Tuesday, May 28, 2013

WAFANYABIASHARA WA KARIAKOO WAKUTANA KUZUNGUMZA KUHUSIANA NA MIZIGO YAO ILIOKWAMA BANADARINI

Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo wameahidi kuendelea kutafuta suluhu kwa njia ya mazungumzo na serikali juu ya mgogoro wa makontena ambayo yamezuiliwa bandarini, kitendo ambacho kimeathiri biashara zao kwa mda mrefu sasa kwani wemeshindwa kufanya biashara ndani na nchi jirani kwa takriban zaidi ya wiki tatu.

Tamko hili lililotolewa na Jumuiya Hii wiki iliopita, limeeleza kuwa tayari wametuma maombi kwa wizara husika na idara za serikali za mapato ili kuwepo na mkutano utakaoweza kutizama jinsi ya kutatua mgogoro wa makontena zaidi ya 400 ambayo yamezuiliwa bandarini.

Katika tamko hilo imeelezwa kuhusu dhamira yao ya kukutana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Waziri wa Viwanda na Uwongozi wa TRA pamoja na vyombo vingine husika ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa kile wanachodai ni ongezeko la kodi.

Wanasisitiza kuwa kuwepo kwa pande zote hizi kwenye mkutano kutawezesha kufikia ufumbuzi.

Jambo lililopelekea kufikia uamuzi huu wa kukutana na viongozi ni kile walichokiita kutekwa nyara kwa kikao cha awali kilichofanyika na Waziri wa Fedha ambapo Chama cha Mawakala wa bandarini kilifunika nafasi hiyo kwa kujadili matatizo yao wenyewe bila ya kujali kero inayowakabili wafanyabiashara ambao tayari wameanza kupata hasara kutokana na makotena yao kukwama.

Wafanyabiashara wamelalamika juu ya mawakala kuingia katika malumbano yao binafsi juu ya ushindani wa kibiashara badala ya kutafuta suluhisho la makontena yalio na bidhaa za wafanyabiashara hawa wadogo wadogo.

Hata hivyo tamko la wafanyabiashara limeweka wazi kuridhika kwao na maelekezo yaliyotelewa na Waziri wa Fedha na maafisa wa TRA juu ya kukubali kwao kufanya kikao haraka na wafanyabiashara hawa.

Wafanyabiashara pia wametakiwa kujaza fomu upya ambazo zitaeleza upya aina za bidhaa walizoleta nchini na vielezo kamili vya bidhaa hizo ili vifanyiwe uhakiki upya.

Pia wamehakikishiwa kuwa hawatatozwa faini kwa makosa yoyote yatayobainika baada ya kuhakiki fomu zao upya, iwapo zitakuwa na dosari. 

Jumuiya hiyo pia imesema kwamba iwapo kulikuwa na ukwepaji wa kodi basi badala ya TRA kuwaadhibu wao nivema wangechukua hatua dhidi ya wale wote waliokwenda kinyume.

Katika malalamiko yao wanadai kuwa ushuru wa forodha (Import duty) na VAT zimeongeka mara mbili bila ya wao kupewa taarifa.

Pia wanadai kuwa TRA haikufuata utaratibu katika kuongeza kodi.Wanadai pia wafanyabiashara wanalalamika juu ya HS Code ambayo inatumika kuonyesha aina ya bidhaa mbali mbali na ushuru wake kwa madai ya kuwa imechakachuliwa.

Lakini wafanyabiashara wameendelea kusisitiza kuwa wao ni wananchi wenye kutii sharia za nchi na wako tayari kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili katika meza ya mazungumzo.

Wameelezea jinsi walivyoanza kupoteza wateja wao mara baada ya mizigo yao kuzuiliwa bandarini, ikiwa ni pamoja na usumbufu mkubwa kwa wateja wao ambao wanatoka katika nchi za Afrika mashariki na nyinginezo.

Wamesema hivi sasa kuna uwezekano wa wateja wao kuhama na kufanya biashara nchi nyingine jambo ambalo litaipotezea taifa kiwango kikubwa cha pato la taifa.

Wafanyabiashara hao wanadai kuwa tayari wapo wenzao ambao wamekufa kutokana na kutetereka kwa biashara zao baada ya kuambiwa walipe kodi kubwa ambayo imewaletea mshituko mkubwa hadi kufikia kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na jumuiya, tayari mali ya mabilioni imekwama na gharama za kuukomboa zinaongezeka.

1 comment:

  1. HAWA WATU ASIDANGANYE UMMA WASEME UKWELI WA JAMBO HILI.KAMA KUFAIDIKA WAMEFAIDIKA SANA KWA KUDECLARE VITU AMBAVYO SI SAHIHI HIVYO KUKWEPA KULIPA USHURU.LAKINI HII INACHANGIWA NA MA AGENTS AMBAO SI WAAMINIFU. MZIGO UKIPITA BILA KUSTUKIWA CHA JUU WANAGAWANA WASITUFANYE WAPUMBAVU

    ReplyDelete