Sunday, November 11, 2012

BURIANI ASKOFU ALOYSIUS BALINA


Na  Emmanuel Makene

Wapendwa Wana wa Shinyanga;
UTANGULIZI
Kifo cha Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Aloysius Balina, aliyefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza siku ya Jumanne 06 Novemba 2012; kimeacha pengo kubwa kwa Kanisa Katoloki Tanzania. Askofu Balina amefariki akiwa amebakiza siku 10 tu afikishe miaka 15 kamili kama Askofu wa Jimbo la Shinyanga. Alikuwa ni Askofu wa tatu wa Jimbo la Shinyanga na wa kwanza wa Jimbo la Geita (Geita & Sengerema). Maaskofu wa Shinyanga waliomtangulia ni Askofu Edward Aloysius McGurkin aliyekuwa Askofu wa Shinyanga kati ya tarehe 04 Julai 1956 hadi alipostaafu 30 Januari 1975. Pia alitanguliwa katika kiti cha uaskofu wa Shinyanga na Askofu Castor Sekwa aliyekuwa Askofu wa Shinyanga kati ya tarehe 08 Agosti 1975 hadi O4 Juni 1996. Askofu McGurkin, ambaye alikuwa raia wa Marekani alifariki tarehe 28 Agosti 1983 na Askofu Sekwa alifariki tarehe 04 Juni 1996.
Kuna hadithi ambayo sikuwai kuidhibitisha; lakini inasemekana Askofu Balina alibatizwa kwa jina la ‘Aloysius’ baada ya wazazi wake kuchagua jina hilo ili afuate mifano mizuri ya kumcha mungu kama alivyofanya Padri Edward Aloysius McGurkin mbaye alikuwa Paroko wao. Na jambo hili kweli lilitimia kwani ‘Aloysius mkubwa’ na ‘Aloysius mdogo’ wote waliweza kuwa maaskofu kama nilivyoelezea hapo awali.
Askofu Balina alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani ya ini kwa muda mrefu. Alikwishatibiwa Ujerumani na Vaticani, na akarejea nchini akiwa mwenye afya njema.
Wapendwa Wana wa Shinyanga;
Kama ilivyo kwa wagonjwa wengine wa kansa; miezi michache alianza tena kusumbuliwa na ugonjwa huo, na afya yake ilizidi kudorora hadi mwezi oktoba 2012, alipolazwa katika Hospitali ya Bugando kabla ya kufikwa na umauti.
Watu wa Shinyanga walilia sana kufuatia msiba huu. Naomba niwaambieni kuwa mwenye shamba huvuna tunda lilostawi katika shamba na ambalo amelipenda sana. Vivyo hivyo kwa Askofu Balina ni mfano wa tunda lililostawi katika shamba na Mwenyezi Mungu amemchukua kutoka katika dunia. “Ni mwanaume gani atakayeishi asione mauti?” (Zaburi 89:48). Nawaombeeni mpate nguvu na faraja ya kuendelea kumcha Mungu.
Mjifariji kama Mtume Paulo alivyowaambia Wathesalonike. “Ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauiti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Sisi tunaamini kwamba yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.” (1 Wathesalonike 4 :13 -14)


