Sunday, October 13, 2013

VIJANA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA BIDII NA KUACHA KULALAMIKA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa somo kwa vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini kuhusu namna wanavyoweza kutumia fursa zilizopo kupambana na umasikini na tatizo la ajira wakati wa mdahalo wa Wiki ya Vijana leo mkoani Iringa.
Mbunge wa jimbo la Mchinga Mh. Saidi Mtanda akizungumza na Vijana wakati wa mdahalo leo mkoani Iringa.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi akizungumza waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa leo kuhusu Wiki ya Vijana, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2013 zitakazofanyika katika uwanja wa Samora mjini Iringa . Picha na Aron Msigwa -MAELEZO.

Vijana kote nchini wametakiwa kuacha tabia ya kulalamika na badala yake wazitumie fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao kubuni miradi mbalimbali na kufanya kazi kwa bidii ili jamii iweze kuwaheshimu na kuthamini mchango wao.

Akizungumza na vijana wakati wa mdahalo wa vijana uliofanyika katika chuo cha Ufundi (VETA) mkoani Iringa leo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo Prof.Elisante Ole Gabriel amesema kuwa vijana ndio nguvu kazi ya taifa hivyo hawapaswi kulalamika badala yake washiriki kikamilifu katika kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa kuyatumia mazingira yanayowazunguka.

Amesema kuwa tatizo la vijana wengi Tanzania kukabiriwa na changamoto ya ukosefu wa ajira hasa maeneo ya mijini linatokana na wengi wa vijana kushindwa kubaini fursa za ajira zilizopo katika mazingira wanayoishi hivyo kuishia kuilaumu serikali.

Amesema vijana wengi wanakosa moyo wa kuthubutu kuingia katika biashara halali za kuweza kuwapatia kipato na kujikuta wakitumia muda mwingi kukaa viweni na kusubiri serikali iwatafutie ajira jambo ambalo linachangia vijana wengi kuendelea kuwa maskini.

“Ifike mahali tukubali kuwa hakuna changamoto yoyote duniani ambayo siyo fursa,hapa Tanzania yapo maeneo mengi ambayo vijana mkikaa vizuri mnaweza kutajirika"

Profesa Elisante amesema kuwa yapo maeneo mengi ambayo vijana wanaweza kuyatumia wakatajirika huku akiwataka vijana kote nchini walioajiriwa na kujiajiri kuepuka uvivu na kufanya kazi kwa bidii katika maeneo kazi yao.

“Lazima vijana kwa namna yoyote ile mkubari kuwa hali tuliyonayo maisha yamebadilika , ni lazima tubadilishe mitazamo na mawazo tuliyonayo ili tuweze kuona mabadiliko”Amesema.

Amewataka vijana kote nchini kuungana na kuwa chanzo cha mapinduzi ya kiuchumi na na kuacha kufanya kazi kwa mazoea bila malengo huku akisisitiza kuwa vijana wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kokote duniani.

Aidha amewataka vijana kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kuanza kuona mbali tofauti na ilivyo sasa ili taifa liweze kuendelea na kuwakumbuka kwa michango yao na kuongeza kuwa serikali kwa upande wake itaendelea kuunga mkono juhudi zao kwa kuwawezesha kupata mikopo ya kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo kwa wale walio tayari kufanya hivyo.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana nchini Bw. James Kajugusi ametoa wito kwa vijana kote nchini kuendelea kulinda na kudumisha amani iliyopo nchini na kuepuka kutumiwa kuvuruga amani na utulivu.

Akizungumza na waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa wakati alipokutana nao kuzungumzia Wiki ya Vijana Kitaifa, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere na Kilele cha mbio za Mwenge 2013 leo Bw. Kajugusi amefafanua kuwa maadhimisho ya Wiki ya Vijana yametoa fursa kwa Vijana kukutana pamoja na kujadili namna ya kutatua changamoto zinazowakabili kwa maendeleo ya taifa. Amesema kuwa vijana kama kundi muhimu katika taifa wanayo nafasi nzuri ya kushiriki katika shughuli za maendeleo na taifa linawategemea.

Amefafanua kuwa serikali inathamini mchango wa Vijana nchini na kuongeza kuwa katika bajeti ya mwaka huu 2013/2014 imetenga kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 6.1 kwa ajili ya kuwakopesha vijana. Bw. Kajugusi amesema kuwa kiasi hicho cha fedha watakopeshwa vijana kupitia mfuko wao wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana ulio mahususi kwa ajili ya kuwahudumia vijana kulingana na masharti yaliyowekwa.

Amefafanua kuwa serikali kwa kuwajali vijana imeendelea kutoa mikopo kwa vijana kote nchini kupitia Vikundi mbalimbali vya vijana kulingana na miradi wanayotekeleza na kuongeza kuwa kufikia mwaka 2012 vikundi takribani 241 sawa na vikundi 2 kwa kila wilaya kote nchini.

Aidha ameeleza kuwa utoaji wa mikopo hiyo kwa vijana hauna ubaguzi wa kabila, rangi, dini wala itikadi za vyama vya siasa bali ni kwa ajili ya vijana wote nchini waliojiunga na vikundi vyinavyofanya shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment