Saturday, July 7, 2012

ZIARA YA KIKAZI YA KAMATI YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA(NUU) UMOJA WA MATAIFA NA WABUNGE WASEMA ASHA- ROSE MIGIRO NI HAZINA KUBWA

ZIARA YA  KIKAZI YA KAMATI YA  MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA(NUU) UMOJA WA MATAIFA
Na  Mwandishi Maalum
Wabunge wa  Kamati ya  Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) ya Bunge la  Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, wameanza ziara yao ya kikazi na mafunzo hapa Umoja wa Mataifa. New York
Wabunge hao  watano wakiongozwa na mwenyekiti wa Kamati, Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa ( Mb),  waliwasili Jijini  New   York siku ya Alhamisi, ambapo siku ya  Ijumaa walianza ziara yao kwa kuutembelea  Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Wabunge hao ni Mhe. Beatrice Shelukindo, Mhe. Rachel Masishanga, Mhe. Khalifa Khalifa na Mhe. Vita Kawawa.
Akielezea  madhumuni ya ziara hiyo, baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mwenyekiti wa Kamati. Mhe. Beatrice Shelukindo aliwaeleza maafisa wa Ubalozi kwamba, ziara yao ilikuwa inalenga  pamoja na mambo mengine, kujifunza na kupata uelewa wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Balozi za Tanzania nje ya nchi.
Aidha akasema  ziara hii ni ya kwanza ya aina yake kufanywa na kamati hiyo na kwamba itawapa fursa ya,  siyo tu kufahamu kazi  zinazofanywa na Balozi, lakini pia namna bora ya  kuishauri serikali  hususani  katika kuangalia ni kwa namna gani bora zaidi ambapo balozi za Tanzania zinaweza kuchangia katika kukuza pato la taifa, lakini pia kutekeleza kwa ufanisi  na tija sera ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa  na Diplomasia ya Uchumi.
Halikadhalika wabunge  hao, kupitia ziara hiyo wanataka kujifunza  mafanikio ya yatokanayo na kazi za kila siku zinazofanywa na Balozi hizo, changamoto wanazokabiliana nazo, na maeneo gani yanayotakiwa kutiliwa mkazo au kutafutiwa ufumbuzi.
Wabunge wakiwa hapa  New York watapata pia  fursa ya kutembelea  na kukagua majengo yanayomilikiwa na serikali
Wakiwa ubalozini hapa, walipata fursa ya  kuwasikiliza  maafisa wa Ubalozi wanaosimamia Kamati  Sita za Balaza Kuu la Umoja wa Mataifa. Wakiongozwa na Kaimu Balozi, Dkt. Justin Seruhere   kila mmoja alitoa muhtasari wa kamati anayoifanyia kazi, akielezea  mafanikio na changamoto wanazokabiliana zao wakati  wa utekelezaji wa majukumu yao.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge hao pia walipata fursa ya kwenda  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo walihudhuria majadiliano ya mikutano miwili mikubwa inayoendelea kwa sasa hapa   Umoja wa Mataifa.
Mikutano waliyohudhuria wabunge hao ni ule  wa mchakato wa maandalizi ya Mkataba wa  Biashara ya Silaha ( ATT),  na  Mkutano wa Baraza la  Umoja wa Mataifa linalohusika na  Masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC). Mikutano hii imeanza  mwanzoni mwa wiki hii.
Wakiwa  katika ukumbi wa mkutano wa majaliano ya ATT,  wabunge waliweza kujionea  na kufuatilia namna ambavyo majadiliano  yalivyokuwa yakifanyika, huku  kila nchi ilivyokuwa ikiwasilisha  hoja  huku zikiteteza misimamo  na maslahi ya nchi zao.
Mkutano wa nchi wanachama kuhusu Mkataba wa   Biashara ya Silaha Duniani, ambao Tanzania inashiriki kikamilifu na  kufuatilia kwa karibu   masuala ya udhibiti  wa silaha ndogo ndogo na za kati .   Silaha ambazo zimekuwa na madhara mkubwa kwa maisha na uhai wa watu barani  Afrika.
Mkutano huu  ambao ni  na nyeti  dhumuni na lengo lake kuu ni kuandaa    Mkataba wa kisheria utakaoratibu  na kudhibiti biashara ya  silaha  Duniani.
Tanzania katika   mkutano huu ukiacha maafisa wa ubalozi, inawakilishwa  na ujumbe mzito  wa wataalamu  kutoka,  Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao ni Brigedia  Generali Dkt. Charles Muzanila, na Brigedia Generali  Venance Mabeyo, kutoka Jeshi la Polisi ni Kamishina Msaidizi, Esaka Mugasa,    Bw. Theobald Kazora kutoka Ofisi ya Rais ( Ikulu) na  Bw. John Kinuno, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
 Kwa  Upande wa  Mkutano wa katika mkutano wa ECOSOC ambao ajenda yake kuu ni uhuishaji na uchagiaji wa ajira kwa vijana   ujumbe wake unaongozwa na Mhe. Gaudentia Kabaka(Mb) Waziri wa  Kazi na  Ajira, ujumbe ambao   unaojumuisha pia wawakilishi kutoka Serikali ya  Mapinduzi ya Zanzibar.
----------------------------------------------------------
 ASHA- ROSE MIGIRO NI HAZINA KUBWA – WABUNGE

