Saturday, April 9, 2011

MAMBO YAMEANZA- ZANZIBAR WAUKANA MUSWADA MABADILIKO YA KATIBA

*Wasema imeegemea upande mmoja wa Muungano

*Wahoji kutoshirikishwa SMZ katika maandalizi yake

*Wasema haiwahusu kwa kuzuiwa kujadili Muungano

*Wajipanga kuunda Kamati yao kukusanya maoni hayo

*Walazimisha Mkataba wa Muungano kuwa msingi


Na Mwantanga Ame

WANANCHI wa Zanzibar wameipinga rasimu ya uandaaji wa Tume itayoandaa Katiba mpya ya Muungano, wakidai haiko kihalali na pindipo serikali ya Muungano ikiifisha Bungeni itakuwa imekiuka Katiba ya Muungano.

Maoni hayo waliyatoa jana mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, inayoratibu maoni ya kuweza kupatikana mswaada wa sheria wa kuweza kukusanya maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba ya Tanzania, mjadala ambao umefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.

Mjadala huo ambao uliwashirikisha viongozi wa serikali ya SMZ, vyama vya siasa na Jumuiya binafsi, wameipinga rasimu hiyo huku wakionekana kuchukizwa nayo kutokana na sehemu kubwa ya mjadala huo ukichangiwa kwa jazba na maoni makali.

Kila kiongozi aliyepata fursa ya kutoa maoni alitamka wazi wazi kuikataa rasimu hiyo na kutaka irudishwe ilipotoka kutokana na kushindwa kuishirikisha Zanzibar kikamilifu katika maandalizi yake kiasi ambacho haina matakwa ya yanayohusu Zanzibar na Rais wa Zanzibar hakuwekwa kama ni mtu muhimu katika uundaji wa Tume hiyo.

Othman Masoud Othman (Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar)

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud, akitoa mchango wake alisema kuwa Bunge liliopo halina uwezo wa kuunda Bunge la katiba, huku akitaka aonyeshwe madaraka hayo yako ibara gani.

Alisema sheria ziliopo zinaelekeza ni namna vilivyotowa uwezo katika kifungu cha 68 ambacho kinatoa mamlaka ya kufanyika kwa marekebisho ya Katiba na sio kazi kuunda sheria.

Alisema jambo ambalo walitakiwa kulifanya kama serikali katika kuunda sheria hiyo walitakiwa kuwepo mapatano kati ya serikali mbili na kinyume cha hivyo watakuwa wanavunja Katiba ya Muungano.

Abukar Khamis Bakary

Alisema sio kweli kama serikali ya Muungano iliihusisha vilivyo serikali ya Zanzibar katika uandaji wa mswada huo kwani hata utaratibu uliotumika ulionekana haukuwa wa kawaida kutokana na mwanasheria wa serikali ya Muungano kumuandikia Mwanasheria wa Zanzibar barua kutaka mapendekezo ya Zanzibar.

Alisema kiutaratibu Waziri Mkuu alitakiwa kumuandikia Makamu wa Pili wa Rais na kumuelezea nia yao lakini hata barua waliyotuma ilikuwa na kasoro huku ikishindwa kuyazingatia mambo ya Zanzibar 14 waliyopendekeza na badala yake kuyaingiza mambo mawili ambayo yanawakandamiza Wazanzibar.

Alisema kilichotakiwa serikali ya Muungao kusema kama iliyapata mapendekezo ya Zanzibar lakini baada ya kuyapata walikaa kimya huku wakiengeza mapya manne ambayo SMZ hiyajui wala Wajumbe wa Baraza la wawakilishi.

Hamza Hassan Juma Mwakilishi (Kwamtipura)

Mwakilishi wa Kwamtipura Hamza Hassan Juma, akitoa mchango wake alisema mswada huo bado haujafikia muda wa kupelekwa Bungeni kwani serikali ya Zanzibar haijashirikishwa kikamilifu na kutaka mjadala wake usiharakishwe.

Alisema mswada huo kwa vile utakuwa na sehemu inayohusu Zanzibar ulitakiwa upelekwe katika Baraza la Mapinduzi kabla ya maandalizi yake ili uweze kujadiliwa na Zanzibar iweze kutoa mapendekezo yake vipi tume hiyo iweze kuundwa.

Kinachotakiwa kuona mswada huo unamshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar huku baadhi ya vipengele vyake vilitakiwa kumpa hadhi Rais wa Zanzibar kutokana na suala litalofanywa litahitaji kuihusisha Zanzibar.

Mansour Yussuf Himid (Kiembesamaki)

Alisema kuletwa kwa mswada huo ni kudanganywa kwa Wazanzibar, akiita siku ya jana kuwa ni siku ya huzuni kwa Wazanzibari.

“Siku hii ya leo (jana), kamati ya Bunge imekuja kutudanganya Wazanzibari na siku ya leo (jana) ni huzuni kubwa sana, kama Mtanzania kama Mzanzibari naona tunafanyiwa kiini macho, kama Baraza la Wawakilishi hatujashirikishwa, basi hakuna haja ya kukubali hilo”, alisema Mansoor.

