAGCOT.
(b)
Katika Sekta ya
Nishati ya Umeme, jumla ya Wateja wapya 27,494
wameunganishwa na kupatiwa umeme, ikiwa ni Asilimia 18.3 ya lengo la kuunganisha wateja wapya 150,000 hadi mwisho wa mwaka 2013/2014. Aidha, vipande vya Bomba la
Gesi 20,491 vinavyotosheleza ujenzi wa
Kilomita 243.8 za Bomba la Gesi tayari
vimewasili Nchini, na uchomeleaji wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi
Dar es Salaam umekamilika kwa Kilomita 124.3.
Vilevile,
Kilomita 447 za njia ya Bomba la
Gesi zimesafishwa;
(c)
Katika Sekta ya
Elimu, Shule za msingi 5,916
zilipatiwa mitihani ya marejeo na mazoezi, sawa na Asilimia 100 ya lengo la
mwaka. Aidha, Mafunzo Kazini kuhusu ufundishaji yametolewa kwa Walimu katika
Shule 1,325 sawa na Asilimia 65 ya lengo la Shule 2,048 kwa mwaka huu wa fedha;
(d)
Kwa upande wa huduma za maji, wananchi wapatao 752,000 waishio Vijijini wamepatiwa huduma ya maji. Mafanikio haya yanafanya idadi ya Wananchi waishio Vijijini ambao wanapata
majisafi na salama kufikia takribani Milioni
15.9. Kasi hii ya upanuzi wa huduma za Maji Vijijini imewezekana baada ya Wizara
ya Maji kugatua madaraka ya usimamizi wa miradi
husika kwa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, jambo ambalo
limewafanya Watendaji kuwajibika na kuharakisha utendaji wao wa kazi. Aidha, hatua
zilizochukuliwa zimeiwezesha Wizara ya Maji kuongeza ufanisi katika masuala ya
ununuzi wa huduma, ikiwemo ujenzi na vifaa vyake, kutoka wastani wa siku 265 za hapo awali hadi siku 90 za sasa.
Mheshimiwa
Spika,
15.
Mafanikio haya na mengine mengi ambayo sikuyataja hapa
yameonyesha kuwa tukidhamiria, tunaweza kubadilisha kabisa matokeo ya juhudi
zetu na kuifikia dhamira yetu ya kuwa ni Taifa la Kipato cha Kati ifikapo mwaka
2025;
Mheshimiwa Spika,
16.
Kufuatia mafunzo yaliyotolewa mapema mwezi Juni, 2013 kwa
Watendaji wa Wizara husika, Wakuu wa Mikoa wote, Makatibu Tawala wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya zote Nchini, mnamo Mwezi Septemba 2013 nilikutana na Wakuu wa
Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara ili kujadili kwa kina
Taarifa za utekelezaji wa Miradi ya kipaumbele chini ya Mfumo huu. Aidha, katika
Vikao hivyo, nimezielekeza Wizara, Mikoa na Halmashauri zote Nchini kufanya
yafuatayo:-
(a)
Kuchambua miradi
iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha ambayo ipo nje ya Mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” kwa
kutambua manufaa yanayotarajiwa baada ya kukamilika na mahitaji halisi;
(b)
Kuipanga miradi hiyo kwa kipaumbele ili kuweka mkazo katika miradi itakayokamilika haraka
na kuwa na manufaa makubwa kwa Wananchi; na,
(c)
Kuweka utaratibu wa
Kimfumo na Kitaasisi wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kipaumbele.
Mheshimiwa Spika,
17.
Ninafurahi kutoa taarifa kuwa Wizara na Tawala za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeupokea mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo
Makubwa Sasa kwa hamasa kubwa. Ili kuhakikisha azma yao ya kutekeleza majukumu
yao katika Mfumo huu kikamilifu, iliamuliwa kuwa Viundwe Vitengo vya kusimamia
utekelezaji katika Ngazi ya Mkoa (Regional
Delivery Units (RDUs), sambamba na vile Vitengo vya ufuatiliaji vya Wizara
ili utekelezaji katika Maeneo Makuu ya Matokeo Kitaifa ufanyike kwa ufanisi na
umakini stahiki. Hatua hii inazingatia umuhimu wa kuhakikisha kuwa maeneo kama
Elimu na Maji ambayo Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zina mchango mkubwa
katika utekelezaji yanapata msukumo wa kutosha. Kazi hii imeshaanza, na taarifa
zilizowasilishwa ni za kutia moyo sana.
Mheshishimiwa Spika,
18.
Kwa kuzingatia mafanikio ya awali
yaliyopatikana, Serikali imetoa maelekezo kwa Wizara, Idara na Taasisi ambazo
bado hazijaingia katika Mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa zisisubiri
hadi zitakapoingia rasmi bali zianze kujipanga na kutekeleza mipango, miradi na
program zao kwa kutumia mbinu ambazo zinatumika katika Mfumo huo pamoja na
Rasilimali fedha na Wataalam waliopo.
Msisitizo ni kwamba Wizara zote na Mikoa ijipange upya na kuongeza
ubunifu na kufanya vizuri zaidi katika kuimarisha usimamizi wa miradi ya
maendeleo ili kuhakikisha kwamba Taifa letu linafikia malengo ya maendeleo
tuliyojiwekea katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Aidha, napenda kutumia
fursa hii kutoa wito kwa Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuimarisha usimamizi wa Watendaji wao kwa kuzingatia taratibu za uwajibikaji
zilizowekwa chini ya mfumo huu mpya ili kuleta ufanisi na tija ya utendaji
Serikalini pamoja na kupata matokeo makubwa tarajiwa ya Kukuza Uchumi na
kuondoa umaskini;
IV: MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO YA TAIFA
WA MWAKA 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
19.
Mwanzoni mwa Mkutano huu
wa Bunge Serikali iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2014/2015. Napenda
kutumia fursa hii tena kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na michango
yao mizuri ambayo itatuwezesha kuboresha Mpango na Bajeti ya Mwaka ujao wa
Fedha 2014/2015. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Stephen Wasira (Mb.) pamoja na
Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta waliotoa maelezo fasaha ya ufafanuzi wa Hoja
zilizojitokeza wakati wa Mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo. Kwa
kuzingatia michango mizuri na yenye tija iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na
Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya
Taifa wa mwaka 2014/2015, nami naomba uniruhusu kusisitiza mambo machache kama
ifuatavyo:
Mheshimiwa
Spika,
20.
Kama Waheshimiwa Wabunge watakavyokumbuka katika majadiliano yaliyokuwa yanaendelea, moja ya jambo ambalo Waheshimiwa
Wabunge wamelizungumzia kwa kina, ni juu ya wingi wa vipaumbele vya Taifa.
Aidha, imeonekana pia kuwa miradi ya
maendeleo ni mingi sana kiasi kinachosababisha
miradi hiyo kutotekelezeka kutokana na ufinyu wa rasilimali fedha.
Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Vipaumbele vilivyopendekezwa na
Serikali vinategemeana na vinalenga kutanzua vikwazo vikuu vya kiuchumi Nchini
ili kufungua fursa za ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuharakisha maendeleo na
ustawi wa Wananchi wa Tanzania. Pendekezo la Serikali ni kuwa njia bora si
kupunguza vipaumbele hivi sasa, bali ni kupanga vizuri mtiririko wa utekelezaji
wa miradi ndani ya kila kipengele ili kuongeza jitihada za kuongeza Mapato, na
kusimamia nidhamu ya matumizi.