Wabunge wa Kamati ya  Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ( NUU)  ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamemuelezea  Naibu Katibu Mkuu Dkt. Asha- Rose Migiro, ambaye amemaliza muda wake wa utumishi UN kama hazina ambayo  Tanzania na watanzania wanatakiwa  kuiezi na kuitumia.
Hayo yameelezwa  kwa nyakati tofauti  na  wabunge  wa kamati hiyo  wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati , Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa wakati walipokutana na kufanya mazungumzo na  Dkt. Asha- Rose Migiro jijini  New York siku ya Ijumaa.
Wabunge hao ambao ni Mhe.  Khalifa Khalifa, Mhe. Vita Kawawa, Mhe. Beatrice Shelukindo na Mhe. Rachel Masishanga, wapo Jijini New  York kwa ziara ya kikazi na mafunzo .
Wabunge wakabainisha kwamba litakuwa jambo la ajabu na la kushangaza kama  watanzania  watashindwa   siyo  tu kutambua  mchango mkubwa wa  Asha- Rose Migiro bali hata kuchota na kumtumia kupitia uzefu na utalamu  aliojipatia akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja.
Aidha Wabunge hao walitumia nafasi  ya mazungumzo hayo kumpongeza Asha-Rose Migiro, kwa  kumaliza salama jukumu hilo zito na kwamba ameiwakilisha vema Tanzania na Bara   la Afrika kwa ujumla.
“  Kwa niaba ya wajumbe wa Kamati yangu,  tukupongeze kwa kumaliza salama jukumu hili zito na kubwa, kwa hakika umetuwakilisha na umeipeperusha vema  bendera ya Tanzania na umeliwakilisha vema Bara la Afrika na  waafrika”  akasema Mhe. Lowassa.
Wakasema kwamba ni matarajio yao kuwa ushirikiano ambao   dkt. Migiro alikuwa akiutoa wakati akiwa Naibu Katibu Mkuu atauendeleza  na  maslahi ya taifa na  nasa sasa  baada ya kumaliza wadhifa huo  na kurejea nyumbani.
Kwa upande wake, Dkt. Migiro amewashukuru wabunge hao  kwa pongezi zao na kwamba kama mtanzania daima atakuwa tayari kutoa mchango wake pale atakapohitajika kufanya hivyo.
Aidha amesema amefurahishwa  na  uamuzi wa   Kamati hiyo wa kufanya ziara  za kikazi na mafunzo  katika Balozi za Tanzania nje ya nchi.
Akasema ziara hizo si  tu zinawapatia uzoefu na utambuzi ya kile kinachojiri katika ngazi ya kimataifa, lakini inaweka katika nafasi nzuri ya kuwa wachangiaji wazuri  linapokuja suala  la  uhusiano wa kimataifa, ulinzi na usalama.
Aidha amewashuri wabunge wa Kamati hiyo kujijengea utaratibu wa kuhuhudhuria mikutano  na mijadala ya wazi  inayofanyika hapa Umoja wa Mataifa hasa ile inayohusu masuala ya ulinzi na usalama.
Amewataka  pia wabunge wa kamati hiyo, kujijengea uwezo na ufahamu  kuhusu ushiriki wa Tanzani katika  Operesheni za Kulinda Amani zinazosimamiwa na  Umoja wa Mataifa.
Akabainisha kwamba wabunge wa Kamati hiyo wanapashwa pia kufahamu nini kinachoendelea katika operesheni hizo, hali ya wanajeshi  wa Tanzania waliomo katika opereshi  hizo wakiwamo  Polisi na  Askari Magereza na kubwa zaidi kujifunza manufaa makubwa  ya kiulinzi na kiuzoefu yanayotokana na wanajeshi wa Tanzania   kushiriki operesheni hizo.’
Akawaeleza wabunge  hao kwamba ingawa Tanzania imeingia katika  siku za hivi karibuni katika operesheni za ulinzi wa amani , lakini wanajeshi wake,    jeshi la polisi na askari magereza wamejizolea sifa kemkem kutokana na uhodari, nidhamu na utendaji wao makini katika jukumu hilo.
 Akielezea nini ambazo amejifunza katika utumishi wake wa miaka mitano na nusu akiwa naibu katibu  mkuu .  Migiro alikuwa na haya ya kusema.
“  Yapo mengi ambayo nimejifunza,  lakini kwa  ufupi  tu niseme  nimejifunza,  uadilifu,  uwajibikaji,  kujituma, uzalendo, utii, kujiamini, matumizi sahihi  ya yenye tija  ya raslimali,  kuthamini muda wa kazi, ushirikiano wa pamoja na maelewano”.

No comments:

Post a Comment