Sunday, May 13, 2012

MJADALA WA HAZINA YA TAIFA ZITTO KABWE VS MWIGULU NCHEMBA

Benki Kuu: Hazina ya Taifa imekauka?

by zittokabwe


Benki Kuu ya Taifa lolote ndio taasisi pekee yenye takwimu zote nyeti na za uhakika zinazohusu uchumi wa Taifa hilo. Katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania eneo la Machapisho kuna Taarifa nyeti sana mbili, Mapitio ya Uchumi ya Mwezi (Monthly Economic Review) inayotoka kila Mwezi katika Mwaka na Mapitio ya Uchumi ya Robo Mwaka (Quarterly Economic Bulletin). Taarifa hizi hutoa taarifa kuhusu masuala yote muhimu yanayohusu Uchumi wa Jamhuri ya Muungano na Uchumi wa Zanzibar ikiwemo taarifa za Mfumuko wa Bei, Mapato na Matumizi ya Serikali, Mwenendo wa Biashara ya Kimataifa na Deni la Taifa.
Ukienda kwenye tovuti ya Benki Kuu leo utakuta Taarifa hizi. Lakini Taarifa hizi zimeishia Desemba mwaka 2011 zikitaarifu masuala ya Uchumi ya Mwezi Novemba na robo ya mwaka inayoishia Desemba. Ukitaka kujua Bajeti ya Serikali na mwenendo wake hutapata taarifa za sasa bali za Mwezi Novemba mwaka 2011, miezi sita nyuma. Huu sio utendaji uliotukuka. Hii ni kuficha taarifa kwa wananchi. Taarifa zinafichwa ili iwe nini? Nani anafaidika na kufichwa kwa taarifa muhimu kama hizi?
Kuna tetesi kwamba Hazina ya Taifa (Hifadhi ya Fedha za kigeni – foreign reserve) inakauka, kwamba tuna hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa mwezi mmoja tu. Niliposikia tetesi hizi sikuamini. Nilipoenda katika tovuti ya Benki Kuu ili kuweza kuwa na habari rasmi (authoritative) nimekuta takwimu za Novemba 2011.
Takwimu ya Mfumuko wa Bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ni ya mwezi Novemba mwaka 2011!
Ukitaka kujua mwenendo wa Bajeti ya Serikali kama makusanyo ya Kodi na Matumizi utapata Taarifa ya Mwezi Novemba mwaka 2011.
Ukitaka kujua manunuzi ya Mafuta (fuel imports) kwa miezi 3 ya mwanzo ya mwaka 2012 ili kuweza kuona namna Umeme wa dharura umeathiri urari wetu wa Biashara ya Nje hupati taarifa hiyo katika tovuti ya Benki Kuu.
Taarifa zinafichwa.
Ndio. Zinafichwa tena makusudi maana taarifa hizi zipo Benki Kuu. Huu ni uzembe maana Nchi inawalipa wafanyakazi wa Benki Kuu mishahara minono ili wafanye kazi hizi. Benki Kuu pia imetoa zabuni kwa Kampuni Binafsi kuchapisha Taarifa hizi. Kama Taarifa hazitoki kwa wakati ni wizi. Wizi ambao haupaswi kufumbiwa macho.
Benki Kuu ya Tanzania ipo miezi Sita nyuma. Aibu kubwa sana.
Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano akihakikishia mataifa duniani kuhusu uwazi Serikalini (#OGP), Taasisi kubwa kama Benki Kuu inaficha Taarifa ambazo ni nyeti kwa wananchi na muhimu kwa wafuatiliaji wa sera za Serikali. Rais wa nchi anaongea Buluu, Gavana wa Benki Kuu anasimamia Kijani!
Inaudhi na kukera sana kwenda kwenye tovuti ya Benki Kuu na kukuta taarifa za miezi Sita iliyopita. Benki Kuu hamstahili kuitwa Benki Kuu, labda benki kuu kuu. Rekebisheni jambo hili haraka sana maana kuficha taarifa kwa Umma ni ufisadi. Haki ya kupata taarifa ni haki ya msingi katika Katiba yetu.  Hatutaki kushtukizwa na kuambiwa Hazina ya Taifa imekauka.
Prof. Ndulu hakikisha Taarifa ya Mapitio ya Uchumi wa kila Mwezi imewekwa kwenye tovuti kwa muda mwafaka. Ifikapo mwisho wa Wiki inayoanzia Jumatatu Mei 14, tovuti ya Benki Kuu iwe na Taarifa za miezi yote (Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili). Taarifa hizi ni muhimu ili nasi tutekeleze majukumu yetu ya Kikatiba kama Wabunge, Mawaziri vivuli na Wananchi wa Tanzania.


