Friday, January 4, 2013
HOJA YA HAJA YA MBUNGE WA KILWA KASKAZINI KUHUSU GESI ASILIA
Sekta ya gesi na mafuta ni moja kati ya sekta kubwa na ngeni kwa kiasi fulani hapa nchini.
Kwa kipindi cha miaka mingi na haswa miaka ya sabini na themanini Serikali ya awamu ya kwanza ilifanya kazi kubwa ya uwekezaji katika utafiti wa mafuta na gesi nchini lakini bila ya mafanikio ya uwekezaji.
Hii inaweza kuwa ilichangiwa sana na siasa zilizokuwapo kwa wakati ule kwa maana ya umagharibi na umashariki na pengine imani ya wawekezaji kutokana na msimamo tuliokuwa nao kama nchi katika suala la ukombozi wa bara la afrika dhidi ya ukoloni pia uduni wa hali ya teknologia ya wakati ule na ukweli kwamba eneo letu la nchi za mashariki mwa Afrika ilijulikana kuwa ni ukanda wa gesi asilia tu na enzi zile gesi asilia ilikuwa haina thamani kuliko mafuta.
Kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni , nchi yetu imefanikiwa sana kuwavuta wawekezaji katika sekta na nyanja tofauti sana ikiwamo katika gesi na utafiti wa mafuta. Hii ni nafasi nzuri tuliyoikosa kwa miaka mingi kiasi cha kutuweka nyuma kimaendeleo ukilinganisha na nchi nyingi za afrika na dunia ya tatu.
Lakini sasa kiasi kikubwa tumeanza kuona manufaa ya uwekezaji ule japo kwa uchache na changamoto nyingi ndani yake.
Tumeanza mwaka 2012 na kumaliza na mfululizo wa matukio ya aina tofauti kwa waandishi kuandika makala na habari nyingi kuhusu shughuli na sekta nzima ya gesi nchini ,na mara ya mwisho kabisa kufuatia maandamano ya wanachi wa Mtwara ambao walitokea katika vyama tofauti.
Sikuona tatizo la waandamanaji wale pamoja na ujumbe ulitolewa bali baadhi ya ujumbe unaonyesha zipo tafsiri nyingi zaidi ya madai ya mahitajio ya manufaa ya mapato katika uwekezaji wa gesi na bomba la gesi.
Nilipata wasisiwasi mkubwa sana baada ya kuona wanaojua ukweli wa jinsi mambo yalivyo na wale wasiojua kuamua kwa dhati kabisa kuuposha umma wa watanzania na dunia kwa ujumla.
Niliwahi kujifunza kuwa ukweli utabaki kuwa ukweli na inastahili tuseme ukweli hata kama inauma kiasi gani kwa maana hakutakuwa na dhambi wala madhara zaidi ya ukweli huo. Pia uongo inatakiwa uwekwe mahali ambapo kila mmoja utauona.
Madai ya wale wanaojiita waandamanaji ni kuwa gesi isitoke hadi pale Serikali itakaposema wananchi watanufaikaje lakini pamoja na mambo yote ambayo wamesema na kuungwa mkono naomba tuambizane kwa kuulizana . Ni lini ambapo Serikali au wawekezaji wamesema kuwa bomba litafanya kazi ya kutoa gesi Mtwara kwenda Dar es salaam pekee ? Nielewavyo mie leo hii kuwa bomba linaweza pia kutumika kutoa gesi Dar es salaam kwenda Mtwara pale ambapo patakuwa na mahitaji au matumizi ya ziada katika viwanda.
Msumbiji ambao wamegundua gasi nyingi zaidi yetu wanaweza kutumia bomba la gesi kupeleka katika masoko ya Kenya,Uganda sudan Rwanda Burundi na kadhalika au nchi kama Kenya ambazo nazo zimegundua gesi wanaweza kutumia kupitisha gesi kwenda Afrika ya kusini au kwingineko.Yote haya itatupa mapato makubwa sana kama vile nchi ya Ukraine inavyonufaika kupitisha bomba la gesi inayotoka Russia kwenda Ulaya magharibi.
