Monday, September 30, 2013

TIC yawahakikishia wawekezaji ushirikiano zaidi

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesisitiza kuwa kitaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanaotaka kuwekeza katika mikoa ya kanda ya kaskazini na maeneo mengine nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kongamano la uwekezaji kanda ya kaskazini lililomalizika hivi karibuni mjini Tanga, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Bi. Juliet Kairuki alisema kuwa kituo chake kiko tayari kupokea wale wote walio tayari kuwekeza katika kanda hiyo. 

“Kwa wale ambao watakuwa tayari kuwekeza katika mikoa ya kanda ya kaskazini, milango ipo wazi kuandikisha miradi yao TIC,” alisema mjini Tanga hivi karibuni.

Akielezea kongamano hilo ambalo ni la kwanza kufanyika katika kanda hiyo alisema huo ni mwanzo wa juhudi kama hizo katika kutangaza vivutio vya uwekezaji katika kanda hiyo na maeneo mengine ya nchi.

Alitoa shukrani kwa mikoa ya kanda hiyo kwa kushirikiana katika kongamano hilo na kusema kuwa hiyo ni njia nzuri na yenye matokeo makubwa na mazuri kwa uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.

Alisema kongamano hilo limetoa fursa nzuri kwa wawekezaji, wafanyabiashara na wajasiriamali kufahamu fursa mbalimbali za uwekezaji zilizo katika mikoa ya kanda ya kaskazini na pia kuelezea ambavyo serikali inasaidia uanzishwaji wa miradi ya uwekezaji.

Alisema katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, Tanzania imefanya vizuri katika eneo la uwekezaji ambapo uwekezaji mkubwa umefanywa kwenye sekta za kilimo, utalii, viwanda, mawasiliano, miundombinu na usafirishaji.

Alisema katika kipindi hicho, miradi ya uwekezaji imekuwa kutoka 178 hadi 869 mwaka 2012 huku uwekezaji uliofanywa na watanzania wenyewe ukiwa ni asilimia 53 ya miradi yote.

Alifafanua kuwa kuongezeka kwa miradi kumechangia kukua kwa mitaji kutoka dola za kimarekani 874 milioni hadi USD 12 bilioni. “Miradi hii imevutia ajira mpya zinazofikia 135,760 mwaka 2012,” alisema.

Mkuu wa wilaya ya Hanan’g, mkoa wa Manyara, Bi. Christina Mndeme alisema kongamano hilo limekuwa la manufaa makubwa kwa wilaya yake.

Alisema kutokana na kongamano hilo, tayari amefikia makubaliano na baadhi ya wawekezaji ambao wako tayari katika kujenga kiwanda cha kuongeza thamani mazao mbalimbali pamoja na mwekezaji mwingine, Manyara Cement, anayetaka kujenga kiwanda cha sementi.

“Makongamano kama haya ni muhimu sana, tuko tayari kufanya kazi na wawekezaji na TIC,” alisema.

Awali, akielezea umuhimu wa makongamano hayo ya uwekezaji, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema ni ya muhimu na kuwa yanatakiwa kuimarishwa zaidi.

Akitoa mfano alisema tayari matokeo mazuri yameshaonekana kutokana na kongamano la uwekezaji lililofanyika mwezi Oktoba mwaka 2012 katika kanda ya Nyanda ya Juu Kusini mkoani katavi.

“Sasa kuna ongezeko kubwa la vyumba vya hoteli vinavyofikia elfu moja kutokana na uwekezaji katika sekta ya utalii katika mkoa wa Katavi,” alisema.

Kongamano la uwekezaji kanda ya kaskazini lilihudhuriwa na wawekezaji zaidi ya 1,500 toka ndani na nje ya nchi pamoja na maafisa wengine toka sekta binafsi na umma, viongozi wa dini, mabalozi na wadau wengine wa maendeleo.

No comments:

Post a Comment