Wednesday, March 6, 2013

Vodacom Foundation yasaidia vifaa vya hedhi shule za msingi mkoani manyara


Meneja Idara ya wateja wakubwa wa Vodacom Tanzania Bi.Stela Mamuya akigawa msaada wa pedi za kisasa zinazofuliwa na zenye uwezo wa kudumu kwa mwaka mmoja pamoja na nguo za ndani kwa wanafunzi wakike wa shule za msingi Barazani na Qambasirong zilizoko Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara,msaada huo uliotolewa na Vodacom Foundation umegharimu zaidi ya shilingi Milioni saba.
Mfanyakazi wa Idara ya wateja wakubwa wa Vodacom Tanzania,Bw.Simon Martin akimkabidhi pedi za kisasa zinazofuliwa na zenye uwezo wa kudumu kwa mwaka mmoja pamoja na nguo za ndani mwanafunzi wa kidato cha sita Bi.Getrude Boniphace, zilizotolewa na Vodacom Foundation kama msaada kwa wanafunzi wa shule za msingi Barazani na Qambasirong zilizoko mkoani manyara,thamani ya vifaa hivyo vimegharimu zaidi ya shilingi milioni saba,anaeshuhudia katikati ni Mkuu wa kitengo cha msaada kwa wateja wakubwa Bw.Ally Zuber.
Meneja wa Vodacom Foundation Bi.Grace Lyon,akimfundisha mtoto wa kidato cha saba Sarah Moses,namna ya kutumia pedi ya kisasa zinazofuliwa mbele ya wanafunzi wenzake,Vodacom Foundation ilitoa msaada wa pedi za kisasa zinazofuliwa na kudumu kwa muda wa mwaka mmoja pamoja na nguo za ndani, kwa wanafunzi wa shule za msingi Barazani na Qambasirong zilizoko Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara,uliogharimu zaidi ya shilingi milioni saba.
Baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania,wakifurahia jambo pamoja na wanafunzi wa shule za msingi Barazani na Qambasirong zilizoko mkoani manyara,wakati walipofanya ziara ya kutembelea shule hizo na kutoa msaada wa pedi za kisasa zinazofuliwa na zenye uwezo wa kudumu kwa mwaka mmoja pamoja na nguo za ndani vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni saba.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Barazani, Haydom mkoani Manyara,Bi.Magreth Shirima wapili toka kushoto akielekezwa na mfanyakazi wa Vodacom kitengo cha huduma kwa wateja Bw.Ndaro Laban kulia na Esther Mattle namna bora ya matumizi ya pedi za kisasa zinazofuliwa na zenye uwezo wa kudumu kwa mwaka mmoja zilizotolewa na Vodacom Foundation kama msaada kwa wanafunzi wa shule za msingi Barazani na Qambasirong zilizoko mkoani humo,thamani ya vifaa hivyo vimegharimu zaidi ya shilingi milioni saba.
HATIMAYE tatizo linaloikabili idadi kubwa ya wanafunzi wa kike kushindwa kuhudhuria masomo kwa kukosa vifaa (pedi) wakati wa hedhi limeanza kupatiwa suluhisho, kufuatia Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la TMARC, kuanzisha kampeni ya kuwawezesha wanafunzi hao kuhudhuria masomo wakati wote.

Utafiti uliofanywa na TMARC hivi karibuni umebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi wa kike nchini, wanaoshindwa kuhudhuria masomo kwa sababu ya kuona aibu wanapokuwa kwenye hedhi, kwa sababu ya kukosa pedi za kuwastili.

Akizungumza wakati wa kampeni maalumu ya kukabiliana na tatizo hilo, lililokwenda sambamba na ugawaji wa nguo nne za ndani pamoja na pedi mbili za kisasa zenye uwezo wa kufuliwa na kisha kuvaliwa kwa mwaka mzima, kwa wanafunzi wa shule za msingi Barazani na Qambasirong zilizopo eneo la Haydom wilayani Mbulu mkoani hapa, mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Mfuko wa Kusaidia Jamii wa Vodacom, Yessaya Mwakifulefule, alisema mradi huo ni endelevu.