============================================


KWA HILI ZITTO ANAPOTOSHA UMMA WA WATANZANIA.


Nimesikitishwa na kushangazwa na taarifa iliyosambazwa  kwenye vyombo vya habari  hivi leo na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Zuberi Kabwe.

Mimi nilikuwa ni Mchumi Daraja la Kwanza katika Benki Kuu ya Tanzania na nilikuwa nafanya kazi kwenye Kurugenzi ya Utafiti wa Uchumi na Sera. Hivyo, nafahamu jinsi Benki Kuu inavyofanya kazi. Na nasikitika kwamba wanasiasa sasa, katika kujitafutia umaarufu, tunaingia kwenye kushambulia taasisi muhimu inayoendeshwa kwa weledi na uadilifu mkubwa.

Baada ya Mhe. Zitto Kabwe kukosa taarifa muhimu mtandaoni, ningetegemea Mbunge kama Zitto, ambaye Kamati yake inakagua mahesabu ya BOT, kuwasiliana na Benki na kuuliza kulikoni, badala ya kusambaza taarifa katika vyombo vya habari kulaani Benki Kuu na kusambaza tetesi kuhusu hali ya Hazina ya Taifa. 


Lakini vilevile, ningetegemea kwamba, kama ameamua kusambaza  taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, basi taarifa hiyo ingejumuisha yale aliyoyabaini baada ya kuzungumza na Benki Kuu. Yeye kama kiongozi, kama anaamua kuwasiliana na umma kwa kusambaza taarifa kwa vyombo vya habari, basi walau aonyeshe umma jitihada nyingine alizofanya za kupata ripoti hizo zaidi ya kwenda tu mtandaoni, kwasababu sote tunajua kwamba hata namba ya Gavana wa Benki Kuu anayo.

Pili, kutokuwepo kwa ripoti mtandaoni hakumaanishi kwamba ripoti hizo aidha zimefichwa au hazipo. Ni muhimu sana viongozi wakawa wa kweli na wakaacha mtindo wa kungoja siku ambayo haina habari (Jumapili) na kuamua kutengeneza habari kwa ajili ya vichwa vya habari vya Jumatatu.

Naomba kutoa ufafanuzi wa jinsi ukweli ulivyo, kwasababu hata sisi katika Chama tumekuwa tunafuatilia taarifa hizi za Uchumi kutoka Benki Kuu.

Kwanza, katika taarifa yake Zitto anaomba taarifa za mwezi Januari, Februari, Machi na Aprili zitolewe. Hili limenishangaza kwa sababu nilitegemea kwamba mtu kama Zitto, ambaye ni mchumi na ambaye kamati yake  hupitia hesabu za BOT, angefahamu kwamba ripoti ya mwezi husika inaanza kuandaliwa tarehe 15 ya mwezi unaofuatia – kwa maana kwamba report ya mwezi Machi ilianza kuandaliwa tarehe 15 Aprili, report ya mwezi Aprili, itaanza kuandaliwa tarehe 15 Mei, na report ya mwezi Mei itaanza kuandaliwa tarehe 15 Juni. Huu ni utaratibu wa kimataifa, ambapo inategemewa kwamba katika kipindi hicho cha wiki mbili baada ya mwezi kuisha, takwimu muhimu kutoka sehemu mbalimbali zitakuwa zimekusanywa na kuhakikiwa.

Pili, ningetegemea pia Mhe.  Zitto awe anafahamu kwamba  kabla ya taarifa hizi za Benki Kuu kuchapishwa ni lazima zipitishwe na Kamati ya Sera za Fedha ya Bodi ya Benki Kuu (Monetary Policy Committee of the Board). 