KAZI ALIZOZIFANYA AKIWA PADRI MCHAPAKAZI NA MPENDA MAENDELEO
Wapendwa Wana wa Shinyanga;
Askofu Balina alizaliwa Juni 21,1945, Isoso, Ntuzu, Bariadi mkoani Shinyanga. Nilipokuwa sekondari mtu aliyependa kunielezea wasifu wa Askofu Balina ni rafiki yangu wa siku nyingi Peter Bunyazu. Peter ambaye kabla ya pilika zangu za uchaguzi mkuu wa 2010, nakumbuka alikuwa afisa uajiri ofisi ya waziri mkuu pale Ikulu. Peter anatoka kijiji cha jirani na kwao na Baba Askofu Balina. Alimfahamu vizuri Askofu Balina. Na wote wawili, afisa uajiri Peter na Askofu Balina wote wanaongea Kiswahili cha Kinyantuzu hivi.(Nyantuzu ni kikabila ndani ya Wasukuma).
Kwa masomo yangu ya sekondari nilisoma shule ambazo Askofu Balina alisoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, hivyo ilikuwa rahisi kupata watu waliomfahamu ambao walikuwa wakimuongelea uchapa kazi wake na umahiri wake katika kupenda maendeleo. Askofu Balina alisoma Seminari ya Mt. Pius wa Kumi, Makoko, Musoma na baadae Seminari ya Mt. Bikira Maria, Nyegezi, Mwanza kwa masomo ya Kidato cha Tano na cha Sita; shule nilizosoma mimi pia. Mara kadhaa Askofu Balina alikuwa akitembelea seminari hizi. Alisali na kuongea na wanafunzi.
Tulipo kuwa pale Makoko (1992 hadi 1995) tuliwakuta walimu na Mkuu wa Seminari, Padri Krzyszstof Chromy ambaye alikuwa raia wa Poland na mzungumzaji mzuri wa Kiswahili. Tulikuwa tukiwatania wenzetu waliokuwa wakitoka parokia za vijijini kuwa Krzyszstof Chromy alikuwa mahiri katika lugha ya Kiswahili kuliko wao.
Padri Krzyszstof Chromy alitueleza kuwa kati ya mwaka 1975 hadi 1983; akiwa padri, Aloysius  Balina alikuwa Mkuu wa seminari ya Makoko. Mmoja wa wanafunzi wa Askofu Balina ni Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo la Bunda (Bunda & Ukerewe) aliyesoma kidato cha kwanza hadi cha nne pale Makoko Seminari kati ya mwaka 1981 hadi 1984. Askofu Balina aliiwezesha Seminari ya Makoko kununua Boti ya kisasa ya kuvulia samaki. Boti hiyo ipo mpaka leo hii ila sina uhakika kama bado inafanya kazi kwa ufanisi kama hapo awali. Boti hiyo ilikuwa na uwezo wa kwenda umbali wa zaidi ya kilometa 1,000 na kuvua samaki kwani ilikuwa na mashine ya umeme ya kisasa ya kuvulia samaki.
Wapendwa Wana wa Shinyanga;
Nakumbuka tulipokuwa seminari kuna siku boti ile ilivua samaki wengi na sisi wanafunzi mara fulani tuliruhusiwa kwenda kuvua na ile boti katika maji marefu. Siku hiyo ambayo na mimi nilienda tulipata samaki wengi sana hadi yule nahidha wa boti alishangaa sana. Nahodha aliwasiliana na Padri Chromy kwa njia ya radio call, akatushauri kuwa inabidi tuuze samaki wengine kwa wavuvi wadogo wadogo wenye mitumbwi ili tusije tukazama kwa kubeba samaki wengi zaidi ya tani mbili na nusu. Pia nakumbuka Padri Kromy alimtania yule nahodha kuwa lazima samaki wawe wengi kwani mpo pamoja na Yesu (akimaanisha mimi; unajua naitwa Emmanuel kwa vile nilizaliwa siku ya kristmas); na pia akikumbushia muujiza wa Yesu Kristu Katika Injili ya Mt. Luka 5: 1- 13, ambapo Simoni Petro na nduguye Adrea walipata samaki wengi baada ya Bwana Mkubwa Yesu Kristu kuwepo katika mashua yao.
Boti hiyo inayoitwa MV Makoko ilisaidia sana kukuza uchumi wa seminari ya Makoko na kutusaidia kupata samaki kwa ajili ya kitoweo. Wakati ule unajua ndiyo kiwanda cha samaki kimejengwa pale Musoma Mjini na nina kumbuka kilo mmoja ya samaki aina ya sangara ilikuwa Shilingi 800/= hadi 1,000/=. Na kila siku boti ya shule ilikuwa ina uwezo wa kuvua kati ya kilo 1,000 hadi 2,000 kwa masaa sita tu. Seminari ilipata hela kwa ajiri ya kutunisha uchumi wa shule. Niliona kweli Askofu Balina aliona mbali alipoamua kutafuta fedha na kunua boti hiyo kwa ajili ya Seminari. Mpaka leo hii, sijawai kusikia hapa Afrika Mashariki kama kuna shule ya sekondari ambayo ina miliki boti kama ile ya Makoko Seminari. Hakuna shule hata yenye mtumbwi.
