Saturday, May 25, 2013

Wabunge wanawake wajinoa kuhusu namna bora ya uwasilishaji wa Miswada na Hoja Binafisi Bungeni

Chama cha Wabunge wanawake katika Bunge la Tanzania (TWGP) leo wamefanya semina ya siku moja kwa wabunge wote wanawake kwa lengo la kuongeza uelewa mpana katika namna bora ya uwasilishaji Miswada au hoja binafsi Bungeni.

Akifungua semina hiyo, Mwenyekiti wa chama hicho cha Wabunge wanawake Bungeni. Mhe. Anna Abdallah amewataka wabunge wanawake wote bila kujali vyama vyao kuhakikisha wanaitumia vizuri Ofisi ya mshauri mkuu wa mambo ya sheria wa Bunge katika kuwasilisha Miswada au hoja Binafisi.

Amesema wabunge wanawake wanawajibu wa kutatua matatizo yanayowakabili wananchi hususani wanawake nchini ikiwa ni pamoja na kuleta hoja au miswada Bungeni yenye kulenga kuifanya serikali iweze kutatua kero zinazowakabili wananchi wake.

“Waheshimiwa wabunge, pamoja na kwamba mimi nikipindi changu cha nane hivi sasa bado kuna mwamko mdogo kwa waheshimiwa wabunge wanawake kuleta miswada au hoja binafsi bungeni. Naamini tukiitumia vizuri Ofisi hii pale tutakapokuwa tuna mawazo yetu, watatusaidia sana kutuandalia hoja binafisi au miswada kulingana na matakwa yaliyopo ya kikanuni”alisema Mhe. Anna Abdallah

wakichangia mada zilizowasilishwa hapo, wabunge wengi wanawake wameomba kuwe na utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa kila mara elimu hii inatolewa kwa lengo la kujikumbusha baadhi ya taratibu za kikanuni na hata kisheria katika uwasilishaji wa hoja binafsi na miswada binafsi Bungeni.

“Kuna haja ya kuwa na semina katika maswala haya angalau mara moja kila wakati wa vikao vya Bunge ili kujikumbusha mambo kadhaa yanayotawala katika uwasilishwaji wa miswada binafsi au hoja Binafsi mwenyekiti kwa kuwa tuna mambo mengi tungependa kuyaleta Bungeni kupata baraka zake. Kwa kujikumbusha na mambo haya tutaiva kwelikweli katika kuwawakilisha wananchi wetu mwenyekiti”. Alichangia Mhe. Anne Kilango Malecela.

Jumla ya mada tatu ziliwasilishwa katika Semina hiyo iliyoandaliwa na chama hicho cha wabunge wanawake Bungeni (TWGP) kwa kushirikiana na Ofisi ya msahuri wa maswala ya sheria wa Bunge ambazo zote zililenga kuwapa uelewa wabunge kuhusu namna bora na mambo ya kuzingatia wakati wa kuwasilisha miswada binafsi na hoja binafsi Bungeni kwa wabunge wanawake.
Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wanawake Bungeni (TWGP) . Mhe. Anna Abdallah (Mb) akifungua rasmi semina hiyo siku moja kuhusu namna bora ya uwasilishaji wa Miswada binafsi na hoja Binafisi Bungeni kwa wabunge wanawake. Kushoto ni katibu wa chama hicho Mhe. Angela kairuki na aliyekulia ni Makamu Mwenyekiti Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa.
Mtoa mada kutoka Ofisi ya Mshauri Mkuu wa mambo ya Sheria wa Bunge Ndg. Matamusi Fungo akiwasilisha mada kwa wabunge wanawake kuhusu uwasilishwaji wa Miswada ya Serikali Bungeni.
Bi. Stella Bwimbo nae kutoka Ofisi ya Mshauri Mkuu wa mambo ya Sheria wa Bunge akiwasilisha mada kuhusu uwasilishwaji wa Miswada binafsi ya sheria Bungeni.
Ndg. Mosi Lukuvi kutoka Ofisi ya Mshauri Mkuu wa mambo ya Sheria wa Bunge akiwasilisha mada kuhusu uwasilishwaji wa Hoja binafsi Bungeni kwa waheshimiwa wabunge wanawake.
Katibu wa Chama cha Wabunge wanawake Bungeni Mhe. Angela kairuki akikaribisha michango kwa waheshimiwa wabunge mara baada ya kusikiliza mada. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa.
Mbunge wa Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malecela akichangia mada wakati wa semina hiyo.
Mbunge wa viti Maalum (CCM) Diana Chilolo akiuliza swali kwa mtoa mada.
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) Mhe. Cecilia Paresso akiuliza swali kwa watoa mada.
Mbunge wa viti Maalum (CCM) Devota Likokola nae akichangia.
Mbunge wa viti Maalum (CCM) Maria Hewa akitoa mawazo yake.

No comments:

Post a Comment