Huko nyuma, Kamati hii ilikuwa inakutana kila mwezi, lakini kutokana na maagizo ya Kamati ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mhe. Zitto kwamba vikao katika Benki Kuu vipunguzwe. Hivyo, ikaamuliwa kwamba Kamati  hii inayopitisha taarifa hizi muhimu iwe inakaa mara moja kila baada ya miezi miwili. Matokeo yake ni kuchelewa kupitia na kupitisha taarifa hizi muhimu. Mara ya mwisho kikao kilikaa mwezi Machi kupitia taarifa ya mwezi Januari, ambayo imekwishasambazwa.

Tatu, si kweli kwamba Hazina ya Fedha za Kigeni Taifa imekauka. Ambacho angeweza kufanya Zitto na ana mamlaka hayo na uwezo anao ni kumpigia simu Gavana au wasaidizi wake na kuwauliza ni kiasi gani cha Hazina kilichopo. 


Mimi ndicho nilichofanya, na taarifa rasmi, ni kwamba hazina iliyopo ni kiasi cha dola za kimarekani bilioni 3.6, ambazo zinawezesha kuagiza mahitaji yetu yote ya bidhaa kwa kipindi cha miezi minne, na wala sio mwezi mmoja  kama alivyodai Mhe ZITTO. Na akiba ya watanzania iliyoko kwenye benki zetu nchini ni takribani dola za kimarekani 1.8 bilioni na taarifa hii pia IMF wanayo, (taarifa hii ni kwa kipindi kinachoishia tarehe 11 May 2012). 


Binafsi nimesikitika sana kwamba kiongozi anaweza kuwa irresponsible kiasi hiki cha kusambaza taarifa za uvumi wakati anao uwezo wa kupata taarifa sahihi za maandishi na kuujulisha umma ukweli.

Mwisho, napenda kumsihi Mbunge mwenzangu kwamba ni muhimu kuwa makini na kutokurupuka katika mambo muhimu kama haya na ni muhimu kufanya utafiti kidogo kabla ya kuwasiliana na umma kwani sisi viongozi tunasikilizwa na kuaminiwa na watu na tunategemewa kuwa sahihi na wakweli wakati wote.

Imetolewa na:
Mwigulu Lameck Nchemba (MB)
Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa
Dodoma
13 Mei 2012.

28 comments:

  1. longo longo kawaida yetu! hizo direct contact mnazo nyie mlio kwenye system...issue hapa raia tuna haki ya kuwa informed tena on time: maelezo ya mpaka vikao ndiyo longolongo ninalolisema 'urasimu' leo tuko mei update iliyopo ni mpaka december??? Ofisi nyingi za umma zina milolongo nyingi ya nenda rudi mpaka fulani awepo ooh mpaka tuunde kamati, yote hayo hayana tija kwa nchi, yanaongeza usumbufu tu nakupoteza muda mwingi kwa kitu cha masaa 2!! Longolongo bwana Nchemba ndiyo tatizo!! Taasisi za serikali zote lazima ziwe 'smart na efficient' ili kuondoa viwingu kama hivi!! vya ooh unapotosha umma! Sisi raia tuna kero nyingi mpaka visogoni...we dont care whether anapotosha au la!! Tunataka ofisi za umma ziwe mfano...na kutoa statement zilizonyooka siyo kila siku ''Excuse''

    Hapo sijagusia hao wapokea simu huko maofisini kabla hata yakuruhusiwa kumfikia mhusika??? kero??? WATANZANIA TUBADILIKE!
    Mdau Kaju!!

    ReplyDelete
  2. Kwanza, binafsi sikutegemea Mh. Zitto kutafuta taarifa kama hizi kwenye mtandao kwa madaraka aliyonayo. Mheshimiwa Zitto alikuwa na uwezo wa kuomba ufafanuzi kutoka BOT kwa nini taarifa alizozianishwa hazipo kwenye mtandao. Majibu kutoka BOT ndio yangeonyesha kuwa kuna uzembe au la na alikuwa wajibu wa kurekebisha suala hili. Binafsi namuamini sana na kumuamini sana Mh. Zitto lakini kwa hili amekuwa mbinafsi sana kwa kutaka kupata umaarufu wake ninafsi na si kwa nia ya kurekebisha upatikanaji wa taarifa.

