Monday, February 27, 2012

Kampuni ya Simon Group yanunua mabasi 30 ya UDA

Meneja Biashara wa Kampuni ya TATA, Srinivas Nemalapuri akionesha baadhi ya mabasi ya UDA yaliyonunuliwa na Kampuni ya Simon G.

Na Oscar Mbuza

HATIMAYE Kampuni ya Simon Group imeanza mikakati ya kulifufua Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) baada ya kununua mabasi 30 yenye uwezo wa kubeba abiria 40 kwa lengo la kuboresha sekta ya usafirishaji jijini Dar es Salaam .

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa UDA kununua magari mengi kwa wakati mmoja tangu kuanzishwa kwa shirika hilo zaidi ya miaka 38 iliyopita.

Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group, Robert Kisena aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba kampuni yake imejizatiti katika kuifufua UDA kama ilivyoahidi wakati iliponunua hisa za kuliendesha shirika hilo.

“Tayari yamewasili nchini ili kusaidia kuboresha hali ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa sasa mabasi hayo yamehifadhiwa kwa ajili kupigwa nembo ya UDA.”

Hatua hiyo ya Kampuni ya Simon Group kuagiza mabasi mengi kwa wakati mmoja ina badili taswira na mitazamo iliyokuwepo kwamba kampuni hiyo ya Tanzania haina uwezo wa kuweza kuhimili kikamilifu changamoto zilizopo kwenye sekta ya usafirishaji.

Baadhi ya Wabunge wa Jiji la Dar es Salaam walipokuwa wakichangia bungeni mwishoni mwa mwaka jana walieleza wasiwasi kwa kampuni hiyo kuweza kuliendesha Shirika la UDA kwa ufanisi kwa madai kwamba haina uzoefu wa masuala ya usafirishaji.

“Kimsingi ni kwamba kampuni yetu imejizatiti katika kuleta mageuzi makubwa sana katika sekta ya usafirishaji abiria hapa nchini, tunayo mipango mikubwa ni suala la kupewa muda wa kutosha na tutaweza kuthibitisha na kuondoa wasiwasi kwa abiria pamoja na watanzania wenzetu,” alisema Kisena

Kisena alisema katika kipindi cha miezi sita iliyopita Kampuni ya Simon Group imeweza kuingiza kati ya Sh. bilioni 2.7 na Sh. bilioni 3 katika uwekezaji ndani ya UDA.

Alisema kiasi hicho cha fedha ni zile za kulipa mishahara ya watumishi wa UDA, kununua vipuli vya magari pamoja na kununua magari mapya ikiwa ni fedha kutoka kwenye vyanzo vingine vya mapato kutokana na akaunti za UDA kusitishwa ili kuweka sawa baadhi ya kasoro zilizojitokeza wakati shirika hilo lilipokuwa chini ya usimamizi wa Bodi ya Wakurugenzi ya zamani, chini ya uenyekiti wa Idd Simba.

Kisena alisema anashindwa kuendelea na harakati nyingine za kuwekeza zaidi katika UDA hasa kutokana na ukiritimba katika kutatua tatizo lililopo. Lakini mwekezaji anasema kwamba ameambiwa kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja ujao Serikali itakuwa imekamilisha masuala yake.

“Kazi iliyobaki kwa Serikali ni namna ya kujiondoa ili sasa Simon Group iweze kuwa na udhibiti wa kampuni pamoja na uendeshaji wake…ninaamini kazi hiyo itakamilika katika kipindi hicho cha mwezi mmoja ambacho kinakadiriwa,” alisema Kisena

Anasema kama kampuni hiyo itakabidhiwa Shirika la UDA analenga kutoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi kutokana na wingi wa mabasi makubwa ya kubeba abiria jijini Dar es Salaam. “Tunataraji kutoa ajira nyingi zaidi kwa Watanzania, maana tunao mpango wa kuingiza nchini mabasi zaidi ya 1,000,” alisema Kisena

Aidha taratibu za ukaguzi wa mahesabu ya UDA zimeshakamilika na pengine Serikali inasuburi dokezo hilo ili taratibu nyingine za kumkabidhi mwekezaji mpya Simon Group ziweze kufuata.

Mapema mwezi huu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Ludovick Utouh alisema kuwa ripoti hiyo imewasilishwa Makao Makuu ya Kampuni ya KPMG nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuihakiki na kuangalia ubora wa ukaguzi wenyewe ndipo waikabidhi kwake aweze kuipitia.

Utouh alisema anatarajia kuipata ripoti hiyo wakati wowote ili aweze kuipitia na kuiwasilisha serikalini kwa ajili ya hatua zaidi. Alisema kwamba ripoti hiyo ilitakiwa kuwasilishwa Januari mwishoni, lakini kinachofanyika sasa ni kuhakiki zaidi ili iwe kwenye kiwango kinachokubalika.

Utouh alisema kuwa KPMG ni miongoni mwa kampuni zinazoanya vizuri kwenye kazi hiyo na kwamba, hakuna mashaka yatakayoweza kujitokeza juu ya utendaji wa kazi zao, bali kinachotakiwa kufanyika ni kusubiri wakati wa kuiwasilisha serikalini.

Kabla ya ubinafsishaji huo, UDA ilikuwa inamilikiwa kwa pamoja kati ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Serikali Kuu, kupitia Hazina, wakiwa na jumla ya hisa 15 milioni ambapo kila hisa moja ilikuwa na thamani ya Sh100.

Kwa mchanganuo, Halmashauri ya Jiji ilikuwa inamiliki asilimia 51 ya hisa hizo, huku Hazina ikimiliki asilimia 49. Februari 11, Bodi ya Wakurugenzi ya UDA, chini ya Idd Simba, ilikutana na uongozi wa Simon Group ikiongozwa na Mwenyekiti Mtendaji Kisena na kusaini mkataba, ambao ulithibitisha kwamba UDA ilikuwa imeiuzia Simon hisa milioni 7.8 sawa na asilimia 52.535 ya hisa zote.

Mkataba huo ungeifanya Simon Group kuwa mwanahisa mkubwa katika umiliki wa UDA kwa vile Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Hazina, wangebaki na hisa milioni 7.7, ambazo ni sawa na asilimia 47.465.

Baada ya mkataba kusainiwa, kipengele cha kwanza kiliitaka Simon Group kulipa asilimia 25 ya fedha za ununuzi wa hisa za UDA (Sh bilioni 1.142) ambazo ni sawa na Sh milioni 285.669, ndani ya siku 14, tangu kusainiwa ili kuufanya mkataba utambulike kisheria, na Simon Group ililipa fedha hizo siku hiyo hiyo.

No comments:

Post a Comment