Mjomba wangu Nkomola ambaye alikuwa nahodha wa meli za Shirika la Reli zilizoko katika Ziwa Victoria; ndiye aliyekuwa nahodha wa kwanza wa boti ile ya MV Makoko. Kwa sasa mjomba wangu huyo anaendesha MV Nyehunge inayofanya safari kati ya Mwanza na Ukerewe. Siku mmoja alinieleza boti kama ile ya MV Makoko kwa sasa ukitaka kuinunua ni lazima uwe na hela za madafu sizozopungua Shilingi Milioni Mia Nane. Wakati inanunuliwa hiyo boti kati ya mwaka 1980/1982 ilinunuliwa kwa USD 250,000. Wakati huo USD 1 ilikuwa sawa na Shilingi za Tanzania 100/=. Mwaka 1983, Toyota Land Cruiser FJ 55 Station Wagon (lilikuwa gari la kisasa wakati huo) kama ile ambayo Waziri Mkuu Edward Sokoine alipata nayo ajali mwaka 1984 ilikuwa ikiuzwa USD 20,000. Dhamani ya FJ 55 Station Wagon ni sawa na dhamani ya VX V8 Station Wagon kwa sasa.
Nayaandika haya ili mjue jinsi gani Askofu Balina alivyolipenda kanisa na watu wake kuliko yeye binafsi. Haki ya nani…..wangekuwa wenzangu na mimi wala hata boti wasingenunua. Sana sana wangejitaidi wangeleta boti mbovu na visingizio kibao.
Kipindi ambacho Askofu Balina alikuwa Mkuu wa Seminari ya Makoko; Askofu Justine Samba ndiye aliyekuwa Makamu Mkuu wa Seminari. Unaweza ukajiuliza seminari ilikuwaje kinidhamu na kitaaluma.
Wapendwa Wana wa Shinyanga;
Askofu Balina alipokuja kututembelea pale Makoko akiwa Askofu wa Geita, mimi nilikuwa kidato cha kwanza, alituhusia tusome kwa bidii. Na kweli tulikuwa tunasoma sana. Hata tulipokuwa kidato cha pili pale Makoko, shule yetu ilikuwa ya kwanza katika kanda ya ziwa kwenye mtihani wa taifa wa kidato cha pili ikumbukwe wakati huo matokeo ya taifa ya kidato cha pili yalikuwa yakitolewa kikanda. Na nina kumbuka kabisa nilipata 79% kwenye somo la Kemia na ni kawa wa pili katika somo la Kemia na wa pili kikanda kwa masomo yote. Sikustahili kabisa kuwa mwanasheria. Nimekuwa wakili kwa bahati mbaya. Manake wote waliokuwa nyuma yangu ni madakatari. Nakumbuka yule aliyekuwa wa 12 kwa shule zote za kanda ya ziwa katika mtihani wa taifa wa kidato cha pili ni daktari, alihitimu Muhimbili mwaka 2004.
Na darasa langu la kidato cha nne mwaka 1995; Makoko Seminari ilishika nafasi ya 7 kitaifa katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne. Nafasi ambayo mpaka leo hii; Makoko seminari hawajaipata, labda waliosoma seminari hiyo nyuma yangu mnirekebishe. Ila najua hakuna darasa tangu 1995 kufikia nafasi hiyo.
ALIVYOPATA UASKOFU
Kutokana na utumishi wake mwema, Papa Yohane Paulo II alimteua Padri Aloysius Balina kuwa askofu wa Jimbo la Geita. Jumapili, 06 Januari 1985, siku kuu ya epifania na ikiwa ni wiki moja kamili kabla sijaanza darasa la kwanza, Papa Yohane Paulo II alimweka wakfu Padri Balina kuwa Askofu wa Geita huko Vatikani. Mapadri wengine sita waliwekwa wakfu kuwa maaskofu pamoja na Padri Balina mbele ya waamini 10,000 walihudhuria misa huko Vatikani. Mapadri hao ni Padri Kazimierz Gorny (Askofu msaidizi Krakow, Poland) , Padri Bernard Patrick Devlin (Askofu wa Porto e Santa Rufina, Italy), Padri Afonso Nteka (Askofu wa Mbanza Congo, Angola, Padri Fernando Saenz Lacalle (Askofu Msaidizi wa Santa Ana, El Salvador na Padri Jorge Medina Estevez (Askofu Msaidizi wa Rancagua, Chile).
ASKOFU BALINA KATIKA HUDUMA YA AFYA NA MASUALA YA JAMII
Wapendwa Wana wa Shinyanga;
Wakati wa uhai wake, Askofu Balina alishikilia nafasi kadhaa ndani ya Baraza la Maaskofu ambako tangu 1985 alikuwa mwenyekiti wa idara ya afya ya baraza hilo, na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Bugando kwa kipindi cha miaka 27 hadi alipofariki.
Ikumbukwe pia mwaka 1985, Askofu Balina alikuwa muasisi na mwenyekiti wa Tume ya Kikristu ya Huduma za Jamii (Chrisian Social Services Commission-CSSC). Tume hii ina shughulikia shule na hospitali zinazomilikiwa na kanisa ya katoliki, luterani, anglikani na baadhi ya makanisa ya pentekoste. Makao Makuu ya Tume hii yako barabara ya Ali H. Mwinji karibu na kituo cha daladala cha Aga Khan, jijini Dar Es Salaam.
CSSC waliwai kumpa mtu fulani zabuni ya kuweka radio call na mashine za radio call katika shule 12, hospital 4 na magari 6 ili kurahisisha mawasiliano kwani shule na hospitali hizo ziko vijijini. Zabuni hiyo ilikuwa na dhamani ya Milioni 24. Kwa bahati mbaya huyo fisadi aliweka radio call 4 tu akaingia mitini. Nikapewa kazi na hiyo Tume ya kumstaki huyo bwana mahakamani. Nakumbuka ndio ilikuwa kesi yangu ya kwanza ya madai mara baada ya kuanza kazi za uwakili. Nika-mbuliza mahakamani. Unajua kazi ya kupewa na baba Askofu nikaifanya kwa ufundi kiasi kwamba hadi hakimu akanisifia kwenye hukumu kuwa nimefanya kazi kama vile nina miaka 30 ya uwakili wakati nilikuwa na miezi miwili tu kwenye taaluma. Yule fisadi akaambiwa ailipe fidia Tume/CSSC pamoja na gharama ya usumbufu zaidi ya milioni 46. Unadhani nililipwa shilingi ngapi na Tume? Na unaweza fikiri Askofu Balina alisema nini kuhusu kesi hii?
Ila sitasahau siku mmoja nilichanganya namba za simu kati ya namba ya Askofu Aloysius Balina na Aloysius (Aloyce) Bahebe. Naelewa kilichokea ila sisemi ng’o.
Askofu Balina ni mmoja wa maaskofu wachache wa Kikatoliki ambaye alitazama maisha ya waamini wake na watu wote wa majimbo ya Geita na Shinyanga, katika mahitaji yote ya kiroho na kimwili. Aidha, ni mmoja wa viongozi wa dini aliyesimamia kikamilifu kuinua Hospitali ya Bugando na hasa juhudi zake zilizosukuma kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Afya Bugando. Wakati Jakaya Kikwete akiwa waziri wa mambo ya nje, pia rafiki yake na mtani wake alimsaidia katika kutafuta fedha za kuanzisha Chuo hicho kwa wafadhiri mbalimbali huko Marekani. Raisi Kikwete alisema kuwa aliongea na Askofu Balina kwa simu kumjulia hali na alipanga kwenda kumsalimu Askofu Balina hospitalini Bugando mara atakapomaliza kikao cha Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM mjini, Dodoma. Kwa bahati mbaya Raisi Kikwete hakuweza kutumiza nia yake kwani Askofu Balina alifariki Jumanne wiki hii.
Kadhalika askofu Balina, alifanya kazi kubwa akishirikiana na maaskofu wenzake, kuhakikisha kuwa kinaanzishwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine, na hatimaye kufikia mafanikio makubwa.
Pia Baba Askofu alikuwa mmoja wa makamishina wa kwanza wa Tume ya Ukimwi ya Tanzania na amekuwa mwenyekiti wa kwanza wa Chuo cha Tiba na Sayansi za Afya cha Bungando kilipo anzishwa mwaka 2000 mpaka alipofariki.Ni faraja pia kuona hata padri mmoja wa jimbo la Shinyanga ambaye tulikuwa naye Makoko seminari, Padri Steven Kadilo amekuwa daktari wa binadamu baada ya kusoma katika chuo hicho.
Alimekuwa muda mrefu katika harakati za mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI. Na nina kumbuka wakati Raisi Mstaafu wa Marekani Bill Clintoni na Raisi George Bush wa Marekani walipotembbelea mradi wa kanisa katoliki wa PASADA, Askofu Balina alikuwepo, kati ya viongozi wa kanisa waliokuwepo katika msafara ule. Mimi wakati huo bado kiongozi wa vijana mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na vijana wenzangu wakakamavu tulipewa kazi maalumu na viongozi wa serikali wa mkoa. Tulikuwa pale PASADA tangu jana yake hadi wageni walipofika. Tuliongea na Baba Balina sana katika wakati walinzi wa Clinton/Bush walipokuwa wanafanya ukaguzi wa awali.  

