Saturday, September 14, 2013

HOJA YA HAJA - MABONDIA NA UNGA: TUNAPONZWA NA NJAA ZETU ZA MAISHA

Asili ya mabondia wengi  duniani wanatoka katika familia duni kwa mfano hapa kwetu Dar es salaam ni mara chache kumkuta bondia ametoka Upanga, Oysterbay, au Masaki ushuwani, nikiwa na maana  mabondia wengi wanatoka uswahilini na ni watu wa hali duni kimaisha, ambapo wengi wetu hatujakalia madawati ya shule ama wengine tuliojitahidi tumefika darasa la tano au sita; kama wazazi walikomaa ndio tunamaliza la saba. Baadhi yetu tukiwa na umri wa kuanzia miaka sita nyumbani huwa tunaanza kupewa uzowefu wa kuuza visheti,maandazi, vitumbua, karanga n.k.  na vikibaki nyumbani hauli chakula mpaka viishe. 

Shuleni mwalimu mkali balaa, darasani hafundishi mpaka usome tuisheni kwake ndio unapata kufundishwa kidogo na ukishindwa maswali yake unakula viboko vya ghadhabu ,hapo ndipo tunapoamua kuachana na shule na kutinga mitaani.  Michezo yetu ni katika madampo na vichochoroni na tukifikia umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea tunajua jinsi ya kutafuta pesa kwa kuuza njiwa,kucheza kamari,malani,kuiba kuku na bata. Kwa wale walio watukutu zaidi kuuza na kuvuta bangi ni sehemu ya maisha ya kawaida tu huku mitaani kwetu. Aghalabu mlo kwetu ni mmoja tu kiubishoo au kuna wageni nyumbani ndio tunakula milo miwili. Katika maisha yetu muda mwingi tupo huru na michezo kuliko kusoma hasa kolokolo,ngoma,mpira na ngumi, mpira tunacheza mabarabarani ,vichochoroni na madampo wakati ngumi tunajifundisha katika makamali vichochoroni au uwani kwa kina masta, begi au tairi limefungwa juu ya  mti tizi linaendelea bila vifanyio vya mazoezi vilivyo rasmi mwendo mdundo tunasonga na tunashinda au kufanya vizuri  katika mashindano yetu tunayoshiriki na hali yetu duni hihi hii ya kimaisha, na majina yetu kutangazwa sana katika vyombo vya habari na kupata umaarufu mkubwa nchini,nchi jirani  na hata nchi za ulaya. Lakini ukibahatika kututembelea na kuangalia tunapoishi na familia zetu na umaarufu tulionao na maisha yetu mabovu inasikitisha.


siku za hivi karibuni kuna vimaendeleo kidogo baadhi ya mabondia tunafanya mazoezi katika vilabu vya pombe kwa kuwalipa kodi ya mazoezi wenye bar. Naweza sema Tanzania hakuna sehemu rasmi  za kufanyia mazoezi ya ndani zilizotengwa na serikali kwa ajili ya raia wake wapenda michezo na kama zipo ni chache katika makambi ya jeshi kwa masharti magumu kwa raia wa kwawaida.

 Siku za nyuma wakazi wa mjini kama vile Kisutu, Gerezani na Kariakoo walikuwa wanafanya mazoezi pale Anatoglou,siku hizi huwezi kusikia kuna mwanamichezo katokea Gerezani au Kariakoo. Iliyobaki kwao ni kuuza na kutumia madawa ya kulevya na kukimbizana na wafanyabiashara wa maeneo hayo. Naweza ilaumu serikali kwa kutoendeleza michezo bali ilishiriki kuuwa kabisa michezo maeneo hayo na mengineyo mengi zaidi.
Mbwana Matumla
Kwa sisi tulionza kukua kimchezo pambano la ngumi likiandaliwa huwa tunalipwa kuanzia shilingi alfu 5 mpaka 20 kwa mapambano haya madogomadogo na iwapo kutakuwa na pambano kubwa na kupata bahati ya kucheza unaweza lipwa shilingi alfu 40 mpaka laki moja. Mapambano makubwa yanaweza kuwa moja,mawili au matatu kwa mwaka hayazidi hapo! Haya mapambano madogo tunaweza pata mawili mpaka sita kwa mwaka. Msiwaone mabondia wakicheza mkadhani wana kipato kikubwa la hasha, ni wale tu wachache waliobahatika kupata wadhamini au waratibu wenye uwezo wa kipesa ndio kidogo hutoka.
Kwa sisi wengine ukiangalia elimu ya kusoma hatuna kazi hakuna na mchezo wa ngumi tunaupenda na pengine tuna vipaji na kwa kufanya vizuri katika mapambano yetu,hivyo mchezo ndio huwa kama ajira zetu kwa sababu tunapata chochote kidogo kupitia mchezo huo kuliko kuiba au kukimbizana na mapolisi katika kamari na kuishia jela.
Kwetu sisi mabondia huona ni jambo la kifahari na hufurahi mno pale tu tunapopata pambano la nje ya nchi na hufurahia kupanda ndege na vile vimisosimisosi tunavyopata tukiwa mahotelini ugenini, tukihadithiana mambo ya safari uswahilini kwetu tunahisi tunakosa mambo mengi ya raha.