Inaweza kuwa kweli Rais alitoa ahadi kuwa lazima gesi iwanufaishe watu wa mtwara kwa kuweka viwanda mtwara. Hivi ni kweli hatufahamu kuwa upo mradi wa ujenzi wa kiwanda cha saruji ,kiwanda cha uyayushaji chuma(iron smelter) na vinginevyo ?
Siamini sana kuwa itakua ni kazi rahisi kuhamisha viwanda vya chuma, saruji, chupa, rangi na mengineyo ambayo kwa sasa vipo Dar es Salaam kutokana na uwekezaji uliofanyika kwa zaidi ya miaka 40 au zaidi kuvihamisha na kuvipeleka mtwara? Ni kweli kuwa bidhaa zizalishwazo hivi sasa wananchi wa mtwara na lindi hawazitumii ?
Nimekuwa nikiona magari mengi sana kutoka Dar es salaam kwenda Lindi na Mtwara na bidhaa za aina tofauti ,ambazo zinazalishwa kutokana na umeme unatokana na gesi kutoka songo songo Kilwa. Hivi manufaa tuyasemayo ni ya namna ipi ?
Katika uwekezaji wa gesi na mafuta kampuni huhitaji uwekezaji mkubwa sana ambao mara zote huhitaji kuuza hisa katika masoko ya hisa au kutegemea makampuni mengineyo kujiingiza kushiriki kuwekeza(farm in). Je, kwa maandamano haya hatutaishia kulipa fidia kwa wawekezaji baada ya kuharibu mazingira mazuri ya ufanyaji kazi ?
Wakati haya yakiendelea kufanyika , tayari yapo makubaliano kadhaa ambayo yamewekwa baina ya Serikali na makampuni ya uwekezaji kwa ajili ya kuendeleza gesi iliyopatikana . Mfano mzuri ni eneo la Rushungi Kilwa kuna kampuni kubwa kutoka Norway na mshirika wake kutoka Marekani wanafanya uchunguzi wa uwezekano wa kujenga LNG terminal ili kuisindika gesi hiyo na sehemu mbali mbali za mwambao wa Mkoa wa Lindi na Mtwara zinafanyiwa uchunguzi wa aina huo.
Uwekezaji huu umechelewa sana kufanyika haswa ukizingatia kuwa gharama zinapanda siku hadi siku. Dunia haikusubiri na uchumi unazidi kuwa wa aina tofauti na siku za nyuma. Imani ya wawekezaji ikipotea dhidi yetu tutatumia miaka mingapi kuirejesha?
Pia ikumbukwe kuwa Serikali imewekeza pesa nyingi sana kwa kusomesha na kulipa mishahara watumishi wa sekta husika lakini pia katika uwekezaji kwa sekta hii
Inawezekana kabisa kuwa bado manufaa hayajaonekana moja kwa moja , lakini tujiulize kuwa gharama za chakula zilizopanda hivi sasa Lindi na Mtwara zimesababishwa na nini. Pia haitoshi kuwa thamani ya ardhi imepanda mara ngapi na kuwanufaisha watu wa mikoa hii?
Hivi tangu Serikali iweke chuo cha VETA wanafunzi wangapi kutoka Lindi na Mtwara wamekubali kujianadikisha katika masomo ili kuja kupata ajira na kushiri katika sekta gesi
Tusitarajie kuna siku zitagawiwa pesa kwa mafungu kutoka katika mapato yatokanayo na gesi na wala hakuna nchi duniani imewahi kufanya hivyo Manufaa ya pekee ambayo wananchi wa Mtwara na Lindi na Tanzania kwa ujumla wanaweza kuyapata ni kama ifuatavyo.
