Sunday, July 8, 2012

WABUNGE WA KAMATI YA MAMBO YA NJE,ULINZI NA USALAMA WAENDELEA NA ZIARA YAO YA KIKAZI NA MAFUNZO JIJINI NEW YORK

Mkutano wa kubadilishana mawazo ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya NUU mara baada ya wajumbe wa Kamati hiyo kutembelea na kukagua majengo yanayomilikiwa na Serikali. Aliyesimama ni Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Esaka Mugasa, akijibu na kutoa maelezo kuhusu hoja zilizoulizwa na Mwenyekiti, Mhe. Edward Lowassa.
Mwenyekiti akifurahia jambo pamoja na wajumbe ambao hawapo pichani, kutoka kushoto ni Birigedia Jenerali Venance Mabeyo, Kaibu Balozi Dkt Justin Seruhere, Mhe. Edward Lowassa ( Mb) na Mama Regina Lowassa.
Mweyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje,Ulinzi na Usalama Mhe. Edward Lowass ( Mb) na Waziri Mkuu Mstaafu akisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Brigedia Generali, Dkt. Charles Muzanila kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) wakati wa kikao cha majadiliano na kubadilishana mawazo kilichofanyika siku ya pili ya ziara ya kikazi ya Ujumbe wa NUU. Mazungumzo hayo yalifanyika katika Makazi ya Balozi yaliyoko eneo la Dobbs Ferry.
Mwenyekiti akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati na wajumbe wengine wanaohudhuria mkutano wa ATT na ECOSOC.
Mhe. Lowassa, Mama Regina na Brigedia Jenerali Mabeyo wakikumbushana jambo.
" Nadhani hiki kinamtosha Mzee" ndivyo anavyoelekea kusema Mama Regina Lowassa, wakati akimsevia Mhe. Mwenyekiti mahanjumati yaliyoandaliwa na Ubalozi kwa heshima ya wanakamati na wajumbe wanaohudhuria mikutano katika Umoja wa Mataifa. Maandazi yalikuwapo na kachumbari ilikuwapo.

Na Mwandishi Maalum

Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ( NUU) Mhe, Edward Lowassa(Mb) na Waziri Mkuu Mstaafu, amewataka wajumbe wanaohudhuria mkutano wa majadiliano kuhusu Mkataba wa Biashara ya Silaha ( ATT), kuhakikisha kwamba maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanazingatiwa.

Mhe. Lowassa ametoa ushauri huo siku ya jumamosi wakati alipokutana na kubadilishana mawazo na wajumbe wanaohudhuria mkutano huo wakiongozwa na Brigedia Generali, Dkt. Charles Muzanila kutoka JWTZ.

“ Mkutano unaendeleaje, na je kuna mwelekeo wowote” akahoji Mwenyekiti na kuongeza. “ Hakikisheni mnafuatilia kikamilifu majadiliano haya ili kuhakikisha maslahi ya nchi yetu yanazingatiwa.

Mazungumzo kati ya Ujumbe wa NUU wataalamu wanaohudhutia mkutano wa ATT yalifanyika katika makazi ya Balozi wa Tanzania, yakihudhuriwa pia na wajumbe wengine wanaohudhuria mkutano wa masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC) na Maafisa wa Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa.

Wajumbe wa Kamati hiyo unaowajumuisha wabunge watano akiwamo Mwenyekiti Mhe. Lowassa jana jumamosi uliingia katika siku yake ya pili ya ziara yake ya Kikazi na Mafunzo hapa Jijini New York, ambapo ni makazi ya Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania katika Umoja wa Mataifa.

Katika siku hiyo ya pili wajumbe walianza siku yao kwa kupata taarifa ya masuala ya Utawala na Fedha iliyotolewa na Mkuu wa Utawala wa Ubalozi, Bw. Modest Mero akishirikiana na Mshauri wa Masuala ya fedha wa Ubalozi Bw. Alfred Swere.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, wabunge hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Edward Lowassa ( Mb), walitembelea , kukagua na kujionea hali halisi ya majengo yanayomilikiwa na Serikali.

Majengo hayo ni lile ambalo limenunuliwa na serikali na ambalo litatumika kama ofisi za Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika UMoja wa Mataifa , jengo ambalo baadhi ya ghorofa zake zitatumika kama kitega uchumi.

Kununuliwa kwa Jengo hili lenye ghorofa sita na ambalo liko eneo la Manhattan sasa kunaifanya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na jengo la kudumu na lenye hadhi ya Ubalozi.

Kwa miaka yote tangu kufunguliwa kwa Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, huduma za Ubalozi huo zimekuwa zikifanyika katika ofisi za kupanga na hivyo kuigharimu serikali gharama kubwa za kodi ya pango.

Kununuliwa kwa jengo hili kutasaidia sana kupunguza gharama za kulipia pango lakini pia kuogeza ufanisi na tija katika utendaji kazi na kulingizia pato taifa.

Baadaye ujumbe wa Kamati hiyo ulitembelea jengo la pili ambalo ni mali ya serikali na makazi ya Balozi wa Tanzania. Jengo hili liko eneo la Mt. Vernon lina historia ya aina yake lakini kwa sasa halitumiki kama makazi ya Balozi kutokana na uchakavu na hivyo kuhitaji matengenezo makubwa.

Baada ya kukagua na kujionea hali halisi ya jengo hilo , wabunge walikwenda eneo la Dobbs Ferry ambako ndipo yaliyo makazi ya muda ya Balozi.

Wakiwa katika makazi hayo, Mwenyekiti wa NUU ujumbe wake, walipata chakula cha mchana kilichoandaliwa na Ubalozi.

Baada ya chakula hicho ambacho alishiriki pia Mama Regina Lowassa, kulifuatia kikao cha kazi,kikao ambacho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati kikiwashirikisha wabunge, wajumbe wanaohudhuria mkutano wa ATT na ECOSOC, na Maafisa wa Ubalozi ambapo kwa zaidi ya saa mbili wajumbe walijadiliana na kubadilishana mawazo ikiwa ni pamoja na kupeana majukumu na mikakati kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mstakabali na maslahi ya Taifa na Watanzania.

No comments:

Post a Comment