Sunday, September 30, 2012

kampeni ya kutoa elimu, utetezi na msada kwa gonjwa saratani ya tezi dume.


Ndugu Dismas Massawe, (aliyeinua gazeti) CEO na Mkurugenzi Mtendaji wa MAN Magazine akiongea na waandishi kwa nini kampuni yake inajihusisha kwa karibu katika kampeini ya kutoa elimu, utetezi na msada kwa gonjwa saratni ya tezi dume. Wengine katika picha ni Dr. Kandusi, Mratibu wa Tanzania 50 Plus Campaign na Mr. Kaale mtaalamu wa tiba ya mionzi wa
 Ocean Road Cancer Institute.

Mimi nimefuatana na Mch. Dr. Emmanuel Kandusi ambaye ni mwaathirika, muhanga na manusura wa saratani ya tezi dume (prostate cancer) ili niongee nanyi machache. Dr. Kandusi baada ya kuugua gonjwa hilo, gonjwa linalowasibu wanaume tu, akiwajali wanaume wenzake, aliona kukaa kimya si faida “alivunja ukimya” na kuanza kutoa elimu na kuwasaidia wanaume wenzake katika kukabiliana na saratani ya tezi dume. Saratani ni gonjwa ambalo limepamba moto dunia nzima lakini sisi huku Afrika tunaathirika sana. Zipo aina zaidi ya 100 za saratani, lakini saratani ya tezi dume ndio saratani hatari sana inayowapata wanaume tu na hasa kuanzia hata miaka 40 na kuendelea.

Kati ya nukta ninazoweza kuzitaja kwa haraka haraka ni hizi:
·        Katika wanaume 5, mmoja atapata saratani ya tezi dume;
·        Kila dakika 5 wanaume wawili wanagunduliwa wana saratani ya tezi dume;
·        Katika wanaume 100 wanaogundulika na saratani za aina mbali mbali, 25 wanakuwa na saratani ya tezi dume;
·        Mtu ambaye ana ndugu wa karibu (baba, babu, kaka etc) yuko katika hali hatarishi kupata saratani ya tezi dume;
·        Saratani ya tezi dume inaua mtu mmoja kila dakika 13;
·        Mbaya zaidi saratani ya tezi dume huwezi kuigundua mwanzoni. Inachukua miaka zaidi ya 8 ndipo dalili zinmapoanza kujitokeza.
Kwa uchache ukiangalia haya niliyogusia utaona kuna umuhimu mkubwa kutoa elimu kwa jamii ili akina baba na hata akina mama wajue hali hatarishi, dalili za saratani   ya tezi dume na hasa umuhimu wa kufanya uchunguzi wa tezi dume kwa wanaume wote ikibidi kuanzia miaka 40. Kama ilivyo kwa saratani nyingi, saratani ya tezi dume ikigundulika mapema inatibika kwa urahisi zaidi.
Sisi wa MAN Magazine, gazeti linalochapisha maswala mengi yanayomhusu mwanaume, tulivutiwa tokea mwanzo wa Tanzania 50 Plus Campaign na tukaona wadau wa kampeini hii na wadau wa MAN Magazine ni wamoja – WANAUME. Tumekuwa mstari wa mbele kuchapisha makala nyingi toka Tanzania 50 Plus Campaign na wasomaji wetu wame-appreciate sana elimu hiyo. Pia tumekuwa kila tunapoweza kuchangia Tanzania 50 Plus Campaign katika hali na mali.
Namalizia kwa kutoa changamoto kwa wenzangu waandishi wa habari, lishikieni bango gonjwa hili – saratani na hususani saratani ya tezi dume. Serikali iweke mikakati mtambuka kuhusu saratani na kuitekeleza kwa vitendo. Wafanyabiashara na makampuni mbalimbali yaunge mkono kampeini zote za saratani – za matiti, shingo ya uzazi, ngozi nk na pia saratani ya tezi dume inayoendeshwa na Tanzania 50 Plus Campaign. Gonjwa hili si la kitabaka, leo kwangu kesho kwako !
Ahsanteni kwa kunisikiliza !

Dismus Massawe
Mkurugenzi Mtendaji
MAN Magazine
September 28, 2012 AD

No comments:

Post a Comment