    ReplyDelete
  3. Mie sijamuelewa muheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba. Hoja ya Mh. Zitto iko wazi kabisa. Kuwa tovuti ya BOT haina taarifa zilizo up to date, na ni wajibu wa BOT kuhakikisha taarifa hizo zinatolewa kwa wakati. ni haki ya kila mtanzania kupata taarifa hizo, si suala la nani anamjua Gavana au wasaidizi wake kupiga simu na kupewa taarifa. Hatutegemei kila mtanzania anayetaka taarifa kama hizi awe anamtafuta Gavana kwenye simu na kupiga simu. Huyo Gavana atafanya kazi za uGavana kweli.
    Cha msingi ningetengema Mh mwigune naye awakemehe BOT kwa kuzembea kutoa taarifa kwenye tovuti yao ambao ni current ili kuleta tija. Katika taarifa ya Mh Kabwe amekili BOT wanzo hizo Taarifa, kama wanalipwa mishahara na mazingira mazuri kuiko wafanyakazi wote wa umma hapa nchini kwanini wanazembea. Hiyo ndiyo hoja ya msingi.
    nawakilisha
    mpendda maendleo

    ReplyDelete
    Replies
    1. Jamani hapa DITTO kakosea wapi!!!

      Delete
  4. kwa nini taarifa hazipatikani kwa wakati?.hili ndio suala na wala si sababu kuwa eti jumapili si siku ya kuwa na habari...we mchumi wa daraja la kwanza wapi?..kama ni ccm sawa lakn si kwingineko..zitto ongeza juhudi tutafika tu...haya mimi ningeyajua wapi bwana.

    ReplyDelete
  5. Ni kweli, Mheshimiwa Zitto yupo sahihi kabisa.Taarifa za mwenendo wa uchumi ni haki ya kila mwananchi kuifahamu tena bila jasho. Binafsi ningependa tu ninapofungua tu tovuti ya BOT nakutana na up todate report..si kazi yangu kujua kamati ngapi zinakaa kupitisha taarifa...tunachotaka ni taarifa basi na sio tori...Mfano mzuri ni NECTA, sio kwamba hawana kamati kama hizo za BOT..bali siku ambayo matokeo yametangazwa...jana yake tayari yapo kwenye mtandao kwa sababu wanajua wananchi hawataki longolongo bali kuona matokeo...
    Tuache siasa kwa hili BOT wamechemka mbaya sana.

    ReplyDelete
  6. Mimi nipo huku Namtumbo, uwezo wa kupata habari kama hizi ni adimu sana. Namshukuru sana Zitto Kabwe kwa taarifa yake kwani imetufumbua macho kuhusu kufilisika kwa serikali yetu. Sasa hivi hatujui tarehe rasmi tarehe ya kupata mishahara yetu kwani hadi leo sisi wafanyakazi wa serikali bado kulipwa mishahara yetu ya March.Kama kweli benki kuu ina pesa hiyo Bil 3.6 pesa ya kimarekani, kwanini wasiitumie kuiongezea thamani shilingi yetu? Inakuwaje Dr. Balali aliweza, lakini huyu Mh. Ndulu anashindwa pamoja na U-Professa wake?

    ReplyDelete
  7. Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, hapa kachemka, sijui hujaelewa dhana na dhamira ya Mhe Kabwe, hii ni nchi yetu sote sisi kama watanzania, tunahaki ya kujuwa kihakiba chetu kikoje, siyo kuwe na mzunguko wa kumtafuta Gavana, why? Gavana ni muajiriwa wetu sisi wtznia, atimize wajibu wake hapa siyo dhambi na si kweli kuwa ni upotoshwaji kwa umma, time ile siyo Mwigulu, mambo tunayataka hadharani, siyo kiuficho uficho why?

    ReplyDelete
  8. Jamani! Hapa hoja si Zitto na MWigulu, hapa hoja ni taarifa zinazistahili kufahamika kwa umma kwa wakati.
    Mwigulu wewe ni mchumi mweledi embu acha siasa,
    Hapa Zitto ana hoja! ana vitu vingi angeweza kupiga simu kuvijua, hapa kaweka vyeo na nydhifa zake pembeni, anatutetea sisi raia wa kawaida ambao hutuwezi kupiga simu.
    Tafakali!!

    ReplyDelete
  9. Mh Mwigulu, hamna lolote utakalotuambia. Tulishawazoea uwa CCM ni watu wa "funika kombe mwanaharamu apite". Mlishazoea kufunikafunika mambo ndio maana nchi inaendeshwa kwa ujanjaujanja. Taarifa ni haki ya watanzania. Hamna haja ya Zitto kuanza kuwafuata huko BOT ili mfunikefunike wakati anajua ni haki yetu kuzipata kwenye mtandao.