1. Kilimo: gesi asilia itakuza sekta nyingine kwa maana ya kilimo. Gesi pia inaweza kukuza kilimo kwa kuinua sekta ya kilimo kwa maana ya uzalisha wa mbolea na viatilifu vingine kama sulphur ambayo inatumika sana kuthibiti ubwiri unga ambayo inasumbua sana mikorosho.Pia wananchi wataongeza kipato kutokana na kuwa na uzalisha mkubwa katika kilimo.
2. Umeme: gharama za umeme zinaweza kushuka kwa kiasi kikubwa sana haswa ukizingatia kuwa kwa sasa bado gharama ziko juu.Kama ni mfano mzuri, hivi sasa Tanesco imeshusha gharama za uunganishaji umeme ili kuvutia wateja wengi kupata huduma hiyo na kuongeza uzalishaji lakini pia kushusha gharama za uzalishaji kwa ujumla ambapo itachangia kushusha gharama za maisha na kukabiliana na mfumuko wa bei.
3. Elimu : gesi itasaidia kukuza elimu nchini haswa maeneo ya Lindi na Mtwara kwa maana ichangie kuboresha ,lakini pia kuinua elimu kwa watanzania wengi zaidi ili kuweza kunufaisha katika sekta ya gesi na nyinginezo mtambuka
4. Ufugaji: itasaidia katika ufugaji haswa ikizingatiwa sekta hii inahitaji nyama, maziwa na mayai kwa kiasi kikubwa hivyo wananchi wakishikishwa vema itasaidia sana kukuza kipato chao na kuinua uchumi wao na nchi kwa ujumla.
5. Viwanda: uanzishwaji wa viwanda vya mazao ya gesi kwa maana ya petrochemical industries, hii yote itachangia kukuza ajira na mapato kwa Serikali Kuu hadi kufikia ngazi Serikali za vijiji kwa ujumla
6. Mazingira: gesi itasaidia kuhifadhi mazingira kwani matumizi yake yatapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya kuni na mkaa lakini pia inaweza kuwa mbadala wa petroli na dieseli katika magari na mitambo. Hakuna atakae kataa kuwa itasaidia pia kupunguza emission na kuokoa pesa nyingi za kigeni ambazo zingeweza kufanya shghuli nyingine za kiuchumi nchini.
6. Uwekezaji: utalenga kutoa ajira kwa watanzania haswa vijana, lakini watanzania pia wajue haya hayatapatikana kama hawatashiriki kusoma na kupata mafunzo ya kutosha ili kuweza kupata ajira hizo. Tunapozungumzia elimu haihusu sana kupata degree au diploma, hata ngazi ya cheti tu , kwa kozi za kawaida za ufundi kama magari,umeme ,uchomeaji n.k
Serikali kwa kushirikiana na taasisi za kama TPDC,Tanesco,NDC,Narco ,Veta,TPA na wengineo washirikiane kujenga uwezo kwa watanzania kushiriki kwenye sekta na si kutegemea kuagiza kila kitu kutoka nje na wageni wakashika kazi zote kwa kigezo kuwa hatujafikia viwango vya kimataifa kufanya kazi hizo. Changamoto ya makampuni ya uwekezaji (Mult national Companies) kutumia viwango kama ni kigezo cha kuyanyima kazi makampuni yetu ya ndani haswa ya wazawa iangaliwe kwa jicho pana zaidi
Katika maelezo ya Rais ni kuwa tuanzishe mfuko wa kuhifadhi pesa mapato yatokanayo na gesi (gas fund ), naona tukubaliane na hili ila maoni yangu ni vema kuanzisha sovereign development fund ambayo mapato yatumike katika uwekezaji tu na si kwa ajili ya kula na kulipa mishahara au matumizi ya kawaida.