Mheshimiwa Spika,
21.
Kwa kuwa Mpango huu wa
Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016) ni wa kwanza unaojenga msingi
wa mipango mingine ya maendeleo ya miaka
mitano itakayoandaliwa, ni dhahiri kuwa kasi ya utekelezaji wake itarahisisha
utengenezaji wa mipango mingine na kupunguza vipaumbele vya msingi katika
mipango ijayo. Hivyo, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge washirikiane kwa karibu na
Serikali kuhakikisha kuwa miradi iliyopangwa katika ngazi zote inatekelezwa kwa ufanisi ili Mpango huu wa
mwanzo utekelezeke kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika,
22.
Mjadala na Hoja nyingine
zilijielekeza katika changamoto za upatikanaji wa Ajira kwa Vijana Nchini. Kulingana na Sensa ya Watu
na Makazi ya mwaka 2012, Asilimia 34.7
ya nguvu kazi ya Tanzania ni Vijana wa umri wa kati ya miaka 15 - 35. Kundi hili la Vijana ndilo
lenye kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira cha Asilimia 13.4 hapa Nchini. Pamoja na kuwa Vijana hawa wamekuwa wakipata kazi
hususan katika Sekta za Ujenzi, Kilimo na Hoteli, ajira zao nyingi zimekuwa za
muda.
23.
Katika kukabiliana na
changamoto hii, Serikali imeandaa Programu ya Ajira kwa Vijana itakayotekelezwa
kwa kipindi cha miaka mitatu. Malengo ni kupatikana fursa za ajira 840,000 kwa kuwezesha jumla ya Miradi 10,000 ya Wahitimu wa Elimu ya Juu
wapatao 30,000 kutoka Vyuo
mbalimbali ambao watatoa ajira za moja
kwa moja kwa wahitimu wengine 270,000
na ajira zisizo za moja kwa moja 540,000.
Programu hii itajengea Vijana uwezo katika stadi za kazi; ujasiriamali; na
kuwapatia Vijana mitaji, nyenzo na vifaa vya kufanyia kazi; na kuwapatia Vijana
maeneo ya uzalishaji na biashara. Serikali inatarajia kuelekeza fedha zaidi
katika kipindi husika ili kuwezesha utekelezaji wa Programu hiyo. Aidha,
naipongeza Sekta Binafsi kwa mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi na
kuongeza ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Spika,
24.
Kilimo ni moja ya maeneo
ya kipaumbele katika Mpango wa mwaka 2014/2015. Hili ndilo eneo kubwa kwa maana
ya kuongeza fursa za ajira na kipato kwa Wananchi wanaoishi Vijijini, kuongeza
kasi ya ukuaji wa uchumi kwa namna ambayo ni shirikishi ili kupunguza
umaskini. Hivyo, ili kujibu matatizo ya
msingi ya umasikini wa kipato Mpango wa Maendeleo 2014/2015 utatoa kipaumbele katika mambo
muhimu yafuatayo:
(i)
Utafiti wa kilimo cha
mazao, hususan katika uzalishaji wa mbegu bora, mifugo na uvuvi;
(ii)
Kuimarisha huduma za
ugani kwa kilimo, mifugo na uvuvi na
kuimarisha upatikanaji na matumizi ya mbolea kwa ajili ya kilimo;
(iii) Kuimarisha Ushirika wa Wakulima na Wafugaji;
(iv) Kuongeza fursa za mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ikiwa ni pamoja
na kukamilisha uanzishwaji wa Benki ya Kilimo mwezi Januari 2014;
(v)
Kuwezesha upatikanaji wa
masoko ya mazao ya kilimo, na mifugo;
(vi)
Kujenga na kukarabati
skimu za umwagiliaji;
(vii)
Upatikanaji wa ardhi kwa
kilimo na mifugo kwa kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi; na
(viii) Kuendeleza shughuli za kuongeza thamani ya mazao
ya kilimo, mifugo na uvuvi;
Mheshimiwa Spika,
25.
Mpango wa Maendeleo
huandaliwa katika ngazi zote Tano za Utawala kulingana na majukumu ya Serikali
ambazo ni:
Moja: Vijiji na Mitaa;
Pili: Kata;
Tatu: Mamlaka za
Serikali za Mitaa (Halmashauri);
Nne: Mikoa; na
Tano:
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali.
Mamlaka husika katika ngazi zote zinatakiwa kuandaa Mipango yao kwa
kuzingatia maeneo ya vipaumbele kama yalivyoainishwa katika Mapendekezo ya
Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015. Mipango lazima ilenge katika maeneo
yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka hususan katika kuchochea maendeleo ya
maeneo mengine na Programu nyingine katika ukuaji wa uchumi na kupunguza
umaskini.
Katika kila ngazi, Wadau wengine kama vile Sekta Binafsi, Asasi Zisizo za
Kiserikali, Mashirika ya Dini na Washirika wa Maendeleo washirikishwe
kikamilifu. Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali
ziandae Mpango na kuuwasilisha Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Wiki ya Nne ya
mwezi Januari, Mwaka 2014.
Katika ngazi za Mikoa na Wilaya, uandaaji uanze katika ngazi ya Kijiji na
Mtaa, Kata, Halmashauri na hatimaye kwenye Mkoa. Mpango uliopitishwa na Mkoa
uwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na
Wizara ya Fedha, Wiki ya Nne ya Mwezi Januari, 2014. Mpango wa Maendeleo wa Taifa utajadiliwa na
Bunge kuanzia Mwezi Aprili hadi Juni, 2014 na utekelezaji wake utaanza Mwezi
Julai 2014 hadi Juni 2015;
Mheshimiwa Spika,
26.
Mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo wa Mwaka 2014/2015 ndiyo yatatumika katika utayarishaji wa Mipango ya
Maendeleo ya Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa
Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka ujao wa fedha
2014/2015. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge kutumia taarifa zilizotolewa
hapa Bungeni kutoa ufafanuzi kwenye Vikao vya Baraza la Madiwani katika
Halmashauri zao wakati wa kujadili Mipango yao. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuzihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuainisha vipaumbele vinavyolenga
katika maeneo yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka ya Kiuchumi na Kijamii;
na pia yenye kuchochea maendeleo ya maeneo mengine. Vilevile, vipaumbele vya
Halmashauri vilenge kufungulia fursa za ajira, kuongeza mapato ya ndani na
kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi katika maeneo yao.
V: SEKTA YA KILIMO
a)
Hali ya
chakula Nchini
Mheshimiwa
Spika,
27.
Kwa ujumla hali ya upatikanaji wa Chakula
Nchini hadi kufikia Mwezi Oktoba 2013 ni ya kuridhisha kufuatia mavuno mazuri
ya msimu wa kilimo wa 2012/2013 ambapo mazao yake yanaendelea kuingia sokoni
kutoka maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya awali iliyofanyika mwezi
Julai/Agosti, 2013 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika Msimu
wa kilimo wa 2012/2013 utafikia Tani
14,383,845 za chakula zikiwemo Tani
7,613,221 za mazao ya nafaka na Tani
6,770,624 za mazao yasiyo ya nafaka. Kiasi hicho cha chakula
kilichozalishwa ni ongezeko la Tani
2,234,726 za chakula, ikilinganishwa na mahitaji ya chakula kwa mwaka
2013/2014 ya Tani 12,149,120. Kiwango hicho kinajumuisha Tani
354,015 za mahindi na Tani 466,821
za mchele. Hivyo napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa
ujumla kuwa tutakuwa na chakula cha kutosha Nchini kwa Asilimia 118.