“Lazima tushirikishwe ipasavyo na Muungano huu tumeungana kwa hiari sisi tumekwenda katika Jamhuri wenyewe hii ni Jamhuri ya pande mbili tumekwenda kwa hiayari tutarudi kwa hiyari tutabaki kwa hiyari”, alisema Mansoor.

Alisema hiyo ni nafasi pekee ya kuhakikisha Muungano unafanyiwa marekebisho kwani kukaa bila ya kukataa hilo hiyo ni fursa ya mwisho ambayo wananchi wa Zanzibar hawataipata tena iwapo mswada huo ukenda Bungeni na kupitishwa.

“Hii ndio fursa yetu ya mwisho Wazanzibari na kwamba tukicheza hapa ndio basi hatutakiona kitu chochote ndio basi tena” ,alisisitiza.

Mohmoud Abdulla Musaa (Kikwajuni)

Alisema haiwezekani kubakia na mfumo unaotaka kutumiwa na Bunge kutokana na kuwa haujazingatia matakwa ya Zanzibar.

Omar Dadi Shajak

Akitoa maoni yake alisema ndani ya mswada huo kinachoonekana umeandaliwa kama sheria nyenginezo zilizopelekwa Bungeni na kusahau kuwa Zanzibar ina mamlaka yake na kinachoonekana ni kuzingatia maoni ya upande mmoja pekee.

Alisema kuwa aina iliyotumiwa katika maandalizi ya rasimu hiyo Zanzibar haiwezi kukubaliana nayo kwani imefanywa kama ni mshiriki na ni vyema ikarejeshwa katika kiti cha Bunge.

“Wameiweka mashariki kwenye jua kali ili kipa asiweze kuona wapate kutufunga hili halikubaliki kwani kutompa mamlaka Rais wa Zanzibar kushauriana na Rais wa Muungano hili ni hatari na Rais wa Muungano atakuwa anamuamulia Rais wa Zanzibar” , alisema Dk. Shajak.

Katibu Mkuu huyo, alikosoa kipengele kinachoipa mamlaka Tume itayoundwa baada ya kukamilisha kazi yake ripoti itayoiandaa kukabidhiwa Rais wa Muungano pekee na badala kutaka ripoti hiyo wakabidhiwe marais wote kwani Muungano ni wa nchi mbili.

Alisema hatua hiyo itaweza kuwasaidia viongozi hao kuweza kukaa na kuiangalia kwa pamoja na badae kutoa mapendekezo yao kama viongozi wa nchi mbili balada ya Rais wa Muungano pekee.

Ali Saleh (Alberto)

Mwandishi huyo wa habari Muandamizi wa Shirika la BBC, alisema muswada huo haukugusa katiba ya Zanzibar hivyo ni kuzarau makubaliano ya Muungano ambayo yapo mambo yangepaswa yawemo haki za binadamu lakini jambo la kusikitisha halijaumuishwa.

“Kura ya maoni ni kitu gani je! Wazanzibari wakisema hawataki athari yake itakuwa nini? tusifikiri Wazanzibari watapinga katiba je! athari zake zitakuwa ni nini? Na kuhojia kwanini Tume hiyo isipelekwe mahkamani, akisema huko ni kuizuiya Demokrasia”.

Alisema mabadiliko hayo yamekuwa ni mazowea kutoka upande mmoja wa Muungano ndio maana watu hawashirikishwi ambapo alisema ni lazima katiba ibadilishwe na huo ni wajibu wa baraza la Wawakilishi.

Hassan Nassor Moyo

Akitoa mchango wake alisema wakati umefika hivi sasa wa serikali ya Muungano kukubali kuwapo kwa mabadiliko katika mambo ya Muungano na kuacha kung’anag’ania mambo waliyozoweya.

Alisema mambo waliyofanya miaka iliopita wakati wa kina Lusinde, Hassan Moyo na Sitta, hivi sasa hayapo tena na wasizuie kuwapo kwa mabadiliko kwani kazi yao imekwisha na watafanya makosa kuzuia mambo ya Muungano Wazanzibari waasiyajadili katika katika mpya.

“Haiwezekani hata kidogo wapewe nafasi waseme kwani hili nalisema ndani ya moyo wangu Nyerere alikuja Zanzibar na karatasi ina mambo 11, mimi nilikuwa Waziri wa Sheria alinipa faili na hakuna hata sentesi moja iliotolewa leo tunaambiwa kuna mambo 22 na Jumbe alipotaka kuengeza alifukuzwa kazi, sasa mnaposema tusizungumze mambo ya Muungano maana yake nini mnawaambia nini Wazanzibari”,alisema Mzee Moyo.

Alisema amesikitishwa kuona Mwanasheria wa Zanzibar kueleza kuwa hana taarifa ya mswada huo jambo ambalo ni la maajabu kwa serikali kwani kinachotengenezwa ni katiba mpya na sio kutia viraka na ni vyema kamati hiyo ikapeleka ujumbe wa Wazanzibari nini wanachotaka.