Wapendwa Wana wa Shinyanga;

Kufariki kwa Askofu Balina ni huzuni kubwa sana pia huko nyumbani kwao Parokia ya Mtakatifu Yohana Mwinjili, Bariadi (ambayo kwa sasa imo ndani ya mkoa mpya wa Simuyu).Paroko wa Bariadi Padri FK (Fabiani Kushoka) ambaye tulisoma nae pale Nyegezi Seminari ana jukumu kubwa sana katika msiba huu.

Rafiki yangu Padri Adolf Makandago na muelewa si mtu anayeweza kuwa na moyo wa kuaminini kwa haraka kuwa Askofu Balina amefariki. Lakini itabidi ajitaidi kuamini hivyo. Sijui ni jinsi gani rafiki yangu Padri Emmanuel Makolo ameweza kuupokea msiba huu.

SHULE ALIZOANZISHA NA MCHANGO WAKE KATIKA ELIMU

 Alipokuwa Askofu wa Geita alianzisha seminari ya Sengerema inayotoa mafunzo ya kidato cha kwanza hadi cha nne. Pia ni moja kati ya shule bora kabisa Tanzania ingawa haina miaka 20 tangu ianzishwe.

Askofu Balina alikuwa mpenda maendeleo ya elimu sana. Alipoteuliwa kuwa Askofu wa Shinyanga alianzisha Seminari ya Pre-form one ya Sayusayu tarehe 16th February, 2004 pale Sayusayu. Seminari hii inachukuwa wanafunzi zaidi ya 300.  Wanafunzi katika seminari hii hutokea majimbo ya Musoma, Mwanza, Geita, Shinyanga, and jimbo jipya la Bunda. Wanafunzi husoma kwa mwaka mmoja  baada ya kumaliza darasa la saba na kisha hupelekwa kuanza kidatao cha kwanza katika seminari za Nyegezi, Makoko, Sengerema and Shanwa.
Seminary ya Shanwa, Maswa yenye kidato cha kwanza hadi cha nne amabayo aliianzisha Askofu Balina kwani jimbo la Shinyanga walikuwa hawana seminari hata mmoja.  Vilevile Askofu Balina alianzisha shule ya Balina English Medium School.
Aliweza kuwasomesha kwa kuwalipia ada za masomo ya vyuo vikuu wanafunzi mbalimbali wanaotoka katika familia maskini kama vile Mhe. Vick Kamata ambaye alilipiwa ada ya Chuo Kikuu na Askofu Balina. Kwa sasa Vick kamata ni mbunge wa Bunge la Tanzania. Hata Vick Kamata mwenyewe amewahi kukiri kuwa kama siyo Askofu Balina basi yeye asingeweza kusoma hadi chuo kikuu. Pia Mhe Vick Kamata aliwai kumtungia wimbo Askofu Balina. Wimbo huo ni wa Kisukuma na una msifu Askofu kwa moyo wake wa kusaidia wanyonge. Lakini cha ajabu, rafiki yangu Mwalimu Renatus Mashimba, mwanaharakati wa Kisukuma hajawai kuusikia huo wimbo.

KUDHAMINI HAKI ZA BINADAMU NA MAFUNDISHO YAKE

Ukiacha moyo wake wa kujituma katika kushughulikia wagonjwa wa UKIMWI, kusaidia utoaji wa huduma za afya na elimu ; Askofu Balina alikuwa ni mstari wa mbele katika kudai na kutetea haki za binadamu. Alisimama kidete kuhakikisha mauaji ya albino yanakomeshwa. Vilevile alihamasisha watu waachane na mila potofu za kuuwa akina mama wazee kwa kuwatuhumu kuwa wachawi. Alipigania haki za kiraia na alipenda kila raia wa Tanzania apate haki anayostahili.

Baba Balina alipinga utoaji wa mimba na kufundisha kuwa kutoa mimba ni kuuwa kwani mimba ni uhai pia. Unapotoa mimba ujue umetoa uhai wa binadamu mchanga. Na mimi huwa naunga mkono suala hili. Kwani kuna hawa watu wanaojiita ‘wanaharakati wa haki za binadamu’ waliwai kuniuliza maoni yangu kuhusu kutoa mimba kama ni sahihi au la ?. Niliwajibu jibu ambalo hawatalisahau. Niliwaambia kama mnaona kutoa mimba ni jambo sahihi basi kwanza jiulize, je mama yako angetoa mimba wewe ungekuwepo ? Je ungeweza kuja kuniuliza hilo swali ? Kisha nikawaeleza mimi nimeishazaliwa inawezekana sijui uchungu wa kutoa mimba, nendeni mkawaulize watoto wachanga ambao bado hawajazaliwa kama wanapenda wazaliwe au mimba hizo ziharibiwe! Muulize ambaye bado hajazaliwa kama anataka azaliwe au la ! ‘Hivi Bikira Maria angetoa mimba na kumuua Yesu, leo hii kungekuwa na ukristu ?’ aliwai kuhoji Askofu Balina katika moja ya mahubiri yake.

Wakati Umoja wa Mataifa uliposhindwa kupitisha itifaki ya kuruhusu utoaji mimba ; siku hiyo hiyo Aprili 24, 1994 Papa Johana Paulo wa II alimtangaza daktari bingwa wa watoto wa Italia aliyeitwa Gianna Beretta Molla kuwa mwenye heri. Dakatari huyu alikuwa mjamzito katika uzao wake wa nne baada ya mbili kuharibika. Madaktari wenzie walimshauri mapema kabla ya mimba kufika miezi tisa ; achague kutoa mimba au kuruhusu mtoto azaliwe ila yeye atakufa kutokana na hali ya ujauzito kuwa mbaya kama atakataa kutoa mimba. Yeye alichagua mtoto apone na alikataa kutoa mimba kuokoa maisha yake. Siku ya Ijumaa Kuu tarehe 21 Aprili 1962,  Dkt. Giana alienda hospitali alifungua mtoto wake wa nne aliyemwita Gianna Emanuela ila yeye Dkt. Gianna alipata maumivu makali sana na alifariki siku saba baadae. Aliamini kuwa hata mtoto aliyeko tumboni anastahili na ana haki ya kuishi.

