Kuna tishio kubwa dhidi ya Muungano wetu. Tishio hilo liko zaidi kwenye dhana kuliko
udhaifu wa dhamira ya Muungano wenyewe. Tishio hilo limedhihirika katika
kipindi hiki cha Mchakato wa Kuandaa Katiba Mpya ya nchi yetu.
Mjadala wa rasimu ya Katiba mpya umetawaliwa
kwa kiasi kikubwa na agenda ya Muungano.
Yamejitokeza makundi yenye mitazamo tofauti juu ya Muungano. Wako
wanaoutaka uendelee, wako wasioutaka, wako wanaotaka urekebishwe, ilihali kuna
kugongana kwa fikra. Kinachowaunganisha wote ni muungano huohuo wanaoujadili.
Mgongano wa maoni juu ya Muungano ni jambo
jema na la kujivunia. Mgongano huu unadhihirisha jinsi ambavyo Muungano uko hai
maana Muungano usiokuwa hai haujadiliwi. Mgongano huu wa fikra umetufunulia
kile ambacho hatukuwa tukikijua au tukikipuuza. Mara zote tumekuwa tukiamini
kuwa ni Wazanzibari pekee wenye ulalamishi juu ya Muungano, lakini mjadala
unavyokwenda tumeona pia kwamba hata wabara nao wana malalamiko yao. Hivyo, ni
sahihi kusema kuwa mjadala wa Muungano na mgongano wa fikra juu ya Muungano
wenyewe vinatupa fursa ya kuuboresha Muungano kuliko kuuvunja.
Sio sahihi kuogopa watu kuujadili Muungano
wao, wala hatuwezi kuujenga Muungano wenyewe kwa kuukinga dhidi ya mjadala.
Ikiwa sababu na dhamira ya kuungana ni njema, busara ile ile iliyopelekea
kuungana itaendelea kutawala na hatimaye kushinda jaribio lolote la kuuvunja.
Muungano wa hila ndio Muungano pekee ambao unapaswa kukingwa dhidi ya mjadala na
kuhojiwa. Muungano wetu sio Muungano wa hila, hivyo unapaswa kujadiliwa na
kuhojiwa. Wananchi wanayo haki ya kuutathmini ikiwa umetimiza malengo na
matarajio yao, maana tatizo laweza kuwa ni kubadilika kwa matarajio ya wananchi
kuliko kufeli kwa Muungano wenyewe.
Tatizo tulilo nalo ni kuwa wenye dhamana
ya kurithisha Muungano huu kwa vizazi vilivyofuatia wanagwaya kufanya hivyo.
Kugwaya kwao, kwa maoni yangu hakutokani na Muungano wenyewe kuwa wa hila, bali
udhaifu wa viongozi hao katika kuuelezea na kujenga hoja. Kuusimamia ukweli
daima huhitaji ujasiri, wakati mwingine, ujasiri pekee hautoshi, ujasiri huo
hutakiwa kuambatana na uadilifu. Maadam baadhi ya viongozi wetu wamekengeuka
kimaadili, wanakosa ujasiri wa kusema na kuusimamia ukweli wanaouamini. Huusema
ukweli huu pembeni tu lakini sio mbele ya jamii. Upungufu huu hufanya kusiwepo
na watetezi wa Muungano mbele ya jamii.
Silaumu hata kidogo wale wanaohoji
Muungano wetu haswa Muundo na umuhimu wake leo. Ukiwasikiliza wanazo hoja, tena
hoja nzuri na za kimantiki. Hili linadhihirisha kuwa hawana tatizo la uelewa,
na wakipatiwa hoja mbadala wanaweza kuelewa. Wengi wa hawa hawana taarifa za
kutosha juu ya Muungano wenyewe, hivyo wanauhoji kwa taarifa chache za
kuokoteza. Hata mimi nimewahi kuwa mhanga wa hilo hadi nilipofanikiwa kudadisi na
kupata taarifa zaidi kwa njia ya mapokeo, kwa kuwa nyingi ya taarifa hizi
hazijahifadhiwa kwenye maandiko. Haiyumkini, hali hii inatokana na utamaduni
wetu wa kutokuandika historia na matukio.
Kutokana na pengo la taarifa juu ya
Muungano, kumepelekea kuibuka kwa dhana mbalimbali nyingi zikiwa potofu. Uwepo
wa dhana potofu ni kielelezo cha ombwe, na kawaida, ombwe huvutia ghasia na mwangwi.
Katika mwangwi huo, dhana potofu hupata uhalali na huweza kuzaa nadharia.
Katika mjadala unaoendelea kuhusu Muungano hivi sasa, zipo walau dhana kumi
potofu ambazo zimetamalaki maoni ya wengi kuhusu Muungano. Dhana hizi potofu
zinaainishwa na kuchambuliwa katika aya zinazofutia.
1)
Tatizo ni Muundo na Suluhisho ni Serikali
Tatu
Imejengeka dhana kwa muda mrefu kwamba
tatizo la Muungano wetu ni Muundo wake wa Serikali mbili. Dhana hii inatuaminisha
kuwa mwarobaini wa tatizo hilo ni Serikali moja au tatu. Ajabu zaidi, Serikali
moja haipigiwi sana upatu kama serikali tatu.
Hapa tatizo linasemekana ni Tanzania Bara
kukosa Serikali yake. Wengine huenda mbele na kusema kwamba, kitendo cha
Serikali ya Muungano kuwa ni hiyo hiyo inayoshughulikia masuala ya Tanganyika,
kunaifanya Tanganyika kutumia rasilimali za Muungano kujinufaisha. Aidha, upande
mwingine unasema, Serikali ya Muungano kuwa ndio hiyo hiyo ya Tanganyika
kunainufaisha Zanzibar kwa kunufaika na mapato yatokanayo na uzalishaji ndani
ya Tanganyika. Hivyo, Serikali tatu zitasaidia kutenganisha shughuli za
Muungano na shughuli za Tanganyika na Zanzibar, hivyo, kuepusha kupunjana. Ni
wazi, kila upande una mashaka juu ya upande mwingine. Hivyo, msingi wa kutaka
Serikali tatu unatokana na kutokuaminiana tu. Kutokuaminiana huku hakutatuliwi
kwa kuongeza idadi ya Serikali.
Hoja ya Serikali tatu sio mpya, ilikuwapo
mezani wakati waasisi wa Muungano walipokubaliana kuwa na Serikali mbili badala
ya tatu au moja. Busara ya waasisi ilitawala katika kutafuta msawazo kati ya
gharama za uendeshaji wa Serikali ya Muungano na utaifa wa Mzanzibari. Muundo
wa Serikali tatu ulionekana ungekuwa wa gharama kubwa haswa kwa Serikali ya
Tanganyika ambayo ndio ingelazimika kubeba gharama kubwa. Hali kadhalika,
Serikali moja ilihofiwa ingeufuta utaifa wa mzanzibari kwa kuzingatia udogo wa
kisiwa chenyewe ikilinganishwa na Tanganyika na idadi ndogo ya watu ambayo
wakati huo ilikuwa inakadiriwa kuwa laki tatu. Utaifa wa mtanganyika na
utamaduni wake usingeweza kutishiwa kumezwa na Uzanzibari.
Maumbile ya Tanganyika na Zanzibar
hayajabadilika kwa miaka 49 kiasi cha kuifanya hoja ya Serikali tatu kuwa na
mashiko sasa. Tanganyika ina kilometa za mraba 942,553 na Zanzibar ina kilometa
za mraba 2650 (Eneo la Zanzibar linaingia mara 355 katika eneo la Tanganyika).
Tangayika na Zanzibar kwa pamoja zina jumla ya kilometa za mraba 945,203. Tanganyika ina idadi ya watu milioni
43,625,354 na Zanzibar ina watu 1,303,569 kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya 2012.
Tanganyika ina kaya milioni 9,109,150 na Zanzibar 253,608. Ujazo wa idadi ya
watu Zanzibar ni watu 530 kwa kilometa moja ya mraba wakati Tanganyika ni watu
49 kwa kilometa ya mraba. Takwimu hizi zingali zinahalalisha hoja ya Serikali
mbili ya Waasisi wa Muungano.
Tukienda na maelezo aliyotoa Mheshimiwa Jaji
Warioba kuwa gharama za kuendesha mambo saba ya muungano yanayopendekezwa katika
mfumo wa Serikali ya tatu ni Trilioni tatu, hoja ya serikali mbili inaimarika.
Tukiwa na Serikali tatu, mantiki itataka nchi washirika wa Muungano waongeze
michango ya gharama za uendeshaji wa Serikali hiyo ya tatu. Aidha, kutokana na
ukweli kuwa Serikali ya Tatu inazaliwa katika mazingira ya kutoaminiana, hisia
mbaya na dhamira ovu, utayari wa kila upande kuchangia gharama utabeba hulka
hizo hizo. Bajeti ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ni shilingi Trilioni
18.2 na bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa 2013/2014 ni shilingi
bilioni 658.5. Ikiwa tutaondoa masuala ya Muungano, bajeti ya Tanganyika
itakuwa ni Trilioni 15.2.
Ndani ya mfumo wa Serikali mbili, kuna
unafuu mkubwa wa gharama kwa kuwa gharama za kiuendeshaji zinapungua kwa sababu
Serikali ya Muungano kwa kutumia nguvu kazi na vitendea kazi hivyo hivyo
inatekeleza pia shughuli za Tanganyika. Katika mfumo wa Serikali tatu, nachelea
kuwa gharama zitakuwa zaidi ya trilioni tatu zinazosemwa na Jaji Warioba kwa
kuwa hatutaweza kukwepa gharama mpya za kiuendeshaji za Serikali ya muungano
inayojitegemea kama vile majengo, watumishi vitendea kazi nk. Ongezeko hilo
maana yake ni kodi zaidi na michango zaidi kutoka nchi washirika. Serikali tatu
ni neema kwa wanasiasa maana itapanua vyeo lakini msiba kwa wananchi maana
watalazimika kuigharania kwa kodi zaidi.
Takwimu hapo juu zinashindwa kunishawishi
kuwa mantiki ya Serikali mbili kama ilivyokubaliwa na waasisi wetu imepitwa na
wakati. Sioni ni kwa vipi, Muundo wa Serikali tatu leo hii utalinda utaifa wa
Zanzibar dhidi ya hofu ya kumezwa huku ikipunguza gharama za uendeshaji wa
Muungano wenyewe. Utaifa wa Tanganyika haujatoweka kutokana na ukubwa wake na
tishio la Uzanzibar kutoweka bado lipo ikiwa tutakuwa na Serikali moja kama
takwimu za idadi ya watu zinavyoonyesha.
Ikiwa kweli tunayo dhamira ya kuendelea na
Muungano, basi njia yenye uhalisia ni Serikali mbili sio tatu wala moja.
Mazingira yaliyopelekea Serikali mbili yangali hayajabadilika hata sasa. Ni
kweli Muundo wa Serikali mbili una changamoto zake, lakini changamoto hizo
zinatokana na mfumo zaidi kuliko Muundo, na kuwa tunaweza kurekebisha mfumo
ndani ya Muundo uliopo. Changamoto za Muundo wa Serikali mbili zinahimilika
kuliko changamoto za Serikali tatu au moja zitakazoleta changamoto za gharama
na utaifa wa Uzanzibari. Hivyo, nachelea kusema kuwa dhana kuwa tatizo ni muundo
wa Serikali mbili na kwamba Serikali tatu ni suluhisho ni dhana potofu.
2)
Zanzibar inanyonywa, Tanganyika inafaidi
kuliko Zanzibar (na kinyume chake)
Ipo dhana nyingine kuwa Zanzibar
inanyonywa ndani ya Muungano na Tanganyika inafaidi ndani ya Muungano.
Kinachostaajabisha, pia wapo wanaosema Tanganyika inanyonywa na Zanzibar
inafaidi. Zote hizi ni hoja ambazo msingi wake ni husuda, na husuda haiondolewi
na idadi ya Serikali. Watu wenye husuda wataendelea kuwa na husuda hiyo ndani
ya Serikali moja au tatu.
Wenye kuunga mkono dhana ya Zanzibar
kunufaika kushinda Tanganyika wanatumia mifano ya haki ya kumiliki ardhi,
makazi na mgawanyo wa madaraka wanaoupata wananchi wa Zanzibar. Ni kweli kuwa
wazanzibari wengi (inasadikiwa si chini ya laki nne) wanaishi bara na
wanamiliki ardhi na nyumba. Aidha, wazanzibari wanashikilia nyadhifa kwenye
Wizara na Sekta zisizo za Muungano kama afya na mawasiliano. Ni kweli pia
watanganyika nao wanashikilia nyadhifa nyingi kwenye Wizara na Sekta za
Muungano, na watanganyika wanashikilia ajira nyingi kwenye sekta ya utalii
Zanzibar. Isitoshe, wafanyabiashara wa
Tanganyika wanauza bidhaa nyingi Zanzibar.
Kilicho dhahiri ni kuwa hakuna upande wa Muungano
ambao haufaidiki kabisa kutokana na uwepo wa Muungano. Sina mashaka, manufaa
hayo yaweza kupishana kutokana na maumbile yenyewe ya nchi hizi mbili.
Mathalani, watanganyika hawana tatizo kubwa la ardhi kiasi cha kuathirika kwa
kukosa ardhi Zanzibar. Kupata ardhi ya makazi Zanzibar yaweza kuwa tabu kwa
mtanganyika lakini sio ardhi ya uwekezaji, maana hata wawekezaji kutoka nje
hupata ardhi Zanzibar. Tukirejea kwenye takwimu za ujazo wa watu Zanzibar kwa
kilometa ya mraba, ni dhahiri kuwa tayari Zanzibar kuna tatizo la ardhi, sio tu
kwa mbara, hata kwa mzanzibari mwenyewe. Hivyo, dhana ya kuwa upande mmoja
unanufaika na mwingine haunufaiki ni dhana potofu. Pande zote zinanufaika,
pengine, upo uwezekano wa kunufaika zaidi Ikiwa tutarekebisha mifumo ndani ya
muundo wa Serikali mbili zilizopo.
3)
Nje ya Muungano Zanzibar itanufaika zaidi
na Tanganyika itatua mzigo
Ipo dhana kuwa nje ya Muungano, Zanzibar
itanufaika zaidi na Tanganyika itatua mzigo. Wenye kujenga dhana hii, hujenga hoja
kuwa Zanzibar itaweza kujenga mashirikiano yake yenyewe na dunia na nchi za
kiarabu na kiislamu zenye uchumi imara. Wengine huzungumzia Zanzibar kuja kuwa
bandari huru kama ilivyo Singapore. Tanganyika au Muungano huonekana kuwa ni
kikwazo kwa Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC). Tunazidi
kuaminishwa kuwa kwa kujiunga OIC, Zanzibar itajikwamua na umasikini.
Waumini wa Tanganyika wanatuaminisha
kwamba nje ya Muungano, Tanganyika itakuwa imetua mzigo. Hawa wanataka tuamini
kuwa Zanzibar inaielemea Tanganyika na kwamba gharama za kuendesha muungano
zingeliweza kutumika kwenye miradi ya maendeleo. Wanatuaminisha kuwa Tanganyika
imekuwa ikibeba gharama hizi peke yake na kwamba Tanganyika itaendelea kwa kasi
sana baada ya kuachana na Zanzibar.
Dhana hii kuwa Zanzibar itanufaika nje ya
Muungano ni dhana muflisi na potofu. Hoja ya kuwa kwa kujiunga na OIC Zanzibar
itaneemeka ni ya kusadikika. Visiwa vya Comoro vina ukubwa wa kilometa za mraba
2170, vina idadi ya watu wapatao 984,500 na ni mwanachama wa OIC na Jumuiya ya
Kiarabu (Arab League). Visiwa vya Comoro
vingali masikini kuliko Zanzibar na ukuaji wake wa uchumi kwa mwaka 2012
ulikuwa ni asilimia 2.7. Tunachokipata hapa ni kuwa sio OIC wala Arab League
yenyewe inayoweza kubadili uchumi na maisha ya mzanzibari.
Uchumi wa Zanzibar kama ilivyo Comoro kwa
muda mrefu umefifishwa na migogoro ya kisiasa. Zanzibar ina tabaka kubwa la
wanasiasa na utawala kuliko uwezo wa uchumi kuhimili, hivyo migogoro ya kisiasa
haiepukiki. Nje ya Muungano, wanasiasa wengi wa Zanzibar watakosa ajira, hawa
watajiunga na siasa za ndani za Zanzibar, hapatatosha. Migogoro ya kisiasa
baina ya visiwa huko Comoro ina athari kubwa kiuchumi kuliko migogoro ya
kisiasa baina ya Unguja na Pemba kutokana na siasa hizo kumezwa na siasa za
Muungano.
Isitoshe, nje ya Muungano, Tanganyika na
Zanzibar zote kwa pamoja zitalazimika kubeba mzigo wa kugharamia ulinzi na
usalama pamoja na uendeshaji wa Ofisi za Balozi nje ya nchi. Gharama hizi zikigawanywa
kwa kila nchi kuendesha mambo haya yenyewe ni kubwa kwa kila nchi. Pengine
tunapofushwa na gharama za kifedha pekee na kuacha kuangalia gharama za
kiusalama. Usalama wa Zanzibar na Tanganyika unategemeana sana na Muungano ni
chombo muhimu cha kuhakikisha usalama wa pande zote mbili. Tanganyika
itagharimika sana kiusalama nje ya Muungano kuliko tunavyofikiria, hususan
katika kipindi ambacho Tanganyika inatarajia kuvuna gesi katika pwani ya bahari
ya Hindi. Mahasimu wa Tanganyika watakuwa wamepata upenyo mzuri wa kutimiza
azma yao ya kuidhuru Tanganyika, au mahasimu wa Zanzibar kuidhuru Zanzibar.
Hivyo, ustawi wa Zanzibar na Tanganyika unategemeana, wala sio kweli kuwa yuko
mmoja anayembeba mwenzake au atakayekuwa salama zaidi nje ya Muungano.
4)
Wananchi wengi wa Zanzibar hawataki
Muungano na Wananchi wengi wa Tanganyika hawataki Muungano
Wanasiasa wetu wa pande mbili wasioupenda
Muungano kwa sababu wanazozijua wao, wanatuaminisha kwamba Muungano umechokwa
na Watanzania wa pande zote mbili. Wanasiasa
hawa hawa walifanikiwa kutushawishi kuwa Watanzania wengi wanataka Katiba mpya.
Takwimu ya waliojitokeza mbele ya Tume kutoa maoni juu ya Katiba mpya ni za
kushtua. Katika nchi ya wapiga kura wanaokadiriwa kufikia milioni 20 kwa mujibu
wa Tume ya Uchaguzi, waliojitokeza kutoa maoni yao hawakufika laki tano. Aidha,
mwamko mdogo ulioonyeshwa katika ushiriki wa mabaraza ya Katiba unaacha maswali
mengi.
Wanasiasa na wanaharakati hutumia
shinikizo kama mojawapo ya nyenzo kufikia malengo yao. Mojawapo ya nyenzo
wanayoipenda sana ni kutumia umma kuhalalisha matakwa yao. Kwa sababu hiyo
haishangazi kwa wanasiasa kupenda kutumia njia ya maandamano na lugha ya
‘wingi’ katika kujenga hoja zao. Kwa mbinu hii, lugha ya ‘wingi’ imetumika
kutuaminisha kwamba wazanzibari wengi hawautaki muungano, hali kadhalika,
watanganyika wengi hawautaki muungano.
Lugha ya jumla imetumika pia kujenga dhana
kuwa wanachama wa CUF wote hawaupendi muungano, wapemba wote ni CUF na waunguja
wote ni CCM na wanaupenda Muungano tena wa Serikali mbili. Hali kadhalika,
tunaaminishwa kuwa wanachama wa CHADEMA wote wanapenda Serikali tatu na wana
CCM wanapenda Serikali mbili. Katika kunogesha dhana yenyewe, inajengwa hoja
kwamba, iwapo kura ya maoni ya kutaka au kutotaka muungano itapigwa, basi
haitapatikana theluthi mbili Zanzibar, kwa kuwa katika matokeo ya uchaguzi
uliopita, hakuna chama kilichopata theluthi mbili ya kura.
Wanaoshabikia dhana hii wanawachukulia
wananchi kama misukule. Wanaamini wananchi watapiga kura kwa mlinganyo ule ule
hata kama jambo ambalo wanalolipigia kura limebadilika. Kwa kutumia dhana hii,
tunakatishwa tamaa ya kuutafuta ukweli kwa kuwapa fursa wananchi ya kuchagua
iwapo wanautaka muungano au hawautaki, wanataka Serikali mbili au tatu. Hata
Tume ya Katiba imetuingiza katika mkenge huu kwa kutuambia kuwa ‘wengi’
waliohojiwa wametaka Serikali tatu. Hatujaambiwa waliotaka serikali mbili
wangapi na waliotaka moja wangapi. Tunatakiwa tukubaliane tu kuwa wengi
hawautaki muungano pande zote mbili.
Dhana hii haiakisi hali halisi.
Wazanzibari na Watanganyika wameoleana, kuzaliana na wengine wanaendesha
biashara kwa ubia. Ukisikiliza Sauti ya Radio Zanzibar katika taarifa za vifo
utastaajabu kuwa karibu kila msiba una ndugu na jamaa bara tena sio Dar es
Salaam pekee. Ukikaa katika bandari ya Dar es Salaam au Zanzibar utashangazwa
na idadi ya wasafiri kutoka pande zote mbili za mbili za Muungano. Wananchi wa
kawaida wa pande zote mbili hawana tatizo na muungano maana hauathiri maisha
yao ya kila siku zaidi ya kuyarahisisha. Hawa, haswa wafanyabiashara, wanazo
kero zinazohusiana na mifumo ya kodi zaidi kuliko muundo wa muungano, au muungano
wenyewe. Hapana shaka, watakapoulizwa juu ya uwepo au kutokuwepo kwa muungano,
maamuzi yao yatakuwa tofauti, kwa kuwa hatma ya muungano ina athari kubwa sana
kwao. Ni vyema tukaruhusu kura ya maoni juu ya uwepo au kutokuwepo kwa
muungano. Kura hii ya maoni, itatukwamua kutoka kwenye tope la wanasiasa, ambao
ndio kero kuu ya muungano.
5)
Muungano umepitwa na wakati
Waswahili husema, ukitaka kumuua mbwa mpe
jina baya. Ukimuita Mbwa Koko au Kichaa unapata uhalali wa kumuua. Ukimpa jina zuri
unamuhamishia sebuleni. Katika kutimiza azma yao, wale wasioupenda Muungano
hutoa dhana ya Muungano kupitwa na wakati. Kwao suala la Muungano huchukuliwa
kama tukio la kupita na sio suala la kudumu. Hivyo, tunatakiwa tuamini kuwa
muungano wetu umepitwa na wakati, na ulikuwa na mantiki tu wakati ule wa vita
baridi na umajumui wa Afrika (Pan-Africanism). Zama hizo zimepita na hivyo
Muungano nao umepitwa na wakati.
Hoja hii nayo inajibika. Muungano wowote
unaingiwa kwa lengo la kuwa Muungano wa kudumu. Chini ya Sheria za Kimataifa,
uko msingi kuwa nchi huingia Mkataba kwa dhamira njema ya kuutekeleza. Hivyo, Muungano wetu kama ilivyo miungano
mingine ikiwemo ule wa Marekani na Ujerumani, inadhamiriwa kuwa ya kudumu.
Tukirudi kwenye hoja yenyewe, Muungano
wetu haujapitwa na wakati, labda baadhi ya viongozi wetu wamepitwa na wakati.
Taifa letu linapita katika dunia ya utandawazi. Katika dunia ya utandawazi, nchi
zinachukuliwa kuwa ni masoko. Muelekeo wa dunia ni kuunganisha nchi kuelekea
kwenye utaifa mkubwa zaidi na na sio kinyuke chake. Nchi ndogo zina nafasi
finyu katika dunia ya utandawazi hususan pale nchi zenyewe ndogo zinapokuwa
masikini. Nchi za Ulaya zinafanyia kazi wazo la kuungana kuwa nchi moja chini
ya Umoja wa Ulaya. Nchi ya Ubeligiji yenye pato kubwa la uchumi kuliko jumla ya
nchi zote kusini mwa jangwa la Sahara inajiunga na nchi nyingine za Ulaya kujenga
utaifa mkubwa kukabiliana na utandawazi. Aidha, tunaona jinsi ambavyo nchi
zenye watu wengi kama India, China na Brazil zinavyotikisa katika utandawazi
kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu. Ni kichekesho kuwa sisi nchi masikini
tunafanya kinyume chake. Tunadanganyana kuwa tunayo fursa ya kuneemeka zaidi
katika utandawazi tunapokuwa nje ya Muungano. Ukweli ni kuwa hatujiimarishi kwa
kuwa nje ya Muungano bali tunajidhoofisha. Muungano unahitajika zaidi katika
dunia ya utandawazi kuliko tunavyojifariji.
6)
“Sisi” ni Muhimu Kuliko “Wao”
Tunalo tatizo la kimtazamo miongoni mwa
watanganyika na wazanzibari ambalo kwa maoni yangu msingi wake ni ubaguzi. Iko
dhana ya ‘sisi’ na ‘wao’. Wananchi wa kila upande wamepandikizwa mitazamo dhidi
ya wenzao wa upande mwingine. Baadhi ya Wabara huwaona wazanzibari kama watu
goigoi na huwaita ‘yakhe’ au ‘mdebwedo’. Hali kadhalika baadhi ya wazanzibari
huwaona wabara kama watu wa shamba na wasio staarabika, huwaita ‘machogo’.
Mitazamo hii imeathiri kwa kiasi kikubwa mahusiano baina ya wananchi wetu,
lakini baya zaidi, imetulewesha kwa kutupa majivuno kuwa ‘sisi’ ni bora kuliko
‘wao’.
Athari kubwa itokanayo ni mitazamo hiyo ni
kujenga kutokuaminiana. Wabara wanadhani wazanzibari wote ni wazembe, hawana
uwezo wa kiakili. Wazanzibari hali kadhalika wanawaona wabara kama watu
wasiostaarabika, wenye majivuno na kupenda kuburuza. Matokeo yake, mitazamo hii
huambukiza vizazi na vizazi.
Wananchi wa Zanzibari na Tanganyika
waliopata bahati ya ama kuishi au kusoma na wenzao wa upande wa pili,
watakubaliana nami kuwa mitazamo hii ni potofu. Binafsi, nimesoma na
wazanzibari na kufanya kazi na wazanzibari wenye uwezo mkubwa sana kushinda
wabara. Kama ilivyo kwa wabara, tunao wazanzibari wengi nje ya nchi kwenye
mashirika ya kimataifa wanaotujengea heshima kubwa.
Changamoto ya kimfumo iliyopo ni kwamba,
kutokana na wingi wa wabara, wengi wao hujikuta hawajawahi kufika wala kuishi
Zanzibar, Isitoshe, hawajawahi kusoma ama kuishi na wazanzibari. Hivyo,
wanasiasa hutumia mwanya huo kupandikiza mitazamo ya ‘sisi’ na ‘wao’ katika
kutafuta kujijenga kisiasa. Maoni yangu ni kuwa, ‘sisi’ sio bora kuliko ‘wao’,
wala ‘wao’ sio bora kushinda ‘sisi’. Wazanzibari, kama walivyo watanganyika
wamelifia taifa letu la Tanzania katika kulinda na kutetea heshima na uhuru
wake. Watanganyika na Wazanzibar wamekufa katika vita vya Uganda wakipigania
taifa letu. Majuzi, watanganyika na mzanzibari wamekufa huko Darfur wakiwa
katika shughuli za kulinda amani. Maadui waliowaua wanajeshi wetu kule Darfur
hawakutofautisha mzanzibari wala mbara, waliua wanajeshi wa Tanzania katika jeshi
la kulinda amani la Umoja wa Mataifa. Haya yanayotuunganisha, ni muhimu zaidi,
kuliko yale yanayotugawa.
