Thursday, September 27, 2012

JE DESEMBA HII KUTAKUWA NA SIKU TATU ZA GIZA?

Na Dkt N. T. Jiwaji

Masuala ya angani ni ya ajabu na ya kumvutia kila mtu kiasi cha kuamini kila kitakachowekwa mbele yetu kwa kutumia taswira za Mwezi mkubwa, mkusanyiko wa nyota zinazomeremeta, na magimba ya angani yenye maumbo ya ajabu na ya kutatanisha, na kadhalika.  

Matukio mawili ya hivi karibuni yanaonesha umaasuma wetu katika kuamini habari yoyote inayotolewa, ikichanganyika na shauku tunayopata kwa kusikia habari za maajabu ya angani.  Lakini je hayo maajabu kweli yanaweza kutokea?  Je tumejiuliza ukweli wa maelezo tuliyosikia?

Mkanganyiko wa kwanza ulitokea mwezi uliopita tarehe 31 Agosti, ulikuwa unahusu kuwapo Miezi miwili ya rangi ya bluu. Baadhi ya tovuti katika mtandao, zilionesha Mwezi mpevu uliowekewa rangi ya bluu. Kwa bahati nzuri, usiku wa tarehe 31 Agosti, hakukuwa na Mwezi wa rangi ya bluu ila ulionekana Mwezi mpevu mmoja unaong’ara kwa mwanga mweupe kama unavyo kuwa kawaida.

Kilichotokea ni kwamba, kwa vile mzunguko mmoja wa Mwezi huchukuwa siku 29 na nusu, na mwezi mmoja kawaida una siku 30 au 31, inawezekana kwamba katika mwezi mmoja kukawa na Miezi pevu miwili.  Hali hii hutokea kwa nadra sana, kwa wastani wa mara moja kila mwaka mmoja na nusu au mara moja katika siku 600 hivi, ambayo ni nadra sana.  

Katika semi ya Kiingereza, Mwezi mpevu wa pili katika mwezi kama huo huitwa “blue Moon” (yaani Mwezi bluu) kutokana na usemi wao “Once in a blue Moon” (yaani, “mara moja katika Mwezi bluu”).  Usemi huu hutumika kuelezea tukio ambalo si la kawaida.  Haina maana kwamba rangi ya Mwezi itabadilika - ni usemi tu wa Kimombo. Kisayansi haiwezekani kabisa kwa Mwezi kugeuka kuwa rangi bluu.

Mwezi mpevu wa kwanza katika Agosti ulikuwa tarehe 2 na Mwezi mpevu wa pili ulitokea tarehe 31 Agosti.  Kwa hiyo usiku wa tarehe 31 Agosti, baadhi ya watu ambao hawaelewi kuwa rangi ya Mwezi haiwezi kubadilika kuwa bluu walikiri kwa msisitizo kuwa waliona Mwezi mpevu ukiwa na rangi bluu!! 

Kwa vile Agosti ilikuwa na Miezi pevu miwili, wengine walidai kwa nguvu kuwa kulikuwa na Miezi pevu bluu miwili usiku wa tarehe 31 Agosti. Akili ikikubali utaona hata yasiyokuwepo.  Tahadhari, na usiamini yote unayoona katika mtandao.

Uzushi mwingine ambao unazungushwa kwa miaka zaidi ya minne inahusu Miale ya Cosmo itakayoingia Dunia LEO USIKU saa 6:30 usiku hadi saa 9:30.  Miale inasemwa inatoka sayari ya Mirih (Mars) na kulipua simu yako kama imewashwa, na kukutahadhari uzime simu.  

Tatizo la usushi kama huu ni kuwa inahusu kitu cha kukudhuru LEO HII ambayo inaweza kuwa siku yoyote inaposemwa.  Kwa hiyo kama usuzhi huu hauondoki, hata baada ya kuvuma kwa miaka minne sasa.