‘Kama kuna haja ya kuchagua nani aishi kati yangu na mtoto aliye tumboni mwangu....sina shaka kabisa nitachagua mtoto aokolewe.’ Alisema Dkt. Gianna.

Tarehe 16 Mei 2004, Papa Yohana Paulo wa II alimtangaza Gianna Molla kuwa Mtakatifu. Mume wa Dkt. Gianna, aliyeitwa Pietro Molla alikuwepo siku hiyo na alihudhuria sherehe ya mke wake kutangazwa mtakatifu. Na ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia ya kanisa kwa mume kushuhudia mke wake akitangazwa mtakatifu. Kwa sasa Mt. Dkt. Gianna Beretta Molla ni mzimamizi wa kiroho wa watoto ambao hawajazaliwa, madaktari na wakina mama. Vituo mbali mbali vya kuwasaidia afya za wajawazito ili waweze kujifungua salama vimefunguliwa huko Marekani na Ulaya kwa heshima ya jina lake. Mume wa Mt. Dkt. Gianna Beretta Molla alifariki mwaka 2010 karibu miaka 50 baada ya mkewe kufariki.

Wapendwa Wana wa Shinyanga;

Siku hizi nchi yetu imevamiwa na hawa wanaijiita wanaharakati wa haki za binadamu wakati ni wababaishaji wakubwa.  Hebu kuna li-NGO moja kubwa kweli bajeti yake zaidi ya Bilioni Mbili kwa mwaka. Kila siku linalipia Shilingi Milioni Tano hadi Kumi za matangazo kwenye TV, Radio na Magazeti. Mimi nimefanya kazi katika vyombovikubwa vya habari nalifahamu hili fika. Matangazo hayo ni yakutuonesha eti wanafunzi wanavyosoma katika hali duni ya kutokuwa na madawati, vitabu, upungufu wa walimu na ubovu wa majengo ya shule za serikali. Sasa mimi huwa najiuliza kwa akili yangu ya kishamba. Kwanini hizo hela wanazitumia kulipia matangzo kwenye vyombo vya habari kwanini hilo li-NGO lisiende kununua madawati, vitabu, kulipa walimu na kujenga madarasa. Kazi ya hili li-NGO ni kutukejeli, na wenye akili tunachekelea. Kila mtu anajua hali ya shule zetu ni duni. Hakuna haja ya kutuonesha......eti li-NGO lenu linasema..... ‘Tafakari...Chukua hatua !’.  Kama lengo la li-NGO hili ni kutaka serikali ijue. Kwa nini wakuu wa hili li-NGO hawamwandiki barua waziri wa elimu ambayo ni gharama nafuu. Kama hela zimewazidi mngempatia Hayati Askofu Balina aendeleze miradi yake ya afya na elimu ili Mungu awabariki. Na hlo li-NGO lenu mlilolianzisha kwa dhambi na mtadumu nalo kwa dhambi.

Askofu Balina alipinga ndoa za watu wenye jinsi mmoja kwani zinaweza kuleta maangamizi kwa binadamu kama yale ya Sodoma na Gomora (Mwanzo 19). Alisisitiza kuwa Mungu aliwaumba mume na mke na akawabariki ikiwa ni ishara ya kuanzisha sakramenti ya ndoa (Mwanzo 2 : 22-24). Lakini leo hii ni mambo ya ajabu ajabu tu. Mimi nimepata bahati ya kuwa kiongozi wa vijana kwa muda mrefu. Nimejionea jinsi vijana wa kitanzania walivyoharibikiwa. Si wa kike, si wa kiume.

ASKOFU BALINA NA SIASA ZA TANZANIA

Wapendwa Wana wa Shinyanga;

Askofu Balina alikemea sana rushwa na alichukizwa sana na vitendo vya rushwa. Alipenda Tanzania iwe nchi isiyosumbuliwa na dhambi ya tamaa na rushwa.

Alikuwa ni mjamaa wa kweli kabisa na mfuasi mkubwa wa siasa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Ndiyo maana hakujilimbikizia mali. Miradi aliyoianzisha na kuitafutia fedha za kuiendesha inaendelezwa na watu wengine na yeye hakuwa mbia. Na tena miradi mingine haipo jimboni kwake Shinyanga. Tangu mfumo wa vyama vingi uanze rasmi tarehe 01 Julai 1992; sikuwai kusikia kama Askofu Balina alirudisha kadi yake ya CCM. Mimi siyo malaika lakini sisemi uongo. Nilijaribu wakati fulani kumuuliza Katibu wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga akaniambia hakuwai kuona akirudisha kadi ya CCM. Kwa vile Askofu Balina hakuwai kuwa mwananchama wa Chama kingine cha siasa zaidi ya CCM; naamini kuwa alibaki kuwa mwananchama mwaminifu wa CCM. Na hata kama hakuwa mwana-CCM; Askofu hakuonekana kama alikuwa akiamini kuwa kuna Chama zaidi ya CCM kinaweza kuiongoza Tanzania. Alikuwa na busara, hakutaka kuwaingilia watanzania katika kuchagua viongozi wao katika chaguzi kuu. Hata hivyo naamini kuwa mpaka Baba Askofu anafariki; amekufa akijua kuwa uchaguzi wa 2010 kuna mahala tulikosea kuchagua viongozi. Tulijifanya tunataka viongozi wa mageuzi ili walete mageuzi. Kumbe tuliitaji viongozi wa kimapinduzi ili walete mapinduzi ya kiuchumi, kilimo na huduma za jamii. Kwani tumesahau kuwa mapinduzi huwa hayana mwisho. Naamini Baba Aksofu mpaka anafariki alitambua kuwa uchaguzi wa 2010 tulishindwa kutambua kati ya mageuzi na mapinduzi.

Kumbukeni kuwa mwaka 1985 alipoanza kazi kama Mwenyekiti wa idara ya afya ya Baraza la Maaskofu na Mwenyekiti wa CSSC; Dr. Wilbroad Slaa alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maskofu. Ingawa Dr. Slaa hajawai kusema hadharani kwanini aliamua kuacha upadri wakati upadri ni agano mpaka kufa. Duniani huwa kuna watu ambao ni wepesi kuapa na wepesi kuasi viapo vyao. Padri hapaswi kuoa kama ilivyokuwa kwa Yesu Kristu,muasisi wa upadri. Ili aweze kutoa sadaka safi kwa mungu, padri hapaswi kuwa na mke wala familia. Kama unaona huwezi kuishi bila mke basi usiwe padri waachie waliobarikiwa. Kwanini unakuwa padri kisha unakimbilia kuoa? Hivi kweli mtu unataka kwenda kuoa Ukerewe halafu unasema unaogopa kuvuka maji!. Hata mitume wa Yesu waliokuwa wameoa kama Mt. Petro waliacha kila kitu kumfuta Yesu. Upadri wa Kanisa la Ulimwengu (Katoliki) siyo ubunge wala maigizo. Papa Yohana Paulo aliwahi kusema maneno haya kuhusu mapadri, namnukuu na sitaki kutafsiri kwa Kiswahili: “You are priests, not social or political leaders. Let us not be under illusion that we are serving the Gospel through an exaggerated interest in the wide field of temporal problems.”

Baba Balina anajua mazuri na mapungufu ya Dr. Slaa. Anajua tulipokuwa tunaenda kwa kufuata muziki badala ya kufuata barabara. Kwa bahati mbaya kwa nafasi yake katika kanisa, Baba Balina alikuwa hawezi kutuzia kwa sauti ya juu. Ila wenye macho, tuliona. Sasa hayupo, sijui nani atatuonyesha njia? Lakini wana-wa-uzao wa Adam ni wagumu kuelekezwa. Hata yale mazuri tunayachukia. Usharobaro na ubishororo umetujaa tangu kwenye unyayo hadi utosini (samahani kwa lugha mbaya ila naamini ujumbe umefika).

Wapendwa Wana wa Shinyanga;

Askofu Balina alikuwa rafiki mkubwa wa Raisi Kikwete. Raisi Kikwete katika salamu za rambirambi mara tu baada ya Askifu kufariki alisema yafuatayo

“Mhashamu Baba Askofu Balina alikuwa kiongozi hodari na mwadilifu ambaye siyo tu alichangia kipekee katika mwenendo mzuri wa kiroho wa waumini wa Kanisa Katoliki bali pia katika maendeleo ya Watanzania wote kwa jumla.”

“Kifo chake kimetuondolea kiongozi mwema ambaye tutazikosa busara zake na uongozi wake. ………… sisi ndani ya Serikali tutaendelea kutambua na kuthamini mchango wa Askofu Balina alioutoa kwa nchi yetu katika maisha yake,” mwisho wa kunukuu.

Raisi Kikwete alipokuwa akitoa salaamu za rambirambi Jumamosi tarehe 10 Novemba 2012 katika Kanisa Kuu la (Cathedral) Shinyanga alisema walikuwa marafiki na Askofu Balina. Mhe Raisi alisema walisumbuka wote kutafuta hela za kuanzisha Chuo Cha Tiba na Sayansi za Afya cha Bugando. Vilevile walisafiri hadi Marekani na Askofu Balina kuwashawishi baadhi wa matajiri wa Marekani akiwemo bilionea Sanford I. Weill ambaye alikubali kwa sharti la kuongeza jina lake katika jina la chuo na hospitali. Huyo bilionea kwa msiomfahamu ni mmiliki mojawapo wa makampuni ya CITI ambayo yanamiliki benki tajiri ya kimarekani ambayo hata hapa Tanzania ipo. Benki hiyo inaitwa CITI BENKI. Ndiyo maana mpaka leo hii chuo na hospitali zina jina ‘Weill Bugando’ badala la ‘Bugando’. Kichekesho kimoja ninachokifahamu kuhusu huyo bilionea ni kuwa jina lake ni Sanford I. Weill. Herufi ‘I’ ambayo ni jina lake la katika halina kirefu chake kwa sababu mama yake alitaka kumpa jina la katikati linaloanza na herufi ‘I’ hivyo akamuandikisha kwa jina hilo ili azidi kutafiti hilo jina. Kwa bahati mbaya mama yake hakufanya hivyo. Kwa hiyo mpaka leo herufi ‘I’ katika jina lake la katikati halina kirefu chake.

Askofu Balina na mtani (wasukuma ni watani wa wakwele) wake Raisi Kikwete waliweka tofauti za dini zao pembeni na wakashilingiana katika kuendeleza sekta ya afya na elimu ya tiba. Lakini leo hii kuna magenge ya waislamu ambao kazi yao ni kubwabwaja. Eti kila sera na mipango ya serikali eti kwao ni dhambi. Kila kukicha maandamano, matusi, kwenye maandamano watu wanaibiwa njiani wanakopita mpaka nyumba za ibada zinachomwa. Hivi wewe ukichomewa nyumba yako au nyumba ya ibada utasikia raha?  Wapo wanasiasa uchwara nao wanajihalalisha kwa sera za udini kisha tunawechekea na kuwashambikia eti ni wa dini yangu.

Askofu Balina atakumbukwa daima kama padri mchapakazi, askofu mwadilifu, mchungaji mwema na kiongozi mpenda maendeleo. Alijitolea sana katika sekta ya afya hadi wako watu walidhani kitaaluma alikuwa daktari wa binadamu.

HITIMISHO

Askofu Balina amekuwa padri kwa miaka 41 na miezi minne na amekuwa askofu kwa miaka 27 na miezi nane. Tunamuombea Askofu Balina apumzike kwa amani. Ingawa kuna hadithi moja huwa inasema maaskofu wakifariki na wakiweza kwenda mbinguni hupokelewa kimya kimya. Ila wanasheria ambao huwa wanaenda mbinguni, Bwana Mungu huwa anawafanyia sherehe. Inasemekana kuna mwanasheria mmoja alifariki. Alipoenda mbinguni Mungu akaamua kumfanyia sherehe ya kumpokea mbinguni. Sasa baadhi ya maaskafu waliokuwa mbinguni wakamwomba Mt. Petro amuulize Mungu swali hili. Kwanini mwanasheria (mtu wa dhambi sana akiwa duniani) amefanyiwa sherehe alipokuja mbinguni na wao maaskofu walipoenda mbinguni baada ya kutumia maisha yao yote katika kumtumikia Mungu lakini hawakufanyiwa sherehe. Inasemekana Mungu alimwambia Mt. Petro kuwa huyu mwanasheria alistahili kufanyiwa sherehe kwani ndiye mwanansheria wa kwanza kufika mbinguni na nyie maaskofu mara kwa mara huwa mnakuja huku.

Baba Balina hakuwa mtu wa kukata tamaa. Amekuwa padri na askofu mpaka mauti yalipomkuta. Hakurudi nyuma katika kulitumia kanisa la kristu. Vijana wa kileo tunaoa leo na kesho kutalaki wake tujifunze kutoka kwa Baba Balina ambaye hakuwaacha kondoo wake. Wale mlio katika miito ya upadri mjifunze kuwa wavumilivu katika kumfuata Yesu Kristu bila kutamanishwa na anasa za kidunia na kuuasi upadri.

Ni vigumu kwa fikra za kibindamu kuelewa fumbo la kifo. Kwani hata ukiwa na kalenda, haiwezi kukueleza utakufa lini. Kifo kiisha bisha hodi huwezi kukizuia hata kwa saa moja. Ni vema kufanya kitubio tukiwa na afya kwani hatujui siku wa saa. Mwalimu Nyerere alikuwa akiungama kila siku ya mungu (fikiria Raisi wa nchi huyo, wewe je, una ngoja nini). “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa”.(Ayubu 14:1-2).

Mungu hana haja ya maua tu bali matunda (Luka 13:7). Tujiulize sisi tulio hai, je tunatenda mema ? Au tu-maua miaka yote na hatuzai matunda ? Hakuna binadamu anayeweza kulimudu fumbo hili kwa urahisi. Imani ni maua na matunda ni matendo mema (Yakobo 2 :14-17). Raha ya milele, umpe ee Bwana, na mwanga wa milele umuangazie, apumzike kwa amani. Amina.

1 comment: