Sunday, June 30, 2013

Kaskazini Unguja yaongoza kwa ajali barabarani

Na Salum Vuai, Maelezo

WATU 52 wamepoteza maisha na wengine 332 wamejeruhiwa kutokana na ajali 175 za barabarani zilizotokea katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kati ya Januari mwaka 2011 hadi katikati ya mwaka 2013.

Takwimu hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Usalama Barabarani wa jeshi la Polisi mkoani humo Ali Muhsin, wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya ‘Safiri Salama’, yaliyofanyika katika viwanja vya Mahonda, Wilaya ya Kaskazini B.

Mkuu huyo alisema, ajali za barabarani ni tishio kubwa kwa watumiaji wote wa barabara, wakiwemo madereva, abiria na watembeao kwa miguu, na kwamba tahadhari kubwa inahitaji kuchukuliwa kuziepuka.

Alieleza kuwa, endapo watumiaji wa barabara hawatakuwa waangalifu, majanga ya maafa, ulemavu wa kudumu, majeraha, hasara kwa mali na uharibifu wa miundombinu, vitaendelea kuliandama taifa.

Alitaja sababu mbalimbali zinazochangia ajali hizo, kuwa ni uhaba wa miundombinu imara, ubovu wa vyombo vya moto, mabadiliko ya hali ya hewa, utendaji mbaya wa wasimamizi wa sheria za usalama barabarani na kasoro za kibinadamu.

Ili kumaliza au kupunguza ajali za barabarani, Muhsin alisema hatua kadhaa zinapaswa kuchukuliwa, ikiwemo kutoruhusu magari na vyombo vyengine visiingizwe barabarani hadi vithibitishe kuwa na sifa kwa mujibu wa sheria.

Aidha alishauri vyombo vyenye majukumu ya kutoa huduma kwa umma na kusimamia sheria kama vile polisi, mahakama, Idara ya Usafiri na Leseni, Bodi ya Mapato Zanzibar na vyengine, vitekeleze majukumu yao kwa uadilifu na uaminifu.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika sherehe hizo Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa, alisema ajali za barabarani ndizo zinazoongoza kwa kuua watu wengi, kuliko vifo vitokanavyo na sababu nyengine.

Alieleza, takwimu zinaonesha kuwa, takriban watu milioni moja na laki mbili hufariki kwa ajali hizo kila mwaka duniani kote.

Kwa Zanzibar, alisema ajali 3869, zimeripotiwa kutokea kati ya mwaka 2009 hadi 2012, ambapo kati ya hizo, watu 450 walipoteza maisha, na 3855 walipata majeraha mbalimbali.

Kamishna huyo aliongeza kuwa, kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2013, jumla ya ajali 196 zimeripotiwa, ambazo zimesababisha vifo vya watu 24 na majeruhi 258.

Aidha alisema, ukiondoa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkoa wa Kaskazini Unguja ndio unaoongoza kwa ajali nyingi za barabarani, kulinganisha na mikoa mingine minne Unguja na Pemba.

Alifahamisha kuwa, kwa kutambua uzito wa jambo hilo, Jeshi la Polisi kamisheni ya Zanzibar, limekuwa likifanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wote wa matumizi ya barabara ili kuimarisha usalama wa watumiaji.

Aliwataja wadau hao kuwa, ni jamii yote ya Zanzibar, taasisi za serikali na binafsi, ikiwemo Bodi ya Mapato Zanzibar na Wizara ya Afya, ambayo imeshirikiana kikamilifu na jeshi hilo kufanikisha wiki hiyo ya ‘Safiri Salama’.

Hata hivyo, alikumbusha kuwa, jukumu la kuhakikisha usalama wa barabarani la jeshi la polisi pekee, bali ni la kila mmoja kwa nafasi yake, huku akisisitiza matumizi mazuri ya barabara ikiweemo kuzitunza badala ya kuziharibu kwa visingizio mbalimbali, pamoja na kung’oa vyuma vya alama za barabarani.

Naye Meneja wa kitengo cha maradhi yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Omar Mwalimu, alisema hospitali kuu ya Mnazimmoja, imekuwa ikipokea majeruhi na maiti wengi kutokana na athari za ajali za barabarani, na kusema zinailazimu serikali kutumia fedha nyingi nje ya bajeti yake, kuwatibu watu wanaopatwa na ajali.

Wiki ya ‘Safiri Salama’ ilianza tarehe 24 Juni mwaka huu, kwa mikutano ya kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara, kama vile madereva na makondakta, wanafunzi, mabagwani na wananchi wengine wa Mkoa wa Kaskazini.

Sherehe hizo zilizopambwa kwa burudani mbalimbali zilizobeba ujumbe wa usalama barabarani kutoka kwa kikundi cha Black Roots chini ya msanii Makombora na utenzi, zilihudhuriwa pia na Wakuu wa Wilaya za Kaskazini B, Khamis Jabir Makame na Riziki Juma Simai wa Kaskazini A, pamoja na makamada wa Polisi wa mikoa mitatu ya Unguja.

No comments:

Post a Comment