"Wenzetu wa TMARC wamefanya utafiti na kubaini kuwa wasichana waliovunja ungo wanashindwa kuhudhuria masomo kwa zaidi ya siku 80 kwa mwaka kutokana na asili ya maumbile yao, hivyo Vodacom Foundation imeguswa na hilo na hatimaye kusaidia vifaa hivi ambavyo ni pedi na chupi, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh milioni 7," alisema Mwakifulefule 

Baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom waliofanya ziara ya kutembelea shule hizo sanjari na kutoa elimu ya namna bora ya kutunza na kutumia vifaa hivyo kwa wanafunzi waliovunja ungo walisema ni fahari yao kuona watoto wanasoma na kuhudhuria vipindi wakati wote kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

"Tumeamua kuanzisha mradi huu ili kuwawezesha wanafunzi hao waweze kujisitiri kwa kuwapatia vitu hivyo ili waweze kuhudhuria masomo wakati wote hivyo kuongeza kiwango chao cha ufaulu" alisema Meneja wa Mfuko wa Kusaidia Jamii wa Vodacom, Grace Lyon Amesema wao kama wafanyakazi wa kampuni hiyo, wanataka wasichana hao wasione kama kuingia katika siku zao kila mwezi kama ni ugonjwa, bali ni maumbile ya asili ya mtoto wa kike.

"Tumeguswa sana kama wanawake na wanaume ambao tumechanga kwa kasi kubwa ili kuwezesha kupatikana kwa msaada huu tuliowaletea ili kuhakikisha kuwa watoto wetu wanafanikisha masomo yao na kufaulu" aliongeza Lyon.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa TMARC, Moris Shirimi, amesema utafiti wao ulilenga kubainisha chanzo cha wasichana wengi kutoroka shule na kuwa na matokeo mabaya katika mitihani yao.

"Sababu mojawapo tuliyobaini ni kwamba wasichana wengi wasio na njia muhimu za kujisitiri wanakacha masomo yao kwa siku tatu hadi tano kila mwezi" alisema Moris Shirimi.

Alisema kutokana na kadhia hiyo, baadhi ya wasichana wamejikuta wakiingia katika mitego ya kushawishiwa na wanaume wenye tamaa kwa kurubuniwa kupewa vitu vinavyoweza kuwasaidia wakiwa katika hedhi na hatimaye kujikuta wakiharibiwa maisha yao.

"Kwahiyo sisi kama shirika kwa kushirikiana na Vodacom Foundation tunawapatia wasichana hawa mbinu za kujilinda kwa kuwawezesha kujikinga kwa staha ili waweze kuishi maisha mazuri na yenye furaha wakati wote" aliongeza Shirimi.

Wakati huo huo, Vodacom Foundation imeahidi kusaidia ujenzi wa darasa la awali katika shule ya msingi Barazani iliyoko kata ya Maghay wilayani Mbulu mkoani hapa.

Ahadi hiyo ilitolewa na Mwakifulefule kufuatia ombi la Mratibu Elimu kata ya Maghay, Festo Sule, aliyeelezea adha wanayopata wanafunzi wa shule ya awali wanaosomea chini ya mti shuleni hapo.

"Tunawashukuru sana kwa kueneza elimu hii ya mabinti zetu kujitambua na kuweza kujisitiri lakini tunaleta ombi kwenu mtujengee darasa hapa tulipo kwasababu watoto hawa wadogo jua ni lao na mvua ni yao kutokana na kukosa darasa"alieleza Mratibu huyo wa elimu Festo Sule.

"Vodacom kupitia mfuko wake wa kusaidia maendeleo ya jamii, tutajenga darasa hapa na kukarabati yaliyopo ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri" alisema Mwakifulefule.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Barazani Magreth Shirima alisema kuwa shule hiyo inaupungufu wa vyumba vitatu vya madarasa, madawati na vitabu vya kiada na ziada.

No comments:

Post a Comment