“Mnasema tusiseme mnataka tuzungumze utumbo, lazima mabadiliko yafanywe kwani hivi sasa vijana wamesoma na hawakubali kuamuliwa, Nyerere alikuwa anakubaliana na mzee Karume hakua anatoa maamuzi, Wewe sita umefanya kazi na Nyerere, Jumbe na Karume msifanye mambo ya wakati ule ‘is over’ ”, alisema Mzee Moyo.

Ali Mwinyi Msuko

Kada huyo wa CCM, alisema wanasheria wa Zanzibar wakae na wanasheria wa Tanzania bara kuupitia upya mswada huo na hakuna sababu ya kuharakisha kupelekwa Bungeni, rais Nyerere na Karume walikubaliana katika Muungao huo na kwa sasa nchi mbili hizi zikubaliane.

Alishauri kwamba mswada huo urudi tena Bungeni na ufuate taratibu kwa kisheria na kwa sasa hakuna sababu yeyote ya kujadiliwa huku akitoa mfano kwamba kujadili mswada huo ni sawa na kutwanga maji kinuni.

Salum Bimani

Mkereketwa huyo wa CUF, alisema anashangazwa na Waziri Sitta kutokana na kujipa maadaraka ya kuandaa taratibu za kuingiza Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki jukumu ambalo halikupata ridhaa ya wazanzibari,

Ali Omar NCCR Mageuzi

Alisema kinachoonekana ni muendelezo wa serikali ya Muungano kuiburuza Zanzibar kwa kuona kuwa haiwashikishi katika mamaunzi makubwa.

Hamad Mussa Yussuf (CHADEMA)

Alisema madaraka ya wananchi yapo mikononi mwao na inashangaza kuona bado serikali ya Muungano imekuwa ikiamua bila ya kuishirikisha Zanzibari.

Awadh Ali Said

Alisema baada ya miaka 50, Wazanzibari wanataka kujua Muungano umewaletea tija gani na una kasoro gani.

Alisema licha ya kuwa hakuna uwiano lakini yeye hakubaliani na hilo kwa kuwa lazima maslahi ya pande mbili yazingatiwe huku akilaumu kwamba mswada huo unaonekana ni wa upande mmoja wa Muungano wakati kuna nchi mbili zilizoungana.

Sheikh Azan Khalid Hamdan

Alisema ipo haja Tume hiyo ikarudi na mswada huo kwani Wazanzibari hawautaki na wanaweza wakasababisha kutokea kwa mgogoro na atahakikisha wanawaeleza waumini wao kuukataa.

Sheikh Muhidini Zubeir Muhidini

Alisema watawaeleza Maimamu wa misikiti yote waukatae mswada huo na watahakikisha wanapinga hadi kwenye madrasa na kuwashawishi Wabunge wa Zanzibar watoke katika Bunge kama rasimu hiyo itajadiliwa na kama watabakia wasirudi Zanzibar.
Salama Aboud

Alisema serikali inahitaji kuyaangalia mahitaji ya Wazanzibari kwani kinachoonekana hakuna uwiano uliotumika katika kutayarisha rasimu hiyo.

Mohammed Ahmed Mugheiry

Alimtatahadharisha Waziri Sita kutokana na kumuona kuwa anacho kifanya kitamharibia sifa yake kwani wanapaswa kutambua kuwa serikali iliopo imechaguliwa na wananchi na hivi sasa Zanzibar kuna serikali ya umoja ya kitaifa ambayo tayari imekaa vizuri.

Samuel Sitta

Akiwasilisha madhumuni na sababu za mswaada huo Samwel Sitta alisema mswada huo umependekeza kutungwa kwa sheria ya mabadiliko ya katiba ya nchi ya mwaka 2011 ambapo mswada unakusudia kuanzishwa kuweka masharti uanzishaji wa tume pamoja na sekretari kwa madhumuni ya kuendesha na kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mchakato wa mabadiliko ya katiba pamoja na muswada pamoja na masuala mengine utaangalia chimbuko na mahusiano ya katiba iliyopo kwa kuzingatia uhuru wa wananchi mfumo wa siasa ambao unatarajiwa kukamilika Aprili 1014.

Alisema pindi mswada huo utakapopitishwa na kuwa sheria utakuwa na utaratibu wa kisheria utakaomwezesha rais kuunda tume ya kukusanya maoni kuhusu katiba na kuunda bunge la katiba kwa madhumuni ya kutunga katiba mpya.

Sitta aliwataka Wajumbe hao kushirikiana na Kamati hiyo kuwashawishi wananchi kukubaliana nayo na itapofikia wakati watoe maoni yao kwani wamelazimika kufanya hivyo kutokana na hivi sasa wanataratajia kuwasilisha kupata bajeti inayokadiriwa kufikia bilioni 30 na mwezi huu wa nne itakuwa ni wa matayarisho ya Bajeti hiyo.

Hata hivyo Sitta aliahidi kuyafikisha maoni ya Wazanzibari kama yalivyotolewa katika mkutano huo.

Wakati watu wakichangia hamasa na jazba zilitanda huku wakipiga makofi ya kukataliwa mswada huo na kuimba nyimbo ya ‘sisi sote tumegomboka kwa ndugu’

1 comment: