Tuesday, March 1, 2011

Hotuba ya Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri Wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Wa Kimataifa Wakati Wa Uzinduzi Wa Mradi Wa Nyumba Poa Februari 28, 2011 Kigamboni, Dar es salaam

Tarehe 28 Februari, 2011

Wakurugenzi wa Nyumba Poa,

Wageni Waalikwa,

Wanahabari,

Mabibi na Mabwana,

Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa watendaji wa Nyumba Poa, kwa heshima mliyonipa ya kushiriki kama Mgeni Rasmi, katika tukio hili muhimu na la kihisoria la kuzindua mradi huu wa Nyumba Poa.

Pili ningependa kuwapongeza Washiriki wote wa Nyumba Poa kwa ubunifu wao wa mradi ambao nimeambiwa unalenga katika kuongeza uwezo wa Watanzania, hususan wa kipato cha chini, kujenga makazi yao binafsi na yaliyo bora kwa gharama nafuu. Wengi wetu tumeshuhudia jinsi Watanzania wanavyohangaika kwa kuishi kwenye nyumba duni na maeneo yasiyopimwa.

Mabibi na Mabwana

Wengi wenu mtakubaliana nami kuwa tatizo kubwa la serikali nyingi duniani, ni tatizo la “squatters”. Tatizo hili sio kwa Tanzania wala Afrika tu, na imedhirika kuwa Serikali haziwezi ku-adress tatizo hili bila ushirikiano wa ‘the prĂ­vate sector’; hususan Diaspora.

Mimi binafsi nimevutiwa sana na mradi huu kwani unawalenga wananchi wa kawaida hususan wenye kipato cha chini. Atakayekuwa na nyumba ya aina hii atakuwa amepata mtaji na atakopesheka; nyumba ni ufunguo wa kujikomboa kiuchumi. Hata wale wenye wadhifa na uwezo kama wa kwangu ambaye naweza kujenga my dream house moja kwa moja, bado naweza kabisa kujenga Nyumba Poa ya millioni 25, nikaipangisha na kujiongezea mtaji.

Ni matumaini yangu kuwa mradi huu utawanufaisha wale wote ambao wamekuwa wakisita kujenga nyumba kwa hofu ya gharama kubwa. Aidha mradi huu una uwezekano mkubwa wa kile kwa lugha ya kiingereza tunaita multiplying effects, kwani licha ya upatikanaji wa nyumba, utachangia pia ustawi wa jamii na kuongeza fursa za ajira nchini.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana

Mniruhusu sasa nielezee kwa nini ni mimi nimekuja kuzindua mradi huu na si mwingine. Kama tulivyoelezwa na Watendaji wa Nyumba Poa, mradi huu umeanzishwa na vijana wa Kitanzania wenye taaluma mbalimbali walizozipata kutokana na kuishi kwao na kufanya kazi katika nchi za Ulaya na Marekani (ughaibuni). Nimejulishwa kuwa baadhi ya Watendaji wa mradi huu wa Nyumba Poa wamekaa nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 20!

Mtakumbuka kuwa Serikali chini ya Uongozi wa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, imekuwa ikiwahimiza wanataaluma wa Kitanzania waishio ughaibuni kutafuta njia bora ya kuchangia maendeleo ya nchi yao, ama kwa kurejea nyumbani au kwa kuwekeza na kukuza uchumi. Mara kadhaa ambazo mimi nimeongozana na Mhe. Rais Kikwete katika ziara hizo, nimeshuhudia akitenga muda maalum kila ilipowezekana, ili kukutana na Watanzania wanaoishi nje na kuwakumbusha juu ya wajibu wao wa kuchangia maendeleo ya nchi.

Wenzetu wa Nyumba Poa, kwa kuitikia mwito huo, waliona ni vyema wakarejea nyumbani ili kutumia taaluma, uzoefu na weledi walioupata huko kama mchango wao. Kama mlivyosikia, hawa wa Nyumba Poa wamekuja kama Wazalendo wakiwa na “collective competencies” ili kuonyesha kwa vitendo kwamba kuna hazina kubwa ughaibuni. Hivyo basi, Wizara yangu inajivunia uzinduzi wa mradi huu wa Nyumba Poa, kwani ni kama sehemu ya mafanikio ya wajibu wetu katika kuhamasisha Watanzania walio ughaibuni kumuendeleza Mtanzania.