Mheshimiwa
Spika,
28.
Vilevile, tathmini hiyo inaonesha kuwa, pamoja
na kuwepo kwa chakula cha kutosha na cha ziada, Halmashauri 61 katika Mikoa ya Manyara, Shinyanga, Simiyu, Arusha, Dodoma, Lindi, Tanga, Singida,
Mara, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Mtwara, Kigoma na Tabora zinatarajiwa kuwa na uhaba wa
chakula.
29.
Natoa wito kwa Halmashauri zinazohusika katika
Mikoa hiyo kufuatilia kwa karibu utaratibu wa kupata chakula kinachotolewa
kutoka maeneo yenye ziada na kuhakikisha kuwa kinafika mapema kwenye maeneo yao
kabla Wananchi wa maeneo hayo hawajaanza kulalamika.
(b)
Mwenendo
wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa
Spika,
30.
Kutokana na hali ya upatikanaji wa chakula
kuwa nzuri, Bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika Soko Nchini
zimeendelea kushuka. Kwa mfano, bei ya mahindi ilishuka kutoka Shilingi 774.30 kwa kilo mwezi
Februari, 2013 hadi Shilingi 535.40
kwa Kilo mwezi Septemba 2013. Kwa upande wa mchele, bei kwa kilo moja imeshuka
kutoka Shilingi 1,825.45 mwezi Februari, 2013 hadi kufikia Shilingi 1,206.70 mwezi
Septemba 2013, na bei ya mchele imeshuka zaidi hadi kufikia Shilingi 1,146.70 katika mwezi Oktoba, 2013.
(c)
Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa
Mheshimiwa
Spika,
31.
Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi
ya Chakula imepanga kununua Tani 250,000
za nafaka katika msimu wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 23 Oktoba, 2013,
Wakala alikuwa amekwishanunua kiasi cha Tani
218,412 za nafaka sawa na Asilimia
87.37 ya lengo lililowekwa ambapo Tani
217,919 kati ya hizo ni za Mahindi na Tani
493 ni za mtama. Aidha, hadi kufikia tarehe 23 Oktoba 2013, maghala ya
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na jumla ya Tani 232, 921 za nafaka, kati ya hizo Tani 232,419 ni za mahindi na Tani
493,103 ni za mtama. Kiasi hiki cha nafaka
kinajumuisha albaki ya Tani 25,452
za mahindi kutoka msimu uliopita wa 2012/2013.
Mheshimiwa
Spika,
32.
Serikali inaendelea na tathmini ya kina ya
hali ya chakula na lishe katika Halmashauri 61 zilizoainishwa kuwa na hali tete ya chakula kwa lengo la
kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu
wa tatizo hili. Nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena kuwaagiza Wakuu wa
Mikoa na Wilaya kuwahimiza Wakulima hasa walioko katika maeneo yenye chakula
cha ziada kuhifadhi Chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao. Aidha, Wakala
wa Taifa na Hifadhi ya Chakula wajipange vizuri kuhamisha Chakula kutoka maeneo
yenye ziada na kupeleka kwenye maeneo yaliyoainishwa kuwa na hali tete mara
taarifa ya upungufu itakapotolewa.
Mheshimiwa Spika,
33.
Pamoja na juhudi za Serikali za kuhakikisha kwamba kuna
chakula cha kutosha, natambua Changamoto zilizopo katika ununuzi wa Chakula
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Natambua kuwepo kwa madeni
yanayotukabili kwenye ununuzi wa nafaka kwa ajili ya Wakala yaani NRFA. Hata hivyo, Mikoa inayohusika na madeni hayo
ni Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga,
Ruvuma, Rukwa na Tanga. Serikali
itahakikisha deni hilo hilo linalipwa ndani ya mwaka huu wa fedha 2013/2014.
(d)
Mpango wa Pembejeo
za Ruzuku
Mheshimiwa
Spika,
34.
Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 12 wa Bunge,
katika msimu wa 2013/2014 Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 112.564
kwa ajili ya ruzuku ya mbolea, na pembejeo. Aidha, nilielezea kuhusu utaratibu
mpya wa kutoa ruzuku utakaohusisha uwiano wa Asilimia 80 kwa Vocha na Asilimia 20 mikopo. Ili kuhakikisha Mfumo huu
mpya unatekelezwa kikamilifu na kuleta matokeo yaliyotarajiwa, Serikali imetoa
mafunzo ya utoaji pembejeo kwa njia ya mikopo kwa Washauri wa Kilimo wa Mikoa,
Maafisa Ushirika wa Mikoa na Wilaya na Maafisa Kilimo wa Wilaya kwa awamu mbili.
Awamu ya kwanza ikihusisha Mikoa ya Shinyanga, Geita na Manyara; na Awamu ya
Pili inahusu Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya
na Iringa. Aidha, uchambuzi wa takwimu za Vyama vya Ushirika na Vikundi vya
Wakulima watakaokopeshwa pembejeo za Kilimo mwaka 2013/2014 umefanyika katika
Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Njombe, Mbeya, Geita na Manyara. Takwimu zinaonesha kuna SACCOS 214, AMCOS 163 na Vikundi vingine 51
vyenye Wakulima 88,290 watakopeshwa
pembejeo za Kilimo. Natoa Wito kwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
kuendeleza mafunzo haya kwa Mikoa iliyobaki.
(e)
Hali ya Usambazaji
wa Vocha za Pembejeo
Mheshimiwa
Spika,
35.
Kuhusu hali ya Usambazaji wa Vocha za
Pembejeo katika Msimu wa 2013/2014 napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, jumla
ya Vocha 2,796,300 kwa ajili ya Kaya
932,100 zikiwemo Vocha 932,100 za mbolea ya kupandia, 932,100 za mbolea ya kukuzia, Vocha 441,100 za mbegu za mahindi chotara;
Vocha 432,000 za mahindi ya OPV na
Vocha 60,000 za mbegu za mpunga zilisambazwa
katika Mikoa yote hapa Nchini. Nitoe wito kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya kwa
kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wengine kuhakikisha kuwa
Wananchi wanapata na wanatumia Vocha hizi kupata pembejeo kama ilivyokusudiwa. Aidha,
tushirikiane kuhakikisha kuwa wale watakaokwenda kinyume na utaratibu huu wa
usambazaji wa Vocha hizo wanashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria.
(f)
Changamoto
za Mbolea ya Minjingu
Mheshimiwa
Spika,
36.
Juhudi za Serikali
katika kuhakikisha upatikanaji wa Pembejeo za ruzuku ziko dhahiri. Hata hivyo, imebainika kwamba katika mahitaji
ya mbolea, kilio kikubwa cha Wakulima ni kupatiwa mbolea kwa wakati. Aidha, wapo Wananchi wanaolalamikia mbolea ya
Minjingu Mazao ambayo ni kweli hapo awali ilikuwa na matatizo. Lakini sasa, mbolea hii imeboreshwa kwa
kiwango kikubwa kwa kuongezewa virutubisho.