Nchi kama Trinidad & Tobago na Thailand leo zinanufaika katika viwanda vya kemikali (petrochemical industries) ambapo hata bandari na sekta nyinginezo maana kuna multiplier effect inayotokana na uwekezaji katika sekta hii. Hivyo hapana budi Bandari ya Mtwara na Kilwa nazo zikapanuliwa ili kuweza kuinua uchumi wa mikoa ya kusini.
Kwa kuzingatia haya na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi na wawakilishi wao kwa ujumla , itasaidia sana kuondoa dhana iliyojengeka sasa na kuwa hali ya uadui ambao hauna tija kwa ustawi wa nchi yetu.
Tumekuwa na mgogoro na nchi ya Malawi kwa muda sasa, chanzo kikubwa inahisiwa ni rasilimali hizi za gesi na mafuta. Huku hili likiendelea kumekuwa na hisia za kujitunga mgogoro mwingine baina ya Tanzania na Congo. Wakati tunayatafakari haya tumeanza kuweka migogoro ndani ya nchi, ni kweli haya ndio tunayokusudia ?
Naamini kila anayeshinikiza haya yatendeke , wanajua vizuri zaidi ya hivyo. Ni kheri kuwa makini kwa matendo na matamshi yetu kwani ipo siku tutawajibika nayo. Amani ,upendo na utulivu una thamani kubwa kuliko gesi na madini. ‘Kama hujui unakokwenda ,huwezi kupotea njia’’
Murtaza Mangungu(MB)
Kilwa Kaskazini na mjumbe wa POAC
amekuwa na majibu ya jumla sana! waelezwe watanzania wa mtwara watanufaika vip na ges na watapata faida gani ya nyongeza kulinganisha na mikoa mingine( added advantange),tuache siasa za majukwaani kwa kutaka sifa kuwa tunataka umoja wa kitaifa kwa wananchi wanaotaka kujua haki yao! umoja gani wa kitaifa tunaujenga kwa viongozi wa nchi kuwa na mishahara mizuri,maisha mazuri,watoto wao kusoma ulaya na shule za gharama,nyumba za kifahari,posho za mara kwa mara wakati wananchi wa mtwara na lindi watoto wao wanakaa chini,hawajui watalala wapi, wanakula nini,ajira zitatolewaje
ReplyDeleteTunataka mipango madhubuti toka serikalini ni vipi watu wa mtwara watafaidika (added advantage kama alivyosema mheshimiwa hapo juu).......serikali itupe dondoo kama kodi kampuni inaweza kulipa kiasi kadhaa...na mtwara watajengewa mfano shule...ama barabara....ama hospitali.......na upande wa ajira......mheshimiwa amezungumzia kujengwa kiwanda cha cement...sasa cement inahusiana nini na gas.....hicho kiwanda kingejengwa tu hata kama hiyo gas isingekuwepo..............tupe figures...sio porojo porojo.....nini ni business plan ya hao wawekezaji........tujue.....tuna haki kama wananchi kufahamu......
ReplyDeleteUpatikanaji wa gesi kwa Mtwara na Lindi ni sawa wanandoa wakipata mtoto wa kike watamgharamikia mtoto kuanzia malezi, afya na elimu atakapokuwa mkubwa anaolewa na kwenda kwa mumewe watakochopata wazazi hawa ni wajukuu na heshima kwa kuwa wamemlea mtoto wao wa kike mpaka kapata mume. Nadhani hayo ndiyo yatakayo kuwa kule mikoa ya kusini, wamachinga wanapata tabu Dar kwa kujishughulisha na kazi za biashara za kutembea siku kucha na jua kali kwa biashara ya faida ndogo bora warudi nyunmbani na kujifunza namna ya kuweza kunufaika na miradi itakayoanzishwa mikoani mwao, huu ni wakati wa watu wa kusini kuweza kujikwamua kiuchumi kwa manufaa ya nchi nzima, eleweni mtoto aliaye ndiye apewaye maziwa.
ReplyDelete