Watendaji wa Nyumba Poa,

Huu mradi wenu ni wa kwanza wa aina yake. Nawapongezeni kwa kuwa mfano bora wa kuigwa. Nawashauri mhakikishe mnatumia uwezo wenu wote, kuwafikia wananchi walio wengi na kuwaelimisha kuhusu ujenzi wa nyumba hizi za gharama nafuu, ambazo yeyote mwenye uwezo wa kawaida atazimudu. Ili taarifa kuhusu nyumba hizi ziwafikie walengwa, pengine mtaona busara ya kuwekeza kidogo katika kutoa elimu kwa kupitia vyombo vya habari na matukio mbalimbali ambayo yanahusiana na sekta ya makazi hapa nchini.

Aidha ningependa kupitia kwenu, kuwakumbusha Watanzania waishio ughaibuni kwamba Serikali inawatazamia waendelee kuchangia maendeleo ya nchi hii kwa kuwekeza na kuleta wawekezaji, fedha (remittances), taarifa za ni wapi duniani kuna fursa za kibiashara n.k. La muhimu zaidi, Serikali inahitaji kuwa na orodha ya Wataalamu wa Kitanzania walioko nje ili kuwashirikisha katika miradi mikubwa mikubwa ya ujenzi na nishati hapa nchini katika kile tunachoita Public Private Partnership (PPP).

Kwa upande wetu tuko tayari kuwasemeeni, na kuwapigia debe pale inapobidi. Mimi binafsi kwa kuwa nashughulikia masuala ya Diaspora na Mkurugenzi wa Diaspora ambaye yuko hapa leo, tutakuwa vipaza sauti kwa niaba yenu. Aidha naahidi kuwa Wizara yangu itahakikisha inafanya kila liwezekanalo, ili kupata ushirikiano unaostahili kutoka katika vyombo vingine vya Serikali na wadau tunaohusiana nao, ili hatimaye malengo ya mradi huu yatimie na yawe ya kudumu.

Mabibi na Mabwana,

Miaka miwili iliyopita nilikwenda Comoro nikaonyshwa eneo ambalo Serikali ya nchi hiyo imetenga kwa ajili ya raia wake wanaoishi ughaibuni. Baada ya kuona mradi huu wa Nyumba Poa, nadhani hii ni changamoto kwa Serikali, pengine na sisi tuangalie uwezekano wa kuiga mfano wa Comoro. Ni wajibu wa Serikali kujenga mazingira mazuri na kuwapa nyezo Watanzania walioko ughaibuni walete utaalamu na rasilimali zao.

Nina taarifa kwamba wapo Watanzania wanashindwa kurudi nyumbani kwa kuwa hawana makazi, na hawana watu wa kuwaamini kuweza kuwajengea kwa bei watakayoidumu. Hawa watawategemea nyie kupitia Nyumba Poa muwaongezee uwezo nao wakopesheke. Huu ndio umuhimu wa Diaspora kwa uchumi wa nchi. Sioni njia bora zaidi ya kupambana na umaskini.

Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana

Nisingependa kuchukua muda zaidi kutoa hotuba, ila naomba mniruhusu kwa mara nyingine tena niwapongeze kwa dhati wenzetu wa Nyumba Poa kwa kurejea nyumbani na kujihusisha na utatuzi wa tatizo kubwa la upatikananji wa makazi bora kwa wote. Ni matumaini yangu kuwa mafanikio ya mradi huu ambao umejengwa na Watanzania wenyewe, wa nyumba ambazo zinaweza kujengwa popote nchini, yatakuwa chachu kwa Watanzania wengine walioko nje kuhamasika kurejea nyumbani na kujiunga na wenzao katika kuleta maendeleo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Mwisho, napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi kwa ujumla, wadau mbalimbali, hususan wale walioko katika sekta za makazi, habari na mabenki, kuwapa ushirikiano unaostahili watendaji wa Nyumba Poa, ili mradi huu uweze kufanikiwa na kuchangia katika kutimiza azma ya kuhakikisha maisha bora zaidi kwa kila Mtanzania.

Baada ya kusema hayo; ninayo furaha kubwa kutamka kuwa Mradi huu wa Nyumba Poa Umezinduliwa Rasmi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza!

No comments:

Post a Comment