Mheshimiwa
Spika,
37.
Mbolea ya Minjingu ya awali ilikuwa na
virutubisho vya udongo viwili tu vya
Kalisiumu na Fosfeti. Mbolea ya Minjingu Mazao imeboreshwa kwa kuongezwa
virutubisho vinne zaidi na kufanya virutubisho hivyo kuwa sita yaani Kalisiumu, Fosfeti, Naitrojeni, Salfa,
Boroni na Zinki.
38.
Kwa
msingi huo, Mbolea ya Minjingu mazao inaweza kutumika katika aina mbalimbali za
udongo tofauti na ilivyokuwa awali. Aidha, Mbolea ya Minjingu Mazao ni ya chengachenga
(granulated) tofauti na ya awali
ambayo ilikuwa katika mfumo wa unga (dust)
ambapo pengine matumizi yake hayakuwa rafiki kwa mkulima. Baada ya kuboreshwa,
kwa sasa Mbolea hii ya Minjingu inatumika kwa mazao mengi hususan mahindi,
mpunga na alizeti katika sehemu mbalimbali na aina mbalimbali za udongo.
Mheshimiwa
Spika
39.
Mkulima anahitaji kutumia mifuko miwili ya mbolea
ya Minjingu Mazao ya kilo 50 kila
mmoja kwa wakati mmoja ikilinganishwa na mfuko mmoja wa kilo 50 wa mbolea ya DAP. Hata hivyo, ukilinganisha na mbolea ya DAP,
mkulima anayetumia Minjingu Mazao anawezesha shamba lake kupata virutubisho
zaidi. Kwa hiyo, Mbolea ya Minjingu Mazao ni nafuu ikilinganishwa na Mbolea ya
DAP.
40.
Bei ya
mbolea ya Minjingu Mazao kwa mfuko mmoja
ni Shilingi 32,500/= hivyo kwa
mifuko miwili ni Shilingi 65,000 katika Wilaya zote Nchini ikilinganishwa na
bei ya wastani ya Shilingi 75,000/=
ya mfuko mmoja wa DAP. Aidha, kwa aina zote mbili za mbolea zinapotumika
kupandia, lazima mkulima aweke mbolea nyingine ya kukuzia ambayo ina
virutubisho vingi vya Naitrogeni kama
CAN au UREA.
41.
Majaribio ya kutumia Mbolea ya Minjingu
yalianza mwaka 1977 kuendelea hadi mwaka 2006 ikiwa katika hali ya unga. Mwaka
2007 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa kuiweka katika hali ya chenga chenga (granulation) ingawa virutubisho
havikuboreshwa. Mbolea hiyo iliendelea kutumika katika hali hiyo hadi mwaka
2009. Hivyo, mwaka 2010 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa kuongezea virutubisho
ambavyo baada ya utafiti wa kuihakiki (validation)
iliingizwa Sokoni mwaka 2012.
42.
Kwa sasa, Mbolea ya Minjingu Mazao inatumika
katika Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Rukwa, Mbeya, Njombe, Katavi, Kigoma na
Morogoro. Aidha, kuna mikoa mingine ambako mbolea hii imepelekwa pamoja na
mbolea nyingine kwa ajili ya Wakulima wenyewe kufanya maamuzi ya kuchagua.
Mheshimiwa Spika
43.
Matumizi ya Mbolea ya Minjingu Mazao katika
mwaka 2012/2013 yamewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi, mpunga na
alizeti kwa ekari hususan katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Changamoto
kubwa ni elimu juu ya matumizi sahihi ya Mbolea hiyo kwenye baadhi ya maeneo.
44.
Katika kutatua changamoto hii, Wizara
inashirikiana na Mmiliki wa Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu kuendesha mashamba
darasa katika Wilaya mbalimbali Nchini.
Vilevile, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo, inaendelea kufanya utafiti katika maeneno mbalimbali ya Nchi ili
kuboresha matumizi sahihi ya Mbolea hiyo katika aina mbalimbali za udongo (site specific validation trials).
45.
Changamoto zinazohusiana na Mbolea ya
Minjingu katika Wilaya ya Mbozi zitaangaliwa kwa namna yake. Kitendo hicho ni
cha udanganyifu kwani Mbolea ya aina nyingine ni bei kubwa ikilinganishwa na ya
Minjingu Mazao. Kutokana na kitendo hicho kuwa kinyume na Sheria ya Mbolea ya
2009, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea kwa kushirikiana na Wakaguzi wa mbolea wa
Wilaya ya Mbozi ilimkamata Wakala husika na kumchukulia hatua za kisheria. Naagiza
Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuchunguza mbolea inayopelekwa katika maeneo yao
isije ikachakachuliwa.
Mheshimiwa Spika,
46.
Kwa kuzingatia Changamoto zilizojitokeza katika matumizi
ya mbolea ya Minjingu katika maeneo mbalimbali Nchini Serikali itaendelea
kuzitafutia ufumbuzi kwa kuchukua hatua zifuatazo:
(a)
Kutoa elimu kwa Wakulima kuhusu namna bora ya kutumia
Mbolea ya Minjingu Mazao kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kuzingatia ushauri wa
kitaalam kuhusu aina ya udongo na mazao yanayofaa kwa mbolea hiyo. Vilevile,
kuwaelimisha Wananchi kuhusu ubora wa Mbolea ya Minjingu Mazao ikilinganishwa
na Mbolea za aina nyingine hasa kutokana na virutubisho vilivyoongezwa katika
mbolea.
(b)
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea imeagizwa kufuatilia na
kufanya uchunguzi wa madai ya Wakulima kuhusu changamoto za matumizi ya mbolea
ya Minjingu Mazao hasa katika Wilaya ya Mbozi na sehemu nyingine zenye matatizo
ya matumizi ya mbolea hiyo Nchini.
(c)
Naomba kuiagiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
kuendelea kushirikiana na Wadau kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali
Nchini. Kutokana na utafiti huo itoe ushauri na mwongozo kwa Wakulima wote
Nchini kuhusu njia sahihi za kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao katika aina
mbalimbali za udongo na mazao yanayofaa kulimwa. Lengo ni kuongeza tija katika
uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa eneo.
Kwa Wilaya ya Mbozi Wizara itoe mwongozo kuhusu nini kifanyike kwa sasa
wakati hatua za utafiti na uchunguzi wa matumizi sahihi ya Mbolea hiyo
zinaendelea.
(g)
Uzalishaji na Ununuzi wa Mazao ya
Biashara
Mheshimiwa Spika,
47.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na
Changamoto mbalimbali za uzalishaji na ununuzi wa baadhi ya mazao ya biashara
hapa Nchini ikiwemo Kilimo cha zao la Pamba, Korosho, Tumbaku na Kahawa. Kwa
kuzingatia ufinyu wa muda, leo naomba mniruhusu nizungumzie kidogo kuhusu
kilimo cha mazao mawili ya Pamba na Korosho.
(h)
Uzalishaji
na Ununuzi wa Zao la Pamba
Mheshimiwa
Spika,
48.
Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa
Wakulima wa Pamba wanazalisha kwa tija
kwa kutumia mbegu bora, utumiaji wa pembejeo (Viuadudu na Mbegu), kutoa huduma za ugani kupitia Maafisa wa Kilimo
katika Halmashauri za Wilaya na pia kuhamasisha Kilimo cha pamba kwa
kushirikiana kwa karibu na Wadau mbalimbali ikiwemo Sekta Binafsi.
49.
Katika kilimo hiki cha Pamba, Zana za kilimo
zinazotumika kwa sasa ni majembe ya kukokotwa na wanyama kazi kwa ajili ya
kulima nah ii ni dhahiri haiwezi kuongeza tija. Ttahakikisha tunatumia Zana za
Kisasa.
(i)
Mkakati wa Wizara kupata masoko ya uhakika ya pamba
50.
Serikali pia inaendelea
kuhakikisha kwamba pamba inaongezwa thamani hapa Nchini kwa kuhamasisha
uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya nyuzi na nguo. Uwekezaji mpya unafanyika
kwa kujenga kiwanda cha nyuzi na nguo cha Dahong Mkoani Shinyanga na pia Mradi
mkubwa wa kuzalisha pamba, kuchambua, kutengeneza nyuzi, kutengeneza vitambaa
na nguo unaotarajiwa kutekelezwa na
Kampuni ya Kijapani (NITORI) katika Wilaya ya Handeni. Kwa sasa mradi huo uko
katika hatua ya umilikishwaji wa Ardhi.
51.
Vilevile, Serikali
imeanzisha mafunzo ya Uhandisi na Ubunifu katika Viwanda vya Nyuzi na Nguo. Pia
tumeanzisha kozi ya ubunifu wa mitindo katika mitaala ya VETA na Mafunzo ya
Shahada ya uzamili katika “Textile”
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Lengo ni kuhakikisha kuwa kuna watalaamu
wa kutosha katika mchakato wa kuongeza thamani ya pamba.
(j)
Tofauti za ubora wa mbegu za pamba manyoya na De – linted
Mheshimiwa Spika,
52.
Sina shaka Watanzania wameshasikia kuwa kwa sasa
tunazo aina mbili za mbegu za Pamba zinazotumika hapa Nchini. Tunayo mbegu yetu ya asili ya Pamba Manyoya
na Mbegu mpya na ya kisasa ya Pamba isiyo na manyoya (De-linted). Aina hizi zinatofautiana sana kwa ubora na
bei. Mbegu ya manyoa ina uotaji wa chini ya Asilimia 50 wakati ile ya De
–linted ni zaidi ya Asilimia 90. Mbegu ya manyoya hutumika nyingi kwa eneo
(kilo 25 kwa Ekari), wakati De – linted ni kilo 6 tu kwa Ekari, sawa na Shilingi 7,200 kwa Ekari kwa bei ya Shilingi 1,200 kwa kilo. Mbegu ya manyoya ina tija ndogo (inazalisha kati ya
kilo 250 na 300 kwa Ekari) ikilinganishwa
ya mbegu ya De-linted inayozalisha Kilo 450 – 1200 kwa Ekari. Mbegu ya manyoya
ina uwiano mdogo wa pamba nyuzi (Asilimia 33) ikilinganishwa na mbegu De-linted
ambayo uwiano wake ni Asilimia 36.
(k)
Jitihada za Wizara kupunguza bei ya mbegu bora
Mheshimiwa Spika,
53.
Ili kuwawezesha Wakulima kutumia mbegu bora
(de-linted) Serikali imetoa ruzuku ya Shilingi Billioni 4.8 ili kufanya mbegu hiyo ipatikane kwa Shilingi 600 kwa kilo kwa mkulima badala ya
Shilingi 1,200 kwa kilo iliyotumika
mwaka 2012/2013.
54.
Serikali pia inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za
kutoa elimu kwa wakulima wa pamba kuhusu mbegu bora. Kwa mfano, Viongozi wa
maeneo yanayolima pamba (Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na baadhi ya
Madiwani) wamepelekwa katika kiwanda cha
kuchakata mbegu bora za Pamba cha
Kampuni ya Quton ili kupata maelezo na
kujionea hali ya utendaji wa mbegu bora katika kilimo.
55.
Kupitia programu ya kuendeleza zao la pamba wakulima
wawezeshaji (Lead Farmers) 3000 wa
vikundi vya Kilimo cha Mkataba wanaendelea kupewa mafunzo ya kilimo bora na
matumizi ya mbegu bora ili watumike kupeleka elimu hii kwa wakulima wenzao.
Mheshimiwa Spika,
56.
Katika msimu huu wa Kilimo wa 2013/14, Serikali
imejipanga kusimamia utekelezaji wa Kilimo cha Mkataba kwa lengo la kuleta
ufanisi katika Kilimo cha Pamba Nchini. Hatua hii inahusisha pia kutoa elimu ya kutosha na kushirikisha kwa karibu Wadau katika
kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo kwenye utaratibu mzima wa kilimo
hicho ambacho kina manufaa makubwa iwapo kitaeleweka na kutekelezwa vyema kwa
misingi ya haki miongoni wa wadau. Baadhi ya manufaa hayo ni:
(i)
Uhakika wa upatikanaji wa pembejeo kwa mkulima kwa
mkopo.
(ii)
Kuongeza tija kutokana
na kupata pembejeo na huduma za ugani.
(iii) Kuongeza ubora wa pamba kutokana na
matumizi makubwa ya pembejeo na huduma za
ugani pamoja na vikundi kutumika kama Mawakala wa kununua Pamba ya
wanachama wake hivyo kusimamia ubora
(iv) Uhakika wa soko la pamba ya mkulima
(v)
Kupunguza wizi kupitia
mizani ya mawakala
(vi) Wakulima kupata teknolojia kupitia uwekezaji
(vii) Kujenga na kuimarisha mfumo wa Ushirika kupitia vikundi vya wakulima.
(l)
Elimu ya kilimo cha mkataba kwa wakulima
Mheshimiwa Spika,
57.
Kupitia programu
ya kuendeleza zao la pamba, wakulima Wawezeshaji zaidi ya 3,000 wamekwisha pokea mafunzo ya kilimo cha Mkataba wanao tumika
kupeleka elimu hii kwa vikundi vya wakulima. Wagani wa Halmashauri wapatao 560 wameshapata mafunzo haya. Chini ya Mpango huu kila mgani anaweza
kuhudumia vikundi hadi 20.
58.
Napenda kuwaagiza Viongozi na
Wataalamu wa Kilimo waendelee kutoa elimu ya matumizi na faida ya mbegu bora za
De-linted au mbegu zisizokuwa na manyoya kwa Wakulima wa Pamba Nchini. Aidha,
mashamba darasa yatumike ipasavyo kuonesha tija inayotokana na aina hiyo
ya mbegu za Pamba inapolinganishwa na mbegu zenye manyoya. Vilevile, Viongozi na Wataalamu wa Kilimo
waendelee kuwakumbusha Wakulima wa Pamba na Watanzania kuwa utaratibu mpya wa
Kilimo cha Mkataba una manufaa mengi na makubwa. Tuendelee kuwashawishi Wakulima kujiunga na
Kilimo cha Mkataba bila kuwashurutisha isipokuwa tuwape elimu hasa kupitia
mashamba darasa. Wale watakaoshawishika kuingia
katika utaratibu huu wasaidiwe kwa kila hali ili wanufaike na kilimo hicho huku
wakisaidia kutoa elimu kwa Wakulima wengine ili wajiunge na aina hii ya kilimo.