    Hata hivyo Mh Mwigulu kwa nini unachukua jukumu la kumjibia Gavana? Muache ajibu mwenyewe. Wewe endelea na kazi za CCM

    ReplyDelete
  10. NAMWUUNGA MKONO KABWE ZITTO.
    TAARIFA ZA BENKI KUU KWA TAIFA LOLOTE NI MUHIMU KUPATIKANA KWA WANANCHI. USIPO KUWA NA TAARIFA SAHIHI HUWEZI KUJUA MWELEKEO WA UCHUMI. TEMBELEA TOVUTI MBALIMBALI ZA MATAIFA MBALIMBALI WAKO UPTODATE.YASHINDIKANA HATA VI BENKI VIDOGO NCHINI UNAKUTA UPTODATE INFORMATION?

    TOFUTI NYINGI ZA SERIKALI ZIMEOZA ZINA TAARIFA ZA MWAKA MMOJA NYUMA, HAMNA UPDATES.

    NA KAMA MNAKANUSHA KWAMBA HAIJAKAUKA SEMENI KILICHOPO!! SI MNAJIFANYA MKO WAZI, SEMENI.

    ReplyDelete
  11. nimekuwa naambiwa kwamba mh Z Kabwe ni mtu wa kutafuta 'cheap popularity'. nikakataa. sasa nimeanza kuamini. iweje yeye kama waziri kivuli wa fedha na uchumi asijue taarifa muhimu kama hazina ya taifa? inflation? Labda benki kuu inachelewa ku-update tovuti yao-hilo lingekuwa neno. lakini yeye kusema hajui takwimu hizo, naanza kujiuliza kama yeye angekuwa mtendaji nchi hii ingeenda wapi. nimezungumza na rafiki yangu pale benki kuu - siyo gavana! maana wenye namba ya gavana ni watu kama mh Zitto, kaniambia maneno yanayofanana na mh M Nchemba. tena kaniambia kwamba benki kuu inachapisha tu takwimu za inflation - wanatangaza ni tz bureau of statistics. nimeenda kwenye tovuti yao na taarifa zipo. mh Zitto umepata credit kwa mabadiliko ya baraza la mawaziri. mimi nimefurahia hilo. prof Ndullu amerithi matatizo mengi ya waliotangulia. amejaribu kuwa m-wazi sana. ameweza kuzuia ushukaji wa thamani ya shilingi, hili la inflation naona linamsumbua kidogo. naomba umpe amani mheshimiwa ili afanye kazi yake. kama una ushauri kwake naomba umwambie. labda sisi tulio nje hatumjui ni haambiliki? otherwise be fair!!
    mchumi mwenzako (if u still are)

    ReplyDelete
  12. zitto, kwa hili umepotosha! taarifa zipo mpaka za january, siyo novemba. labda uanatafuta umaarufu au una lako na ndullu. pole ndugu yangu, naona umeshikwa pabaya!

    ReplyDelete
  13. Nheshimiwa Mwigulu hajaisoma vizuri hoja ya Zitto. Nafikiri anahitaji kuisoma tena. Kitu anachoongea Zitto ni updates za mtandao wa BOT. Hata ningekuwa mimi ningejiuliza kuwa nyuma miezi sita kuna kitu gani?

    Mwigulu usifikirie kila kitu tu ni siasa, mambo mengine siyo siasa. Nakuomba punguza siasa ili mambo yaende. Zitto unaakili sana ya kuchokonoa kila mahali endelea hivyo hivyo achana na wale wanaozungumzia madaraka uliyonayo.

    ReplyDelete
  14. Mimi pia namuunga mkono mheshimiwa Zitto..tunashukuru kwa kuzidi kutufungua macho watanzania..Enzi nza mambo chini ya meza na kwa kificho yamekwisha..zama hizi za ukweli na uwazi..Mimi pia hata sikujua kama kuna hizi taafifa kwa maana hio bila Mheshimiwa Zitto kuibua hili sidhani kama ningejua...Sio tu BoT bado sehemu nyingi sana taafifa zinafichwa fichwa..kwa nn haya mambo yanayuhusu nchi yafichwefichwe???

