Mhe. Waziri Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiingia rasmi katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo mjini Dar es Salaam. Kulia ni Mhe. Balozi Rajabu Gamaha, Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mhe. Waziri Membe akiwa katika mazungumzo na Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mhe. Jaji Warioba akimkaribisha Mhe Waziri Membe wakati wa mazungumzo yao kuhusu uraia wa nchi mbili.
Mhe. Waziri Membe akielezea kuhusu suala la uraia wa nchi mbili.
Mhe. Jaji Warioba akiwa na Dkt. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Tume ya Katiba, Katibu wa Tume ya Katiba na Naibu Katibu Mkuu wa Tume ya Katiba.
Balozi Bertha Semu-Somi (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora, Bw. James Lugaganya, Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango na Bi. Naomi Zegezege, Afisa wa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakisikiliza kwa makini mazungumzo yanayoendelea.
Mhe. Jaji Warioba akielezea maoni ya Watanzania kuhusu uraia wa nchi mbili.
Kikao kikiendelea.
Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akielezea changamoto mbalimbali za wanadiaspora na uraia wa nchi mbili.
Dkt. Salim Ahmed Salim (kushoto), pamoja na Katibu wa Tume ya Katiba (katikati) na Naibu Katibu wa Tume ya Katiba wakimsikiliza Balozi Semu-Somi.
Mkutano ukiendelea.
Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba na Dkt. Salim Ahmed Salim wakisiliza kwa makini maoni ya Waziri Membe (hayupo pichani).
Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhani, Makamu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (katikati) akielezea jambo wakati Mhe. Jaji Warioba na Mhe Waziri Membe wakimsikiliza.
Mhe Waziri Membe akitoka katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba.
Membe alonga na Warioba kuhusu Uraia wa Nchi Mbili
Na Tagie Daisy Mwakawago na Fatma Salum
“Uwepo wa Diaspora ni lazima utambulike Kikatiba,” amesema Waziri Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Waziri Membe aliyasema hayo alipokutana na Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo katika Ofisi za Tume hiyo zilizopo mjini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijadili suala la uraia wa nchi mbili (dual citizenship) ambalo linapiganiwa kwa kiasi kikubwa na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora).
“Tumekuja kuwasilisha masuala muhimu mawili: moja, uwepo wa uraia wa nchi mbili katika Rasimu ya Katiba na pili, Katiba mpya iruhusu raia yoyote wa Tanzania aweze kuwa na uraia wa nchi nyingine pasipo kuukana uraia wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.
Alisema kuwa Wizara yake inatambua suala la uraia wa nchi mbili kuwa ni la msingi, ambalo halikugusiwa katika Rasimu ya Katiba iliyopo.
“Chimbuko la uraia wa nchi mbili lilitokana na wingi wa Watanzania walioko nje ya nchi ambao wanatafuta fursa ya kuwekeza na kuinua maendeleo ya nchi yao,” alisema Waziri Membe.
Aliongeza pia, “Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 inawatambua Watanzania hao na kutaka wapewe fursa ya kuwa na uraia wa nchi mbili katika kuinua maendeleo ya nchi.”
Watanzania hao wamekuwa wakikabiliana na matatizo kadhaa ambayo yanawanyima haki za msingi, kama vile afya, elimu na masuala ya ajira. “Kilio chao kimekuwa kero kubwa kwa vile wakati mwingine wanatibiwa kwa gharama kubwa sana ambazo hazilingani na kipato chao,” alisema Waziri Membe.
Aidha, changamoto hizo zimekuwa ni chanzo kikubwa cha kuwashawishi Watanzania hao kuchukua uraia wa nchi za kigeni ili kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii kama vile elimu na afya.
“Hivi sasa sheria yetu haimruhusu Mtanzania kuchukua uraia wa nchi mbili pasipo kuukana uraia wa nchi yake,” alisema Membe, na kufafanua kuwa “Ilani ya CCM inamuhamasisha Mtanzania huyo achangie maendeleo ya nchi yake kupitia uraia wa nchi mbili.”
Waziri Membe alisema kuwa Watanzania wakiwa nje wanakosa fursa za kazi zenye kipato kikubwa wasipokuwa na uraia wa nchi hiyo, jambo linalopelekea maisha magumu na kushindwa kujikimu na kuchangia kipato chochote kwa ndugu zao walioko nchini.
“Badala yake, unakuta Watanzania wananaswa na tamaa ya ‘kujilipua’ kwa kubadili uraia wa nchi nyingine zinazokubali uraia wa nchi mbili na kuachana na uraia wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.
Kwa upande wake, Mhe. Warioba alisema kuwa maoni hayo ya uraia wa nchi mbili yamekuwa yakijitokeza katika ukusanyaji wa maoni sehemu mbalimbali. Na kuongeza kuwa, hofu kubwa ya wananchi ni usalama wa nchi yao endapo uraia wa nchi mbili utaruhusiwa.
Mhe. Waziri Membe alikuwa ameambatana na Balozi Gamaha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora na Bw. James Lugaganya, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kwa upande wa Mhe. Warioba, alikuwepo Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhani, Makamu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Salim Ahmed Salim, Mjumbe wa Tume, pamoja na Katibu na Naibu Katibu wa Tume ya Mabadiliko.
Hakuna uraia wa ki-popo! Period!
ReplyDeleteHuu uraia wa nchi mbili ni kwa faida ya nani jamani? Kama si kwa faida ya watoto wa vigogo hao hao, hakuna mtoto wa mlalahoi aliyeko nje ya nchi. Mambo ya nje wanaongoza kuwa na watoto nje ya nchi. WATANZANIA Tuwe macho
ReplyDeleteSiyo kweli kuwa walio nje ya Tanzania ni watoto wa vigogo tu, huu ni upotoshaji wa Hoja pasipo fikra. Hata watoto wa familia za kawaida wapo nje na tena ndiyo wanafanya Kazi usiku na mchana kusaidia wadogo na wazazi wao nyumbani. Ni haki ya msingi kuwa na uraia pacha, hili swala haliepukiki daima. Kazi ya usalama ni wahusika wafanye wanalipwa na kodi zetu na wahukumiwe Kwa sheria ya nchi husika inapopaswa.
ReplyDeleteAcheni kuzungumza hivyo, si kila mtu anayeishi nje ni mtoto wa kigogo. Uraia wa nchi mbili ni mzuri kwa kila Mtanzania anaeishi nje na pia kwa familia zao nyumbani na hata kwa uchumi wa nchi wote tunafaidika. Tuache kuwa wabinafsi Watanzania.
ReplyDeleteMimi Binafsi ninaishi hapa Reading Uingereza, lakini baba yangu mzazi hata kazi alikuwa hana, mama yangu ni mama wa nyumbani.
ReplyDeleteKama alivyosema msemaji hapo juu , huu ni upotoshaji a makusudi, watu tuko huku kutafuta maisha, ili tusaidie ndugu na jamaa waliopo nyumbani.
Na kitakia kila la kheri kikao hicho hapo juu, matokeo yawe ni mema, na yaruhusu uraia wa nchi mbili
Wanu
Mkazi Reading UK