Friday, September 7, 2012

MAALIM SEIF SHARIF HAMAD ZIARANI NCHINI MAREKANI

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akibadilishana mawazo na balozi wa Cape Verde nchini Marekani bibi Fatima Veiga (kushoto). Wa pili kushoto ni balozi wa Tanzania nchini Marekani bibi Mwanaidi Maajar na kulia ni afisa ubalozi wa Tanzania nchini humo Suleiman Saleh.
Bw.Suleiman Saleh, Afisa Ubalozi wa Tanzania Washington DC akizungumza na Balozi wa Malaysia nchini Marekani Mhe.Othman Hashim huku Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.Seif Shariff Hamad akisikiliza kwa makini.
Mhe.Seif Sharif Hamad Balozi wa Malaysia nchini Marekani Mhe.Othman Hashim.
Makamu wa Kwanza wa Rais SMZ Mhe.Seif Sharif Hamad akizumngumza na Balozi wa Malaysia nchi Marekani Mhe.Othman Hashim.Mazunngumzo yao yalihusu ushiriakiano baina ya Malaysia na Tanzania.
Balozi Jorge Hernandez wa Honduras (katikati), akisisitiza jambo wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko nchini Marekani. Kulia ni Balozi wa Brazil nchini Marekani, Mauro Vieira.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimia na mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Syracuse cha mjini New York Dr. Horace Campbell. Dr. Horace aliwahi kuwa mkufunzi wa siku nyingi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi kutoka nchi mbali mbali duniani wanaoziwakilisha nchi zao nchini Marekani. Mabalozi hao kutoka kushoto ni balozi Harold Foresyth (Peru), Balozi Mauro Vieira (Brazil) na Balozi Jorge Arguello (Argentina).
Balozi wa Msumbiji nchini Marekani (kushoto) akibadilishana mawazo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko Marekani. Kulia ni balozi wa Cape Verde bibi Fatima Veiga. (Picha zote na mpiga picha maalum, New York).

NEW YORK.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amekutana na mabalozi wa nchi mbali mbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini Marekani na kubadilishana mawazo juu ya masuala tofauti yakiwemo ya kiuchumi, afya na teknolojia ya habari.

Katika mazungumzo yake na balozi wa Malaysia nchini Marekani bwana Othman Hashim, Maalim Seif amesema Zanzibar inaweza kushirikiana na Malaysia katika maeneo mbali mbali ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu ya juu, biashara, uwekezaji na kilimo.

Maeneo mengine ambayo Zanzibar na Malaysia zinaweza kushirikiana ni teknolojia ya habari, benki za kiislamu na utalii. Katika mazungumzo hayo viongozi hao pia wamekubaliana juu ya suala la kufuatilia mazungumzo hayo ambapo Zanzibar itatuma maofisa wake nchini Malaysia, ili kuona namna ya kukuza mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo mbili.

Kabla ya kukutana na mabalozi hao, Makamu wa Kwanza wa Rais alipata fursa ya kushiriki kwenye mikutano na makongamano mbali mbali juu ya mambo ya siasa na mahusiano ya kimataifa yaliyoandaliwa na taasisi ya National Democratic Institute mjini North Carolina, Marekani. 

Makamu wa Kwanza wa Rais pia amefanya mazungumzo na mkuu wa taasisi inayojishughulisha na utoaji wa misaada ya vifaa vya hospitali katika nchi mbali mbali duniani Bwana Abdul Makembe Kimario.

Katika mazungumzo yao viongozi hao walijadiliana juu ya uwezekano wa Zanzibar kuweza kufaidika na misaada hiyo ya vifaa vikiwemo vitanda vya kulazia wagonjwa, vitanda maalum vya kufanyia upasuaji na mashine za uchunguzi wa maradhi mbali mbali katika hospitali zake za Wilaya na hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Taasisi hiyo imekuwa ikijishughulisha na utoaji wa misaada ya vifaa vya hospitali kwa zaidi ya nchi 124 duniani zikiwemo China, India na Israel. Maalim Seif pamoja na viongozi na mabalozi wa nchi mbali mbali pia walihudhuria katika kongamano maalum, ambapo walishuhudia viongozi wa vyama vya Republican na Democratic vya nchini Marekani wakihojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 6 mwaka huu nchini humo, ambapo chama cha Demcratic kinawakilishwa na Rais wa sasa wa Marekani Rais Barack Obama na chama cha Republican kinawakilishwa na Bwana Mitt Romney.

Makamu wa Kwanza wa Rais aliwasili nchini Marekani tarehe 02 mwezi huu kwa ziara ya kikazi. Katika uwanja wa ndege wa New York alipokelewa na Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvaku Manongi na huko Mjini North Carolina alipokewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani bibi Mwanaidi Sinare Maajar.

No comments:

Post a Comment