Mwalimu Nyerere katika hotuba yake ya ‘Nyufa’
aliyoitoa 1995 alionya juu ya dhana hii ya ‘sisi’ na ‘wao’. Katika hotuba ile,
alikumbusha kuwa kinatochufanya tuwe ‘sisi’ ni kutokana na ‘wao’ kuwepo.
Akaonya, Ikiwa ‘wao’ hawapo, basi hata ‘sisi’ hatupo. Sote kwa pamoja ni bora
zaidi kuliko ‘sisi’ au ‘wao’.
7)
Kero za Muungano lazima Zipate Majawabu ya
Kudumu na Ziondoke, Manung’uniko ni kufeli kwa Muungano
Muungano wetu wa miaka 49 unazo changamoto
zake. Changamoto hizi zimebatizwa jina la ‘kero’. Sidhani kama ‘kero’ ni neno
sahihi, na nachelea kama neno ‘kero’ lilizuka tu pasipo kuwa na lengo nyuma
yake. Kwa vyovyote vile, aliyezibatiza changamoto za muungano jina la ‘kero’
amefanikiwa sana. Sisi wengine huamini ‘maneno huumba’. Jina hili
limeshakubalika na sasa changamoto zinaitwa ‘kero’, yaani mambo yanayokera.
Dhana tunayoipata hapa ni kuwa utatuzi wa
‘kero’ ni tofauti na utatuzi wa changamoto. Tofauti yenyewe ni ya kimtazamo.
Changamoto ni vikwazo vya kutatulika, wakati kero ni vikwazo vilivyoshindikana.
Kero zinapaswa kuondoshwa zote, na kama haziondoshwi, basi huwa ni sugu, na
dawa yake ni kuvunja muungano wenyewe. Tunaaminishwa kuwa sio sahihi kuishi na
kero kama hazitatuliki, na kuwa, muungano uliojaa kero ni muungano mfu. Kero
hizi hudaiwa kwamba zinatokana na muundo wa muungano wenyewe. Suluhisho
linalotolewa ni aidha kuwa na serikali tatu ili ‘kuunusuru’ muungano, kinyume
na hivyo, ni muungano kuvunjika.
Tunadanganywa kuwa tunachojaribu kunusuru
ni 'muungano'. Tunachotakiwa kunusuru ni 'utaifa' sio 'muungano', muungano ndio
wenye kunusuru utaifa wetu, sio kinyume chake. Muungano wetu ni muungano
unaoishi. Muungano unaoishi hupita katika nyakati na mazingira tofauti ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii katika maisha yake. Watu hubadilika, matarajio
hubadilika na hali kadhalika mitazamo hubadilika. Changamoto za muungano ni kielelezo
cha uhai wa muungano wenyewe na sio vinginevyo. Wala hakuna muungano duniani
usio kuwa na changamoto, wenye kufurahisha watu wote, wakati wote. Changamoto
za muungano ni fursa ya kuuimarisha muungano na sio kuuvunja. Huko tuendako
tutarajie kujitokeza kwa changamoto nyingine hata tutakapofanikiwa kuzikabili
zilizopo leo. Hivyo, dhana ya kuona changamoto za muungano ni kero na maana
yake ni kufeli kwa muungano ni dhana potofu.
Changamoto za muungano ni kipimo cha
uongozi. Changamoto hujitokeza ili zitatuliwe. Zisipotatuliwa ni udhaifu wa
kiuongozi. Sina budi hapa kuwapongeza viongozi waliotangulia kwa kukabiliana na
Changamoto hizi kila zilipoibuka. Uhodari wao ndio unaoufanya muungano wetu leo
utimize miaka 49 na kuwa muungano pekee ulioweza kudumu katika Afrika. Kwa
uongozi wao tumevuka jaribio la kuvunja muungano mwaka 1984, ambapo Mhe. Seif
Sharrif Hamad, wakati ule alionyesha uzalendo wa kutukuka kulinda muungano wetu
wa Serikali mbili (leo kageuka). Aidha tumevuka jaribio la kuvunjika kwa Muungano
mwaka 1992-93 kufuatia Zanzibar kujiunga na OIC na Wabunge 55 wa Tanzania (G55)
kudai Serikali ya Tanganyika. Tukavuka pia majaribio kadhaa kama hayo ndani ya
mfumo wa vyama vingi hadi sasa.
Katika kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya
Tanzania, Mwalimu Nyerere alisema, “Maadamu matatizo halisi ya muungano
hayazungumzwi wala hayashughulikiwi, watu wenye nia mbaya, wa bara na visiwani,
wanaopenda kutumia hali hiyo kuivunja nchi yetu wanaendelea kufanya hivyo. Na
wale wa huku na huku, wanachocheana kama mifukuto ya shetani. Na hiyo
inawafanya hata watu wasio na nia mbaya, ila kwa ujinga tu, waamini kuwa inafaa
wote tushiriki na tujiandae kuivunja Tanzania tusije tukashtukia kuwa Tanzania
imevunjika na tumeachwa kwenye mataa! Anayedhani viongozi wetu ni wajinga yafaa
achunguze akili zake! Wanajua wafanyalo”
Changamoto nyingi za Muungano zinaweza
kutatuliwa chini ya muundo wa Serikali mbili kama ambavyo tumefanikiwa siku
zote. Pengine, kilichotakiwa ni ubunifu tu wa mfumo mpya ya kutatua kero hizo
kutokana na mifumo ya zamani kupitwa na wakati. Katika hili, ninayo kila sababu
ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa
Mohamed Ally Shein kwa ubunifu wao. Nahodha mzuri hupimwa kwa uwezo wake wa kuhihimili
chombo wakati wa dhoruba sio kukiendesha chombo wakati wa utulivu wa bahari. Chini ya uongozi wao, umeanzishwa mfumo rasmi wa
kukutanisha Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar chini ya uenyekiti wa
Makamu wa Rais kushughulikia changamoto hizo. Tangu kuanza kwa mfumo huo, changamoto
13 zimeshajadiliwa, changamoto 6 zimeshapatiwa ufumbuzi, hoja tatu ziko katika
hatua za mwisho za kutatuliwa na hoja nne zinaendeea kushughulikiwa. Tokea
mwaka 2011 hadi Aprili 2013, vikao 9 baina ya Serikali mbili vimekaa katika
ngazi ya makatibu wakuu na mawaziri.
Kilicho dhahiri ni kuwa, changamoto nyingi
zilitokana na viongozi wa pande mbili kutokutana rasmi. Kutokana na kuzoeana,
mambo mengi yalikuwa yakimalizwa kwa mazungumzo baina ya viongozi wa ngazi za
juu. Tatizo la utaratibu huo wa kindugu, ni kushindwa kupima ufanisi na
kukosekana kwa mrejesho katika ngazi za chini ukiacha viongozi. Aidha, wakati
mwingine kwa sababu za kisiasa, viongozi walipenda kuhodhi mchakato huu na
taarifa zake. Pamoja na kwamba mfumo huo umetuvusha huko nyuma, kilicho wazi ni
kuwa sio mfumo endelevu. Yawezekana ulifanya kazi vizuri chini ya mfumo wa
Chama kimoja, lakini mazingira ya vyama vingi yanahitaji kurasimisha mfumo huu
ili kuwezesha wadau wote wa muungano ndani na nje ya Serikali kupata mrejesho,
na ikiwezekana kushirikishwa. Kinachostaajabisha, hili halizungumzwi,
kinachozungumzwa ni muundo tu. Baadhi ya wanasiasa wamechagua kutoyazungumzia
haya hadharani kwa kuwa yanakinzana na lengo lao la kuvunja muungano. Busara na
umakini unatutaka kusikiliza tu sio kile tunachoambiwa, bali pia na kile
tusichoambiwa na huyo anayetuambia
8)
Muungano wetu ni Batili na hauna Uhalali,
ni wa Ajabu
Wanasheria nao hawako nyuma katika mjadala
wa muungano na hatma yake. Baadhi ya Wanasheria wamehoji juu ya uhalali wa
muungano kisheria. Wamekwepa siku zote kujadili uhalali wa muungano kisiasa kwa
kujificha katika kile kinachoitwa uweledi. Mtazamo wa baadhi ya wanasheria
umejikita katika kuangalia mchakato uliozaa hati ya muungano na matokeo ya
mkataba huo. Mtazamo huo unachagiza dhana kuwa muungano wetu ni batili. Ubatili
huo unatokana na kukosekana unyoofu katika mtiririko wa matukio katika kuelekea
kufikiwa kwa Mkataba wa Muungano. Aidha, muungano wetu kutokufanana na miungano
iliyoko kwenye vitabu vya kisheria kunawakwaza wanasheria. Maana, miungano
iliyoko vitabuni ni mfumo wa muungano wa Serikali moja au mfumo wa majimbo wenye serikali kadhaa za
majimbo na moja ya muungano.
Wanasheria wengi wana matatizo makubwa ya
aina mbili; kwanza wanajiamini kuwa wanajua (wanajiita kimombo ‘learnerd’);
pili, jamii nayo imetokea kuamini kuwa wanasheria
wanajua. Wanasheria hawa hupenda kuwa na kauli ya mwisho kwenye kila jambo, na
hawapendi kukosolewa na mtu asiye mwanasheria. Kinyume na mtazamo huo wa
wanasheria, Muungano ni suala la dhamira kwanza, sheria baadae. Muungano
hauanzi na sheria bali huhitimishwa na sheria, wala sheria pekee haibatilishi
dhamira ya watu kuungana. Sheria yaweza kufa dhamira ikabaki. Watu ama nchi
haziungani kwa lengo la kutekeleza sheria, bali wanaungana kwa malengo ya kupanua maslahi ya kiuchumi au ya kiusalama au
ya ustawi. Sheria na Katiba zinatumika kulinda dhamira hiyo sio kuiumba. Hivyo,
Hati ya Muungano sio lengo, Hati ya Muungano ni matokeo. Hivyo, muungano wetu,
na muundo wake wa Serikali mbili haulazimiki kukidhi au kufanana na miungano
mingine kwenye vitabu, maana kila muungano huibuka katika nyakati, mazingira na
malengo tofuti.
Ufafanuzi mzuri juu ya dhana ya uhalali wa
Muungano imezungumziwa na Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha Uongozi wetu
na Hatma ya Tanzania. Bahati, mbaya Hayati Abeid Karume, hakuishi muda mrefu
kuweza kuacha maandiko, hivyo rejea kuhusu chimbuko la muungano zimetawaliwa na
kauli za Mwalimu Nyerere. Katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere alisema, “Tanzania
ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru. Nchi nyingine zote ni za
kurithi kutoka kwa wakoloni. Wako watanzania wa ajabu kabisa wanaosema kuwa
uamuzi huo, au vyombo vilivyotumiwa au njia iliyotumiwa, au vyote, havikuwa
halali. Hao hawana shaka na uhalali wa Tanganyika, ambayo iliunganishwa na
Wajerumani, na ikamegwa megwa na Waingereza na wenzao. Kwa hao, kama Rwanda na
Burundi na Tanganyika zisingetengwa na mabeberu, tukazirithi kama zilivyokuwa
chini ya Wajerumani, wasingeushuku uhalali wa nchi moja hiyo. Lakini kama baada
ya uhuru, Rwanda na Burundi na Tanganyika zingeamua kuungana ziwe nchi moja,
kwa utaratibu wowote ambao zingekubaliana, ‘wazalendo’ hawa wangesema muungano
huo sio halali.”
Katika aya inayofuatia, Mwalimu Nyerere
akaendelea kujenga hoja juu ya mtiririko wa matukio uliopelekea kufikiwa kwa
makubaliano ya nchi zetu kuungana. Alisema, “Hatukutafuta maoni ya watu kwa
njia ya demokrasia wanayoijua wao. Wajerumani na Waingereza walitafuta maoni ya
wazee wetu kwa mtutu wa bunduki! Hiyo ilikuwa halali. Nchi walizounda kwa njia
hizo zilikuwa halali. Tunatakiwa tujivunie utanganyika na uzanzibari
uliopatikana kwa njia hizo, lakini tuuonee haya Utanzania, tunda la uhuru wetu
wenyewe. Sikuamini kama wakoloni walifaulu kiasi hiki katika kuzinywesha
kasumba na kuzitawala akili za baadhi yetu!”
9)
Muungano na haswa Muundo wa Serikali Mbili
ni Sera ya CCM
Suala la Muundo wa Serikali mbili limekuwa
likihusishwa na CCM. Bahati mbaya, wana CCM nao wametokea kuamini kuwa suala
hili ni Sera yao. Kuunasibisha muundo wa Serikali mbili na CCM kunafanya wale
wengine wasiokubaliana na CCM kutokukubaliana pia kwenye suala la muundo wa
Serikali mbili. Matokeo yake, suala la muundo wa Serikali mbili linapoteza sura
ya utaifa, hivyo wanaopinga mfumo huo, wanaukataa wakati mwingine bila hata ya
kuuelewa na kuuchambua. Ukiondoa CCM hakuna Chama chochote kingine cha siasa
Tanzania kinachosimamia muundo wa Serikali mbili.
Muundo wa Serikali mbili kama
zitakavyokuwa Serikali tatu au moja sio mwarobaini wa Muungano. Muundo wa
Serikali mbili ulichaguliwa baada ya waasisi kujiridhisha kuwa katika mazingira
ya tofauti za kimaumbile za Tanganyika na Zanzibar, ni muundo wa Serikali mbili
tu ndio ungeweza kukidhi hitaji la unafuu wa gharama za uendeshaji na kinga
dhidi ya hatari ya utaifa wa mzanzibari kutoweka. Si muundo wa Serikali mbili
wala tatu ambao ulionyesha kuleta msawazo katika mahitaji hayo mawili wakati
huo na hata sasa. Hoja ya kuwa muundo huu ni wa CCM kwa kuwa ulifikiwa chini ya
vyama vya TANU na ASP ambavyo viliungana na kuzaa CCM ni hoja muflisi. TANU na
ASP ndio vyama vilivyokuwa madarakani wakati huo, na mrithi wao CCM kiko
madarakani hadi sasa. Ukweli huu haufanyi muundo huu kuwa wa CCM. Suala la
Muundo lafaa kuwa suala la Kikatiba ili vyama vyote viuheshimu.
Muundo wa Serikali mbili unalo chimbuko
lake. Haukutokana na nasibu bali tathmini na maamuzi yenye upeo wa hali ya juu.
Mfumo wa Serikali mbili waweza usiwe mfumo bora kushinda mingine duniani,
lakini ni bora kushinda mfumo wa Serikali tatu na moja katika mazingira ya
Tanzania. Hili pia limezungumziwa na Mwalimu Nyerere kwenye kitabu chake cha
Uongozi wetu na Hatma ya Tanganyika, alisema:
“Tanganyika na Zanzibar
zilipoamua kuungana na kuwa nchi moja, tungeweza kufuata mojawapo ya mifumo ya
kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na
ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na
Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali moja
ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania
uhuru na Umoja wa Afrika, hatukutaka tudhaniwe hata kwa makosa kwamba
tunaanzisha ubeberu. Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali moja. Shirikisho
la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar
ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya
Shirikisho; na Tanganyika ingefanya hivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba
mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha Serikali ya shirikisho. Kwa hiyo,
Tanganyika ingeendesha Serikali ya watu milioni 12 na pia ingetoa sehemu kubwa
ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu milioni 12,300,000. Ni watu
wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yoyote kati ya
hizi ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo, hata
bila ya gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli
zingebebwa na Tanganyika. Kwa hiyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka
kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya
Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na Serikali yake,
itaonekana imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali moja
Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute mfumo ambao
utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa bila kuibebesha Tanganyika mzigo
wa kuendesha Serikali mbili zenye uzito unaolingana. Hivyo ndivyo tulivyofanya,
na hiyo ndio asili ya muundo wa Muungano wa serikali mbili. Badala ya kutungua
mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazamia hali halisi yetu ilivyokuwa, na
tukabuni mfumo uliotufaa zaidi".
Tukienda na maelezo hapo juu, lililo
dhahiri ni kuwa, zipo sababu kwa nini muundo wa Serikali mbili ulibuniwa.
Aidha, katika maelezo hayo, kilicho wazi ni kuwa sababu zilizozaa Serikali
mbili hazikuwa sababu za kichama bali kitaifa. Hivyo, dhana kuwa muundo wa
Serikali mbili ni suala la CCM ni dhana potofu. Hali kadhalika, muundo huu sio
msahafu na unaweza kubadilika. Wala hakuna sababu ya kuendekeza muundo ambao
hautakiwi. Muhimu ni kujadili kwa uwazi iwapo mazingira yaliyozaa Serikali
mbili yamebadilika, na kama kwa kubadilika huko, sasa mbadala wake ni Serikali
moja, tatu au kuvunja muungano.
10)
Kuvunja Muungano ni sawa na kuvua koti
Baadhi ya wanasiasa wanazungumzia suala la
kuvunja muungano kwa wepesi sana. Suala la kuvunja muungano linachukuliwa kama
jambo la usiku mmoja. Dhana hii inajengwa kwa makusudi ya kuwatoa hofu wananchi
kwamba hakutakuwa na athari ikiwa tutafanya hivyo. Wanapozungumzia suala la
kuvunjika kwa muungano, hutanguliza picha ya ‘pepo nzuri’ itakayokuja punde
baada ya kuuvunja. Katika kurahisisha hoja yenyewe, inasemwa kuwa ‘muungano ni
kama koti, ukilichoka unalivua’.
Funzo tunalolipata katika maisha ya
kawaida na uzoefu kutoka nchi zilizopita njia tunayoshawishiana kupita,
zinatufunza vinginevyo. Kuvunjika kwa ndoa tu huambatana na changamoto nyingi
na wakati mwingine kusambaratika kwa familia na mali. Uzoefu wa kusambaratika
kwa dola ya kisovieti ya Urusi na dola ya Yugoslavia kuliambatana na machafuko.
Aidha, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, pamoja na kuwa
ulikuwa ni ushirikiano wa kikanda tu, uliambatana na ukakasi mkubwa. Hivyo,
hatuna sababu yoyote ya kuamini kuwa kuvunjika kwa muungano wa Tanganyika na
Zanzibar uliodumu kwa miaka 49 litakuwa ni jambo jepesi na rahisi.
Msingi wa kuvunja muungano ni dhamira
zinazosukumwa na kutoaminiana na chuki miongoni mwa wanasiasa na baadhi ya
wananchi. Hatuwezi kutarajia matokeo ya kuvunjika kwa muungano huo yazae upendo
na mashirikiano. Upo uwezekano mkubwa wa wazanzibari walioko Tanganyika na
watanganyika walioko Zanzibar kupita katika msukosuko mkubwa. Msukosuko huu
waweza kuhatarisha usalama wa maisha na mali zao. Tayari vipo viashiria vya
biashara za wabara kuchomwa moto na watu wasiojulikana Zanzibar. Njia hii,
haitaweza kuzaa mazingira ya mashirikiano nje ya muungano. Hili likitokea,
ustawi wa nchi mbili hizi utakuwa mashakani ikizingatiwa kuwa usalama wa nchi
hizi mbili unategemeana.
Jambo la kuhofia zaidi iwapo muungano
utavunjika ni kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar.
Sina mashaka kuwa, hoja zilezile zilizofanikisha kuvunja muungano ndizo
zitakazovunja jamhuri hizi mbili. Ni vigumu kuweka ukomo wa kutumika kwa hoja
za mgawanyiko, ilihali watu watakuwa wamedhihirisha kuwa zinafanya kazi vizuri.
Sioni ni kwa sababu gani maeneo mengine yasitake kujitenga kwa kujificha katika
Sera ya Majimbo hususan kule zinakotoka rasilimali kama Mtwara, kanda ya Ziwa
na Kanda ya Kaskazini. Nao watahoji uhalali wa Tanganyika na watasema ‘utaifa
ni kama koti, likikubana unalivua’.
Ni hofu yangu kuwa Zanzibar nayo haitabaki
moja. Mgawanyiko wa kisiasa kati ya kisiwa cha Unguja na Pemba, na waunguja na
wapemba ni dhahiri. Chaguzi za Zanzibar kabla ya mapinduzi na baada ya
mapinduzi zimeambatana na mgawanyiko mkubwa. Katika chaguzi mbili za mwaka 2000
na 2010, Chama cha Mapinduzi kinachoaminika kuungwa mkono na waunguja wengi
hakikupata kiti hata kimoja cha Ubunge na Uwakilishi kisiwani Pemba. Ni vyema
kukumbuka kuwa, uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar hakujamaliza
tofauti za wapemba na waunguja. Kikundi cha Wazee wa Pemba kilichoandika barua
Umoja wa Mataifa kikitaka Pemba kujitenga hakijafa. Uamsho nao ni kikundi cha
kukiangalia kwa makini sana. Mgawanyiko huu katika jamii ya wazanzibari ulijionyesha
pia katika utoaji wa maoni ya Katiba mpya.
Tukiangalia kijiografia na kiutawala,
umbali kati ya Tanganyika na Unguja na Tanganyika na Pemba ni mdogo sana
ukilinganisha na umbali kati ya Pemba na Unguja. Mazingira haya ya kijiografia,
na fukuto la mgawanyiko ndani ya Zanzibar, yataipa changamoto kubwa sana
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kujitawala nje ya muungano. Mazingira haya yanatoa
fursa nzuri sana kwa wasioitakia mema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kukamilisha azma yao ya kujitenga kwa Pemba. Gharama ya hili kwa wazanzibari na
ustawi wao itakuwa kubwa sana. Mazingira haya, hayatavutia huo uwekezaji
unaotumainiwa kutoka OIC wala uarabuni. Maana, ustawi hautokani na kuwa na
rasilimali pekee, bali kuwepo kwa amani na utulivu. Hali kadhalika iwapo
Zanzibar itaingia kwenye machafuko na kusambaratika, Tanganyika haitakuwa
salama pia maana usalama wetu unategemeana.
Hitimisho
Hakuna siasa rahisi kama siasa ya kugawa
watu na siasa ya kubomoa. Kuutetea muungano na haswa muundo wa Serikali mbili
kunahitaji ujasiri na uongozi. Ujasiri na uongozi hukaa vifuani mwa viongozi
makini. Wanasiasa makini huunganisha watu na ni jukumu gumu. Ndio maana
haishangazi kuwa tuna wanasiasa wengi wanaohubiri mgawanyiko kuliko wanaohubiri
umoja.
Ukweli unabaki, kutokuendelea kwa
Tanganyika au Zanzibar hakutokani na Muungano bali Muungano ni 'bangusilo' tu.
Zanzibar imerudishwa nyuma na matatizo yanayotokana na historia yake kabla na
baada ya mapinduzi. Vivyo hivyo Tanganyika imerudishwa nyuma na matatizo ya
kiutawala ikiwemo ubadhirifu na ufisadi. Matatizo ya Tanzania bara na Zanzibar
hayatokani na muungano wala muundo wa
Serikali mbili. Kinyume chake Muungano umeijengea Tanganyika na Zanzibar umoja
na utaifa, umoja uliotuwezesha kukabili misukosuko ikiwemo vita dhidi ya
Uganda. Tusijifiche nyuma ya Muungano, tutafute suluhu ya matatizo yetu ya
ndani ya pande zote.
Suala la muungano na muundo wake lafaa
kufafanuliwa na kujadiliwa kwa kina na uwazi. Ikiwa tutajiridhisha kuwa
mazingira yetu yamebadilika kiasi cha kuhitaji muundo mwingine si vibaya
tukaubadili. Ni vizuri tu kuwaeleza wananchi kinagaubaga kuwa, kama ambavyo
muundo wa serikali mbili unawagharimu, mabadiliko kwenda katika mfumo wowote
tutakaokubaliana yatakuwa na gharama zake pia, tena zaweza kuwa kubwa kuliko
zilizopo. Ni vyema wananchi wakafahamishwa gharama hizo ili wawe tayari kufanya
maamuzi sahihi na kuzibeba.
Swali tunalopaswa kujiuliza kwa dhati
mioyoni mwetu ni kama tunataka muungano uendelee au la. Ikiwa tunautaka, Napata
shida kuamini kuwa tunaweza kuuendeleza nje ya muundo wa Serikali mbili. Maoni
yangu, upo uwezekano mkubwa kuwa nje ya muundo wa Serikali mbili, na ikiwa
muungano utaendelea kuwepo hatutakuwa na serikali mbili, bali muundo wa
serikali nne ambazo ni serikali za Tanganyika, Pemba, Unguja na Shirikisho. Maana
ni vigumu kupangua mbili ukasimamia kwenye tatu. Kupangua ni rahisi kuliko
kupanga, kubomoa ni rahisi kuliko kujenga.
Hatimaye, ustawi na hatma ya nchi yetu,
muungano wetu na vyote vile tunavyovithamini viko mikononi mwetu. Wakati
umefika, wanaoamini katika utaifa wa Tanzania wasimame na waseme sasa au wanyamaze na kuishi na majuto milele! Mimi
nimechagua kusema!
Kama kuna mengi ya kusema, huu ni wakati mwaafaka. Referundem ni muhimu katika Demokrasia, bali iwe ya kweri na haki" mimi na simama na utaifa wa TANZANIA. siyo vyama, maelezo yako yamelenga umuhimu wa yote kwa muelewa kutaka nini afahamu,kidemokrasia. mimi nipo Netherland, tokea nchi za ulaya zilipokua 12 na sasa zipo 26, na nimeondoka tanzania mwaka 1993 kwahiyo inamaanisha wanaungana nasio kugawanyika. Mdau Holland.
ReplyDeleteni very biased and weak points
ReplyDelete1,Kilo mita za mraba sijui znz hapatoshi UK ina density ya 259/sq km
hii sio hoja ya sisi kuungana ila ni hoja ya kuhatarisha wa znz kukosa makazi kwa sababu ya muungano.
2.Serikali 3 gharama sijui bajeti
ndio maana tukasema kila nchi ikiwa huru tutachagua kipi tutashirikiana,sisi hatutaki serkali 3 bali MKATABA,hilo la 3 lenu.hata UK wameshtuka kuwa EU haina manufaa nayo
3.kuhusu huo mraba ni kutoelewa takwimu jee huo mraba tanganyika kuna sehemu zinakalika? kwa mfano utakaa juu ya kilimanjaro? utakaa mbugani nk. yote hayo uangalie usilete hisabu za madole.
4.Waznz laki 4 wapo na wamejenga bara hii too much uongo huu ,na hata iwe hivo pia kuna 2% ya Asians UK je wameungana?
sna haja kuendelea hoja za kitoto aliekupa hana elimu ya kutosha
Ni kweli huu uzalendo wa kijinga ni lazima ukemewe, maana hawa wanaojiita wasomi na wanasisiasa wanatumia vibaya uwezo wao ambao kwa kiwango kikubwa ni mchango wa huo muungano wanao ukataa, chini ya muungano walifundishwa na walimu toka pande zote mfano hayati Prof Haroub Othman n.k, jambo la msingi ni kuangalia ukweli ni upi na bila kuficha ukweli ni tuliyo udumisha kwa miaka 49, kwa maana hiki si kipindi ambacho waweza kusema tulikuwa tunafanya majaribio. mimi nadhani wakati umefika wa watu bila kushurutishwa bali kuelimishwa wakae wachague muundo wanao utaka, inashangaza ujerumani mbili zilizotengwa kwa kipindi kirefu sana na kuwa na uchumi tofauti sana kuakaa kama ndugu na kuungana sisi makapuku tunataka kusamabalatika
ReplyDelete