Sayari ya Mirihi haina uwezo wa kutoa miale yoyote kwa vile Inang’aa kwa kuakisi mwanga wa Jua.  Miale ya Cosmo (Cosmic Rays) hutolewa na Jua wakati wote, mara nyingine kwa ukali. Hata hivyo, Dunia yetu inalindwa dhidi ya miale hiyo kwa uga wa usumaku uliotuzungukwe (magnetic field envelope).  Kwa hiyo ukisikia uzushi wa miale ya cosmo, ujue kuwa hauna ukweli wowote.

Tuje sasa katika kisa kingine cha kusisimua kilichowapumbaza wasikilizaji, ingawa ni cha kuvutia.  Tunaelezwa kwamba kutakuwa na kiza kwa siku tatu tarehe 21, 22 na 23 Desemba mwaka huu kwa vile siku hizo, ulimwengu wote utajipanga katika mstari na kusababisha Dunia kusimama katika mzingo wake nakusitisha mzunguko wake wa kuizunguka Jua.

Ukweli ni kuwa ingawa siku hizo Dunia na Jua vitakuwa katika mstari mmoja na kitovu kikali cha Galaxy yetu, hali hii ya vitu vitatu hivyo kuwa katika mstari hutokea KILA Desemba, na siyo tu Desemba ya mwaka huu.  

Je, unajua kuwa Dunia inamwendo haraka kiasi gani? Inasafiri kwa kasi ya kilometa 100,000 kwa saa katika mzingo wake wa kuizunguka Jua.  Pamoja na hiyo inazunguka katika mhimili wake kwa kiasi cha kilometa zaidi ya 1,000 kwa saa katika Ikweta.  Sisi hatuhisi mwendo mkubwa kama huu kwa vile Dunia yetu ni kubwa mmno na tumegandwa Duniani na mvuto wa gravity.

Sasa, jaribu kutafakari ugumu wa kusimamisha gari linalokimbia kwa mwendo wa kilometa 100 tu kwa saa, na utaelewa ugumu wa kusimamisha Dunia inayotembea kwa kasi ya zaidi ya kilometa 100,000 kwa saa. 

Hata kama Dunia ingeweza kusimama siku hizo tatu, bado itaweka nusu ya Dunia inayoangalia Jua kuwa katika mwanga wa mchana na nusu ya upande wa pili utakuwa katika kiza la usiku. 

 Je Jua litaondolewaje siku hizo ikiwa Dunia nzima itatakiwa kuwa katika kiza?  Ni jambo lisilowezekana kisayansi.  Hata mtu mwenye elimu ya msingi ataweza kuona hicho ni kichekesho.  Kwa nini watu wanakubali kisa kisichoaminika kiasi hicho?  Hii ni kwa vile watu huvutiwa sana na mambo ya anga za juu na akili zetu ni ombwe zikisubiri kujazwa na visa vya aina zote.

Habari nyingine iliyochangia suala hili ni tafasiri ya kuisha mwishoni mwaka 2012 kwa kalenda ya Wamaya (watu wa zama za kale walioishi Marekani ya Kusini).  Ilisemwa kuwa kuisha kwa kalenda inamaanisha mwisho wa Dunia.  

Kutokana sababu kama hizi, wananchi wamekuwa tayari zaidi kudanganywa na visa mbali mbali yanayohusu anga za juu.  Kukabili hali ya kukubili uzushi wa mambo ya anga za juu bila kudadisi vizuri, na ili tuweze kukata kiu yetu ya mambo ya anga, tuanzishe elimu ya anga na astronomia kuanzia ngazi za msingi na kuisuka katika mfumo wetu wote wa elimu, hadi elimu ya juu.  

Mwezi bluu mwingine unatarajiwa Julai 2015, ambapo Mwezi mpevu wa kwanza utakuwa Julai 2, 2015 na Mwezi mpevu wa pili (yaani Mwezi bluu) utakuwa tarehe 31 Julai, 2015.  Muda bado upo.  Tujitayarishe TUSIONE Miezi MIWILI yenye rangi ya BLUU Julai 2015.

2 comments:

  1. Asante sana.Je hii ni yale yaliyoko kwenye NASTRADOMAUS DOCTRINE zake.

    ReplyDelete
  2. Nostradamus Prophecy ............je haya tuyasemeje kwa hilo la kuwa GIZA

    ReplyDelete