Wednesday, July 31, 2013

Waasi DRC wapewa saa 48 kusalimisha silaha

Wanajeshi wa Brigedi Maalum wakiwa katika mazoezi makali yaliyofanyika  hivi karibuni huko Goma Mashariki ya Demokrasia ya Kongo
Mmoja wa walinda amani kupitia Brigedi Maalum inayoundwa na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi akiwa katika moja ya mazoezi yaliyofanyika hivi karibu huko Goma. Kamanda Mkuu wa Misheni ya Kulinda Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ( MONUSCO ) Luteni Jenerali Carlos Albeto dos Santos Cruz ametakanza jana jumanne akiwa Goma kwamba MONUSCO itaanza rasmi kuitumia Brigedi Maalum na ametoa saa 48 kuanzia saa kumi jioni kwa saa za Goma jana siku ya Jumanne waasi wote kusalimisha silaha zao, na kwamba ifikapo saa kumi jioni kwa saa za Goma siku ya Alhamisi Agosti Mosi wale wote ambao watakuwa hawajasalimisha silaha zao watachukuliwa kama tishio la usalama kwa wananchi na MONUSCO italazimika kuwapokonya ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kwa mujibu wa Mamlaka iliyopewa na Sheria zinazowaruhusu kufanya hivyo.

Na Mwandishi Maalum

Misheni ya Kutuliza Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( MONUSCO) imetangaza kwamba kwa mara ya kwanza itaanza kuitumia Brigedi Maalum ( Force Intervention Brigade) katika kudhibiti eneo maalum la usalama ( security zone ) kuzunguka mji wa Goma ulioko Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na imewapa saa 48 waasi kusalimisha silaha zao.

Taarifa iliyotolewa na MONUSCO na kusambazwa na Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa jana jumanne, inaeleza kwamba watu binafsi katika eneo la Kivu ya Magharibi ambalo linajumisha Goma na Sake na ambao hawahusiki na vyombo vya usalama watapewa saa 48 kuanzia saa kumi jana kwa saa za Goma ( Jumanne ) kuzisalimisha silaha zao katika Misheni hiyo na kujiunga na mchakato wa DDR/RR unaoratibu upokonyaji, usambaratishaji, urejeshwaji makwao, kuwaunganisha na jamii na kuwapatia makazi.

Baada ya saa kumi jioni ya Alhamisi, Agosti Mosi. Taarifa hiyo inasema. Wale wote ambao watakuwa hawajasalimisha silaha zao watachukuliwa kama tishio kwa usalama wa wananchi na MONUSCO itachukua hatua zote muhimu kuwapokonya silaha hizo ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kama ilivyoainishwa katika Mamlaka na sheria za ushiriki za MONOSCO.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo zaidi ya wananchi milioni moja wanaishi katika eneo dogo la Goma na Sake na kando kando ya barabara ambayo inawaunganisha na kambi ya wakimbizi ya Mugungu ambayo ni makazi ya muda ya watu karibu 70, 000 ambao wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano.

Kwa mujibu wa MONUSCO, tangu kati kati ya mwezi Mei eneo hilo limeshuhudia mapigano ya mara kwa mara kutoka kwa kundi la M23 dhidi ya majeshi ya Serikali ya FARDC ikiwa ni jaribio la wazi la kutaka kusonga mbele kuelekea Goma na Sake.

“ Katika mashambulizi hayo, likiwamo la hivi karibuni la Julai 14, M23 walitumia kiholela silaha zao za moto zikiwamo silaha nzito ambazo zimesababisha wananchi kujeruhiwa” .

Taarifa hiyo imeongeza kwamba kundi hilo la M23 katika mashambulizi hayo limelenga pia Vituo vya Umoja wa Mataifa.

Aidha taarifa hiyo inabainisha kwamba eneo hilo maalum la usalama ( security zone) litasaidia kudhibiti tishio la moja kwa moja mbali na eneo la nje ya Goma na pengine eneo hilo linaweza kupanuliwa na kurudiwa sehemu nyingine kutakako hitajika.

Tamko hilo la kutoa saa 48 kwa waasi kusalimisha silaha zao linafuatia kuwasili katika eneo la Goma kwa Kamanda Mkuu wa MONUSCO, Luteni Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz, ambaye alitangaza kwamba Misheni ya MONUSCO itaunga mkono jeshi la Serikali ( FARDC) katika kuanzisha eneo la usalama kuzunguma eneo la Goma na vitongoji vyake.

Taarifa hiyo inamkariri Kamanda Mkuu wa MONUSCO akiyapongeza majeshi ya serikali kwa kazi nzuri iliyofanya wiki iliyopita ya kuwadhibiti M23. Ingawa anasema eneo la Goma na Sake bado limo katika mazingira magumu sana na kwamba ni wajibu wa wahusika wote kuhakikisha wahalifu wote hawaendelei kuhatarisha raia wa eneo hilo.

Kwa mwaka uliopitia , kundi la M23 pamoja na makundi mengine yenye silaha yamekuwa yakipambana mara kwa mara na majeshi ya serikali katika Mashariki ya Kongo, huku makundi hayo yenye silaha mwezi Novemba mwaka jana yakiikalia Goma kwa muda.

Aidha mapingano ya hivi karibuni ambayo safari hii yalihusisha pia kundi jingine la wanagambo wenye silaha lenye asili yake nchini Uganda, yamesababisha zaidi ya wananchi 100,000 kuyakimbia makazi yao na hivyo kuongeza mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo linalohusisha watu wengine 2.6 milioni ambao wameyakimbia makazi yao huku wengine 6.4 milioni wakihitaji chakula na huduma za dharura.

Wakati huo huo, Kaimu Mkuu wa MONUSCO Bw. Moustapha Soumare katika taarifa yake ametoa wito kwa pande zote kutafuta suluhu ya kisiasa kwa matatizo ya DRC kupitia Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani, usalama na ushirikiano wa maendeleo katika DRC na eneo la Maziwa Makuu uliopitisha mwezi wa Februari na viongozi 11 wa Afrika na Taasisi nne za Kikanda na Kimataifa.

Aidha akasema katika kipindi hiki ambacho suluhu la kisiasa linatafutwa MONUSCO itatumia nguvu iliyonayo kuwalinda wananchi dhidi ya hatari zitokanazo na makundi ya waasi.

No comments:

Post a Comment