Shirika la Afya Muhimbili liliingia mkataba wa pango na REGENT STORE mnamo mwaka 1987 ambapo
katika mkataba huo makubaliano yalikuwa kwa REGENT STORE kujenga jengo ili litumike kuendesha
biashara ya SUPERMARKET katika eneo la Hospitali kwa ajili ya mahitaji ya wagonjwa pamoja na wafanyakazi.
Mkataba huo ulikuwa wa miaka mitano yaani kuanzia mwaka 1987 hadi mwaka 1992 ambapo
REGENT STORE alitakiwa kuwa ameishajenga jengo husika pamoja na kuendesha biashara ya
SUPERMARKET katika hilo jengo kwa kipindi cha miaka mitano na kukabidhi jengo kwa Hospitali.
Kilichotokea:
Hata hivyo, baada ya miaka hiyo mitano kuisha, REGENT STORE hakukabidhi jengo hilo
kwa Hospitali kwa mujibu wa mkataba kwa madai kuwa alikuwa hajarudisha gharama zake za ujenzi.
Kutokana na madai hayo kuwa alikuwa hajarudisha gharama zake za ujenzi, Hospitali ilikubali
kumwongezea muda wa miaka mitatu kuanzia 1992 hadi 1995.
Pamoja na Hospitali kumwongenzea miaka mitatu, ilipoisha miaka hiyo mitatu, REGENT STORE
hakuonesha nia ya kukabidhi jengo kwa Hospitali, na badala yake aliendelea kulitumia bila ya
mkataba wa aina yoyote na bila kukubali kukaa mezani kuzungumza na kutatua suala hilo.
REGENT STORE aliamua kuendelea kutumia jengo hilo kinyume na taratibu na sheria za nchi
kwa kuwa mkataba ulikuwa umeisha na nyongeza ya muda aliopewa pia ilikuwa imeisha.
Mgawanyo wa Mali na 1995-2000
Kama mnakumbuka katika kipindi cha mwaka 1995 hadi 2000 kulikuwa na mchakato wa
kulivunja lililokuwa Shirika la Afya Muhimbili (MMC) ambalo kwa wakati huo lilijumuisha
Hospitali pamoja na Chuo Kikuu cha Tiba. Zoezi ya kulivunja Shirika la afya Muhimbili lilienda
sambamba na kufanya mgawanyo wa mali na madeni ya shirika hilo, na kutokana na
mchakato wa mgawanyo kuendelea suala la kufuatilia kuchukua jengo lililokuwa linakaliwa
na REGENT STORE lilisimama kusubiri mgawanyo ukamilike ili aliyegawiwa eneo hilo ndio afuatilie.
Baada ya mchakato huo kukamilika, Hospitali ya Taifa Muhimbili iliundwa na kupewa hadhi ya
kuwa shirika la umma kwa mjibu wa Sheria ya Bunge Namba 5 ya Mwaka 2000.
Kwa bahati nzuri pia, katika mchatako huo wa kuligawa Shirika la Afya Muhimbili uliojumuisha
mgawanyo wa mali na madeni, jengo hilo la SUPER MARKET ilipewa Hospitali ya Taifa Muhimbili
kama inavyoonekana katika Gazeti la Serikali No. 62 ya 2007.
Hatua iliofuata:
Kufuatiwa hatua hiyo, Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Mwanasheria wake ilimwandikia
barua ya notisi yenye Kumb. CK/GC/2005/I/II/466 ya tarehe 26, Machi 2005 ikimtaka REGENT
STORE akabidhi jengo kwa Hospitali katika kipindi cha siku 14 na kwamba kushindwa kufanya hivyo kutapelekea kuchukuliwa hatua za kisheria.
Ndugu Wanahabari na Wananchi kwa Ujumla:
Baada ya kupokea barua hiyo, REGENT STORE aliamua kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kitengo cha Ardhi na kufungua kesi dhidi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo ilisajiliwa kama Land Case No. 53 ya mwaka 2005.
Katika kesi hiyo, REGENT STORE alikuwa akiomba pamoja na mambo mengine;
Amri ya Mahakama kuwa notisi aliyopewa ya kuondoka katika jengo hilo ni kinyume na sheria;
Aliomba Amri ya Mahakama kurekebisha mkataba ili aendelee kuwa mpangaji halali na aliomba pia
Amri ya kudumu ya Mahakama kuizuia Hospitali ya Taifa Muhimbili kumwondoa REGENT STORE katika jengo hilo hadi pale mkataba utakaporekebishwa.
Mchakato wa Mahakamani:
Kesi hii imekuwa Mahakamani kwa kipindi cha miaka nane tangu mwaka 2005 na hatimaye tarehe
20 Agosti, 2013, Mahakama Kuu imetoa HUKUMU ambapo maombi yote ya REGENT STORE
yametupiliwa mbali na REGENT STORE ameamuriwa kulipa gharama za kesi na kutoka katika jengo mara moja.
Utekeleza wa HUKUMU utaendelea kwa mujibu wa sheria ili Hospitali ya Taifa Muhimbili
ipate matunda ya hukumu ambayo ni haki ya kuendelea kumiliki MALI YAKE.
TUNAPENDA KUTOA SHUKRANI KWA MAHAKAMA KWA KUSIKILIZA KESI HII NA KUTENDA HAKI KWA KILA UPANDE.
nimesoma kwa makini mfululizo wote, lakini nimeshangaa kwanini kesi ilichukua muda wote huo wa miaka minane hali ya kuwa kila kitu kilikuwa kinaeleweka, kwa maana ya mkataba na minutes za makubaliano kati ya mwenye mali na mpangaji. ninachofikiria kulikuwa na mkono wa watu toka muhimbili walikuwa wana masilahi yao binafsi na mpangaji wa eneo hilo lakini pia mahakama zetu ziwe zinashughulikia kwa umakini hizi kesi, kwani kwa miaka yote hiyo ya kesi na ile mingine kabla ya kesi kama ndio ingekuwa muhimbili wanapata faida na eneo hilo wangekuwa wapi au wangekuwa wamepata faida kwa kiasi gani? yangu ni hayo ahsante naomba kuwasilisha ......
ReplyDelete