Monday, October 14, 2013

AMANI NDIYO MTAJI WETU MKUBWA- MHE.JOHN SAMUEL MALECELEA

Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. John Samuel Malecela akisisitiza jambo wakati alipokuwa akibadilishana mawazo na Baadhi ya maafisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ( hawapo pichani) na wajumbe wanaohudhuria mikutano ya Kamati Kuu Sita za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mhe. Malecela ambaye yuko Jijiji New York kwa ziara binafsi, alisisitiza sana umuhimu wa watanzania wote bila ya kujali itikadi na tofauti za kisiasa, kuhakikisha wanaulinda mtaji wao mkubwa ambao ni amani.
Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na Mkewe Upendo wakifuatilia mazungumzo hayo ambayo yalifanyika katika makazi ya Balozi , mazungumzo yaliyoambatana na chakula cha jioni.
Mke wa Mhe. Malecelea, Mhe. Ann Kilango akifurahia jambo pembeni ni Naibu Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi.
Mama Upendo Manongi mke wa Balozi Manongi akiwakarisha wageni wake chakula cha jioni.
Balozi Mwinyi, Balozi Mushy na Kanali Masalla nao wakipata chochote kitu.
Balozi Manongi akiwa na baadhi ya maafisa wake wakiendelea kujipakulia maakuli.
wakipata chakula.
Mhe. Waziri Mkuu Mstaafu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Mhe. Waziri Mkuu Mstaafu akiwa na baadhi ya wajumbe wanaoshiriki mikutano mbalimbali inayoendelea hapa Umoja wa Mataifa


Na Mwandishi Maalum

Waziri Mkuu mstaafu Mhe. John Samue Malecela ameeleza kwamba, hakuna mtaji mkubwa ambao watanzania wanauhitaji kama amani.

Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipokutana na kubadilishana mawazo na maafisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, pamoja na wajumbe wanaohudhuria mikutano inayoendelea ya Kamati Kuu Sita za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mazungumzo hayo yaliyoambatana na chakula cha jioni yalifanyika katika Makazi ya Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi

“ Naomba niliseme hili, ninasema hivi , hakuna mtaji mkubwa tunaouhitaji watanzania wote bila ya kujali itikadi wala tofauti zetu za kisiasa kama amani” akasema Mhe. Malecela .

Na kuongeza. “Nchi yetu inaoutajiri usioelezeka, hakuna wilaya isiyokuwa na utajiri kuanzia gesi, madini ya kila aina, ikiwani madini ya namna ya urani hadi makaa ya mawe, nchi yetu ni tajiri sana. Tunahitaji mitaji ya kuendeleza utajiri huu. Lakini nasisitiza sana utajiri huu tulionao hautakuwa na maana yoyote kwetu watanzania kama hatutadumisha amani, upendo, mshikamano na uzalendo”.

Waziri Mkuu mstaafu na ambaye amefuata na mkewe Mama Ann Kilango yupo jijini New York kwa ziara binafsi.

Akasema uchimbaji wa gesi ukianza na uchimbaji wa madini ya urani ukianza, pamoja na mipango mbalimbali ya maendeleo inayoendelea hivi sasa, basi miaka kumi ijayo Tanzania itapiga hatua kubwa sana za kiuchumi na kimaendeleo.

Katika mazungumzo hayo Mhe. Malecela licha ya kuzungumzia umuhimu wa amani na matumizi mazuri ya raslimali , pia alizungumzia mafanikio na changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa hivi sasa.

Kwa upande wa maendeleo hakusita kuzungumzia mpango wa serikali wa kuwa na shule za sekondari kila kata na kusisitiza kwamba ingawa uamuzi huo umekuwa ukipingwa au kulalamikiwa na baadhi ya watu lakini ni mpango ambazo umewapatia fursa vijana wengi ya kupata elimu ya sekondari na matunda yake yanaonekana.

Kwa upande wa ujenzi wa miundo mbinu na hususani barabara, Mhe. John Malecela, amesema Serikali ya Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete inafanya kazi kubwa na nzuri ya kuendeleza ujenzi wa mitandao ya barabara nchi nzima.

“ Kusema ukweli, Mhe. Kikwete anajitahidi sana katika eneo hili hakuna nchi katika eneo la Afrika Mashariki ambayo inaweza kushindana nasi kwa upande wa barabara.” Akasema Mhe. Malecela

Na kuongeza serikali haijaishia katika ujenzi wa barabara lakini pia inaendelea na jukumu uimarishaji wa reli,ujenzi na upanuzi wa bandari ukiwamo ujenzi wa bandari mpya katika eneo la Bagamoyo. Bandari aliyoieleza kwamba itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuegesha meli kubwa na zenye uwezo wa kubeba tani nyingi za mizigo.

Akizungumzia uzefu wake katika tasnia ya diplomasia na ushirikiano wa Kimataifa. Mhe, John Malecela ambaye pia ni mwanadiplomasia mkomavu aliwataka maafisa hao kutoyumba pale inapobidi kutetea misimamo na maslahi ya nchi yao.

“ kwa kweli ninawaonea huruma sana Mabalozi wa wakati huu, mnafanya kazi katika mazingira magumu sana, enzi zetu nakumbuka nikiwa hapa Umoja wa Mataifa miaka michache baada ya kupata uhuru Balozi ulikuwa na nguvu ya kusimama kwenye majukwaa ya kimataifa na kutetea jambo bila ya kuwaogopa wakubwa”. Akasema.

Na kuongeza, “ Kuna mkutano mmoja nilitoa maneno makali dhidi ya Balozi wa Israel wakati ule. Baada ya mkutano ule, Balozi yule alikuja ofisini kwangu na kuniambia maneno yale niliyoyasema hayakuwa msimamo wa nchi yangu”.

“ Lakini pia niliitwa nyumbani na Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere. akaniambia John umezungumza nini huko, taratibu hao ni wakubwa na mimi nikamjibu, Mhe. Rais naamini nimekuwakilisha vizuri. Ninachotaka kusisitiza ni kwamba msiogope kutetea maslahi ya nchi yetu licha ya changamoto za diplomasia za nyakati hizi”. Akasisitiza

No comments:

Post a Comment