Friday, January 6, 2012

BALOZI SEIF ALI IDDI AKUTANA NA MWENYEKITI WA UMOJA WA WAFANYABIASHARA WA KUPAMBANA NA UKIMWI ZANZIBAR

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDDI AKIZUNGUMZA NA MWENYEKITI WA UMOJA WA WAFANYABIASHARA WA KUPAMBANA NA UKIMWI ZANZIBAR { ABCZ } BWANA ALI ABOUD MZEE.BWANA ALI NA UONGOZI MZIMA WA UMOJA HUO ULIFIKA OFISINI KWA BALOZI SEIF KUJITAMBULISHA RASMI.
MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDDI AKIWA KWENYE PICHA YA PAMOJA NA UONGOZI MZIMA WA UMOJA WA WAFANYABIASHARA WA KUPAMBANA NA UKIMWI ZANZIBAR { ABCZ }. KULIA YA BALOZI SEIF NI MWENYEKITI WA UMOJA HUO BWANA ALI ABOUD MZEE.

Ukosefu wa uchunguzi wa Kiafya kwa Wafanyakazi walio wengi katika Taasisi za umma na hata zile za kibinafsi umekuwa ukiendelea kulaumiwa kwa muda mrefu ndani ya Kanda ya Afrika ya Mashariki.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa kupambana na Ukimwi Zanzibar { ABCZ } Bwana Ali Aboud Mzee alieleza hayo wakati Uongozi wa Umoja wake ulipofika kujitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Ali Aboud Mzee alisema Utafiti uliofanywa na kuwasilishwa katika Mkutano wa Mambo ya Afya wa Afrika Mashariki umethibitisha kuwepo kwa malalamiko mengi ya ukosefu wa Afya za Wafanyakazi katika sehemu zao za Kazi.

Alisema Taasisi yake ya ABCZ kwa kushirikiana na Sekta za Afya imelenga kutoa Taaluma ya afya hasa ile ya mapambanao dhidi ya kuenea kwa virusi vya Ukimwi kwa Watu wa Biashara pamoja na Taasisi za Kazi.

Bwana Aboud alisema muelekeo wa mafanikio katika utekelezaji wa malengo yao umeonyesha mwanga kwa vile kumekuwa na ushirikiano wa karibu zaidi na Viongozi wa ngazi za Juu jambo ambalo alisema limewapa nguvu zaidi.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Taasisi hiyo ya ABCZ kwa maamuzi yao ambayo yana lengo moja na Serikali katika kuhakikisha Jamii haiendelei kuambukizwa Virusi vipya vya Ukimwi.

“ Sote tunajenga Nyumba moja, hakuna haja ya kunyang’anyana mbao wala fito ”. Alitahadharisha Balozi Seif.

Alitahadharisha kwamba janga hili la Ukimwi halichagui Mtu wala Jinsia. Hivyo kila mtu ana wajibu wa kujilinda kwa vile Dawa ya kutibu maradhi haya haijapatikana licha ya juhudi mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa na Taasisi za Uchunguzi likiwemo Shirika la Afya Duniani {WHO }.

“ Liliopo hivi sasa kwa baadhi ya Jamii ni kudanganyana. WHO bado haijathibitisha kama ipo dawa inayoweza kutiba ukimwi ”. Alisema Balozi Seif.

ABCZ ni mkusanyiko wa Wafanyabiashara uliounda Umoja wa Wafanyabiashara wa kupambana na Ukimwi Zanzibar {Aids Business Coalition-Zanzibar }.

No comments:

Post a Comment