Wednesday, September 4, 2013

KUZINDULIWA KWA SHINDANO JIPYA LA TANZANIA TOP MODEL.

Jackson M. Kalikumtima
Mwenyekiti Mtendaji
Shindano la Tanzania Top Model limeanzishwa ili kuziba ombwe lililoko la kuwatafuta,  kuwatayarisha na kuwatafutia mikataba wanamitindo wa kitanzania ambao ndoto zao zimekuwa ni kufanikiwa na kuwa wanamitindo wa Kitaifa na Kimataifa. Ni shindano litakalo wajenga na kuwafanya wajiamini na waaminiwe kwa kazi mbalimbali. Hiki kitakuwa ni kichocheo kingine cha kuitangaza nchi yetu katika mavazi na sanaa nyingine kimataifa na kuwa chimbuko la nyota nyingine katika dunia ya Wanamitindo hapa nchini.
Mashindano ya kumtafuta Tanzania Top Model si mashindano ya kawaida kama tulivyo zoea mashindano ya kuwakutanisha Washiriki na kupima Mshiriki aliye bora tu kuliko wenzake, bali ni Mashindano ya kumtafuta Mwanamitindo bora tena wa Mfano hapa nchini. Haya ni mashindano yatakayo ruhusu Jamii/ Wananchi/ Wadau kushiriki kuchagua mshindi kwa kiwango Fulani. 
Judgement au Maamuzi wa nani ashinde shindano hili yatafanywa na makundi manne tofauti ambapo wananchi watachagua mshindi kwa kupiga kura kwa ujumbe mfupi kupitia simu zao za viganjani na kupitia kwenye mtandao (tunaamini vyombo vya habari mtatusaidia sana katika hili kwa kuhamasisha wananchi wengi iwezekanavyo wapige kura zao na kuchagua mshindi). 
Maamuzi yao yatakuwa ni kwa asilimia 20. Waalimu, Washauri nasaha, Wakufunzi, Wawezeshaji watakao kuwa mafunzo mbalimbali wakati wa kambi ya Washiriki watakuwa na maamuzi ya mshindi kwa asilimia 15. Matron na watu wa kambi walinzi, wafanya usafi watakuwa na maamuzi kwa asilimia 5 ya alama zote. Asilimia 60 zilizobaki zitatolewa na Majaji watakaofanya kazi hiyo kwenye onyesho la mwisho.
Mashindano haya, katika ngazi ya fainali yataendeshwa kama kipindi cha kwenye Televisheni (Reality TV Show) na kurushwa katika kituo kimojawapo hapa nchini kuanzia Novemba moja hadi siku ya Fainali ya Onesho hilo ambalo litakuwa linakwenda sambamba na sherehe za Uhuru wa Tanzania kila mwaka. Kwa kuyafanya mashindano haya kuwa sehemu ya kipindi cha televisheni, tutakuwa tunawapa nafasi wananchi na wadau wa Tanzania Top Model waweze kuona na kumpigia kura mshiriki ambao wanadhani anafaa kuwa mshindi na kuwawakilisha katika mashindano ya kimataifa ya Top Model of the World. Kwa kuwarusha kwenye kipindi cha Televisheni kwa muda mrefu kiasi hiki, tutakuwa tunawajengea nafasi washiriki wetu ya kuwa watu maarufu na kuwafanya wakubalike kwenye jamii na waweze kuajirika.
Kwa kuanzisha shindano hili, Kampuni ya Tanzania Top Model Agency Limited ina malengo makuu ambayo ni  pamoja na Kuenzi, kukuza na kuendeleza vipaji vya wasanii ambao kwa namna mbalimbali watajihusisha na shindano hili ili kuwafanya wajitegemee katika maisha na kuwa na uhakika wa maisha bora. Pamoja na nilichotaja malengo mengine yatakuwa ni
1     Kuwatafuta, kuwainua wanamitindo chipukizi wenye vipaji na wasio           na majina katika fani hii na kuwafanya wajulikane ndani na nje ya nchi, huku tukiwajengea uwezo wa kujiamnini kwa kile wanachokifanya.
2.  Kutoa ushauri wa Kitaalamu unaohusu masuala ya fani mbali mbali ili kuwawezesha washiriki waweze kukubalika katika soko la ajira kwenye mitindo, maonyesho ya mavazi au kazi nyinginezo.
3.   Kumtafuta Mwakilishi wa Tanzania katika Mashindano Top Model of the World.
4.   Kuenzi, kuhifadhi na kuendeleza mavazi ya Kitanzania na hatimaye Tanzania tuwe na vazi moja rasmi la kujivunia wote.
5.  Kuendeleza fani ya mitindo na ubunifu kwa kuwashirikisha wanamitindo, taasisi, mawakala na wabunifu wa Tanzania ili kuiweka sanaa ya maonyesho ya mavazi katika thamani ya kimataifa.
6.  kutoa nafasi ya kutangaza na kuitangaza nchi yetu ya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuhamasisha utalii.
7.  Kuwajengea Washiriki moyo wa kujitolea ili waweze kutumia vipaji vyao katika kulitumikia Taifa kwa kujiajiri.
8.   Kujenga moyo wa mshikamano na Upendo miongoni mwa Wanamitindo.
9.  Kusaidia Jamii iliyo katika shida kutokana na sehemu ya mapato yatakayo tokana mashindano haya.
10.  kuamsha ari ya Wasichana wa kitanzania ili wajishughulishe na ujasiliamali na kujitegemea.