Ni matumaini yangu ndani ya muda mfupi Wakulima watafahamu faida ya kilimo cha
mkataba.
(m)
Zao la
Korosho
Mheshimiwa
Spika,
59.
Kuhusu Zao la Korosho, azma ya Serikali ni
kuimarisha Viwanda vya Korosho na kufufua vile vilivyopobinafsishwa ili viweze
kusaidia kukuza Soko kwa wakulima wa Korosho. Ili kutekeleza azma hiyo,
Serikali imefanya tathmini na kubaini kuwa Wawekezaji wengi katika Viwanda vya
Korosho vilivyobinafsishwa wameshindwa kutekeleza Mikataba ya Ubinafsishaji wa
viwanda hivyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ukosefu wa fedha za
uendeshaji, ukosefu wa nishati ya uhakika na Viwanda kutumia teknolojia
zilizopitwa na wakati. Ili kukabiliana na hali hiyo, Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika kwa kushirikiana na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma
(CHC) pamoja na Wadau wengine inaandaa mapendekezo ya hatua za kuchukua dhidi
ya Wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda hivyo. Dhamira ya Serikali ni kwamba
Mwekezaji ambaye ameshindwa kuendeleza kiwanda alichonunua kwa kuzingatia
Makubaliano ya ununuzi na Serikali, mali hiyo irudishwe Serikalini na ifanyiwe
tathmini na itangazwe upya ili kupata Wawekezaji mahiri na wenye nia thabiti ya
kuendeleza Viwanda husika.
Mheshimiwa
Spika,
60.
Sambamba na hatua hiyo, Bodi ya Korosho
Tanzania imeandaa Mpango wa Ubanguaji wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2012/2013
ambao umelenga kuwasaidia wabanguaji wadogo na wa kati kuendesha shughuli za
ubanguaji kwa ufanisi kwa kuwapatia mafunzo, vifaa vya kubangulia, na
kuwatafutia masoko ya ndani, masoko ya kanda na masoko ya nje;
61.
Hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kwamba, Mfuko
wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho
Tanzania umetenga fedha kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu katika Mikoa ya
Ruvuma, Mtwara, na Pwani kwa ajili ya kuwawezesha Wabanguaji wadogo na wa kati
kumalizia baadhi ya hatua za ubanguaji katika viwanda hivyo kwa ajili ya
kukidhi matakwa ya masoko makubwa ya korosho duniani.
Mheshimiwa
Spika,
62.
Ili kuboresha kilimo cha Korosho, katika
mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya madawa kutoa huduma za
ugani na kuhamasisha wakulima wahudumie mikorosho na kupuliza madawa mapema.
Mheshimiwa
Spika,
63.
Kuhusu ununuzi wa Korosho, katika msimu huu
wa 2013/2014 ununuzi wa Korosho utaendelea kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi za
mazao Ghalani. Ukusanyaji wa Korosho kutoka kwa wakulima umeanza katika maeneo
mbalimbali Nchini. Kwa mfano, katika Mkoa wa Mtwara, mnada wa kwanza wa Korosho
ulianza tarehe 25 Oktoba, 2013 ambapo ulihusisha Vyama vya Msingi vya Mkoa wa
Mtwara. Korosho zote zilizokuwa zimekusanywa na kutangazwa katika kila mnada
zilinunuliwa. Bei ya Korosho katika Mnada wa kwanza ilikuwa kati ya Shilingi 1,402/= na 1,520/= kwa kilo ikilinganishwa
na bei dira ya Shilingi 1,000/= kwa
kilo. Mnada uliofuatia bei ziliongezeka na kuwa kati ya Shilingi 1,481/= na 1,570/= kwa kilo.
Mheshimiwa
Spika,
64.
Kwa upande wa Mkoa wa Lindi, Vyama vya Msingi
vilivyobaki chini ya ILULU vilifanya Mnada wa kwanza tarehe 2 Novemba, 2013
ambapo jumla ya Tani 783.593
ziliuzwa. Vyama vingine 51 vya
kutoka Wilaya ya Ruangwa, Nachingwea na Liwale ambavyo vilijiondoa kutoka
usimamizi wa Chama Kikuu cha ILULU vitafanya mnada baada ya taratibu za kupata
Kamati itakayowasimamia zitakapokamilika. Vyama hivyo vimeomba kufanyiwa Minada
yake katika Wilaya ya Nachingwea ambako ndiko walikoweka Ofisi yao.
Mheshimiwa
Spika,
65.
Kwa upande wa Wilaya ya Tunduru, bado
haijapata mkopo mpaka sasa na juhudi za kufuatilia zinaendelea. Taarifa kutoka
Benki ya NMB inaonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Vyama vya Msingi vya
TAMCU kupata mkopo msimu huu kwani deni ambalo TAMCU walikuwa wanadaiwa na
Benki hiyo ya NMB limelipwa na Serikali.
Mheshimiwa
Spika,
66.
Kwa upande wa Mkoa wa Pwani, uwezekano wa
Vyama vilivyo chini ya Chama Kikuu cha Coast Region Cooperative Union (CORECU)
kupata Mkopo ni mdogo kutokana na kudaiwa fedha nyingi zaidi ya Shilingi Bilioni 7 za msimu wa mwaka 2010/2011.
Serikali imefanya Ukaguzi Maalum katika Vyama hivyo na kubaini kwamba madeni
hayo kwa kiwango kikubwa yamesababishwa na ubadhirifu wa Viongozi na Watendaji
wa Vyama hivyo. Hivyo, kupitia Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika hatua za
kisheria zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwataka wahusika wa ubadhirifu huo kufidia
hasara hiyo. Kwa upande mwingine, Wahusika wamekata rufaa, lakini Mamlaka yenye
dhamana imezitupilia mbali rufaa hizo zote 434,
na kuwataka Wahusika walipe kiasi cha fedha kinachodaiwa na Vyama vyao.
Kutokana na hali hiyo, Wakulima wa Mkoa wa Pwani wanashauriwa kupeleka mavuno
ya Korosho katika maghala yaliyoteuliwa. Minada ya Korosho itafanyika katika
maghala hayo na wakulima watalipwa mara moja baada ya minada kufanyika.
Mheshimiwa
Spika,
67.
Kutokana na jitihada za Serikali
zinazoendelea natoa wito kwa Bodi ya Korosho na Wakuu wa Mikoa husika kuendelea
kusimamia kikamilifu taratibu wa ununuzi wa Korosho ili kuhakikisha kwamba
Wakulima wanauza Korosho zao walizovuna na kulipwa malipo yao halali kwa
wakati.
(n)
Hali ya
mwenendo wa Mvua za vuli mwaka 2013 na athari kwa mazao ya vuli
Mheshimiwa
Spika,
68.
Taarifa ya utabiri wa mwelekeo wa hali ya
hewa hususan mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2013 iliyotolewa na
Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini inaonesha kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa
chini ya wastani katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kaskazini mwa
Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na baadhi ya maeneo katika mikoa ya
Mwanza, Simiyu, Shinyanga Kagera, Geita na Mara. Pamoja na kwamba mvua za msimu
wa vuli zimechelewa kuanza katika maeneo mengi ambayo yalitarajiwa kupata mvua
za vuli, mvua hizi hazitarajiwi kuwa na mtawanyiko wa kuridhisha.