    Nakupongeza sana mheshimiwa Zitto..tunawahitaji vijana wachapa kazi kama ninyi katika nchi hii...ibueni uozo wote uliofichika katika hizo taasisi...kuna uozo sana BOT, Bandari, TRA, TANESCO...

    ReplyDelete
  15. Mh ZITTO kwa hili umechemka, hivi wewe ni mchumi au mwanasheria, siku zote huwa nakuona mstaarabu fulani kumbe unakwenda sasa kwa wenzio wasiofikiri? hebu rudi kwenye mstari , mimi huwa nakuamini ila leo imekula kwako, USIWE MZUSHI EE PATA UKWELI KWANZA, WATANZANIA WOTE SI WAJINGA SASA. Na kwamba sisi ni bendera fuata upepo tu, tunapima na kuona ukweli. ila kuna wale akina mie eti kiyu kikisemwa na upinzani tu basi ni sahihi... UFINYU WA MAWAZO

    ReplyDelete
  16. suala hapa ni kwamba hamjatoa taarifa mtandaoni kwa wakati muafaka, mngetoa Mhe. Zito angepata wapi msemo? anajua angeweza kwasiliana na gavana akazipata, lakini aliamua kuvaa viatu vya mtanzania wa kawaida na sio mbunge ndio maana akaandika kwani taarifa hizo ni kwa ajili ya watu wote na si wabunge wa Tanzani tu!!

    ReplyDelete
  17. Muheshimiwa Mwigulu tunaomba namba ya Gavana hapa mtandaoni ili na sisi tumpigie awe anatupa hizo taarifa..au namba na kwa kina Zitto tu peke yao? Na kama na hivyo, basi tunaomba hizo taarifa za robo mwaka ya kwanza ( Januari hadi Machi ) ambazo kwa mujibu wa maelezo yako ilitakiwa yawe mtandaoni tangu Aprili 15 ( nimekunukuu Mh. Mwigulu katika swala la muda wa upatikanaji wa taarifa ) halafu hizo za Aprili zilizokupatia nafasi ya wewe kutuwekea mdahalo huu, hizo utatupatia kesho kutwa maana zinatakiwa ziwe zimekamilika kesho ( Mei 15 ) kwa mujibu wa vikao vys ki-benki na mpango ambao unafanyika dunka nzima kama ulivyotujuza kwenye maelezo yako Mh. Mwigulu. Asante na Mungu Ibariki Tanzania

    ReplyDelete
  18. Alichokiongea Mh. Zitto ni kitu cha kweli na anawasilisha hilo kwa niaba ya watanzania wengi ambao hawawezi kumpigia simu Gavana au wafanyakazi wa BOT na kuwaulizia kuhusu hizo data. Ni jukumu la BOT kuweka taarifa kwa wakati, hata kama wanakaa kila baada ya miezi miwili ili kuzipitia na kuchapisha, bila shaka ripoti ya mwisho ingekua ni ya Feb. 2012 na sio Nov 2011 kama inavyoonekana.

    Pia Mh. Zitto hajasema kama fedha za kigeni zimeisha ila kasema kuna TETESI na hivyo ni jukumu la BOT kuweka wazi ili kuondoa tetesi. Mh. Zitto kawasaidia katika kutimiza malengo yako maana yeye yupo karibu zaidi na jamii na anasikia mengi kuliko hao waliopo BOT.

    Ifikie wakati Mh. Nchemba ajue kuwa hilo haliihitaji siasa ila takwimu za kina za ukweli. Yeye sio msemaji wa BOT, hivyo angepaswa labda kuwashauri ili watoe takwimu sahihi na sio kuwajibia maana yeye sio RELIABLE source katika hilo.

    ReplyDelete
  19. ctill theres no justification as to why the information is not available online as needed, there's no reason,if they are sitting once a month for the meeting, why is the website not updated till now?its over 5 months.
    useless refutation from the ccm so called mchumi....

    ReplyDelete
  20. Wakati Nchemba akimpigia Ndulu angemtaarifu aweke hizo taarifa kwenye website. Ku update taarifa watu lazima wakae vikao??? Suala la kuwepo taarifa muhimu kwenye tovuti ni tatizo sugu kwenye tovuti za idara za serikali. Kuna watu wanalipwa kwaajili ya kazi hiyo! Wanalipwa kwa kazi gani? Halafu taarifa za mwenendo wa uchumi zinahitajika si kwa wabunge tu, ni muhimu kwa wadau wengi wenye masilahi ya na shughuli za biashara na uwekezaji. Ajabu huyu Nchemba anashindwa kuchambua hoja, wakati anadai alikuwa analyst benki kuu...huko alikuwa analyse kitu gani? Kama ni upotoshaji Nchemba ndiye anayetoa taarifa za kupotosha!