Wakati wa kambi ya Tanzania Top Model, kutafanyika shughuli (Tasks)mbali mbali ambazo zitaandaliwa na kufanywa na washiriki kama njia ya kujifunza, kupimwa uwezo wao katika mambo mbali mbali(km uvumilivu, na kuburudisha watu watakao kuwa wanawaangalia kwenye luninga . Tunaweza kusema kwa kifupi kuwa watu wasubirie Drama za Washiriki watakaofanikiwa kuingia kwenye kambi ya Tanzania Top Model.
 Mashindano ya Mwaka huu yatahusisha nchi nzima lakini kwa kufanya usaili (auditions) katika miji michache ambayo ni Dar es salaam (2), Mwanza, Musoma, Arusha, Moshi, Dodoma, Mbeya na Iringa. Tutaendelea hivyo na kutakuwa na mabadiliko ya kimfumo kila mwaka ili kuondoa uwezekano wa uchovu kwa washabiki wetu wa kuona kitu hicho hicho kila mwaka.
Mshindi wa shindano hili atapatikana baada ya kuonyesha kipaji chochote na kupata wastani wa alama za juu kuliko wengine wane watakao kuwa wameingia kwenye fainali. Kwa kufanikiwa kushinda, Tanzania Top Model atapata mkataba wa kufanya kazi na Kampuni ya Tanzania Top Model Agency Ltd  kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo itakuwa ni pamoja na kushiriki shindano la Top Model of the World.  Wale ambao hawatabahatika kushinda, wanaweza kupata mikataba ya ajira au ya maonyesho mbali mbali kutokana na jinsi watakavyo kuwa wamefanya au kuonekana kwenye vipindi vyetu vya Tamthilia halisi kwenye Televisheni.    
Tunawahakikisha wananchi kuwa hili litakuwa shindano litakalo wafundisha uvaaji wa mavazi stahihiki kwenye maeneo husika na wakati gani na kwa wale tusiojua kuvaa tutakuwa tumepata jukwaa la kutufundishia namna ya kuvaa na kuwa nadhifu muda wote tukiwa wadau wa mavazi na mitindo.  

Natanguliza shukrani.
Jackson M. Kalikumtima
Mwenyekiti Mtendaji





No comments:

Post a Comment