(o)
Athari za
mvua za vuli zinazonyesha chini ya Wastani
Mheshimiwa
Spika,
69.
Kutokana na utabiri huo wa Hali ya Hewa, tathmini
ya awali iliyofanyika katika maeneo yaliyotarajiwa kupata mvua za vuli
inaonesha kuwa:
i.
Hali ya mazao hasa
katika Nyanda za juu Kaskazini na ukanda wa Pwani Kaskazini si ya kuridhisha,
ii. Mategemeo ya mavuno ya vuli ni kidogo isipokuwa katika baadhi ya maeneo ya
ukanda wa Ziwa Viktoria hususan katika Mikoa ya Kagera na Geita ambayo yamepata
mvua za wastani hadi chini ya wastani,
iii. Mchango wa mavuno ya vuli ambao ni kati ya Asilimia 28-30 ya Chakula
kinachozalishwa katika maeneo yanayopata mvua hizo au Asilimia 18 Kitaifa hauwezi kufikiwa katika hali
hii ya mvua.
iv. Hali hii inaashiria kuwa kutakuwepo na upungufu wa Chakula katika maeneo
hayo niliyotaja hapo juu.
Mheshimiwa
Spika,
70.
Kutokana na hali hii, natoa wito kwa Wakulima
katika maeneo haya kuzingatia ushauri wa kupanda mazao yanayostahimili ukame na
yanayokomaa kwa muda mfupi. Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika Halmashauri husika wasimamie
suala hili kwa ukamilifu; ili kuepusha upungufu wa Chakula unaotarajiwa.
VI: NISHATI
(a) Kuongezeka kwa upatikanaji
wa Nishati Vijijni (Miradi ya REA) na hali iliyofikiwa
Mheshimiwa
Spika,
71.
Wakati wa Kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge
nilieleza Mikakati ya Serikali katika kueneza umeme Vijijini na matarajio ya
baadaye. Napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba tumeweza kupiga hatua
katika baadhi ya maeneo katika kuelekea kwenye malengo tuliyojiwekea. Tayari Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
ulitangaza zabuni mwezi Desemba 2012 kwa ajili ya kuwapata Wakandarasi wa
kupeleka umeme Vijijini na kujenga vituo vya kupoozea umeme. Baada ya tathmini
kufanyika, zabuni 15 za kupeleka umeme Vijijini zilipata Wakandarasi. Mikoa
ambayo ilipata Wakandarasi
katika awamu hiyo
ni pamoja na Arusha, Dodoma,
Iringa, Katavi, Kilimanjaro,
Mara, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora. Aidha Wakandarasi
kwa ajili ya
ujenzi wa vituo
vya kupozea umeme vya msongo wa Kilovoti
11 na 33 vya Ngara, Kibondo, Kasulu, Kigoma,
Tunduru na Mbinga
walipatikana. Kwa sasa Wakala unaendelea
na kulipa malipo ya awali (advance
payments) na Wakandarasi wanaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanza
kazi. Miradi hii yenye thamani ya Shilingi Bilioni
430.82 inatarajiwa kukamilika mwezi Juni,
2015.
Mheshimiwa
Spika,
72.
Mwezi
Mei, 2013 zabuni nyingine 10 ya Miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 450 zilitangazwa kwa
ajili yakuwapata Wakandarasi wa kupeleka umeme Vijijini
katika Mikoa ya Geita, Kagera,
Kigoma, Lindi, Manyara, Mbeya,
Morogoro, Pwani, Rukwa na Tanga. Kwa sasa tathmini ya zabuni
hizo inaendelea. Inatarajiwa kwamba Wakandarasi kutokana na Tathmini hiyo
watajulikana ifikapo tarehe 15 Novemba, 2013.
(b) Suala
la Fidia, Sera; na Miongozo ya usambazaji Umeme Vijijini:
Mheshimiwa
Spika
73.
Ili kuharakisha maendeleo ya upatikanaji wa
Nishati Vijijini, suala la Wananchi kuchangia
nguvu kazi na kutoa njia na maeneo ya kupitisha nyaya za umeme bila
fidia pale inapowezekana limekuwa likisititizwa na
Serikali kutokana na ufinyu wa bajeti. Upo ukweli kwamba, Miradi mingi
imechelewa kutekelezwa kutokana na Wananchi kudai fidia ya miti na mazao ya
msimu yanayokutwa kwenye njia ya umeme.
Kwa mfano miradi ya Awamu ya Kwanza katika Mkoa wa Pwani imechelewa
kuanza na kukamilishwa kutokana na Wananchi kudai fidia ilipwe kwanza ndio
ujenzi uendelee. Pia, kwa sasa ujenzi umesimama katika maeneo ya Bungu-Nyamisati
na Kisiwa cha Mafia kutokana na Wananchi kudai fidia kwanza.
Mheshimiwa
Spika,
74.
Ni kweli kwamba kulingana na Sheria zilizopo
kama katika njia ya kupitisha umeme yapo mazao yanayostahili kulipwa fidia.
Hata hivyo kutokana na bajeti finyu Wakala wa Nishati Vijijni unashindwa kutoa
fidia inayohitajika na kuona ni bora wale wanaojitolea maeneo yao wapelekewe
umeme haraka kuliko kusubiri bajeti kwa ajili ya fidia. Serikali inatoa rai kwa
Viongozi na Wananchi kuona umuhimu wa kujitolea maeneo yao ili waweze kupata
huduma hii muhimu mapema. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane katika kuwahamasisha
Wananchi katika maeneo yetu kuhusu umuhimu wa kupata umeme mapema kwa maendeleo
ya maeneo yetu.
(c)
Utekelezaji wa Ujenzi wa Bomba la Gesi
Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
Mheshimiwa
Spika,
75.
Shughuli za ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam zinaendelea vizuri. Mpaka sasa usafishaji wa njia ya kulaza bomba unaendelea na tayari Kilometa
484.17 kati ya Kilometa 517 zimekamilika. Aidha jumla ya
mabomba 20,491 yanayotosheleza kulazwa
umbali wa Kilometa 243.8
yamekwishawasili Nchini. Kazi ya kuchimba mtaro, kuyapanga mabomba katika
mstari mmoja kwenye mkuza na kuyaunganisha pamoja kwa kuchomelea inaendelea na
hadi sasa Kilometa 124.3
zimeshaunganishwa. Kazi zinazoendelea ni ujenzi wa kambi, nyumba za wafanyakazi
katika maeneo ya Songo Songo na Madimba, pamoja na maandalizi ya ujenzi wa
mitambo ya kusafirishia Gesi Asilia. Tutaendelea kutoa taarifa ya hatua iliyofikiwa
ya utekelezaji wa Mradi huu muhimu kwa Taifa letu.
76.
Aidha, katika
kuhakikisha kwamba miradi hii inatekelezwa na kuleta manufaa katika Nchi yetu, ninayo
furaha kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali ilipitisha Sera ya Gesi
Asilia tangu tarehe 10 Oktoba 2013, Utaratibu wa kuichapisha sera hiyo katika lugha
ya Kiswahili na Kiingereza unaendelea. Vilevile Serikali kupitia Wizara ya
Nishati na Madini imeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa
Sera ya Gesi na imeanza kutayarisha Rasimu ya Sheria ya Gesi. Ni matumaini
yangu kwamba vitu vyote hivi vikikamilika Sekta ya Gesi Asilia itaimarika.