    ReplyDelete
  21. Mh Nchemba mi naona unaongea maneno mengi unasahau point, umetoa maelezo marefu lakini hujaeleza sababu kwa nn taarifa hazipo up-to-date. Cha muhimu hapo ni kuwajibika, kosa lipo wazi. Tunategemea kama ripoti ilikuwa tayari utaiweka leo unavyoendelea kuchelewa itaibua maswali zaidi

    ReplyDelete
  22. Anyway anachoongea zitto kuhusu kukosekana kwa taarifa hizo muhimu ni sawa. Lakini nadhani ni kosa kubwa kusambaza uvumi kuwa hazina haina pesa kabisa!!! Kwa hilo anatakiwa achukuliwe hatua, kwani hakuna adhabu dhidi ya uzushi wa jambo nyeti kama hilo? Mimi nimeshtuka sana niliposoma kuhusu hazina kutokuwa na hela kuliko hata kukosekana kwa taarifa!! Source za information zinaweza kuwa zaidi ya internet lakini kukiwa hakuna fedha madhara ni makubwa zaidi, sivyo? Mimi nadhani si lazima kwa mwanasiasa jina lako kusikika kila siku hata kama unachosema ni kupotosha umma. Lakini aliyejibu hoja ya zitto ni msemaji pia wa BOT? Mbona BOT wamekaa kimya? Why? Poa.

    ReplyDelete
  23. viongozi acheni kukurupuka

    ReplyDelete
  24. Kwani mh. Nchemba nimsemaji wa BOT?

    ReplyDelete
  25. Hi Mwigulu,
    Aisee kumbe wewe kijana ovyo sana, samahani bwana Michuzi kwa kuandika neno ilo, lakini ukweli lazima usemwe. Sasa Nchemba wewe unaona Zitto amekosea wapi katika ilo?. Hivi nikweli kila mwenye kuzitaka hizo taharifa lazima atafute namba ya Gavana aongee nae?, jamani badala na wewe kumuunga mkono Zitto eti unakuja kujinadi hapa kuwa ulikuwa mchumi daraja la kwanza!!!, sasa unasema hivyo ili iwe nini?. Suhala hapa Zitto hakatai kuwa BOT hawana data bali anasema hazijawekwa kwenye mtandao sehemu ambazo huwa zinapaswa kuwepo. Hivi ww unajua kutokuwepo hizo data kwenye mtandao kunavyoharibu hata mawasiliano ya kibiasha kati yetu na washirika wetu wa nje, wafanyabiashara makini wanatuona sisi Tanzania kama ni watu longolongo sana, hivi pale BOT hakuna watu wa IT watu wakupost hizo habari, au ndio wamejiwekea vikao kibao vya kuzipitisha taharifa na kila kikao wanalipana mamilioni ya posho. Mwigulu embu acha kujidharirisha bwana ebu jenga jina lako na heshima yako.

    Muddy Nice

    ReplyDelete
  26. Mh. Mwigulu asitake kutulazisha wananchi tuwe tunampigia Gavana simu kuulizia mambo ambayo kimsingi tunaweza kuyapata bila kupiga simu. Nani asiyejua usumbufu tunaoupata kupiga simu hata kwa mkurugenzi wa halmashauri sembuse Gavana. BOT wawe SMART ndicho kinachohitajika hapa hayo mengine Mwigulu ni mbwembwe tu.

    ReplyDelete
  27. Mi nafikiri kila mtu ana point:

    mheshimiwa Kabwe anauliza swali la msingi kwamba hizi taarifa mbona hazijawekwa mtandao baada ya miezi sita.

    Huyu mheshimiwa wa CCM anajibu swali tofauti kabisa, kwamba aelewi kwanini Kabwe analalamika wakati angewatufuta wahusika. Ila haijibu swali la Kabwe!!!

    Hizo info kwanini hazijawekwa hadharani ili wanachi tuzione???

    ReplyDelete