Monday, August 13, 2012

Ni jukumu la kila taasisi kuhuisha masuala ya ajira na kazi zenye staha katika mipango na programu za maendeleo ya serikali

Mkurugenzi Msaidizi, Bwana Ally Msaki (aliyesimama mwenye miwani) alifungua mafunzo ya siku tano ya namna ya kuhuisha ajira na kazi zenye staha katika mipango ya programu za maendeleo ya serikali yanayofanyika Kibaha kuanzia tarehe 13-17 Agosti, 2012.

Ni jukumu la kila taasisi kutoa kipaumbele katika kukuza na kutoa taarifa za ajira ili kuondoa dhana iliyojengeka kwamba jukumu la kukuza na kutoa taarifa za ajira ni la Wizara ya Kazi na Ajira pekee.

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira, Bwana Eric Shitindi alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya namna ya kuhuisha masuala ya ajira na kazi zenye staha katika mipango na programu za maendeleo ya serikali

Katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira, Bwana Ally Msaki, Bwana Shitindi amesema kuwa lengo la mafunzo haya ni kujenga uelewa wa suala la uhuishaji wa ajira na kazi zenye staha katika mipango ya maendeleo ya ngazi mbalimbali, hivyo Wizara ya Kazi na Ajira ina wajibu wa kuratibu, kusimamia na kuwezesha zoezi la uhuishaji wa masuala ya ajira na kazi zenye staha katika bajeti na mipango mbalimbali ya maendeleo ya Serikali kuu na Serikali za mitaa kote nchini.

Amesema kuwa mwaka 2009, Wizara ilizindua Kamati za Kukuza Ajira za Mikoa katika mikoa ya Lindi na Mtwara pamoja na Halmashauri mbili kutoka kila Mkoa; Halmashauri ya Manispaa Mtwara/Mikindani na ya Wilaya ya Mtwara Vijijini kwa Mkoa wa Mtwara na Halmashauri ya Lindi Mjini na Lindi Vijijini kwa Mkoa wa Lindi.

Katika awamu ya kwanza Wizara ilitoa mafunzo elekezi yaliyolenga kuwezesha wajumbe wa kamati kuelewa maudhui na malengo ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008, Mkakati wa Taifa wa Kukuza Ajira, Mpango wa Taifa wa Kukuza Ajira, mfumo wa taarifa na takwimu za Ajira.

Katika awamu ya pili mwezi Machi mwaka huu, wizara ilitoa mafunzo kama haya kwa wizara 5 ambazo ni Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Kilimo na Chakula.

Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zilizopatiwa mafunzo katika mwaka wa fedha 2011/12 kupitia miradi ya maendeleo chini ya mpango wa Miaka Mitano unaotekelezwa na Wizara na Taasisi mbalimbali, Serikali inategemea kutakuwa na fursa za ajira 800,000.

Fursa hizi zitapatikana kutokana na utekelezaji wa baadhi ya miradi na programu za maendeleo. Kwa mfano sekta ya Kilimo itazalisha zaidi ya Ajira 169,189; Ujenzi wa Miundo mbinu ya barabara itazalisha ajira 646,615; Mawasiliano itazalisha ajira 27,600; Viwanda na Biashara itazalisha zaidi ya ajira 5,000. Halmashauri za Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani itazalisha zaidi ya ajira zipatazo 6,885.

Bwana Shitindi amesema kuwa ili Wizara ifikie lengo lake la kuzifikia Wizara na Halmashauri za Wilaya kote nchini katika kuhakikisha masuala ya ajira yanazingatiwa katika kuandaa bajeti na mipango ya maendeleo, imeona ni vema kutumia wataalamu mbalimbali hususan wale wenye wajibu wa kuandaa mipango na bajeti za taasisi zao.

Mojawapo ya masuala yaliyopewa kipaumbele katika matamko ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 ni kuhusu umuhimu wa kuainisha malengo ya kukuza Ajira katika mipango ya ki-sekta hasa kwa kuzingatia kuwa ajira ni suala mtambuka, hivyo kuhitaji ushirikiano wa sekta zote pamoja na wadau mbalimbali kutekeleza.

Tamko hili kwenye sera linaeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau itafanya kazi ya kuhuisha Sera kwa lengo la kujenga uhusiano na ushirikiano ili kupata ufanisi mzuri wa matokeo na mafanikio ya kuongeza nafasi za ajira katika ngazi zote.

Mafunzo haya yaliyoandaliwa kwa mada mbalimbali zitakazowasilishwa na timu ya Wizara ya Kazi na Ajira yanalenga na kuzingatia matamko ya Sera ya Taifa ya Ajira pia malengo na shabaha za MKUKUTA, malengo ya Milenia (MDGs) hasa lengo jipya lililoongezwa chini ya lengo namba moja linalohusu kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira hasa kwa vijana na lengo namba mbili la usawa wa jinsia pamoja na makubaliano mengine ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Amesisitiza kwamba kila sekta ni muhimu na ina mchango mkubwa katika kutoa fursa za ajira kwa watanzania, hivyo ni wajibu wa washiriki kuzingatia falsafa hii wakati wakiendelea na mafunzo

Amewaomba washiriki kuendelea kushirikiana na Wizara ya Kazi na Ajira katika hatua mbalimbali za mchakato wa kuhuisha masuala ya ajira kwenye mipango ya maendeleo.

Washiriki katika mafunzo haya ni kutoka Mkoa wa Morogoro na Halmashauri zake, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Wilaya ya Kisarawe.

Mafunzo haya yameandaliwa na Wizara ya Kazi na Ajira kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), yanafanyika Kibaha Conference Centre kuanzia tarehe 13-17 Agosti, 2012.

Na Mary Mwakapenda
Afisa Habari
Wizara ya Kazi na Ajia

No comments:

Post a Comment