Sunday, July 21, 2013

WILAYA YA HAI YAINGIA USHIRIKIANO NA SWEDEN

Ujumbe wa viongozi kutoka wilaya ya Hai wakiwa na mwnyeji wao ambaye ni mratibu wa miradi mbalimbali ya maendeleo na pia ni diwani,Stina Johansson (wa tatu kulia).Wengine kutoka kulia ni Novatus Makunga[mkuu wa wilaya ya Hai],Clement Kwayu[mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai]Melkizedeck Humbe[Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hai] na Ester Mbatiani ambaye ni Afisa mipango mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Hai.

Na Richard Mwangulube

Halmashauri ya wilaya ya Hai,imeingia mkataba wa miaka minne wa ushirikiano na Manispaa ya Arvidsjaur nchini Sweden unaolenga katika maeneo ya kiuchumi na kijamii ukiwemo wa teknolojia ya kisasa ya udhibiti wa takataka kiuchumi kwa kuziwezesha kutengezwa upya bidhaa kwa ajili ya matumizi.

Mkataba huo ulitiwa saini wakati wa ziara ya ujumbe wa viongozi wa wilaya ya Hai uliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya Hiyo, Novatus Makunga hivi karibuni katika makao Makuu ya Manispaa hiyo nchini Sweden.

Wajumbe wengine Katika ziara hiyo ya siku tano ambao ndiyo waliosaini mkataba huo ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Clement Kwayu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Melkizedeck Humbe pamoja na Afisa Mipango wa Halmashauri Ester Mbatian.

Kufuatia mkataba huo, Halmashauri ya Wilaya ya Hai itapaswa kuandaa na kuwasilisha katika Manispaa ya Arvidsjaur miradi mbalimbali inayolenga katika Nyanja za biashara na viwanda vidogo na vya kati.

Maeneo mengine ya shirikiano huo ni pamoja na elimu na utoaji wa taarifa, uboreshaji na usimamizi wa mazingira endelevu pamoja na miradi inayolenga masuala ya ajira kwa vijana.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Hai mwishoni mwa wiki,Makunga amesema kadhalika ushirikiano ho unalenga katika kuimarisha shughuli mbalimbali zinazohusiana na masuala ya sekta ya utalii na utawala bora kuanzia ngazi ya chini kabisa.

“Kwa kushirikiana na wenzetu tunaandaa mkakati wa kuimarisha mafunzo kwa jamii katika masuala ya uchumi na shughuli za maendeleo ya Kijamii na lengo kubwa zaidi ni kwa kundi la vijana”. Amefafanua Makunga.

Ameeleza kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweden[SIDA] ushirikiano huo pia utatoa fursa kwa Manispaa ya Arvidsjaur kushirikiana na wilaya ya Hai katika ujenga uwezo kwa halmashauri juu ya namna ya kupata taarifa mbalmbali za maendeleo na kiuchumi kutoka maeneo ya vijijini nakuzifanyia kazi.

Amesema pia ushirikiano huo umelenga katika kuhakikisha halmashauri ya Hai inaingia katika mfumo wa kisasa wa namna ya kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za maendeleo, kuboresha mawasiliano na wadau mbalimbali ikiwemo kupitia kituo cha halmashauri hiyo cha redio Boma FM.

Amesemasa Manispaa hiyo ya Sweden itasaidia katika ujenzi,uboreshaji na uendelezaji wa kituo cha mafunzo kwa ajili ya maendeleo ya jamii katika wilayani Hai pamoja na kusaidia katika kuboresha huduma za afya.

Masuala mengine yatakayotekelezwa kutokana na mahusiano hayo ni pamoja na Manispaa ya Arvidsjaur kusaidia katika teknolojia ya urudufishaji wa taka ambapo unawezesha taka ngumu na taka maji kuweza kutumika tena.

Makunga amesema kuwa suala la udhibiti wa takataka ni changamoto kubwa katika mji wa Hai ambao hauna dampo huku kukabiliwa na ongezeko la kasi la watu wanaopenda kuweka makazi ya kuishi na kuendesha shughuli zao za kazi Arusha,Moshi,Siha na Simanjiro.

“Kwa wenzetu taka ni rasilimali, inachambuliwa kuanzia ngazi ya familia na kupelekwa eneo la kutupa taka, kwa kupangwa kuangalia na aina, na hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali vikiwemo vikombe, vijiko, sahani na umeme pamoja na mafuta ya kulainishia vyuma kutumika upya,”amefafanua.

Ametaja mengine ambayo yatatiliwa mkazo kutokana na ushirikiano huo ni pamoja na Manispaa hiyo kusaidia katika kukuza uchumi na kuimarisha miundo mbinu ya kiuchumi.

Makunga ameeleza kuwa manispaa hiyo ambayo inamiliki uwanja wa ndege wa kimataifa imeonyesha kuvutiwa kusaidia uimarishaji wa uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) uliopo wilayani Hai kwa kuongeza shughuli za biashara za Anga pamoja na kuboresha miundo mbinu katika Uwanja huo.

Ujumbe huo uliweza kupata taarifa juu ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Manispaa hiyo zikiwemo za kuchumi, kijamii pamoja na usimamizi bora wa ukusanyaji na matumizi ya Mapato.

Kwa mujibu wa nchi ya Sweden, Mamlaka zote za Serikali za Mitaa zinajulikana kama Manispaa zinaongozwa kwa sheria ya bunge la nchi hiyo ambapo hivi sasa kuna Manispaa zipatazo 260 nchini Sweden.

Manispaa hizi zinawajib wa kusimamia masuala ya elimu kuanzia ngazi ya chekechea hadi Sekondari pamoja na kujenga na kusimamia vituo vya malezi ya wazee na wasiojiweza.

Kadhalika manispaa hizi zinawajibu wa kusimamia vituo vya zimamoto na uokoaji,kusimamia ujenzi na uendeshaji wa viwanja vya ndege,kusaidia walemavu pamoja na kuunganisha wajiri na waajiriwa.

Pia Makunga ameeleza kuwa Manispaa hizi zinajukumu la kusimamia vituo vya elimu ya ujasirimali kwa vijana na masuala ya Utalii ambapo Sweden kila siku hupokea watalii zaidiya 500,000 wanaotembelea vivutio mbalimbali katika Manispaa hizo kutoka nchi za ulaya

No comments:

Post a Comment