Hapo ndipo mawakala wa ngumi hutupata na mabondia huwa wanadiriki kukubali kwenda kucheza popote tukijua tutapanda ndege tunakula raha bila kujali  na wala kuhoji tuendako tutalipwa kiasi gani cha pambano nitakalocheza wala kujua usalama wangu.
Mohamed Matumla
Ukiangalia umbumbumbu na maskini tulionao mabondia,hapo wajanja wenye pesa zao,wafanyabiashara na baadhi ya viongozi wanatumia udhaifu tulionao mabondia kutuhadaa kwa kutupatia safari za nje za kimichezo au matembezi ya kwenda kufanya mazoezi ughaibuni na  hatimae kutubebesha mihadarati(madawa ya kulevya)  bila kujua kwa kutuwekea katika mizigo tunayosafiri nayo. Pindi kuna baadhi ya wafanya biashara hao wenye pesa zao hutuweka wazi wakati unaenda pigana umbebee mzigo wake na atakulipa pesa nyingi ,hapo ndipo tunapobanwa ukiangalia nyumbani tunalalia telemka tukaze tunashindia tembele mlo mmoja msosi wa kengele tena kwa masimango,mfukoni sina kitu na wala sina kazi itakayonipatia pesa ya kula kwa sasa (hapo sijaingiza mambo ya kodi),demu wangu namlinda vipi.
Hii njaa na umaskini tulio nao mabondia,hapo ndio vigogo wanapoamua kututumia kwa  kutubebesha madawa ya kulevya kusafirisha nje wakijua wazi hatuwezi kataa kutokana na dhiki tuliyo nayo, tutakubali tu kwani hakuna apendae kulala njaa , kulala pachafu  au kuvaa midabwada.
’siwezi acha dili la pesa kama hili wakati jina langu kubwa kila kona linatajwa mitaani na vyombo vya habari lakini mimi binafsi nauli ya daladala sina,siku ya tatu leo nakula mlo mmoja kwa siku,watoto hawapo katika hali nzuri, mazoezi yenyewe sifanyi kwa raha nafikiria nitapata wapi mshiko,leo unaniletea ishu ya pesa niikatae si nitakuwa kichaa? 
Wadau wenzangu wa ngumi ,wapambe wao,na walio karibu na sisi mabondia wana nguo za bei kubwa wanapendeza , wana magari, ukiangalia mimi bondia ndie mtendaji wao mkuu nipo ovyo sina kitu mfukoni wala tumboni madeni kibao yaani majanga matupu

Ushauri wangu kwa serikali au taasisi zinazohusika na wanaolichukia jambo hili kiukweli maana wengine hujifanya kulichukia mdomoni pembeni ndio watendaji wakuu wa kuwatumia wanamichezo au wasanii kwa faida zao. 
Mabondia au wanamichezo tuboreshewe maeneo yetu ya michezo ikiwemo katika vilabu vyetu na maeneo ya mazoezi, vifaa viongezwe ikiwezekana kodi ya vifaa vya michezo ipunguzwe ili viwe vingi nchini mabondia wasibabaike na vya kuazima au kuangalia katika tv vifaa nya wenzetu. 
Serikali iwajali mabondia, isaidie kudhamini semina za walimu wa ngumi ili wawaongoze vema vijana wao.magym ya makusudi yajengwe na maeneo ya wazi wasigawane wenye pesa na viongozi kwa faida zao  wajenge sehemu za michezo ya ndani(indoor), na kama pia itatumika njia ya kutoa madarasa matupu katika mashule yetu kwa ajili ya kutuachia sehemu ya mazoezi ya jioni itasaidia sana kukuza mchezo na walimu wenye taaluma kufundisha vizuri kuliko mabondia kufundishana vichochoroni na kutokuwa na nidhamu ya mchezo wala maisha
Na  IBRAHIM ABBAS KAMWE
manager and boxing trainer of  Bigright boxing
Local Promoter via Bigright Promotion
Mwananyamala

Dar es salaam

No comments:

Post a Comment