Saturday, November 17, 2012

KURA YA VETO, MASLAHI BINAFSI NA MISIMAMO YA MAKUNDI VINAPOKWAMISHA KULETA MABADILIKO YA HARAKA KATIKA BARAZA KUU LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA


Na  Mwandishi Maalum
Wajumbe wa Baraza Kuu la 67  la Umoja wa Mataifa (UM) wamekutana mwishoni mwa wiki katika  mkutano ambao pamoja na  kujadili taarifa ya utendaji kazi  wa  Baraza  Kuu la Usalama kwa mwaka uliopita, ulizungumzia pia kuhusu  mageuzi ya kimfumo na uboreshaji wa utendaji  wa majukumu ya Baraza  .
Kwa   miaka 20 sasa, nchi wanachama wa UM wamekuwa wakiendelea  na majadiliano    miongoni kwao, kwa lengo  la kufikia muafaka na kukubaliana ni muundo gani  utakaokidhi matakwa ya  nchi zote  ili kuongeza nafasi za ujumbe wa kudumu, na  nafasi zisizo  kudumu katika chombo hicho muhimu.
Pamoja na ukweli kwamba,  kimsingi  karibu nchi zote zinakubaliana  na hoja na dhana nzima ya kulifumua Baraza hilo, mgawanyiko wa kimakundi, kimaslani, ubinafsi,ubabe na hali ya kutotaka kulegeza misimamo, kunachangia kusuasua na kukatisha tamaa kama kweli itafika wakati ambapo chombo hicho kitakuwa shirikishi na   chenye kutekeleza majukumu yake kwa uwazi zaidi.
Katika mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki, hapa   Makao  Makuu ya UM, karibu wazungumzaji  kutoka nchi hamsini waliochangia mawazo yao katika ajenda hiyo ya  uwakilishi katika Baraza  Kuu, walionyesha  wazi kwamba maneno yamekuwa mengi kuliko vitendo.
Miongoni mwa nchi zilizochangia majadiliano hayo ni Tanzania, ambayo kupitia Mwakilishi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, Balozi  Tuvako Manongi ilisema.
“  Pamoja na utendaji kazi wa kuridhisha wa  Baraza hili,  tunaamini kwamba mfumo mzima wa mageuzi ya  Baraza  hili  umechelewa  mno” akasema Balozi na kuongeza “  Nilazima tulifanyie mabadiliko  Baraza hili ili liweze kuendana  na  hali halisi ya hivi sasa na vilevile kikidhi matarajio ya  nchi wanachama  kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Umoja wa Mataifa”.
Aidha Balozi Manongi akasisitiza kuwa   mageuzi ya  Baraza hilo ni muhimu  pia kwa Baraza lenyewe ili liendelee kuthaminiwa.
Akabainisha kuwa Tanzania  imekuwa ikipigia chapuo umuhimu wa mageuzi ya   Baraza kama iliyoanishwa katika Makubaliano ya Ezulwini na ambao ndio msimamo wa Afrika wa kutaka   ipewe viti viwili vya kudumu na haki zote zikiwamo za kupiga kura ya veto na  viti vitano visivyo vya kudumu.
Mwakilishi huyo wa Tanzania katika UM aliongeza kwamba ni haki wa Afrika kupata viti hivyo kwasababu  karibu mambo yote yanayojadiliwa katika Baraza hilo  yanahusu  Bara hilo.
Akizungumza kuhusu misuguano inayojitokeza ndani ya Baraza hilo,  Balozi Manongi aliungana na wasemaji wengine kwa kuwahisi wajumbe wa baraza   kuzungumza kwa sauti moja hasa pale wanapotakiwa kutolea maamuzi masuala ambayo yanahitaji msimamo wenye   kauli ya pamoja.
Aidha wajumbe wote wanakubaliana na ukweli kwamba Afrika imeonewa kwakutokuwa na uwakilishi wa kudumu licha ya ukubwa wake. Lakini pamoja na kuukubali ukweli huo kumekuwamo na  mikakati na kauli za kusikitisha ambazo kwa namna moja ama nyingine zinalenga katika kuendelea kuibinya Afrika.
Baraza Kuu la Usalama la  UM ,  linaundwa na wajumbe watano wa kudumu maarufu kama P-5,ambao wamekuwapo tangu kuundwa kwa chombo hicho. Na  licha ya kutumia kura yao ya veto, lakini ndiyo wenye maamuzi makubwa ndani ya Baraza  na  kwa kiasi kikubwa kauli zao au misimamo yao ndiyo inayosimama.
Pamoja na  wajumbe hao watano wa kudumu, wapo wajumbe wengine kumi kutoka nchi mbalimbali na ambao  hupigiwa kura za kuingia humo kwa kuzingatia kanda na hudumu kwa miaka  miwili. Wajumbe  hawana haki ya kupiga kura ya veto.
Afrika si bara pekee linalotaka haki ya kuingia katika baraza   yapo mabara  ambayo hayana wawakilishi wa kudumu. Nayo   kupitia makundi ama  au kama nchi moja moja, yamekuwa  yakidai haki hiyo ya kupata kiti cha kudumu au uwakilishi usio wa kudumu.  
Wakubwa ambao ni P-5   licha ya kuwa nao wanaona umuhimu wa kuiboresha hali hiyo,  na wanakubali kwamba Afrika  imebinywa, wamekuwa wakisisitiza kwamba kura ya veto isiguswe, au kupinga nafasi za kudumu kuongozwa.
 Katika majadiliano yote ambayo yamekuwa yakiendelea, baadhi yao wameonyesha wazi wazi nchi gani wanayoitaka  ipatiwe kiti hicho cha kudumu au wamekuwa wakitumia kigezo cha utajiri wa nchi  na utayari wake wa kushiriki au hata kutoa michago ya kifedha, vifaa au rasilimali watu pale linapotokea jambo la dharura.
Kwa maneno mengine   , nchi hizo kubwa katika kulinda nafasi zao hizo tano na kura yao ya veto hawataki kupoteza hadhi  hiyo na hivyo wamekuwa wakitoa kila sababu kujaribu kukwamisha majadiliano ya kurekebisha dhuluma hiyo.
Baadhi ya wajumbe wakichangia majadiliano  hayo, walifikia mahali pa kupashana ukweli, kwamba maslahi binafsi,   ubabe na kila kundi kutokukubali kulegeza msimamo wake   ndiyo iliyowafikisha hapo.

No comments:

Post a Comment