Monday, February 18, 2013

Msanii Mrisho Mpoto na wenzake wang'ara katika maigizo ya jukwaani


Mrisho Mpoto ni moja kati ya wasanii wakubwa wa Muziki na Maigizo ya Jukwani hapa nchini. Michezo hii ya jukwaani ambayo ni adimu na adhimu sana hapa nchini kutokana na umakini na utaalaam mkubwa unao hitajika katika uandishi, uongozaji na hata uchezaji jukwaani.

Hapa nchini kuna wasanii wachache wenye uwezo wa kutimiza hatua zote za maandalizi ya mchezo wa jukwaani. Tumekuwa tukishuhudia  wataalam walio pikwa kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo na wale wa Chuo kikuu cha Mlimani katika Idara ya Sanaa na Maonesho na Chuo kikuu Huria wakishughulika sana na tasnia hii.

Baada ya kuona Tasnia hii inasua sua, Bwana Mrisho Mpoto aliamua kwa dhati kurudisha heshima ya michezo hiyo kwa kuishawishi kampuni inayo jishughulisha na Maonesho ya Jukwaani ya nchini Kenya Kuuleta mchezo ulio jipatia umaarufu mkubwa kwenye nchi mbali mbali ulimwenguni na hata kupata heshima ya nyota tano nchini Uingereza ambapo Mrisho yeye mwenyewe akiucheza mchezo huo kama mhusika mkuu.

Kutokana na kukubali kwa kampuni hiyo Bwana Mrisho aliwashirikisha wadau wapenda maendeleo ya sanaa mchini, Clouds FM na Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam ambao ndio walitoa mchango mkubwa wa kufanikisha onesho hilo lifanyikie hapa nchini.

Mwishoni mwa wiki hii Onesho hilo lilifanyika katika Ukumbi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni na kuhudhuriwa na watazamaji wengi wanao elewa umuhimu wa michezo ya jukwaani.

Watazamaji walisifia Umahiri ulio oneshwa na Mrisho Mpoto na waigizaji wengine ambapo waliwafanya watazamaji kutabasamu kwa furaha kubwa kila wakati wa mchezo huo.

Baadhi ya washabiki walisema kuwa, wameshangazwa sana kwa kuona kuwa wasanii wa filamu hapa nchini hawajajitokeza kabisa kuja kushuhudia uzuri wa sanaa za jukwaani, kwani kwa kufanya hivyo wangeweza kujifunza uigizaji wa kweli, na unao hitaji umakini na taalam wa kutosha tofauti na michezo ya filamu inayo ibuka sasa kila kukicha. Wametoa wito kwa watanzania na wasanii wote nchini kuwa na tabia ya kushiriki katika maonesho mbali mbali hapa nchini yenye sura ya kuelimisha kwakupitia utamaduni wetu.

Nae mmoja wa wasanii kutoka Kenya ambae hakupenda jina lake litaje alisema kuwa, wamependezwa na kufurahishwa sana na jitihada za msanii Mrisho Mpoto anazo zionesha pindi anapo kuwa mazoezini na kisha jukwaani, na ametoa wito kwa wasanii mbali mbali Tanzania kufuata nyao za Msanii huyu katika harakati zake za kuurejesha heshima ya Michezo ya jukwaani kwani ndio inae weza kuhudhuriwa na wanafamilia tofauti na sanaa zingine ambazo ni maarufu kwa sasa.

Akitoa shukrani zake baada ya onesho Bw, Mpoto alimshukuru sana Mkurugenzi wa Clouds Media Bw Ruge Mutahaba kwa kukubali kuisaidia tasnia ya Michezo ya kuigiza ya Jukwaani. Ili kurudisha heshma ya michezo hiyo hapa nchini, pia Bw Mpoto aliushukuru Uongozi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kwa kukubali kutoa mchango wake mkubwa katika kufanikisha onesho hilo na kuonesha moyo wa kuendelea kusaidia wasanii hapa nchini katika kuinua na kuendeleza Utamaduni wa Mtanzania.

Mchezo wa   Wanawake wa Heri wa Winsa uliotokana na kitabu kitabu kilicho andikwa na Shakespeare  takribani miaka 1600 iliyo pita, na kutafasiriwa na Bw Ogutu Mulaya wa nchini Kenya, ulishirikisha waigizaji nane ambapo kila mwigizaji alivaa husika zaidi ya tatu, na wote walizimudu vyema husika hizo.

Habari na SIXMUD J. BEGASHE wa Makumbusho ya Taifa.

No comments:

Post a Comment