VII: MIFUGO
(a)
Operesheni Ondoa Mifugo Katika Maeneo Mbalimbali Nchini
Mheshimiwa
Spika,
77.
Kwa muda mrefu sasa maeneo mbalimbali hapa
Nchini yamekuwa yakikumbwa na migogoro inayotokana na matumizi ya Ardhi hususan
kwa Wafugaji wanaohama kutoka maeneo yaliyokatazwa kisheria kwenda eneo lingine
pasipo na maandalizi ya kutosha ya kuwapokea. Utafiti unaonesha kuwa, migogoro ya ardhi hapa Nchini ina sura nne:
Moja: Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji,
Pili: Migogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji,
Tatu: Migogoro kati ya Wananchi na Serikali, na
Nne: Migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka nyingine ndani ya
Serikali inayotokana na migongano ya kimaslahi.
Mheshimiwa
Spika,
78.
Kuna ukweli kwamba, kuongezeka kwa idadi ya
Watu na kuongezeka kwa matumizi ya ardhi kutaendelea kuongeza kasi na
vipaumbele katika kugawa maeneo yaliyoko wazi. Hali hii imeanza kuonekana katika maeneo ya Wafugaji ambayo yameendelea
kupungua siku hadi siku. Aidha, shughuli za kilimo, maendeleo ya makazi, na
matumizi mengine ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa Vijiji kunakotokana na
ongezeko la idadi ya watu kumeendelea kupunguza eneo la malisho.
Mheshimiwa
Spika,
79.
Kuna ukweli pia kwamba, mabadiliko ya
tabianchi na kuongezeka kwa mifugo katika maeneo ya Nchi kwa ajili ya kutafuta
malisho na maji kumeendelea kuchangia migogoro mingi kati ya wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi. Kati ya mwaka 2005 na sasa, tumeshuhudia uhamiaji
wa mifugo kutoka mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa kwenda katika Mikoa ya
Kusini na Mashariki mwa Nchi. Uhamiaji huo licha ya kusababisha migogoro kati
ya watumiaji wengine pia imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwenye
maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za Taifa. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja
na hifadhi za Wanyama pori za Burigi, Maswa na Meatu, Bonde la Usangu na Bonde
la Kilombero.
Mheshimiwa
Spika,
80.
Ni matumaini yangu kwamba, maadam suala hili
limepewa umuhimu na Bunge lako Tukufu na hivyo kuunda Kamati ya kufuatilia
migogoro hii, ni dhahiri tutapata ufumbuzi wa kudumu katika tatizo hili.
Niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla wanaotoka katika
maeneo yenye migogoro inayotokana na Wafugaji na Wakulima kutoa ushirikiano
katika kutoa taarifa muhimu kwa Kamati iliyoundwa ili kulisaidia Taifa katika
kutatua migogoro hii.
VIII: HALI YA ULINZI NA
USALAMA NCHINI.
Mheshimiwa
Spika,
81.
Kwa ujumla hali ya Ulinzi na Usalama Nchini
imeendelea kuwa shwari, isipokuwa katika maeneo machache ambako kulijitokeza
vitendo vinavyoashiria kuwepo kwa vikundi vya uhalifu na ujambazi. Serikali kupitia Jeshi
la Polisi imeendelea kujipanga kukabiliana na matishio mbalimbali ya kiusalama
ikiwemo ugaidi. Tukio lililotokea Nchini Kenya hivi karibuni na matukio ya
kukamatwa kwa Vijana 12 kule Mtwara
na lile lililotokea Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga ambapo zaidi ya watuhumiwa 46 wamefikishwa mahakamani kwa makosa
mbalimbali yanaashiria kwamba ugaidi hauna mipaka unaweza kutokea katika Nchi
yoyote.
Mheshimiwa Spika
82.
Katika kuhakikisha kuwa
amani na utulivu vinaendelea kudumu Nchini, Serikali imejipanga katika maeneo
hayo kama ifuatavyo:
(i)
Kuhakikisha Vikao vya
Kamati za Ulinzi na Usalama vya Mitaa, Vijiji na Vitongoji vinafanyika mara kwa
mara kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Serikali za Mitaa katika kila
Kata/Shehia kwa kuwashirikisha madiwani ili kujadili na kubaini kero mbalimbali
na kuzitafutia ufumbuzi.
(ii) Kufufua mpango wa Daftari la Wakazi na Wageni katika kila Mtaa/Kitongoji
kwa Tanzania Bara na Zanzibar ili kila Kiongozi wa Mtaa, Kijiji na Kitongoji
ajue Watu wanaoishi katika himaya yake. Zoezi hili litasaidia kuepuka tatizo la
wageni wasiojulikana au wahamiaji haramu. Aidha kamati za Ulinzi na Usalama za
Serikali za Mitaa na Vijiji zinahimizwa kutekeleza mkakati wa Halmashauri wa
kuzuia uhalifu kwa kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi jirani, kwa
kuzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa na Sheria Ndogo zilizotungwa ili
kuimarisha usalama katika Halmashauri
husika.
(iii) Kuhimiza wafanyabiashara wasaidiane na vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi
jirani vilivyo kwenye maeneo jirani na biashara zao kama sehemu ya kuimarisha
usalama wa maeneo yao ya biashara. Pia, kwa wafanyabishara wenye biashara kubwa
zenye mikusanyiko ya Watu wengi wanaagizwa kufunga “CCTV Camera” na
kuziunganisha kimtandao na “Control Room”
ya Polisi ili kutoa msaada wa kuzuia na kutanzua mapema uhalifu wowote
utakaojitokeza.
(iv)
Kuendelea kuunda Zonal Task Force za Jeshi la Polisi
katika kila Tarafa/Jimbo ili kukusanya taarifa za uhalifu na kufanya operesheni
za kuzuia uhalifu katika kila Kata au Shehia zilizo ndani ya Tarafa husika. Kwa
kufanya hiovyo tutaokoa maisha ya watu wengi.
(v)
Kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu
mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu kwa kutumia vyombo mbalimbali vya
habari, mihadhara, mikutano, maonesho na usambazaji wa machapisho na
vipeperushi.
Mheshimiwa
Spika,
83.
Jukumu la kuhakikisha
Ulinzi na Usalama katika Nchi yetu ni letu sote. Kila Mwananchi popote alipo anawajibika
kushiriki kwa vitendo kwa kubaini vitendo vyovyote vya uhalifu katika sehemu za
kazi, biashara na maeneo tunamoishi.
Wito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge wote, ni kuwaomba tuwahimize Wananchi
kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Nchi yetu inadumu katika hali ya Amani
na Utulivu.
IX: HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika,
84.
Kwa kuhitimisha, naomba nitumie nafasi hii ya
mwisho kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee
nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza
vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge
kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge
kwa kazi nzuri na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu. Namshukuru
Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na
Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na
huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa
Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na
maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri
waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge,Viongozi
mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.
Mheshimiwa
Spika,
85.
Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema
mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu. Baada ya kusema hayo, naomba sasa
kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 3 Desemba, 2013 saa 3:00 Asubuhi
litakapokutana katika Mkutano wa 14 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa
Spika,
86.
Naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment