Thursday, May 16, 2013

UMOJA WA MATAIFA WAJARIBU TENA KUISAIDIA SYRIA




Na Mwandishi Maalum
Wakati milipuko ya risasi na mabomu   ikiendelea  kurindima nchi Syria,   huku    mamia kwa maelfu  ya  raia wa nchi hiyo wakiendelea kuwa wahanga wa milipuko hiyo. Kwa mara  ya  tano Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa, limepitisha Azimio kuhusu hali ilivyo nchini humo likichagiza pande zinazohusika kusitisha mapigano.
Jana (Jumatano ) Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipigia kura Azimio nambari A/67/L. 63 kuhusu  Hali nchini Syria. Azimio hilo liliwasilishwa mbele ya  wajumbe wa Baraza na Qatar kwa niaba ya Umoja wa Falme za Kiarabu likiungwa  mkono na nchi kadhaa   yakiwamo baadhi ya mataifa makubwa  isipokuwa China na Urusi.
Azimio hilo  lilipitishwa kwa kura za ndiyo 107,  hapana 12,  na 59 za  kutofungamana na upande wowote.  Kati ya  nchi  zilizopiga kura ya hapana ni Urusi na Uchina, wakati Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa  kati ya nchi 59  zilizopiga kura ya kutofungamana na upande wowote.
Pamoja na  kwamba Azimio  hilo limepitishwa bado nchi nyingi zikiwamo   hata baadhi ya zile zilizopiga kura ya ndiyo, zimeelezea kutoridhishwa na baadhi ya  vipengele vilivyomo ndani ya Azimio  na namna mchakato mzima wa maandalizi yake ulivyofanyika.
Wawakilishi wa Nchi zilizopiga kura ya kutofungamana na    upande wowote akiwamo Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, walipata fursa ya kuelezea sababu zilizowafanya wakafikia uamuzi huo.
Baadhi ya sababu kubwa zilizoelezwa na  wawakilishi hao ni  pamoja na, kwamba,mkachato wa majadiliano ya Azimio  hilo  haukuwa wazi, shirikishi na haukuzingatia hoja zilizotolewa na  wajumbe wengine ikiwamo hoja iliyotolewa na Kundi la Nchi za Afrika ya kutaka uwasilishwaji wa Azimio hilo uahirishwe ili kutoa nafasi ya kulijadili zaidi.
Kwamba, Azimio hilo lilikuwa limeegemea upande mmoja na   kuelekeza lawama  na shutuma dhidi ya  serikali ya rais Al- Assad  kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa , huku likiwa kimya kuhusu ukatili na ukiukwaji unaofaywa na makundi yenye silaha yanayopigana nchi humo.
Kwamba, Azimio hilo lilikuwa linakaribisha  uanzishwaji uliofanyika mwezi Novemba 2012 wa Muungano wa Kitaifa kwajili ya Mapinduzi nchini Syria na  Makundi ya Upinzani(National Coalition for Syrian Revolution and Opposition Forces) kama chombo halali cha kusimamia na kushiriki majadiliano kuelekea mabadiliko ya kisiasa na serikali ya mpito.
Ukaribishwa wa muungano huo ndani ya Azimio, unaelezwa na baadhi ya wanadiplomasia   hao kwamba kwanza haikuwa kazi ya Baraza  Kuu  ya kuutambua Muungano huo likini ilikuwa ni hatua  inayoashiria mwelekeo wa  kuiondoa  kinyemela serikali iliyoko madarakani  hatua  ambayo  siyo tu ni kinyume na sheria za kimataifa lakini pia ni uingiliaji wa mambo ya ndani ya  nchi nyingine na ni  jambo baya.
Kwamba,  Azimio hilo  halikuwa  na chochote kipya ambacho kinaweza kuleta matumaini  kwa  raia wa Syria na kwamba lilikuwa   halitoi usuluhisi wa kisiasa .
Kwamba,  Azimio  hilo halikuwa na mashiko kuletwa wakati huu ili hali ni siku chache tu zilizopita ,  Mawaziri wa    Mambo ya Nje wa Marekani na Urusi  John Kerry na Bw.  Sergey Lavrov  walikuwa wametangaza nia ya kuitisha mkutano wa Kimataifa kuzungumzia hali ya  Syria. Tangazo ambalo lilipokelewa vema na jumuiya ya kimataifa.
Pamoja na hoja hizo na nyingine nyingi wawakilishi wa  nchi zilizopiga kura ya kutofungamana na upande wowote walieleza bayana kwamba kutounga mkono azimio hilo  hakumaanishi kwamba walikuwa wanaunga mkono  ukiukwaji  mkubwa wa haki za binadamu na machafuko yanayoendelea nchini humo.
Kwa upande wa wawakilishi waliopiga kura ya ndiyo kuunga mkono, hoja kubwa kwao ilikuwa ni kwamba kwa kupitisha azimio hilo, ili kuwa ni kujaribu kwa mara nyingine kwamba Jumuiya ya Kimataifa haijawasahau wananchi wa Syria.

No comments:

Post a Comment